Particles. Mlipuko. Mlundiko wa data. Haya ndio yatokanayo kwenye matembezi niliyofanya na wenzangu kwenye saiti ya tafiti ghali kuliko zote duniani: saiti ya Large Hadron Collider pale CERN. Ndani ya bomba la duara lenye uzingo wa kilomita 30 hivi, protoni zinakimbizwa kwa spidi ya kilomita 299000 kwa sekunde ili kusababisha mlipuko mdogo pindi zinapogongana. Mlipuko huu unatumiwa kufahamu sifa za vihimili viundavyo maada (matter), pamoja na siri mbalimbali kuhusu ulimwengu wetu.
Bajeti ya utafiti wa CERN ni T.Shs Trilioni 1 kila mwaka. Wengi wetu tunaweza kushikwa na hisia na kuwakasirikia na kuuliza kwanini wanatumia pesa nyingi hivi kwa tafiti kama hizi zisizokuwa na uhakika? Wakati huohuo mamilioni ya watu wanakufa kwa ukimwi, malaria na njaa kila mwaka. Binafsi ninadhani mpaka tutakapofahamu umuhimu wa sayansi kwa manufaa yetu wenyewe (waTanzania), hatuna haki ya kuwa na hisia hizi. Sayansi yetu ya kupambana na haya majanga inahimizwaje? Au jamii yetu tutabaki kushabikia akina dokta manyau tu.
Spidi ya hatua zilizopigwa na wenzetu kwenye sayansi inastaajabisha. Na kutambaa kwetu katika lengo hili hili halitazaa matunda kama hatutaamka. Tunahitaji kufinywa na kuhimiza sayansi nyumbani.
…Tatizo kubwa la nchi yetu ni kwamba uhamasishaji wa elimu upo kwenye nadharia badala ya vitendo…vile vile napenda kusema kuwa lugha itumiwayo kwenye shule nyingi za umma ni kiswahili…hili tu ni kikwazo kikubwa mno ukizingatia kuwa ngazi yetu kisayansi iko chini sana. Nasema hivi kwa kuwa, makala nyingi na vitabu huchapishwa kwa kiingereza, hata wajerumani na waspanyiola wameamua kuwasilisha uvumbuzi wao kisayansi kwa kutumia kiingereza. Kwa ujumla, kama kilatini kilivoyokuwa lugha ya wasomi zama za kale, kiingereza ni lugha ya wasomi wa zama za sasa. Kwahio, ni vigumu kwa wanafunzi/watoto wetu kujieleza kisayansi au kuelewa sayansi isiyokuwa na visawe au maneno wakilishi kwa lugha ya kiswahili. Sisemi kwamba kiswahili hakifai, la, namaanisha kuwa pamoja na kwamba twahitaji lugha yetu – urithi wetu ukue, ni muhimu sana kwenda na wakati ilhali tunakipigania maendeleo ya kiswahili. Kwa ujumla mitaala ya elimu ya kitanzania kuanzia shule ya awali mpaka chuo kikuu, inabidi iangaliwe upya na mawazo ya kimapinduzi yafikiriwe kulingana na mazingira yetu, yaongezwe na kutumiwa kwa faida ya vizazi vijavyo.