Picha kwa hisani ya Y. Charahani
Na Shaaban bin Robert
Novemba, 1945, binti yangu ambaye alikuwa ni mwanafunzi katika Skuli ya Serikali huko Mpwapwa alifaulu katika mtihani wa darasa la nne. Yeye alikuwa ni mmoja wa watoto watatu wanawake waliokuwa wamefanikiwa katika mtihani huo. Skuli ya Mpwapwa ilikuwa haina darasa la tano kwa ajili ya watoto wanawake. Mtoto mwanamke mmoja tu alipata nafasi ya kwenda katika darasa la tano katika skuli ya Tabora na wawili waliobaki waliachwa wajisaidie wenyewe. Binti yangu alikuwa ameanza kuonyesha maendeleo mema. Ikiwezekana nilitaka apate nafasi ya kufuliza katika masomo na hata ya kuweza kutenda yaliyo bora kuliko bibi yake (mama yangu) ambaye hakujaliwa kuona maisha ya skuli katika utoto wake.
Mama yangu alikuwa na kila hali ambayo mimi mtoto wake niliweza kuona fahari kubwa juu yake. Sithubutu kabisa kumtoa katika fadhili na shukrani. Deni lake kwangu la wema alionitendea halilipiki kabisa. Kasoro yake ilikuwa hakujua kusoma, kuandika, kuhesabu na mengine ambayo ni vyombo bora sana katika matumizi ya mwanadamu katika dunia. Katika wakati wa utoto wake vyombo kama hivi vilikuwa havipatikani katika Afrika. Masoko yake yalikuwa hayajulikani kabisa. Kwahivi wazazi wake waliweza kuepuka lawama juu ya ujinga wa binti yao kwa udhuru kuwa katika wakati wao skuli zilikuwa ni adimu kabisa. Udhuru huu ulitosha sana kwa msamaha.
Wakati tulio nao sisi sasa kosa la kumwelimisha mtoto haliwezi kusameheka hata kidogo pasipo mapatilizo. Mtoto yoyote anyimwaye makusudi nafasi ya kujifunza matumiza ya kusoma, kuandika na hesabu ana haki ya kuwalaumu wazazi wake katika maisha yake atakapojiona kuwa amefungiwa milango yote ya kusitawi baadaye. Kwa mtoto mwenye kujaliwa kuwa na wazazi wake hata utu uzima bila ya kufundishwa mambo haya ubaya wa lawama hii ni mwingi mno kuliko kwa mtoto ambayye bahati mbaya ilimfanya kuwa yatima mapema kabla hajaweza kujiendesha mwenyewe katika dunia.
Kwa sababu hii sikutaka binti yangu akatizwe katika masomo yake wala aishi maisha ya ujinga ambayo yatamwongoza kunishtaki kuwa nimepoteza roho yake kwa sababu sikumpa nafasi ya kujielimisha. Ilikuwa wajibu kabisa nifanye yote niliyoweza ili aweze kuishi maisha ya kunishukuru na kuniombea kwa madua mema badala ya kunilaani kwa madua mabaya katika maisha yake yote……
Mali ya nchi ni watu. Watu hao hawawezi kuwa bora katika nchi yao pasipo kupata malezi bora wakati wa utoto wao. Nilitaka binti yangu aweze kupata nafasi ya kuwa mtu mmoja wa watu bora wa halafu. Ikiwa sadaka ya jambo hili ilikuwa ni mali nilikuwa tayari kulipa kadiri yoyote iliyokuwa katika mfuko wangu; na kama ilikuwa ni taabu nilijiandaa kuikabili hata mwisho wa uvumilivu wangu.
Maisha Yangu Na Baada Ya Miaka Hamsini. (1966) Thomas Nelson and Sons, Ltd.
Sura: Naondoka Mpwapwa
Je, unadhani ni wangapi enzi hizo walikuwa na mtazamo huu kuhusu elimu kwa wasichana?
Ni wananchi wangapi leo hii ndani ya Afrika wana mtazamo huu endelevu?
Labda nyakati hizi mjadala utahusu elimu ya sekondari na chuo kikuu.