Kelele za “mwizi, mwizi!” zinapopigwa, unyama na ukatili usio wa kawaida huamshwa ndani ya roho za baadhi yetu. Huu ni ukweli usiopingika kutokana na maovu tunayowatendea binadamu wenzetu, wanaoitwa wezi. Tunawapiga na hata kuwachoma moto bila kujua kama wana hatia au la; kama wameiba fedha za umma au wamekwepua tu cheni bandia. Kuendelea kwa matendo haya ya kinyama, kikatili na kutisha, ni kosa letu wote. Na ni lazima tugawane lawama sisi sote kama wanajamii.
Inatubidi tujiulize: Huu ukatili uliojengeka na kuwa sehemu ya utamaduni umetoka wapi? Ni kwanini bado tunakubali uendelee katika jamii yetu?
Hoja za majibu hayo ni nyingi, lakini pia nyingi ni za kijinga na kipumbavu, tena hutoka kwa watu wanaojidai kuwa na akili timamu — kumbe ni makunyata tu! Hili suala la kuongezeka kwa hali ngumu ya maisha, huja na ongezeko la hasira, ngeni, hasa pale mtu anapoibiwa kile alichokihangaikia kwa jasho na damu yake, tena kihalali. Hilo linaeleweka, lakini halitoi idhini kwa mwananchi kujichukulia sheria mkononi. Watu wote wanaojichukulia sheria mkononi, wao pia wamevunja sheria sawa sawa na yule muhalifu wanayempiga. Tena uhalifu wao ni mkubwa zaidi kwasababu wao wameua! Wameiba uhai wa mtu ambae aliiba simu, ambayo inayoweza kununuliwa tena. Inaonekana ukatili ukitupanda, basi unatupanda kweli na tunatupa pembeni mawazo na maamuzi ya busara, na kuanza kumcheka nyani na makalio yake bila kujua kuwa yetu ni mekundu pia. Tena yetu ni mekundu zaidi kwani yanatiririka damu ya huyo tunayempiga na kumchoma moto.
Lakini, je, ni sahihi ‘kutetea’ ukatili wa baadhi yetu na kudai unatokana na ukata wa maisha na umasikini unaotusumbua? Labda hasira na misongo yetu binafsi huishia kutolewa kupitia ukatili kwa tunayemtendea unyama mtu anayeiitwa mwizi. Hapa ndipo ninaanza kuona umuhimu wa madaktari wa kisaikolojia, au therapists. Baadhi yetu, ambao ni wehu na wakatili kupindukia, tunadhani kumpiga mwizi itapunguza kuchanganyikiwa au misongo ya maisha yetu. Kwani, kumbonda binadamu mwingine na jiwe kichwani ni kama therapy session… tiba mbadala.
Sasa ujuha na ukatili ndipo hapo huingiliana kwasababu kuna watu – tena tunaishi nao majumbani mwetu, tunafanya nao kazi, tunasalimiana nao mitaani, na hata kwenda kusali au kuswali pamoja – wanadiriki kutetea ukatili huu. Hoja zao za kikatili na kipuuzi hudai kuwa, kuwauwa wezi ni fundisho kwa wengine; tatizo la uhalifu litapungua.
Nasema fikra hizi ni za kikatili, kipumbavu na kipuuzi! Na watu wenye mawazo haya tuwaogope zaidi ya ukoma!
Kwasababu ifuatayo: Hali halisi ni hivi, hata tukiwachapa na kuwachoma moto vibaka kwa kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya, kamwe hawatapungua. Hii ni kwasababu, mwisho wa siku, tumbo lenye njaa litakoroma tu; njaa itauma, na binadamu huna budi kukubali kulitumikia vile uwezavyo. Utake usitake. Na jinsi ajira zilivyokuwa finyu, kwa waliosoma na ambao hawakubahatika au kupata nafasi ya kusoma, hawawezi kuacha kuiba mpaka wapewe maisha mbadala. Sisemi kwamba kama hujasoma na huna kazi basi uibe. Hapana! Lakini ndio hali halisi ya vibaka wengi. Jambo la msingi hapa ni kwamba, kujaribu mabadiliko ya mazingira hubadilisha tabia za watu; kwani hata siku moja mkulima wa mahindi havuni mihogo.
Upande wa pili wa sarafu ni hivi vyombo vyetu vya habari. Waandishi wa habari wanazidi kutuangusha katika kupinga huu ukatili. Vyombo vya habari vimekuwa vikichochea badala ya kukemea, na hata wale ambao wanakemea, wanafanya hivyo kinafiki! Sio wote, ila kuna wale ambao wanakemea huku wakitumia lugha ya uchochezi.
Vyombo vya habari vina nafasi nyeti sana katika jamii, kama tulivyoona katika mauaji ya halaiki Rwanda mwaka 1994. Vyombo hivi vilitumika kujaza watu uhasama na kuchochea mauaji, huku wakiita upande mmoja “mende.” Hiyo ilisaidia kufanya upande huo kuonekana sio binadamu tena, hivyo thamani yao kupotea na utu wao kuyeyuka. Matokeo yake tunayatambua vizuri.
Kwani, si ni vigumu kumuua kuku? Ujue, pindi utakapomuona binadamu mwenzako kama kiumbe tofauti na binadamu, basi kumuua inakuwa sio vigumu tena! Leo hii vyombo vya habari wanadiriki kutumia lugha kama mwizi “akibanikwa.”
Hebu tuangalie matumizi ya lugha hapo. Kuku hubanikwa, mbavu za mbuzi hubanikwa, hao wote ni wanyama! Lakini utumiapo neno hilo kwa binadamu mwenzako, ina maana umemvua utu wake. Thamani ya uhai wake haizidi ya mnyama mwingine yoyote tunayemchinja kama kitoweo. Hivyo, pamoja na kuwa tunaweza tukawa tunapinga mauaji hayo, lakini matumizi ya lugha yetu yanahamasisha na kuchochea.
Halafu vyombo vingi hupenda kutumia maneno “wananchi wenye hasira kali.”
Kuna chembe za kuhalalisha dhana ya ukatili. Eti kwasababu walikuwa na hasira, na tena ni haki yao kuwa na hasira… Huu ni ujinga mtupu ulio tukuka! Kwani mara nyingi hao wananchi wenye ‘hasira kali’ ukiangalia picha kwa ukaribu, utagundua wengi wao wana nyuso za kushangilia, kuchekelea na kushabikia. Hivyo hiyo dhana ya kuwa na hasira ni potofu.
Vyombo vya habari na waandishi wamekuwa wakipotosha jamii kwa kuchapisha na kuongelea mambo ya uongo. Hapo hapo, vikizidi kuwachochea wakatili hawa badala ya kukemea moja kwa moja kwa lugha sahihi — kali. Hivi kwani, tukiwaita wananchi hao wakatili, wauaji, kuwapiga picha na kuwaanika mbele ya jamii, si litakuwa jambo la busara? Mbona wezi wa mali ya umma, mapapa wa nchi hii, tunawaita mafisadi? Kwanini wao tusiwaite wajasiriamali?
Inabidi baadhi ya vyombo vya habari viache unafiki na ushabiki. Mimi na wewe hatuna budi kupinga na kukumea vikali unyama huu! Na kuacha kuwaita hao wauaji ‘wananchi wenye hasira kali’, kwani (nadhani) tunawapa kichwa kwa uwenda wazimu wao.
Tuwapige picha, na tuanze kuwatafuta. Tukianza na huyu aliyebeba tofali na huyu anayemvisha tairi mwizi!
Jeshi la polisi nalo libebeshwe lawama kwa kushindwa kukomesha huu unyama. Tabia ya kuwaachia wahalifu kutokana na sababu wanazozijua wao wenyewe linachangia ukatili huu kuendelea. Wakuu wa Jeshi la Polisi nawashangaa kwani hawaoni aibu kwa kufanyiwa kazi yao na wananchi. Kwani hii imekuwa hadithi ya mkia kuongoza kichwa? Jeshi la Polisi liwatie nguvuni wahalifu na mkondo wa sheria uchukue nafasi yake. Pia, iwatie nguvuni wananchi wanaoshiriki katika haya mauaji ya kutisha. Hata kama atakamatwa mmoja, huo ndio utakuwa mwanzo. Jeshi likikaa na kushangalia haya mauaji, na sisi raia wa kawaida tufanyeje? Mheshimiwa IGP Mwema, hili ni tatizo ambalo nadhani linahitaji suluhisho, au haya maradhi yatazidi kuendelea kwenye jamii, na kidonda kuishia kuwa ndugu.
Mimi ninaamini kunaweza patikana njia mbadala ya kuadhibu wahalifu tunanapowakamata mitaani. Kwanini tusifanye kama nchi nyingine, mwizi akikamatwa, achapwe mijeledi kadhaa, kisha apelekwe polisi? Hili linaweza kusimamiwa na balozi wa nyumba kumi kumi wa mtaa aliokamatiwa mwizi huyo, au hata kiongozi yoyote wa mtaa huo. Lakini utekelezaji wa adhabu hii utafanywa ndani ya vipengele vya sheria na si kienyejienyeji tu.
Hoja ya pili ni hii ya kukata viungo pindi mwizi akamatwapo. Hilo lisipewa hata nafasi, kwani haliwezi kuwa adhabu mbadala. Najua baadhi yetu hapa ambao wanadhani hilo ni jambo la maana katika kukomesha wahalifu. Hilo ni jambo la kikatili sana, kwani ukishamkata mtu mkono umezidi kumrudisha nyuma kimaisha. Kivipi? Wezi wengi ambao tunawakamata mitaani ni watu ambao hufanya kazi za kutumia nguvu “blue collar jobs,” kama zikipatikana. Hivyo basi, pale tunapoamua kumkata mkono, tunamfanya ashindwe kuweza kujitegemea. Kazi gani atapata akishakuwa na mkono mmoja, na hana elimu? Hivi kweli atapata kazi ya kubeba mizigo Kariakoo, au ataishia kuwa omba-omba, halafu aanze kufukuzana na wana-mgambo? Hilo la kukomeshana kwa kukatana viungo halina mantiki, tena ni ukatili mwingine ambao utaongezea watu shida za kimaisha badala ya kuwasaidia.
Kuna mambo mengi sana ambayo yanaweza kufaidisha Taifa letu pindi wezi wanapopatikana na kufungwa jela. Tanzania ina ardhi kubwa tu, kwanini wasilimishwe? Au hata kwenda kusaidia wanavijiji kuvuna na kulima, na kushughulishwa na kazi nyingine za kijamii? Serikali haitakuwa na haja tena ya kuajiri watu wengi kufanya baadhi ya kazi zinazohitaji nguvu nyingi kwani zitashughulikuwa na wafungwa. Tayari, si wanalishwa na kodi zetu? Basi watumiwe ipasavyo katika jamii ambayo inawalisha. Moja, watajifunza mbinu mbadala za kuendesha maisha yao. Pili, watasaidia kujenga jamii badala ya kuendelea kuiharibu kwa matendo yao maovu.
Mwisho, tusikae hapa na kujazana ujinga. Eti jicho kwa jicho, jino kwa jino ndio suluhisho la uhalifu. Sote tutaishia kuwa chongo au vibogoyo. Sasa sijui nani atamwongoza nani baada ya hapo. Wadau wa kwenye vyombo vya habari wajue kwamba wao wana nafasi kubwa sana katika kukemea na kusaidia kutokomeza huu unyama wa baadhi ya manduli wachache katika jamii yetu.
Pia tusisahau kuwa, hata tukichomana moto kila siku, kama hali ya maisha ni ngumu, ni ngumu tu. Na watu watafanya vyovyote kukidhi mahitaji yao; hapo ndipo viongozi wa maisha bora kwa kila Mtanzania inabidi waulizwe, kulikoni? Hivyo, wachochezi wote wa huu unyama, wananchi wenye roho za kikatili za namna hii na viongozi mafisadi wanao sababisha hali ya Mtanzania kuzidi kuwa ngumu, wote ni makunyata!
Vijana wenzangu, hatuwezi kuendelea kufanyiana ukatili kama huu sisi wenyewe kwa wenyewe. Tuelewe kuwa umasikini wetu unasababishwa na mafisadi wachache walio juu… Hao ndio maadui zetu wakubwa.
Tazama video hii kama tu una moyo mgumu.
Mauaji ya albino. Uchunaji Ngozi. Na haya ya kila siku – kupiga mwizi mpaka mauti. Huwezi amini hii ndio Tanzania yetu, ya ‘amani na mshikamano’ yenye watu ‘wapole’.
Binafsi ninakubaliana na Bahati, iwepo sheria ili atakayekamatwa kuhusika na mauaji ya mwizi kwa makusudi (baada ya kumkamata) nae afunguliwe mashtaka – manslaughter. Why not even murder? Wananchi wakimkamata mwizi, na polisi akikuta mfu inabidi hapo hapo wachukuliwe suspects.
Tukumbuke kua hawa wanaohusika na haya mauaji ni wananchi wa kawaida tulio nao kitaa. Unadhani tendo la kumrushia mtu jiwe hadi kumuua ni dogo? Iwe mwizi au la, tendo hilo au la lolote la ukatili linaweza kujirudia kwenye jamii hapo baadaye. Hao hao wanaweza wakawa wanaendelea ukatili huo majumbani mwao, au kuwa waanzilishaji wa vurugu, au hata kufanya matendo ya ujambazi hapo mbeleni hali ikiwa ngumu.
Kwenye moja ja video hizo za ukatili utasikia mtu akisema “Leta shoka tuwapige kichwani maramoja tu… Chap chap… Amekufa wapi, hajafu huyu ms**ge”.
Naukemea huu ufedhuli.
Linki niliyosema nitaitoa hapa muione, jap osi nzuri lakini imebandikwa jana tu, kabla ya wewe kuchapisha posti hii. Habari yenyewe ni hii hapa [bofya].
Narudi kwenye posti yako.
Nimesoma mwanzo hadi mwisho ulichoandika. Nilitarajia kuongeza pointi lakini kadiri nilivyoendelea kusoma ndivyo nilivyokuta kuwa umetaja yale yote niliyokuwa ninayawaza, na zaidi.
Umegusia suluhisho au njia mbadala ya nini kifanyike pindi wanapokamatwa watuhumiwa wa wizi.
Nadhani ikiwa kweli Serikali zetu hudhamiria kutenda wasemayo, basi kesi za watu hawa zingekuwa zinashughulikiwa haraka na kutolewa hukumu ili mtu aanze kutumikia adhabu haraka iwekekanavyo, lakini tatizo lililopo, tunaambiwa mahakimu wapo wachache, wakati mwingine kesi hazisikilizwi kama ilivyopangwa kutokana na dharura jambo ambalo limesababisha mahabusu zikajaa kuliko magereza. Mtu anapokaa muda mrefu mahabusu, hajifunzi mbinu yoyote ya kumsaidia maishani, na inapokuja kusikilizwa kesi yake, aidha mashahidi wameshakata tamaa au walioathirika wameamua kuachana na kesi hiyo, matokeo yake, mtuhumiwa anaachiwa huru na kwa kuwa hakuelezwa kinagaubaga kuhusu kosa lake, anatoka na kuingia kwenye jamii kwa uso wa kujionesha kwamba alionewa, matokeo yake ni mwendelezo wa wizi na kurudia habari ile ile.
Mwishowe, ninaafiki kuwa kuwaadhibu watuhumiwa wa wizi kwa kuwapiga hadi kufa, si suluhisho na kwa mtazamo wangu usio na takwimu, sijaona kama hali hii inapungua, sana sana ninakubali kuwa binadamu yeyote atafanya lolote atakaloweza ili kuweza kukidhi hitaji la njaa na mavazi kwanza, kwa hivyo akikosa kupata kwa njia halali, kuiba ndiyo njia pekee iliyobaki, na atakapoiba mara mbili tatu asikamatwe, ataendelea, hadi hapo atakapopata ajira ya kumwingizia kipato kukishi mahitaji muhimu ya chakula, mavazi na malazi.
Ajira ni changamoto ya Serikali na Wananchi.
Ni kweli usemavyo Bahati, inawezekana ndio maana hata hawa vibaka wakimpata “victim” na wao wanakua hawana huruma, wanaweza kukuchoma kisu, kukupiga sana hata wale wenye bunduki wanakua hawana hiyana ya kukufyatulia risasi.
Ila kama mmoja wa watu waliokua “victims”, kwa kweli nakueleza hawa vibaka wanapokufanyia, sidhani kama utakua na huruma nao, watakuchania nguo, wakutishia kukuchoma bisi bisi na hata kukuchoma visu.
Naomba unielewe kuwa nakemea kwa vibaka kuchukuliwa sheria mkononi, ila na hao vibaka lazima waelewe sisi tunaoibiwa nao tunakuwa na hali mbaya sana wanapotunyizia.
Umetaja solutions nyingi tu za maana, ikiwezekana kuongeza vituo na doria za askari, yote mazuri.
Ila tukumbuke hawa vibaka na hasa majambazi wanapokupata kwa kweli hawana huruma nawe, sasa inakuwa kazi sana mtu kujizuia hasira kwa kweli.
Nionavyo!, nakuelewa.
Lakini nadhani tunachanganya vibaka, waporaji na majambazi. Sidhani ni busara kuwaweka kwenye kundi moja. Kinachotokea ni hiki (kwa mtazamo wangu): Tunatishwa na majambazi wanaotumia silaha kama bunduki, ambao ni wauaji; tunapigwa roba za mbao, kutishiwa kuchomwa bisibisi na waporaji (wanaofanya shughuli zao usiku kwenye vichochoro)… Halafu tunakuja kuwapiga na kuwachoma moto vibaka — wakwapuaji wanaofanya uhuni wao mchana wakati jua linawaka.
Angalia kwenye hizo picha au video, watu wanachoma vibaka, sio majambazi wala waporaji (wanaotumia silaha). Ni kama tunapeleka misongo (frustrations zetu za maisha au uwoga wetu wa majambazi au waporaji) kwa vibaka, wanaochomoa tu simu au pochi.
Hapo ndipo ninapotatizwa, na utakubaliana nami kuwa hicho ndicho tunachofanya.
Nakumbuka mtaa niliokuwa naishi, watu walitaka kumuua kibaka aliyetuhumiwa kuiba NDOO YA PLASTIKI YA MAJI! Kuna la kutetea hapo? Na wengine wamekufa kwa ajili ya uwizi wa simu, mikufu, wallets n.k.
Tunapeleka hasira zetu kusikotakiwa. Tunapenda kulaumu, tukiambiwa ukweli tunatafuta visingizio. Lakini sioni dhana au mantiki ya kuwachoma vijana moto. Wapigeni vibao, wadhalilisheni.. kisha muwakabidhi kwa polisi — na tusikimbie kufuatilia kesi.
Na uchambuzi wa Bahati ni mzuri tu; lugha tunazotumia zinajaribu kuwavua utu tunaowachoma moto. Hatujisikii vibaya kabisa baada ya tukio… Jamani, mtu anapigwa msumari wa kichwa halafu watu wanaangalia na kushangilia (Hii ilitokea Keko/Chang’ombe in late 1990s, karibu na uwanja wa Sigara)? Kuna kitu hakiko sawa kwenye vichwa vyetu.
Ni kweli usemavyo SN:
Na karibu yote uliopendekeza nayakubali, na mie nilikosea kwa kweli kutofautisha kati ya majambazi na vibaka.
Ila tujiulize unafikiri majambazi yanatoka wapi, huwa wanaanza kama vibaka kwanza na kuishia majambazi.
Kupunguza vibaka ni kama ulivyoshauri, lakini kama tujuavyo mapendekezo mengi na mazuri kama hapo juu ya wadau huwa yanaishia kwenye mafile na kusahauliwa na serikali kudai hela hakuna na hawana jinsi ya kusaidia vijana wetu.
Kwa sasa tutafanyaje?
Kutembea mchana inakua kazi, wakati wowote ule kinaweza kutokea chochote, unaweza kuibiwa simu, begi lako, saa au kunyang’anywa vitu vyote na kukuacha na chupi (kama hawataitaka pia!). Usiku ndio usiseme, ni balaa tu, Masaki, Msasani, Oysterbay na labda Mikocheni karibu na wakubwa kidogo hali nzuri, leo hii unatueleza tukiwakamata vibaka (ambao watakua majambazi), tuwapeleke polisi, na kama ujuavyo polisi, kama wewe ndio umeibiwa, polisi wanaweza kukugeuzi kibao kama kibaka ni mjanja, ikawa kazi na shughuli kwako kujikwamua na shutuma zilizokugeukia kibao!
Haya yote lazima tuyafikirie, sio vyema tu kuwalaani watu kwa kuua vibaka, wananchi wanajua ni kama sheria hakuna kwa mwananchi wa kawaida, hasa kama huna pesa na muda.
Swala la mafisadi, huwezi kusikia hata siku moja fisadi kaenda na katumikia kifungo hapa kwetu, mifano ipo, kina Mramba, Yona, Lowassa, Karamagi, Msabaha, Rostam, Chenge, Dr. Idrissa n.k. Hawa vithibiti vimetolewa wanahusika, je kuna lolote hasa la maana katika hiyio sheria unayoisema imewashughulikia?
Wananachi tumechoka, sheria inakua upande wako kama ni mmoja wa watu kwenye “elite”, otherwise hakuna sheria kwa wananchi. Na kama sheria ikifanya kazi basi ujue mkubwa kaingilia hilo swala. Hatuna confidence ya aina yoyote na sheria za nchi.
Umesikia Tony Tzamburakis kapewa dhamana akilipa 4m/- na hati za mali zisizohamishika, baada ya kudaiwa kuiba 400m/-! Wapi na wapi?
Kwa kweli wananchi hasa walalahoi tusiokukua na majina makubwa tumechanganyikiwa, hatujui la kufanya na ndio maana wananchi wanaona heri wachukue sheria mkononi, PAMOJA NA KUWA MIE NAPINGA KABISA!
Mimi ninaanza kuamini, matukio kama haya hutokea zaidi kuliko tuzaniavyo. Na kila tukio, utasikia wananchi wamechoshwa na hiki au kile, hivyo wameona wawe wanasheria na mawakili wao wenyewe. Kwa mfano hii habari hapa kutoka kwenye blog ya Jiachie..