Ras Innocent Nganyagwa

Napenda kuchukua nafasi hii kutumia blog ya Vijana FM kumtafuta Ras Inno. Kama una mawasiliano naye, tafadhali mwambie kuwa Vijana FM inahitaji kuwasiliana naye ili kuangalia uwezekano wa yeye – kama Kijana muhamasishaji – anaweza kuwa mmoja wa wachangiaji kwa njia ya blogs.

Kwa wale ambao hawafahamu kazi zake, soma moja ya makala zake ambazo alikuwa anaziandika kupitia Free Media Tanzania kuhusu kabila la Wahaya.

__________________________________________________________________

WAHAYA – Kabila lisilokuwa na mila za tohara

SHUMARAM waitu! Amakuru! Naam msomaji ni baadhi ya salamu za kabila la Wahaya kutoka katika himaya yao ya Buhaya iliyoko mkoani Kagera, kaskazini mwa nchi yetu.

Zipo salamu za aina nyingi za kabila hilo kutokana na umri wa msalimiwa, daraja yake katika jamii na wakati husika. Hayo na mengine, ni baadhi ya mambo tutakayoyaona japo kwa uchache kati ya mambo mengi yanayolihusu kabila hilo ambalo wengi hudhania wanalifahamu, lakini kumbe sivyo, hasa wale waliowahi kuishi jirani na watu wa kabila hilo katika maeneo ya mbali na mkoa wao wa asili. Nitakufafanulia vyema kadiri tunavyoendelea na safu yetu kwa siku ya leo.

Buhaya ni himaya ya watu wa kabila hilo iliyomo ndani ya mkoa wao wa Kagera ambao zamani ulikuwa ukiitwa Bukoba. Kagera ni jina la mto lililopewa msisitizo na kuanza kutumika hasa baada ya vita baina ya nchi yetu na Uganda katika ugomvi wa mpaka mwaka 1978. Jina la himaya hiyo ya Wahaya ni sawa na unavyoona baadhi ya majina ya himaya za jirani nao kama ile ya Baganda.

Tofauti na picha ya ujumla wanayoijenga watu wengi wasio wa kabila hilo wanapokutana na watu wa kabila hilo, Wahaya hawako sawa wala si wa aina moja, wana makundi mbalimbali yaliyoko katika mafungu mawili au matatu hivi.

Tofauti hiyo ya mafungu husababishwa na tofauti ya asili na mgawanyiko wa kiutawala wa ‘abakama’ ambapo kila kundi lilikuwa na ‘mkama’ wake. Msomaji ‘mkama’ ni chifu na abakama ni wingi wa neno hilo, yaani machifu. Tuyaangalie makundi hayo ya Wahaya kama ifuatavyo:

Kutoka fungu la kwanza, kuna Wayoza wanaotokea maeneo ya Kyamtwara, wanaosemekana kuwa ndio Wahaya halisi kwa asili, mkama wao anaitwa Rukamba, ambaye aliyepo sasa ni Emmanuel Rukamba. Rukamba ndio jina la mkama wa Kyamtwara tangu zamani, ambaye baba yake alikuwa Rwaijumba.

Makundi mengine kutoka fungu hilo ni pamoja na Waendangabo wanaotokea Bugabo, Wahamba wanaotokea Kihanja, Wanyambo wanaotokea Karagwe, Waziba wanaotokea Kiziba na Wanyahiyangiro wanaotokea Muleba.

Fungu la pili lina makundi au makabila mawili ambayo mara nyingi watu wamekuwa wakiyahusisha na Wahaya, lakini wao wenyewe hawajihusishi nao kwenye asili yao kwa maana huchukuliwa kuwa ni wageni, hawa ni Wahangaza na Wasubi wanaotokea Ngara mpakani na Burundi na Biharamuro, wanajitofautisha na makundi haya, hasa kutokana hata na lugha za watu wanaosikilizana nao ambao ni Warundi, Wanyarwanda na Waha wa Kigoma ambao wanapatikana pia Kakonko karibu na Ngara.

Fungu la mwisho lenye kundi moja ni lile lenye Wakara wa kutoka Bukara Maruku na wale wa Bukara Kisiwani. Pana utata fulani kuhusu kundi hili, lakini nitaufafanua hapo baadae. Katika hayo majina ya makundi, tofauti inasababishwa pia na asili licha ya ule mgawanyiko wa utawala wa kihimaya.

Na katika hilo la asili, kabila hili hata katika baadhi ya mambo lina tofauti na makabila mengine, tuangalie namna watoto wanavyopewa majina. Mtoto akizaliwa hupewa jina na babu au bibi upande wa baba, majina hutolewa kutokana na jinsia, wakati au tukio fulani lenye kuonyeshwa kwenye jina hilo. Kwa mfano, wasichana wanaoitwa Koku unaweza kukuta kuna Kokubanza, Kokusima au Kokushekya.

Banza maana yake wa kwanza, Shekya maana yake ni kitu chenye kuchekesha, Sima ni shukurani. Upande wa wavulana unaweza kukuta mtu anaitwa Muta ambapo kimalizio kinaweza kuwa Lemwa (Mutalemwa), au Kyawa (Mutakyawa) au Kyamirwa (Mutakyamirwa).

Lemwa maana yake ni kuwezekana, yaani jambo linalowezekana au jina kama Ruge ambapo kimalizio kikiwa ni ‘malila’ na kupata jina la Rugemalila. Malila maana yake ni kumalizia mwenyewe.

Aidha, katika kabila hili kuna hali ya kuthamini sana heshima ya mtoto wa kike kiasi cha kuwa na kanuni nyingi juu ya mahusiano yake na jinsia ya kiume, ambazo zikikiukwa adhabu zake huwa ni kali na zinazoonekana kandamizi kwa wanawake, kwa sababu wanaume ambao ni wahusika pia katika makosa hayo hawachukuliwi hatua yoyote.

Tuone baadhi ya mambo ya mfano huo. Binti akipata mchumba siku ya kuagwa kwake, ‘kasiki’, shangazi mtu humpa mafunzo ya jinsi ya kwenda kuishi na kumhimili mume, kasiki ni sawa na kusema ‘Send off’. Kwa kawaida Wahaya hawana mafunzo yoyote kabla ya hapo kama vile unyago na hata jando kama ilivyo kwenye makabila mengine.

Kwa ufupi, hata kwa watoto wa kiume, Wahaya hawana tohara kwa asili na kama wanafanya hivyo kwa sasa, ni kutokana na kuchanganyika na watu wa jamii za makabila mengine.

Msichana anatakiwa kuwa bikira anapoolewa, na ndoa hiyo lazima ijibu na kithibitisho kuonyesha kuwa alikuwa bikira, binti anayefaulu kujitunza na kuwa katika hali hiyo mpaka siku ya ndoa, huchukuliwa kuwa ‘yamwebola’, yaani mali mpya.

Nini humtokea binti mtukutu asiyefuata maadili anayopaswa? Tuone baadhi ya mifano, mathalan msichana akitoroka nyumbani na kulala nje ya nyumba ya wazazi waje, japo kwa usiku mmoja tu, hukanwa na kuchukuliwa kuwa mwenye mapungufu na hakubaliki kikamilifu pale nyumbani kama binti mwadilifu, hivyo huitwa ‘Nyailya’. Huyu hawezi kuolewa na kijana ambaye hajaoa bali ataolewa na mtu ambaye ameshataliki au kufiwa na mkewe.

Sasa nikusimulie juu ya lile fungu la mwisho kati ya makundi ya Wahaya lenye Wakara, ambapo wapo wa pande mbili, wale wa visiwani na wale wa bara, yaani Maruku na kumekuwa na mvutano, ubishani na kutokukubaliana kina nani walitokana na kina nani. Kuweka sawa hilo kuna simulizi hii.

Hapo zamani kwa amri ya machifu, msichana akishika mimba kabla ya ndoa huuawa ama kwa kutupwa kutoka kilele cha mlima mrefu mahsusi kwa kazi hiyo, ‘ruasha’, mlima wa Itahwa ulitumika sana kwa kazi hiyo, adhabu hiyo ilitolewa ili kufuta aibu na kuuepusha ule ukoo wa binti aliyefanya hivyo na matatizo.

Au huweza hata kutoswa ziwani, katika kuona uchungu wa kuuawa kwa watoto wao, baadhi ya wazazi waliwaokoa watoto wao kisirisiri kwa kuwapakiza kwenye boti na kuwapeleka kisiwani Bukara, kilicho karibu na Ukerewe.

Kizazi cha wazaliwa wengi waliokolewa kwa mtindo huo, kilitokea zaidi Bukara ya Makuru na kufanya kuwe na Bukara Kisiwani. Lakini Wakara wa Kisiwani waliongezeka na kuwa kabila linalojitegemea na ni moja kati ya makabila watani wakubwa wa Wahaya na mpaka leo hawakubali hoja ya kuwa wao walitokana na Wakara wa Makuru, Bukoba bara.

Kuna kanuni nyingine katika zile kanuni kandamizi kwa wanawake, mathalan machifu waliwachagua mabinti tangu wakiwa wadogo tu wamezaliwa na kuwaoa wanapokuwa wakubwa, iwe wameridhiwa au hawakuridhiwa, na walifanya hivyo ili kuongeza uzao wa watoto wengi kwa wake zao wa mafungu wa kuchagua tangu utotoni ili kujihakikishia mrithi wa utawala wake kati ya watoto wake hao wengi.

Jambo jingine ni ndoa za kubebwa ‘kulea’ ambapo kijana akimpenda msichana huwaagiza vijana wenzake kumvizia na kumbeba, labda mathalan kama ameenda kuchota maji, akishakuwa naye kwa usiku mzima asubuhi huenda kujitambulisha kwa wazazi wake kwa kutuma ujumbe na hupigwa faini ambayo mara nyingi huwa kubwa na baada ya hapo taratibu za kuidhinisha ndoa hiyo kwa njia za kawaida hufuata.

Msomaji, bado yapo mambo mengi juu ya kabila hili, lakini kwa sasa nikuachie hapa, tukutane tena wiki ijayo nitakapokumalizia simulizi hizi, tutakapoangalia kwa kina juu ya matambiko na mizimu yao.

Tutapata pia simulizi za kusisimua kama ile ya ‘chungu cha chem chem’ kilichosababisha kuwepo kwa Ziwa Kihanja na hatimaye tutaweka sawa dhana potofu zinazojengewa sifa tofauti na maana halisi ya baadhi ya maneno ambayo hulinganishwa na maneno ya baadhi ya himaya za jirani kama vile Baganda.
__________________________________________________________________

Nadhani baada ya kusoma nakala hii, utakubaliana nami kuwa Inno atatusaidia Vijana kupitia uzoefu na ujuzi kuhusu Tanzania aliokuwa anakusanya wakati akifanya ziara zake za muziki.

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend