Swala la ujasiliamali linakwenda bega kwa bega na ubunifu, na ubunifu unachangiwa kwa namna moja au nyingine na elimu. Tukikubali kuwa ujasilimali, elimu na ubunifu vinauwiano wa karibu, tutaanza kuona kwa ukaribu nyufa ambazo zinazozorotesha maendeleo katika elimu Tanzania na ujasiliamali kwa ujumla. Elimu inayotolewa haina changamoto ya kuchochea maendeleo. Hivi leo katika zama hizi za sayansi na teknolojia ungetegemea kuona tunatumia maendeleo ya kiteknolojia kukuza ubunifu, lakini ndio kwanza tunazidi kung’aa macho.
Sasa ni wapi ninakwenda na hayo yote niliyosema, ni hivi yote haya yanalenga maswala mawili, kwanza elimu na teknolojia na pili ubunifu ndani ya ujasiliamali kwa kutumia teknolojia. Hili tunaweza kuliona katika video ifuatayo ya huyu bwana Khan ambaye anatumia youtube kuelimisha dunia. Sasa Khan ni mfano wa jinsi gani teknolojia inaweza kuboresha elimu/ ufundishaji na jinsi ambavyo walimu wanaweza kufanya kama alivyofanya Khan na kutengeneza pesa kwa madarasa watakayo weza kuweka mtandaoni. Sio kazi rahisi lakini hakuna mwanzo mrahisi kwa kawaida.
Madarasa hayo siyo lazima yawe ya hisabati, sayansi, n.k bali madarasa ya sanaa, kwa mfano namna ya kuchora tingatinga. Internet imetupa uwezo wa sisi kuweza kuwa wabunifu bila mipaka lakini bado tumeng’ang’ania ku-surf tu. Mfumo kama huo wa Khan Academy unaweza boresha sekta ya elimu na jinsi tunavyo elimisha vijana. Kwanza, itawapa wale watu wenye uwezo kuelimisha lakini hawataki kujihusisha na mfumo dhaifu wa elimu ya Tanzania nafasi ya kusaidia. Pili, watu wataweza kujiwezesha kiujasiliamali kwa kutumia mbinu kama ya Khan. Najua kutakuwa na matatizo ya hapa na pale, hasa ukizingatia miundo mbinu yetu bado inamatatizo, lakini ni swala ambalo siyo baya kulitupia macho na kuanza kulifanyia kazi.
Sasa mimi nawaachia vijana wenzangu changamoto hiyo. Tanzania bado tupo nyuma, na wenye uwezo tuanze kuanzisha Khan Academy zetu japo kusaidia wale ambao hawakupata bahati au nafasi ya kwenda shule kwa sababu moja au nyingine. Wakereketwa mpoooooooooooooo…kazi ni kubwa na safari si fupi, na maendeleo ya Tanzania yapo juu ya migongo yetu vijana.
Kuhusiana na suala la ujasiriamali kwetu vijana ni mchezo mgumu kwani kwetu mitaji ni nothing.