Picha za vitendo vya ushirikina na uchawi nilizoziona kwenye blogs mbalimbali wiki iliyopita bado zipo kwenye mawazo yangu. Kuandika makala mara nyingi huwa ni jambo rahisi kwangu, muda tu ndio kitu ninachohitaji. Lakini nashindwa…Sijui nianzie wapi; sijui niandike nini; na wala sijui dondoo za makala ziwe vipi. Napata hisia ngeni — hasira, simanzi na nadhani ubongo wangu unashindwa kutoa ujumbe ambao nataka uwafikie Watanzania wenzangu.
Tumemkosea nani kwenye dunia hii? Je, tunastahili kushuhudia vitendo vinavyoendelea kufanywa na Watanzania wenzetu? Akili changa za wadogo zangu hazipaswi kuanza kutafakari ushirikina unaofanywa na wanajamii wenzetu. Vilio vya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi vinatua kwenye ngoma safi za masikio ya watoto wetu. Mboni nadhifu zinapokea mwanga unaobeba taswira ambazo…Ah! Nalengwa na machozi.
Viganja vyangu nahisi vimekuwa vizito na siwezi kuandika kwa kasi ya kawaida. Nawakumbuka ndugu na rafiki zangu wenye ulemavu wa ngozi na naamua kupiga moyo konde kukemea upumbavu, ujinga na fikra potofu zilizopo kwenye vichwa vya Watanzania — sijui ni wachache au wengi.
Ripoti yenye takwimu kuhusu tabia na desturi za Waafrika bila shaka ilitushtua wengi! Sidhani kama takwimu zilizotolewa kuhusu imani za ushirikina na uchawi Tanzania ni sahihi. Lakini hata kama wangesema ni asilimia moja tu ya Watanzania, bado ningejiuliza maswali mengi sana.
Miaka iliyopita tulikuwa tunaongelea suala la ushirikina na uchawi kwa utani. Ilikuwa ni kichekesho tu pale tuliposikia timu fulani imeingia uwanja wa Taifa kwa kuruka ukuta. Au mashabiki kuchimbia hirizi kwenye viwanja vya mpira. Na hata hatukushtuka pale watu walipoamua kufukia vichwa vya mbuzi.
Wale ambao tulikuwa ‘tumelala’ tuliamshwa na kelele za vilio vya wazee Shinyanga, Mwanza na Mara mwanzoni mwa miaka ya 2000. Vikongwe (ambao walikuwa hawana jinsi, bali kuwapikia chakula wajukuu na vitukuu vyao kwa kutumia kuni zinazotoa moshi) walipigwa mapanga bila huruma. Angalia tulipofika sasa.
Itachukua miaka mingi sana kusafisha jina la nchi yetu.
Natamani haya yote yangetokea kwenye ndoto…