na Lisa Boyd
[A similar article in English can be found here. Do not hesitate to comment in English, too!]
lisa from Trust Tour on Vimeo.
Katika vijiji vingi vya Tanzania, ukosekanaji wa maji safi ya kunywa na matumizi mengine husababishwa na kutokuwepo mipango ya kudumu ambayo huwawezesha wanavijiji kujitegemea. Kwahiyo nimeamua kuanzisha organization, “JamiiWater“, ambayo inahakikisha mipango ya maji safi inadumu kwa muda mrefu. Tofauti na programu nyingine, JamiiWater inalenga kuwashirikisha na kuwahamasisha wanajamii kujiendesha bila usimamizi wowote kutoka nje.
Vijiji vingi vina vyanzo vya maji ya kunywa ambavyo vinapaswa kuangaliwa na jamii yenyewe husika. Kwa maneno mengine, sidhani sekta husika za Serikali na NGOs mbalimbali zina mafanikio makubwa, hasa linapokuja suala la udumishaji wa vyanzo vya maji. Programu zao huwa na kamati za jamii ambazo huundwa na makundi ya watu wanaojitolea kuendesha mambo yote ya mfumo mzima wa maji. Lakini, kama nilivyoambiwa na kiongozi wa kijiji kimoja mkoani Dodoma, “Wanaojitolea (kuendesha mipango hii) wanakuwa wanajali hadi pale jambo muhimu zaidi (kwenye maisha yao) linapotokea!”
Katika jamii ambazo JamiiWater inafanya kazi, kila mpango na mfumo mzima wa maji huwa unaendeshwa na kuongozwa na mwanakijiji (a Community Water Manager) ambaye anachaguliwa na wanakijiji.
Utendaji na utekelezaji wa malengo ya JamiiWater unatokana na utafiti nilioufanya kwenye vijiji 23 Tanzania na programu za awali nilizozianzisha mwaka 2009 kwenye wilaya ya Mpwapwa. Katika programu hizi, mwanakijiji mmoja (ambaye hulipwa) huendesha mfumo wa maji kila siku, hukarabati/hulipia ukarabati, hukusanya fedha/michango kwa ajili ya matumizi ya maji, na huipa Serikali ya Mtaa asilimia fulani ya fedha kila mwezi, ambazo huhifandhiwa kwa ajili ya ukarabati mkubwa pale unapohitajika. Kiongozi huyu hufundishwa na JamiiWater jinsi ya kufanya ukarabati na kuhakikisha mfumo wa maji unaendelea kufanya kazi ipasavyo. Kazi zote za kiongozi mteule ‘huangaliwa’ na wazee wa kijiji na bodi husika.
Mfumo huu umesaidia kuondoa tatizo la vikundi vya watu wanaojitolea — ambao mara nyingi hutoweka baada ya muda fulani — na umesaidia kudumisha mifumo ya maji safi vijijini.
Je, unafahamu vijiji ambavyo vinahitaji msaada wetu? Umefurahishwa na kazi tunayofanya na ungependa kujiunga nasi?
Kwa taarifa na habari zaidi kuhusu JamiiWater, tembelea tovuti yetu: www.jamiiwater.org. Au tuandikie barua pepe: jamiiwater@gmail.com.
Maoni yenu yanakaribishwa.