Msomaji, nina uhakika unajua tarehe yako ya kuzaliwa. Lakini sijui kama unakumbuka mambo yaliyokuwa yanajiri wakati mama yako anajifungua. Kumbukumbu zote ulizonazo kuanzia sekunde ulipoanza kupumua mwenyewe hadi kipindi unaanza kutambaa zimetokana na picha au hadithi na simulizi ulizosikia kutoka kwa wazazi, ndugu na marafiki wa karibu na familia yako.
Je, kuna wakati unakaa chini na kutafakari mwanzo wako ulikuwaje? Nini kilikuwa kinatokea kwenye maisha yako kabla hujaanza kuota meno?
Au kama una bahati, ulikuwa na watu ambao walikuwa wako tayari kukuelezea mambo mbalimbali yaliyokuwa yanakutatiza. Na kama ulikuwa una bahati sana, ulizungukwa na watu ambao walikuwa wako tayari kukupa hata vifaa vilivyokusaidia kuona na kuelewa vitu gani hasa vipo karibu na sayari yetu.
Kizazi chetu kimekuwa na bahati ya kushuhudia mapinduzi katika teknolojia ambayo hutusaidia kujifunza mambo mbalimbali na kuturahisishia maisha kwa ujumla. Bahati mbaya teknolojia hiyo hiyo imekuwa inatuletea zahma mara nyingine (soma kuhusu Manhattan Project 1942-46; huu ni mjadala wa siku nyingine)!
Ukitafakari kwa makini utaona kuwa tabia za watoto wadogo na sayari yetu zinarandana. Wakati uko mdogo unakuwa kwenye fikra zako ambazo hakuna kiumbe mwingine anazielewa na unadhani uko peke yako. Lakini kadri unavyozidi kukua ule mtazamo unabadilika — watu walio karibu nawe hukusaidia kuelewa yanayokuzunguka.
Kwa upande mwingine, sayari yetu tulidhani ni pekee. Lakini sasa hivi tunajua kuwa kuna vitu vingine ukiacha hii dunia. Teknolojia (ambayo unaweza kuilinganisha na watu wanaomzunguka mtoto mdogo) imetusaidia kujifunza nini hasa kilichopo karibu na hii sayari yetu.
Kuna wanasayansi ambao wanajaribu kutafuta viumbe hai nje ya sayari yetu. Na hawaishii hapo tu; wanaamini wameanza kuona dalili za uwepo wa viumbe vyenye akili. Hapa nazungumzia intelligence — uwezo wa kufikiria, kutatua matatizo, kuwasiliana, kujifunza vitu vipya n.k.
Kwenye filamu fupi ifuatayo Jill Tarter anaongelea programu ya SETI na utafiti wao wa kutafuta civilizations nje ya sayari yetu:
Unadhani tuko wenyewe kwenye ulimwengu mzima? Au unaamini watu wa SETI watafanikiwa? Je, teknojia yetu inatupumbaza tu na kutupa ‘kiburi’?
Kwa kuwa hakuna faida yoyote, hizi hela si zingetumiwa kutatua matatizo ya nishati kwenye sayari yetu?…Napenda kusikia mawazo yenu!