Katika muongo huu, ndoto ya Prof. Shayo yaweza kutimia. Kuna mpango mkubwa wa kuanzisha vituo vya sayansi kama vya Prof. Shayo barani Afrika unaosimamiwa na mwanafizikia maarufu kutoka bondeni Prof. Neil Turok. Kupitia chuo alichokianzisha cha African Institute for Mathematical Science chenye makao makuu huko bondeni, Prof. Turok nae ana ndoto ya kujenga vituo kama hivi kila kona ya bara la Afrika ili kusaidia kukuza mafunzo ya hisabati na sayansi. Ndoto yake ni kumpata gwiji wa fizikia/hisabati kutoka Afrika atakayeleta mabadiliko katika sayansi kama aliyoleta Albert Einstein katika karne ya 20. Tanzania ni moja ya nchi ambayo kituo cha AIMS kinatarajiwa kujengwa. Hadi hivi sasa mchakato huu bado upo katika majadiliano.
Tunajua kuwa elimu ya sayansi na hisabati inazembewa na wengi nchini. Ila hii isiwe sababu ya kutohimiza suala hili kwa hali na mali kwa wanafunzi wetu. Nina imani pia, Tanzania yaweza zalisha akina Einstein iwapo tukiwa na jitihada maalumu kusimamia somo la hisabati katika mitaala ya elimu yetu. Kwa wanaosimamia mazungumzo ya mchakato wa kuanzisha kituo cha AIMS Tanzania, msituangushe.