Nimefurahi kuwa leo nimejifunza kitu kipya.
Inaonekana kuwa Vijana wenzetu wako karibu na viongozi wetu. Na cha muhimu zaidi ni kwamba wanajihusisha kwenye shughuli muhimu za siasa — kampeni na (labda) kupiga kura muda utakapowadia.
Ni jambo jema nadhani; lakini nashindwa kujizuia kufikiria na kujiuliza: Hizi juhudi zingekuwa zinapelekwa kwenye nyanja nyingine muhimu kwenye jamii zetu, mambo si yangekuwa angalau afadhali kulinganisha na hali ilivyo sasa hivi? Mara ngapi umesikia kampeni kama hizi kwa ajili ya kununua madawati au kujenga shule? Au kununua vifaa muhimu kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu hospitalini?
Nawaomba chonde chonde jamani Vijana wenzangu mliopata nafasi kama hizi za kuwa “karibu” na viongozi na chama tawala, endeleeni kupiga kelele tunazosikia kwenye nyimbo zenu!
Ukiacha hayo, ingekuwa jambo la busara kama hawa Vijana wenzetu wangetupa sababu za kujihusisha na siasa au chama husika. Kwa mfano: ‘Mimi Mwakipesile Albas’tini, nimeamua kujihusisha na kampeni za chama fulani kwasababu zifuatavyo… (a), (b), (c) na (d).’ Kuonekana kwenye mabango tu bila kusema chochote inachefua. Je, hizo hela zitatumiwa vipi?
Na mwisho ningependa kutupia jicho suala la Mh. PINDA kutawazwa kuwa kamanda wa VIJANA (CCM) mkoani Rukwa na kaimu kamanda wa VIJANA Taifa, KINGUNGE NGOMBALE MWIRU. Macho yangu yamekuwa kengeza nadhani…