Miti ya mianzi inapatikana kila kona ya bara letu. Mti huu una sifa ya kuwa na ugumu wa hali ya juu na hudumu kwa muda mrefu baada ya kukatwa. Wajomba zangu kule Mbeya wanatumia mti huu kutengeneza nyumba zao, na sehemu mbali mbali za Tanzania na Afrika Mashariki huutumia kutengeneza vitanda, fensi za nyumba/boma, na kadhalika.
Nimefurahi kusikia kuwa kuna miradi kadha wa kadha iliyoanzishwa ili kutengeneza baiskeli za mianzi kwa ajili ya matumizi vijijini Afrika. Mradi unaoongoza ni ule wa Columbia University – Bamboo Bike Project. Walianza Ghana, na sasa wamefika Kenya katika kusaidia ujenzi na kuhamasisha utumiaji wa baiskeli hizi vijijini. Baiskeli hizi zina uwezo wa kubeba mizigo mizito, na utengenezaji wake ni rahisi, pamoja na gharama zake ni ndogo ukilinganisha na baiskeli za kuagiza.
Kwa muhtasari tazama video:
Tembelea tovuti ya Bamboo Bike project kupata taarifa zaidi, na labda wewe kijana hapo Ileje, Mbeya waweza tengeneza baiskeli yako ya mianzi. Kama u mjasiriamali, wasiliana na timu ya Bamboo Bike Project ili kutathmini uwezekano wa mass production nchini Tanzania.