Na Paul Sarwatt
NDOTO ya Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutumia mradi wa ujenzi wa barabara ya kuunganisha mikoa ya Arusha na Mara inayopita katikati ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kama mtaji wa kuombea kura kwa wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu iko katika hatari ya “kuyeyuka” kutokana na jumuiya za kimataifa kupinga ujenzi huo.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita takribani 421 inatarajiwa kuanza kujengwa mwaka 2012 na tayari watalaamu wa upembuzi yakinifu wameanza kazi wakitarajiwa kuikamilisha mwishoni mwa mwaka huu. Taarifa kwamba ujenzi wa barabara hiyo kuwa “ulimbo” wa kura kwa wapiga kura wa Kanda ya Ziwa zinathibitishwa na kauli ya hivi karibuni ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga. Waziri huyo amekaririwa na vyombo vya habari akisema ujenzi wa barabara hiyo kupitia Hifadhi ya Serengeti uko palepale kwa kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM.
“Barabara hiyo ni ahadi iliyoko kwenye Ilani ya CCM kwa wapiga kura wa Kanda ya Ziwa kwa hiyo ujenzi wake ni lazima utekelezwe,” anasema Waziri Mwangunga. Aliwatoa wasiwasi wanaharakati wa uhifadhi wa ndani na nje ya nchi kuwa ujenzi huo utazingatia ushauri wa kitaalamu utakaotolewa kabla ya kuanza kutekeleza mradi huo. “Tuko makini sana na suala la uhifadhi kwa hiyo ningependa kuwatoa hofu wanaharakati wa uhifadhi kwamba mradi wa barabara hautakuwa na madhara kwa wanyama na Hifadhi yenyewe ya Serengeti,” alisema.
Pamoja na kauli hiyo ya Mwangunga habari kuwa barabara hiyo ingerahisisha zaidi kampeni za CCM katika mikoa hiyo katika uchaguzi wa mwaka huu zilithibitishwa na moja wa watendaji wa CCM mkoani Mara ambaye alizungumza kwa simu na Raia Mwema mwishoni mwa wiki. “Ni kweli suala la ujenzi wa barabara hiyo ni moja ya ajenda za kampeni ya mikoa ya Kanda yetu…..unajua kabla ya kubuniwa kwa barabara hiyo na hadi sasa wananchi wengi wanataka kusafiri kwenda mikoa ya Kanda ya Kaskazini au hata Dar es Salaam wanapitia nchi jirani ya Kenya,” alisema. Aliongeza: “Na safari hiyo ya kupita nchi jirani inakuwa na gharama kubwa lakini pia ni mbali na inachosha, hivyo kujengwa kwa barabara hiyo kungewapunguzia adha hiyo wananchi wetu na hilo tulipanga kuliweka wazi katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.”
Hata hivyo, kauli hizo za Waziri Mwangunga zinapingana na ripoti ya utafiti uliofanywa na jopo la wataalamu watatu waliobobea katika masuala ya uhifadhi na mazingira unaoonyesha kuwa barabara hiyo italeta madhara makubwa kwa Hifadhi ya Serengeti na misafara ya wanyama. Ripoti hiyo yenye kursa zaidi ya 30 imeandaliwa na aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Hifadhi za Taifa (TANAPA) Gerald Bigurube, Profesa Anthony Sinclair wa Chuo Kikuu cha British-Columbia cha Canada na Marcus Bonner wa Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS).
Ripoti hiyo ambayo Raia Mwema imefanikiwa kuona nakala yake tayari imetumwa kwa Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mwangunga ikiainisha athari kadhaa ambazo zitatokea endapo barabara hiyo itajengwa. Miongoni mwa madhara makubwa yaliyoainishwa ni pamoja na kuingilia mapito ya misafara ya wanyama hasa nyumbu kutoka Hifadhi ya Serengeti na Maasai Mara nchini Kenya.
Uhamaji wa nyumbu wanaokadiriwa kufikia milioni mbili kutoka katika hifadhi moja kwenda nyinigine mwaka jana iliingizwa katika kundi la maajabu saba ya dunia na tukio hilo limewavuta watalii wengi kutoka sehemu mbalimbali za dunia pamoja na vyombo vya habari vya kimataifa. Wataalamu hao wanasema kuwa barabara hiyo ambayo inatarajiwa kuwa na magari mengi kutokana na shughuli za kiuchumi kati ya mikoa ya Kanda ya Ziwa na ile ya Kanda ya Kaskazini itayaweka rehani maisha ya viumbe adimu wanaopatikana katika Hifadhi ya Serengeti.