Na Jenerali Ulimwengu
MAMBO tunayoyashuhudia siku hizi katika kile kinachoitwa ‘kura za maoni’ yananikumbusha lugha niliyojifunza wilayani Nachingwea miaka arobaini iliyopita. Nikiwa kijana wa miaka 20, nilipelekwa wilayani humo kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa katika kambo iliyojulikana kama ‘Farm Seventeen’ ambako shughuli kubwa ilikuwa ni kilimo, ingawaje lengo kuu lilikuwa ni kuwazoeza vijana masiha ya kambini wakiandaliwa kwenda katika kambi nyingine mahsusi kwa ajili ya mafunzo ya kijeshi.
Safari ya Nachingwea na maisha ya kambini vilikuwa ni sehemu muhimu katika kujifunza juu ya Tanzania na watu wake. Kwanza safari yenyewe ilichukua siku mbili hadi tatu, kutoka Dar es Salaam, kupitia Iringa, Njombe, Songea, Tunduru, Masasi hadi Nachingwea… safari ndefu kuliko yo yote niliyokuwa nimewahi kufanya. Ulikuwa ni wakati wa kushangaa kuhusu ukubwa wa nchi hii, uzuri wa mandhari mbali mbali, tofauti baina ya watu tuliokutana nao, na utajiri mkubwa wa tamaduni tulizogusana nazo.
Jambo moja nalikumbuka vyema hadi leo, nalo ni kuhusu tofauti katika lugha ya Kiswahili niliyoikuta Nachingwea. Niligundua mapema kabisa kwamba vijana wa Kimwera waliokuwa kambini pamoja na sisi (waliojiunga na JKT kwa hiari, tofauti na sisi tuliojiunga kwa mujibu wa sheria) walikuwa wanazungumza Kiswahili chao wenyewe, tofauti na kile nilichokizoea. Baada ya muda mfupi nilikipenda Kiswahili chao.
Kwa mfano, kijana wa Kimwera akitaka kusema kwamba anataka kuvua nguo, atasema anataka ‘kuchojoa’ na mifano mingine mingi ya Kiswahili wanachoelewa wamwera wenyewe, na labda majirani zao Wamakonde. Bila shaka hizi ni zile tofauti zinazoipamba lugha yetu kutokana na lugha za asili ambazo mara nyingi hatuzipi umuhimu. Nilijikuta nikivutia na ‘msikiko’ wa neno ‘kuchojoa’ kuliko ‘kuvua’ ambalo, isitoshe, linaweza kuhusishwa na shughuli za wavuvi wa samaki.
Lakini miongoni mwa maneno ya Kimwera niliyojifunza wakati ule (mengine nimeyasahau) moja limejenga makazi ya kudumu katika kumbukumbu yangu, nalo ni neno ‘kunyata.’ Mmwera akisema ‘Ntu yule kunyata’ ana maana kwamba huyo mtu anayemzungumzia ana sura mbaya mno.
Leo hii ninapoona vitendo vya wanasiasa waliojitumbukiza katika michakato ya kisiasa, nakumbuka ndugu zangu wa Nachingwea na ‘kunyata.’ Nadhani maana halisi ya ‘kunyata’ ni haya tunayoyaona yanafanywa na wanasiasa uchwara, matendo ya aibu tupu yanayofanywa na watu wazima bila kuona haya. Kunyata!
Kuna wakati tuliambiwa kwamba Rais wa Jamuhuri alitia saini sheria inayokataza vitendo vya ununuzi na uuzaji wa kura katika chaguzi zetu. Tunajua sote kwamba Rais wa Jamuhuri ndiye pia mwenyekiti wa chama-tawala. Swali la kujiuliza ni, je Rais wa Jamuhuri ametia saini sheria hiyo, na wafuasi wake wanajua hivyo, lakini wameamua kumdharau na kuendelea na biashara zao kama kawaida? Kunyata!
Tumeshuhudia (au tumesoma kuhusu) wagombea watarajiwa wakihaha kila pembe, wakisafirisha unga, mchele, mafuta ya kupikia, kanga, vitenge na kadhalika kuwapelekea wapiga kura, huku wakijua kwamba mambo hayo yamekatazwa. Inaelekea, kama sikio la kufa, watu hawa hawasikii dawa.
Kama mkuu wa chama na mkuu wa nchi amekemea vitendo hivi, na kama mkuu wa nchi ndiye mwenye maamuzi ya mwisho katika mambo mengi yanayohusu siasa na utawala katika nchi hii, hao wanaofanya madudu yao tuwaeleje? Ni kwamba haweajamwelewa mkuu wao huyo, au wamemwelewa lakini hawachelei lo lote kutoka kwake kwa sababu wanajua “hana ubavu” wa kuwatia adabu?
Kama ni hili la pili labda kuna mantiki, ambayo tunaweza kuichunguza hapa. TAKUKURU wamejaribu kuonyesha kwamba wanayo meno na kwamba sasa wataanza kuuma. Tumeona waliyoyafanya, na inaelekea wanayo meno mawili au matatu kinywa kizima, na nyama wanayong’ata wanashindwa kuitafuna na kuimeza; hivyo watabaki na njaa ingawa katikati ya meno watakuwa na mapande makubwa ya nyama.
Hii ni kwa sababu wanafanya kazi ambayo si yao, ingawa ni rahisi kufikiri kwamba wametumwa waifanye. Aliyewatuma naye kakosea. Kazi ya kusafisha uoza katika chama cha siasa ni ya chama chenyewe, si kazi ya polisi. Kuwaita polisi wafanye kazi ya kukusafishia chama chako ni ishara kwamba chama chako kimekushinda. Nitaeleza.
hii safi sana, CCM imejaa ma-kunyata