Na RM – Arusha, Tanzania
Vijana bwana! Sijui wakoje siku hizi. Wakati sisi tulikuwa tayari kukubali tunayoambiwa, tuliwaamini watu, vijana wa siku hizi wanataka kuhoji kila kitu. Wanataka kupima na kujiamulia wenyewe. Hebu angalia pepe hilo hapo chini:
* * *
Mwishiwa Makengeza,
Shikamoo! Na baada ya kushika miguu yako bila sababu (hivi kweli hatuwezi kupata salamu nyingine ya heshima?) naomba nitoe dukuduku langu kwako kama kijana wa nchi yetu. Sisi vijana ndio walio wengi katika nchi hii, tena walio wengi sana, lakini inavyoonekana, watu wanataka tushike miguu yao tu, badala ya kuelewa na kutenda kwa faida ya nchi. Kwa kuwa wametuona tumeinama tu wanatudharau, na tukiasi kuinama wanatuita wahuni wasio na heshima blaa blaa blaa hadi balaa.
Ngoja nijieleze kidogo. Kwanza nakuandikia wewe kwa sababu naamini unataka mabadiliko chanya kwa ajili ya taifa letu. Si kwa sababu ya chama hiki au kile, bali uchaguzi huu unatoa fursa nzuri kuachana na miaka hii mitano ya kashfa baada ya kashfa. Unatoa fursa kwa ajili ya kupeleka kizazi kipya (si kiumri, kimtazamo) Bungeni ili, wawe wa chama hiki au kile, waweze kuweka misimamo na sera bora zaidi.
Lakini ili kufanya hivyo, tunahitaji kuwasikia wagombea mbalimbali wakibadilishana mawazo, wakipeana changamoto, kukosoana na kurekebishana, sio tu kutamba jukwaani, bali kukutana pamoja ili tuweze kupima nani anasema ukweli zaidi, nani ana sera zaidi, nani amefikiria kwa kina zaidi kwa ajili kututoa katika lindi la kukata tamaa linalowameza vijana wengi.
Ndiyo. Huwezi kumpima mtu jukwaani maana anatamba peke yake na wapambe wanampamba akitamba (na kumjaza pamba masikioni). Tunataka kumsikia akikabiliwa na changamoto kutoka kwa mwingine, asiyekubaliana na mtazamo wake, au sera zake, au takwimu zake. Kwa kiasi fulani kazi hii inaweza kufanywa na vyombo vya habari lakini mpaka sasa sijaona uchambuzi wowote wa sera za vyama mbalimbali, tofauti zao, na kadhalika. Sijawaona wakihoji au kuchambua takwimu zinazotolewa na upande wowote.
Lakini zaidi ya yote tunataka kupima na kuamua mwenyewe kwa kuwasikiliza laivu. Hapa hakuna mpambe wala pamba bali mapambano ya hoja na sera badala ya sura. Ndiyo maana vijana tunasema:
Kwa maana kwamba asiyekubali kushiriki mdahalo ili kutuwezesha kupima na kuamua tumchague nani kwa faida ya taifa hawezi kupata kura zetu. Na tunasisitiza mdahalo utangazwe na wagombea wote wakaribishwe kushiriki. Asiyekubali atawakilishwa na kiti kitupu na wengine watapewa nafasi ya kujieleza bila upinzani kutoka kwa yule au wale waliokataa kushiriki. Kwa njia hii, tunaamini kwamba wote watakubali kushiriki kwa faida yetu. Maana tunaamini kabisa kwamba asiyekubali kushiriki ni mwoga, hajiamini. Tuliona hata mfano wa Uingereza juzi. Waziri Mkuu alidengua, alidengua, lakini mwisho ilibidi akubali na Waingereza walifaidi sana. Karibu nchi nzima waliangalia na kuweza kupima na kuamua. Kama hawa wakoloni waliotutesa waliweza kufanya hivyo, kwa nini sisi tuliomtoa mkoloni yuleyule hatuwezi kufanya vile? Nilisoma katika facebook (njia yetu sisi vijana kuwasiliana ndiyo maana tunawashukuru wagombea wenye kurasa zao humu… ingawa wanatakiwa kujibu maswali yetu pia!), jamaa mmoja akapinga kuwepo kwa mdahalo eti kisa rais ni mtawala wetu hivyo hawezi kuongea na sisi watawaliwa, ni kinyume cha itifaki. Ha ha ha ha ha! Sasa kama mtawala haongei na sisi watawaliwa ataongea na nani? Wafadhili na mafedhuli? Ama kweli watu wengine wanachekesha.
Na hatuongelei upande wa urais tu. Siku hizi maredio ya FM yametapakaa kila mahali. Basi wagombea ubunge wa jimbo fulani na hata wagombea wa udiwani wafanye midahalo yao tuweze kupima na kuamua. Tunasema tena, mihotuba kibao, na ahadi dafrao hazitusaidii kuamua hata kidogo. Tunataka, kila mmoja aonyeshe umahiri wa sera zake kwa kukabiliana na wenzake. Na mwenye sura badala ya sera, atokomee huko. Hatumtaki.
Kwenye ngazi zote!
Haya. Nije kwa wengine ambao pia wanataka tushike miguu ya watu (na ni wazi ukishika miguu ya mtu, lazima upige magoti mbele yake!) ni hao ambao wanadai wanataka kuendesha elimu ya uraia kwa wapiga kura. Nasikia mashirika mbalimbali, yakiwemo ya vijana wamepewa pesa kibao kujua kutuhubiria umuhimu wa kura zetu, tupige kura badala ya kuiuza, na maneno mengine yasiyo na mwisho. Kwani, hatuyajui yote hayo? Ni sawa na kutuambia UKIMWI unaua na tubadili tabia. Tunajua na watu wanapewa nafasi ya kutafuna pesa kama wehu kwa kuja kututambia kwa kutuambia sifuri. Bora hata wangetuambia ufisadi unaua, mafisadi wabadili tabia, na kutupa nafasi ya kutafakari jinsi ya kuwakomesha mafisi wa ufisadi kabla hawajatutafuna wazimawazima.
Ndiyo, Makengeza. Sisi vijana tulifikiri elimu ya wapiga kura maana yake ni kutuwezesha sisi wapiga kura kukutana na kutoa mawazo yetu na kuandaa hoja za kumkabili kila mgombea si kukaa na kusikiliza hubiri zilezile kutokana na mamluki waliopewa pesa kwa ajili ya hubiri hizo. Bora wangekuja kutuhubiri kwa kujitolea ha ha lakini lini hayo yatatokea? Hivi lini watu, wakiwemo wafadhili na mafedhuli, watajifunza kwamba hatusikilizi mihotuba ya walio nacho. Sisi tunatenda kutokana na kupewa nafasi ya kushiriki kikamilifu sisi wenyewe.
Kwa hiyo sisi vijana tunasema tunataka kushiriki kwa vitendo si masikio tu. Tunasema watu wasipoteze muda kutuhonga. Tumedhamiria na tutahongwa na mipango mizuri kwa vijana inayotekelezeka, si fedha, si ahadi ya fedha kama mabilioni ya huyu au yule. Tutahongwa na sera si sura. Na kama vijana tutasimama imara kuhakikisha kwamba katika kila kituo cha kupiga kura, kila kata, na kila jimbo mafisadi hawatapewa nafasi ya kuharibu uchaguzi kwa kujaza kura feki, au kununua kura au mbinu zozote chafu. Na kama sote tumedhamiria hivyo, na tunatekeleza, tunao uhakika kwamba wenye nia mbaya ya uchaguzi, wanaoamini kwamba sisi tutakumbatia magoti ya watu ili mradi pesa tu, watakuja kujuta kwa nini walimwaga pesa zao zote bila mafanikio. Ufisadi na wizi unawezekana kama tunauruhusu kwa kutofanya lolote.
Narudia kusema Makengeza. Laiti vijana tungekuwa na chama chetu … lakini kwa kuwa hatuna, tutakuwa makini kusikiliza sera za kila chama, kila mgombea ili tuweze kumchagua yule ambaye kweli ataleta mabadiliko mazuri katika maisha yetu. Au vipi?
Kijana asiyeinama bali anasimama imara.
Jamani wasikia hayo. Vijana hawana utani mwaka huu. Asiyesikiliza asije akajuta baadaye.
* * *
Ujumbe kutoka kwa mhariri:
Najua kuna baadhi ambao hawawezi kufungua tovuti kama hizi wakiwa ofisini n.k.; kwahiyo unaweza ukawatumia ujumbe huu [bofya] kwa njia ya barua pepe. Pia, Vijana wengine mnaotaka kuwaamsha wenzenu, huu ni ukumbi wenu. Kwahiyo msisite kututumia makala. Timu ya Vijana FM itawasaidia kuhariri na mambo mengine ya kiufundi.
What a great read to start my week. Thanks RM for writing this. Ngoja niirudie kabla sijaongeza maoni.
Vijana wote wenye akili timamu na upeo wa kuchambua taarifa na habari wakajua punje zipi, pumba zipi, wanapaswa wasome ujumbe huu na akili iwagonge. How truthful do you want the truth to be? This is as true as true itself is.
I loved reading this. Shabash!
Asante sana ndugu mwandishi kwa kuamsha mawazo ya wale wengi wanaosinzia!
Ukiangalia au ukasoma kwa juu juu tu halafu ukazima tarakilishi yako na kwenda kulala, hii kampeni haitafanikiwa. Tujaribu kuwasilisha huu ujumbe kwa watu wote! Ni kitu kidogo tu, lakini watu wakijipanga vizuri na kuweka msukumo wenye hoja za maana (kama alizotoa mwandishi hapo juu), ni matumaini yangu kuwa ujumbe utafika na mdahalo utafanyika tu; hata kama JK asipokuja.
Mhusika (JK) akisema hatatokea, sawa. Maswali yaendelee kama kawaida. Ikifika zamu yake, maswali yaendelee kuulizwa… Kama atapewa dakika tano kujieleza, basi kwenye wakati huo watu wanyamaze au muda huo utumiwe kwa matangazo.
Suala lingine, mbona vyombo vya habari vimesinzia kwenye hili suala; ninachoona kila siku ni taarifa za vijembe tu. Yaani wameshindwa kuandika makala za maana zinazoweza kuamsha watu? Wanashindwa hata kulinganisha sera za wagombea?? Kila siku ninaona KERO TU: Picha za wahusika kwenye magazeti, blogs na tovuti “wakitangaza nia.” Sera ziko wapi??
Kwahiyo, waandishi wa habari wavivu, na nyie amkeni! Tumechoka…
Wonderful message! I loved this:
Ni kweli nakubaliana kabisa na mwandishi wa makala hii. Nchi yetu ina vijana wengi sana ila bahati mbaya wengi ndio hao walishajikatia tamaa na wengine wapo ila wanajua kabisa walitakiwa wafanye nini, ila kwa sababu ya mfumo wenyewe kutojali vijana husika “labda uwe mtoto wa kigogo kama tunavyoona wote wanapewa kazi ikulu na sehemu mbalimbali nyeti serikalini” basi wanaona ni kama kazi bure.
Vijana tukiamua kweli linawezekana na tunaweza fanya mabadiliko makubwa sana katika nchi yetu ambayo hayajawahi tokea.
(Niliwahi kuandika hivi: Soma hapa )
Kweli tumechoka kusikia kila siku bila vitendo .Tuungane vijana kokote tuliko na kwa kutambua wajibu wetu tufanye mabadiliko, si kazi kubwa kama tukielewa maana pa kuwabana hao ni kuwanyima tu kura zetu.
Tatizo watu wana njaa na kudanganyika na vijizawadi vya muda mfupi. Kama unaweza fikiri juu ya maisha yako au jirani yako miaka 10 ijayo, hutokubali kufanywa kichwa cha mwendawazimu.
mwandishi naona umeangalia mambo mengi kwa kina. sasa kikubwa ni kuweka hilo azimio liwe azimio letu vijana kwa umoja, tuache kutoa maoni tu – tuchukue taswira mpya ya utendaji kwa kina jamani na tuanze kwa hili…sasa liwe azimio letu na tuweke nira mbele na dhamira ya utaifa na wala si ya uchama.
Bado nina ndoto, ipo siku wanangu watatu watathaminiwa katika nchi yao si kwa sababu ya jina au nyadhifa ya baba yao, si kwa aina ya elimu waliyopata, si kwa kiwango cha fedha na PENZI walilohonga bali kwa uwezo wao wa kufikiri kuibua hoja na moyo wa kizalendo. asilimia sitini ya binadamu waliokosa nguvu ya kusema na kuthubutu sasa imeamka. hongera RM, TUPO PAMOJA MAPAMBANONI.
Hakika nimefurahi sana kaka. Umesema mambo makubwa, ambayo kwa kweli, ni funzo kubwa kwetu sisi vijana. Tumechoka kwa kweli, Hivi ni nani wa kusimama, kutokomeza udhalimu, mikwara, ubabe, dharau, matusi ya wazi kwa Baba, Mama, watoto, na ndugu zetu, kama si sisi vijana?
Vijana si ndo nguvu kazi ya Taifa? Si ndo wajibu wetu?
Ukishindwa fanya wajibu waka ilhali una nguvu, akili si afadhali ukafe maana si msaada kwetu, na taifa lako? Tunahaja gani ya kuwatesa watu ambao hawana hatia kwasababu tunataka utajiri wa kijinga ambao, huwezi kuwa na furaha maishani.
Kura yako italeta mageuzi mwaka huu kijana. AMKA.