Nkaba nyin’embwa yange

Na Jenerali Ulimwengu

WIKI jana nilijadili suala la watu wazito, wenye nyadhifa kubwa, wenye historia zinazoeleweka, na wenye wingi wa miaka inayowatambulisha kama wazee, lakini hujidharaulisha kwa kutoa matamko ya kipuuzi yasiyofanana na sifa hizo alimradi wajibu hoja za kudumu kwa majibu mepesi ya mpito. Wiki jana ilikuwa ni ya Pius Msekwa, Makamu wa Mwenyekiti wa CCM na matamko yake kuhusu uoza ndani ya chama chake.

Wiki hii tena, mzee mwingine wa CCM, Katibu wa Uenezi, John Chiligati, naye ameamua kujiingiza katika kundi hilo la kujisemea ‘bora liende”.

Chiligati, yeye, ameamua kumzungumzia kijana wa CCM, Hussein Bashe, ambaye hivi majuzi tu, mjini Dodoma, amekatizwa safari yake ya kuwania ubunge kutokana na kile kilichoelezwa kuwa tatizo la uraia.

Chiligati aliwaelezea waandishi wa habari mjini Dodoma alfajiri ya Jumapili kwamba Bashe ameachwa katika mchujo wa wagombea kwa sababu yeye ni raia wa Somalia, na kwa hiyo si raia wa Tanzania. Aliongeza kusema kwamba chama chake kilifanya uchunguzi kikishirikiana na Idara ya Uhamiaji na ndipo ikagundulika kwamba Bashe si raia wa Tanzania, hata kama alizaliwa Tanzania.

Hadi hapo sioni tatizo. Tatizo linakuja pale Chiligati alipotamka kwamba kesi ya Bashe ni sawa na ile ya mwandishi wa makala hii , “aliyekuwa kada wa CCM” na akavuliwa uraia wake katika miaka ya nyuma.

Nakiri kungali na mapema kwamba haipendezi kwa mwandishi wa makala hii kutumia safu hii kuzungumzia suala linalomhusu binafsi. Nasema haipendezi, lakini ni halali katika hali fulani fulani. Nitajaribu kueleza hapa chini.

Wahaya husema kwamba mtu akibanwa mbavu kuhusu jambo alilotenda na akataka kusema uongo atasema, nkaba nyin’embwa yange. Nilikuwa pamoja na mbwa wangu. Maana yake ni kwamba, kama mnataka ushahidi wa hili ninalosema muulizeni mbwa wangu.

Kwa mitindo mbali mbali na katika mazingira tofauti hii ni silaha inayotumiwa na watu wanaotaka kusema uongo unaofanana na ukweli. Kwa mfano, inawezekana kweli Bwana Bigambo alikuwa na mbwa wake wakati wa tukio husika, lakini haiwezekani kwa mbwa wake kutoa ushahidi, kwa hiyo kuwapo au kutokuwapo kwa mbwa huyo hakuna uhusiano na ushahidi wa Bigambo. Anapoteza lengo tu, na ingawa kwa juu juu anasema ukweli (mbwa wake alikuwapo) lakini anasema uongo (mbwa hawezi kutoa ushahidi).

Ili kuwafariji akina Chiligati, ninaweza kuwaarifu kwamba hawako peke yao, kwani hata wakubwa wa dunia wanatumia vijisilaha kama hivyo wanapokuwa wameshikwa ‘pabaya.’ Miaka kadhaa iliyopita, wakati Marekani wanang’ang’ana kwenda Iraq kumwondoa Saddam Hussein, Marekani walipambana na upinzani mkali mno kutoka kwa maswahiba wao wa Magharibi waliokataa kubariki vita ya Marekani dhidi ya Iraq. Tunamkumbuka Dominique de Vilpein, waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa na jinsi walivyoshikana mashati (kwa maneno) ndani ya mkutano wa Baraza la Usalama.

Katika mabishano makali yaliyofanyika katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kila aina ya mbinu zilitumika kutetea upande huu na ule, kila mmoja akivutia upande wake. Ilikuwa dhahiri kwamba dunia haikukubaliana na mantiki ya Marekani kuivamia Iraq, na kwamba Marekani walikuwa wamedhamiria kufanya kile walichoazimia na kwamba wangetumia maguvu, hata kama Umoja wa Mataifa ungewakataza.

Lakini, kwangu mimi binafsi, tamko lililoashiria kuchoka kwa uchovu na ubabaishaji wa mantiki ya Marekani ni pale ofisa wake mwandamizi alipoiingiza Tanzania katika ubishi huo, kwa kutamka kwamba hata Tanzania ilipoivamia Uganda haikufanya hivyo kwa kibali cha Umoja wa Mataifa. Ati nkaba nyin’embwa yange.

Huyu msemaji wa Marekani alifanya purukushani (hii ndiyo maana halisi ya neno hili) kuhusu chanzo cha vita baina ya Tanzania na Idd Amin, yaani uvamizi alioufanya Amin dhidi ya Tanzania, na kwamba ilichofanya Tanzania ilikuwa ni kutumia haki yake ya msingi ya kujibu mapigo katika ulinzi wa ardhi yake. Msemaji wa Marekani alisema ukweli (Tanzania haikupata ridhaa ya Umoja wa Mataifa) wakati papo hapo akisema uongo (Iraq haikuivamia Marekani).

Mantiki ya nkaba niny’embwa yange huweza kupata mashiko miongoni mwa wasemaji na wasikilizaji waliojijengea utamaduni wa fikra nyepesi zinazotafsirika katika matamko mepesi sawia. Katika jamii iliyojizoeza kufanya mambo yake (pamoja na kufikiri) fasta-fasta, muhimili mmoja wa mtazamo wa maisha ni kwamba hutakiwi kuumiza kichwa chako kufikiri. Unachotakiwa ni kuwa mjanja ili uweze kubakia bambucha.

Hebu tuangalie Chiligati anasema nini kuhusu kijana Bashe na mwandishi wa safu hii. Kijana huyu alikuwa, hadi juzi (sijui leo) kada wa chama-tawala, tena kada wa mstari wa mbele ambaye amekifanyia kazi chama hicho hadi juzi. Mwandishi huyu wakati akivuliwa uraia hakuwa tena kada wa chama hicho, akiwa amehitilafiana na uongozi/utawala wa juu wa chama hicho kuhusu masuala ya msingi.

Kijana Hussein Bashe, ambaye sasa anatolewa kafara na wale alioamini ni wazee wake, alikuwa bado anayo hamu ya kukitumikia chama chake katika wadhifa wa juu zaidi. Mwandishi huyu alikuwa amestaafu ubunge na ujumbe wa NEC na alikuwa amejikita katika harakati za asasi za utetezi pamoja na uandishi na uchapishaji wa magazeti makini ambayo hayakusita kuiambia serikali na chama-tawala kwamba “mfalme yu uchi, na korodani zinaonekana.”

Endelea kusoma hapa…

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 2 Comments

2
  1. Mzee wa Changamoto, kwenye mambo ya siasa nadhani huyu ndio role model wangu! Nilikuwa nafuatilia sana makala zake enzi zile kwenye gazeti ya Rai, na kipindi chake kile DTV… Nikamsahau kidogo, lakini baada ya kuzipata makala zake kwenye gazeti la Raia Mwema, mambo yamerudi kuwa mazuri sana!

    Anaijua historia ya Tanzania, anawafahamu vigogo na mengi yamemkuta wakati yuko CCM (na baada ya kumaliza shughuli zake CCM). Inatia moyo sana unapoona kuna “kiongozi” anayethubutu kusema mambo kama anavyoyaona.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend