“Mwendo ni kula raha – 2″

Kama kumbukumbu yako sio nzuri sana, itakuwa vizuri ukisoma sehemu ya kwanza ya hadithi kwanza…

Nahesabu haraka-haraka watu waliopo mezani ni kama sita hivi. Namuona Jimmy, Dullah, Issa, Kingo, Neema na binti mwingine ambaye nadhani ni rafiki yake. Tunafika mezani na kuwasalimia, “Vipi mambo?”

Karibia kundi zima linajibu kwa mpigo, “Poa!”

Deo anatoa salamu nyingine, “Kina dada mliopendeza, vipi mambo? Mbona meza tupu?”

Neema na rafiki yake wanatabasamu tu, ila Dullah huwa haishiwi na maneno akikutana na Deo, “Hebu kaa chini kwanza, Deo! Mbona mmechelewa? Si tusha’oda mbuzi katoliki na pawa nyagi. Vinywaji vinakuja sasa hivi!”

Deo anamjibu, “Ah! Huyu mzee wa busara Magirini nd’o kanichelewesha. Safari nzima ananipa nasaha kama dingi yake. Mara endesha gari taratibu, Deo. Tunakaribia kufika, anaanza kuniambia zile hadithi za mazimwi za Deborah Mwenda!”

Wakati watu wote wakinicheka, nawaambia, “Jamani! Deo si ulikuwa unaniambia unapenda ile hadithi ya Binti Chura? Au sio wewe? Kuanzia leo jina lako la utani litakuwa Binti Chura.” Kauli yangu ya mwisho inasababisha vicheko zaidi, na tunapata fursa ya kuchukua viti vilivyopo kwenye meza tupu ya jirani na kuketi. Dullah yuko upande wangu wa kuume na Deo yuko upande wa kushoto. Naangalia nyuso za vijana wenzangu; sura zao zimejawa na furaha, utani na vicheko vimetawala na wanajihisi kama wako kwenye dunia nyingine.

Mhudumu analeta vinywaji mezani, anaweka chupa nne za konyagi katikati ya meza, glasi nane, fanta moja, chupa za coca-cola mbili na club soda kama nne hivi. Baada ya mhudumu kuondoka, Deo anauliza, “Nani kaagiza fanta? Mizengwe tu, inaleta nzi na nyuki mezani!”

Dullah anadakia, “Mimi nilifika wa kwanza hapa na nd’o nikaagiza kila kitu. Deo, hiyo fanta ni ya kwako mzee. Binti Chura huwezi mambo ya wakubwa. Tuache sisi tunywe mpaka mzee nyagi ashushe mikono!”

Issa anamuunga mkono Dullah, “Tuache utani jamani. Binti Chura… Samahani. Deo, ujue wewe ndio mwenye usukani leo, kwahiyo huruhusiwi kupata kilaji kama unavyojua. Masela walitaka kukununulia coca sijui, mi’ nikawaambia hata hiyo itakulewesha kichwa panzi. Nd’o tukaamua kununua fanta kwa ajili yako Binti Chura!”

Kwa jinsi Deo anavyopenda kutania watu, ni ahueni kumona yeye akitaniwa. Uzuri wake ni kwamba hana hasira. Baada ya vicheko kutulia na watu kuanza kunywa, anatuambia, “Kweli leo mmeniamulia. Kiti moto kikiletwa hapa ninajua watu wangu wa kuwatania.” Sote tunajua anawaongelea Dullah na Issa, ambao wote wanacheka kwa sauti tu. Deo anaendelea, “Yule mnyama, kama sikosei, anaitwa nguruwe. Lakini watu wamembatiza majina ya ajabu-ajabu.”

Dullah anamjibu, “Nguruwe ndio nini tena? Mi’ sijawahi kumsikia!”

Issa naye, “Aaaah, nadhani anaongelea mbuzi kibonge tuliyeagiza. Tena huyoooo analetwa! Deo… Samahani, Binti Chura. Yule mnyama anaitwa mbuzi katoliki!”

Mimi huwa muongeaji sana, ila muda kama huu nadhani huwa nafaidi zaidi kukaa pembeni na kuwasikiliza kina Deo, Dullah na Issa wakitupiana vijembe. Ni burudani tosha kusema ukweli; huwa wananikumbusha ile michezo ya kuigiza ya kina Majuto, Mzee Small na Mwanachia.

Kelele zinapungua baada ya kiti moto kuletwa mezani. Napata fursa nyingine ya kuwaangalia watu wote walio mezani. Taratibu naangalia mtu mmoja-mmoja kwa kuanzia upande wa kulia Dullah alipokaa, Kingo, Issa, Jimmy, rafiki yake Neema; naongeza mwendo na kumruka Neema na nakutana na uso kwa uso na Deo, ambaye anatabasamu. Nadhani nimetegua bomu!

Deo anapayuka, “My bway Maaaagzzz! Magirini, mbona umekuwa kimya sana leo?”

Nadhani mimi na Deo tu ndio tunaojua kinachoendelea. Namjibu, “Mshika mawili moja humponyoka. Acha nifaidi msosi.” Deo anaashiria kuwa ameona jinsi ninavyomkwepa Neema na kuendelea kula.

Tunamaliza kula na kuendelea kunywa taratibu huku watu wakiendelea kutaniana, pombe ikisaidia watu zaidi kujiunga kwenye vita ya kutupiana vijembe. Labda kutokana na kutoruhusiwa kunywa pombe, Deo pekee ndiye anaonekana ameboreka, “Jamani, muda umefika. Malizieni kunywa tuzuke kiwanja. Leo patafurika kinoma.”

Jimmy anasema, “Kama Bills pamejaa, tuzuke The Place uwanja wa nyumbani.”

Karibia wote tunampinga kutokana na sababu zetu tofauti, ila Dullah anaamua kutuambia sababu yake, “The Place ina masista duu. Kuna siku nilienda pale, sasa DJ akacheza ule mpini “Sonia” wa Sir Nature, mi’ nikajitoa muhanga kwenda kumuomba dada mmoja mkali kucheza naye. Unajua alichoniambia? ‘Eti wimbo huu hauchezeki.’ Tokea siku ile nikasema sikanyagi tena pale! Ile kitu classic hata viziwi wanaucheza baba’ake!”

Leo nadhani nimecheka sana, lakini kituko cha mwisho cha Dullah kinaniumiza mbavu zangu, “Dullah, unajua wewe ni msanii. Basi tu Bongo michosho. Ungekuwa nchi za watu, nina uhakika ungekuwa mwandishi wa vipindi vya vichekesho. Mzee una matani balaa.”

Deo ananijibu, “Aaah, wapi! Huyu? Dullah anapenda kuku wa kienyeji ndio maana hapapendi The Place. Hicho alichokwambia ni kisa cha kweli lakini.” Ananyanyuka na kutuambia, “Haya jamani tulipe tuondoke hapa. Usiku umeshakuwa mnene.”

*      *      *

Kama tulivyotegemea, Club Billicanas pamefurika. Bahati nzuri foleni sio ndefu sana, kwahiyo tunafanikiwa kuingia baada ya muda mfupi tu. Ndani tunakuta vijana, wengi wao nina uhakika wamemaliza mitihani yao ya kidato cha nne. Mwendo ni kula raha tu kama nilivyotegemea. Tunajaribu kutafuta sehemu ambayo watu wote nane tunaweza kukaa pamoja lakini juhudi zetu zinagonga mwamba na hatuna budi kutawanyika.

Dullah, Issa  na Deo wanaamua kwenda kucheza pool. Nawakumbusha, “Hakikisheni Deo hanywi. Sana sana mwachieni labda coca moja tu!”

Deo anaonekana hajafurahishwa, “Jamani, yaani siku kama ya leo mnataka nisipate hata matone mawili matatu ya mkojo wa mende? Acheni hizo masela.” Anatuangalia lakini hatusemi lolote. “Poa tu. Twen’ zetu tukacheze pool.”

Waliobakia wanaonekana bado hawajui pa kwenda, hivyo nawaacha, napanda ngazi na kwenda juu kuona nini kinaendelea. Ukiwa juu unaona vitu vingi; ukumbi umejaa,  sehemu ya kucheza muziki imejaa pomoni, kuna watu wanaocheza juu ya spika kubwa na wengine wamekaa kwenye viti na kulonga. Najisikia vizuri tu, ila nadhani chupa tatu hivi za bia zitafanya siku hii iwe nzuri zaidi na kuniondolea soni.

Muziki umekolea na najisikia mwepesi baada ya kuongezea kinywaji! Naamua kushuka chini kuwakusanya marafiki zangu niliokuja nao (pamoja na Neema na rafiki yake) na kuelekea sehemu ya kucheza muziki. Baada ya kucheza nyimbo kama tano hivi mfululizo, DJ anacheza wimbo “Wife” wa Daz Baba. Wenzangu wanaamua kuondoka, Deo ananinong’oneza, “Nyimbo kama hizi kucheza na masela sio ishu wala nini. Wewe baki hapa na Neema. Zali!”

Mimi naupenda sana huu wimbo na nilikuwa napanga kubaki kucheza, ila ishu ya kubaki mwenyewe kucheza na Neema au rafiki yake haiingii akilini. Kwahiyo naamua kuondoka. Deo na Dullah wananiona nikiwafuata na wananisukuma kunirudisha nilipotoka na kuishia mbele ya Neema, ambaye ananiambia, “Vipi, hutaki kucheza na mimi?”

Mimi kidume bwana! Nitaogopaje kucheza na demu? Namjibu, “Hapana, nilikuwa nataka kwenda kununua kinywaji kwanza.”

Anasema kitu lakini nashindwa kumsikia kutokana na kelele za muziki. Hivyo nainamisha kichwa na kutega sikio karibu na mdomo wake ili aninong’oneze, “Umekuwa unanikwepa leo. Tucheze basi…” Sauti yake nyororo ikiambatana na joto la pumzi yake inatua kwenye sikio langu la kulia. Natabasamu tu na kumsogelea ili tucheze pamoja. Neema anaweka mikono yake kwenye mabega yangu. Mimi namshika… No! Siwezi kukwambia nilipoweka mikono yangu kwasababu dingi anasomaga hadithi zangu!

Tokea nitoke nyumbani mpaka sasa hivi siku imekuwa inaenda haraka sana. Lakini burudani ninayoipata sasa hivi inafanya muda usimame; nahisi kila kitu, nasikia kila mdundo, naona uso wa Neema ukiwa na tabasamu na jasho kidogo kwenye paji la uso. Wakati wimbo unayoyoma, Neema ananishika mkono wangu wa kushoto na kunivuta karibu, kisha ananiambia, “Nasikia joto. Twende nje tukapunge upepo.”

Sehemu ya tatu na ya mwisho… wiki ijayo.

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 4 Comments

4

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend