Nimekulia Keko Juu, wilaya ya Temeke. Safari za kwenda Uwanja wa Ndani wa Taifa au ‘Fegi’ (Chang’ombe Sigara — TCC) kucheki mechi za kikapu ilikuwa desturi. Kama hakuna mechi, basi utanikuta kwenye mechi za mchangani mitaa ya Kurasini, Keko au Chang’ombe.
Wakati nipo darasa la tano, vijana ambao nilikuwa nawaona kwenye mitaa yetu, Gangstas With Matatizo (GWM), walikuwa wanatikisa na wimbo ‘Yamenikuta’ (ft. 2 Proud). Kwa hiyo, labda utaelewa kwanini naithamini sana Hip Hop.
Mwanzoni mwa miaka ya 2000… Juma Nature aliamua kuwashirikisha “GWM” na wasanii wengine, na kuunda kundi la Wachuja Nafaka. Bila shaka utakuwa unakumbuka ule wimbo ‘Mzee wa Busara’.
Baada ya albamu yao kutoka, mzee nikajipinda, nikabana hela ya matumizi shuleni na kununua kaseti ya Wachuja Nafaka. Ili tu niweze kusikiliza “malaria inapanda weeeeeeh, inapungua; inapanda weeeeeeh inapungua” muda wowote nitakaotaka!
Nadhani ile shilingi 700 niliyotumia kununua ile kaseti ilinipa zawadi ambayo sidhani kama kuna zawadi nyingine yoyote ile ambayo shilingi 700 nyingine itanipa. Kwenye wimbo ‘Ukweli na Uwazi’ kulikuwa na mistari ya msanii mpya kutoka Mwanza! Nikabaki kurudia kuusikiliza huo wimbo, hasa ubeti wa Fid Q.
Binafsi, mtu akitaja Fid Q tu, basi ile mistari yake (yenye metaphors) inayokufanya ufikirie inaanza kuchukua ukumbi kwenye fikra. Bila shaka Fid Q hatufundishi kuongoza kumfuata; bali anatufundisha kuongoza.
Wakati nyimbo na albamu yake nzito ya ‘Propaganda’ ikiwa inagombewa mitaani, tuliona hatuna budi kumtafuta na kumuuliza maswali matano.
Alianza hivi:
Kwanza kabisa ningependa kuwapongeza kwa juhudi za kimakusudi kuhakikisha ukweli unatengana na uongo for a better tomorrow!
Baada ya pongezi, ningependa kuwashukuru kwa kunipa nafasi hii ya mahojiano na nyinyi ambao ni wanajamii wenzangu; ambao kwa pamoja tukiungana, basi nina uhakika hakuna kitakachoshindikana chini ya jua.
Baada ya pongezi na shukrani zangu toka kwenye uvungu wa moyo wangu, ningependa kuyajibu maswali yenu ya msingi.
1. Umetoka wapi, uko wapi na unakwenda wapi? Uko mwenyewe kwenye hiyo safari?
Kusema ukweli, nilikotoka ni mbali sana! Tangu enzi za ku-rap ni uhuni, mpaka hii leo, miaka ambayo baadhi yetu tumepewa vyeo vya ubalozi wa jamii. Kwa sababu tu ya kuitumia sanaa hii ya muziki wa Hip Hop — kama kioo cha kuutazamia ukweli, na pia kama nyundo ya kuukazia.
Ufanisi huu wa kazi umepelekea wadau mbalimbali kutupa vipaumbele katika shughuli mbalimbali za kijamii, kama uelimishaji mashuleni juu ya suala zima la maambukizi ya virusi vya Ukimwi, jinsi ya kupiga vita malaria n.k. Yote haya yameletwa na kitu kimoja kinachoitwa nguvu ya msanii na sanaa yake.
Hakika nathubutu kutamka kwa ulimi ya kwamba, japokuwa jamii yetu iko ‘off balance’ katika nyanja mbalimbali, bado inaonesha kuwa na imani sana na wasanii wake. Na hiki ndio kitu ambacho kiliwafanya mpaka wanasiasa “kuwatumia” wasanii katika kuendesha kampeni zao kwenye kipindi cha uchaguzi. Ili kupata idadi kubwa ya wahudhuriaji watakaosikiliza sera zao; kwahiyo kumbe yule muhuni wa zamani amekuwa mheshimiwa wa sasa…
2. Mzee wa Kitaaolojia, nimesikiliza Propaganda zako kwa kina. Hivi, ulikuwa na lengo gani hasa?
Kabla ya kuandika Propaganda au kufikiria kuiita albamu jina hilo, nilikua nina mpango wa kuiita ‘Darwinz Naitmea’. Hata hivyo, huo mpango ulipotea ghafla baada ya kufanya mdahalo wa siku mbili na baadhi ya maprofesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambao mpaka tunarudi mitamboni waliniacha na maswali mazito ambayo ni:
Je, humu ndani ya hii ‘Darwinz Naitmea’, wewe kama mwanaharakati ulikuwa unataka kumlaumu Hubert Sauper kwa kukutusi au unataka kuichukulia hii documentary yake kama changamoto?
Bila shaka, wale ambao wameiona hii documentary watakubaliana nami nitakaposema: hii documentary ina mengi ndani yake. Nikimaanisha, kilichoongelewa ni zaidi ya ile kashfa ya wakazi wenzangu wa Mwanza kulishwa mapanki, pamoja na wimbi kubwa la watoto wa mitaani au hata suala la maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Naam, kuna mengi mule ndani kiasi kwamba hata kama ningechukulia ‘amenitusi’ ni sawa na mimi ku-sell out. Na ule mtazamo wa kupata changamoto ulikuwa mkubwa sana kwangu, na mara nyingi ilikuwa inanifanya niote ndoto za michoro ya joka kubwa tena lenye miguu! Sitaki kukubali kama kuna kitu nilikuwa nakihofia, isipokuwa niliona itanigharimu muda mwingi sana ili kukamilisha utafiti wangu na tayari mashabiki walikua wamesha’anza kulalamika kuhusiana na ukimya wangu.
Wazo la Propaganda likanidondokea mithili ya theluji toka mbinguni; nami nikawawashia mshumaa Wabongo wenzangu ili tuache kulilaani giza.
3. Kama mmoja wa mashabiki wako wakubwa, nimeshuhudia kipaji na uwezo wako wa kufikiri kwa kina ukikua kwa kasi ya ajabu. Ni utu uzima tu au kuna juhudi nyingine?
Nilichagua sanaa tangu nikiwa mdogo, kwasababu niliamini ubongo wangu una zawadi, ambayo nikiipiga msasa wa vitabu, [basi] itakuwa ni ya kipekee na ya kuvutia zaidi kama sitokuwa mchoyo; kiasi cha kuwagawia wenzangu wanaonisikiliza kwa kupitia mlango wa fikra mbadala.
Hapa naongelea Hip Hop! Hivyo basi: I am Hip Hop… and I do this under the name of God.
4. Chimbuko la Hip Hop lilitokana na mazingira na mazingara ya taabu, hivyo kuchochea uanaharakati. Je, unadhani Bongo Hip Hop imekuwa ikifanya hivyo? Au nyumbani imekuwa na jukumu tofauti kidogo, hasa ukizingatia na tuliyoyaona katika mchakato wa Uchaguzi?
Nasikitika kukutaarifu kwamba Bongo bado hawajajua kutofautisha kati ya “rapper” na “mwana-Hip Hop”. Na bado hawajajua kuwa: Rap + Reality = Hip Hop!
Kwa hiyo wengi wao hawaangalii kile walichokiandika kabla hawajaanza kughani. Wala hawazingatii misingi na katiba nzima ya Hip Hop; na bado wanapewa heshima kama wana-Bongo Hip Hop.
Ku-rap hata Mao Santiago wa Machozi Band ana-rap. Lakini, je, hicho ndio kitamfanya aitwe mwana-Hip Hop? Hapana!
Mi’ binafsi nimeshangazwa na mwamko wa Wabongo safari hii kwa kuielewa Propaganda mapema, kiasi cha kuiita album bora ya Mwaka 2010. Nasema nimeshangazwa kwasababu mapokezi ya Propaganda yamekuwa ni makubwa kuliko hata yale ya awali kwenye ile albamu yangu ya kwanza ‘Vina mwanzo, kati na mwisho’.
Hata hivyo, sitaki kushangaa sana kwasababu tofauti ya ‘Vina mwanzo’ na ‘Propa’ ni kama ifuatavyo: ‘Vina’ aliisuka Majani pale Bongo Records; ambamo ndani yake nilitoa hits kama ‘August 13’, ‘Chagua moja’, ‘Mwanza-Mwanza’, ‘Kadi na Ua Rose’ n.k. Na Propa niliisuka mwenyewe… kuanzia beats mpaka song titles, contents, nani wa kumshirikisha na vitu kama hivyo.
Tofauti iliyopo: Ile ya kwanza nilikua chini ya Majani. Hii ya pili nilionesha ukuaji wangu kimuziki kwa kuchangia machozi, damu, jasho na moyo wangu wote katika kuhakikisha napata kitu sahihi kabisa!
Hiyo ndio maana halisi ya kuwajibika na sanaa kama msanii. Na unapoamua kuwa MC, ni lazima uwe kama balozi ambaye amewekeza maisha yake yote kwenye Hip Hop. Vinginevyo utafanya map#&%@zeze waendelee kuamini wabana pua wanaweza kuwashika hata ya zaidi ya ma-hardcore.
5. Ule mradi wako wa utafiti wa nafasi ya Hip Hop katika jamii, hasa Afrika, unaendeleaje? Nini hasa dhamira yako?
Dhamira yangu ni kuhakikisha sanaa na muziki wa Hip Hop Tanzania kwa ujumla unatumika kuelimisha, ukiachilia mbali burudani iliyomo ndani yake. Nimekuwa nikisisitiza suala la elimu mara kwa mara kwasababu elimu ndio kitu pekee kitakachotukomboa sisi Waafrika tuishio ndani ya hizi nchi zenye umasikini wa kupindukia, ndani ya hili bara lenye giza. Nchi ambazo hata uchumi wake haupo kwa ajili ya maslahi ya watu wengi. Na mbaya zaidi, zina wasomi wachache sana, ambao nao bado wanaashiria kama [vile] walishawahi kuuogopa umande kipindi fulani.
Sababu hizo chache za msingi zilinipelekea kupata mtazamo mpya wa matumizi ya sanaa yangu na nguvu nilizonazo, kama msanii; kwa kuliamsha Taifa [sehemu] lilipo, huku nikijaribu kuliandaa Taifa lijalo kwa kupitia elimu ndani ya burudani inayoletwa na muziki wangu kwa ujumla.
Hivyo basi nilipokabidhiwa Certificate of Educational Art and Culture pale Bell Air, nilishukuru Mungu na pia niliwaahidi wadau wa State Department ya kwamba sitotamba kwa kukabidhiwa cheti nchini Marekani. Isopokuwa, nitazingatia kipi nitafanya baada ya kuwa na hiyo certificate… Mpaka sasa hivi nina projects zaidi ya tatu ambazo natarajia kuanza Machi mwaka huu, ikiwemo pamoja na kuingiza somo la ‘KitaaOLOJIA’ vyuoni!
Maneno mazito kutoka kwa Fareed Kubanda. Bila shaka nasaha zake zimevaa huu ushairi kutoka kwenye wimbo ‘Propaganda’: Tunachukiana kwasababu tunaogopana; tunaogopana kwasababu hatujajuana; hatujuani kwasababu tunatengana; dunia ni nzuri, walimwengu hawana maana.
Nasubiri nipate wajukuu ili nije kuwahadithia kuhusu albamu ya Propaganda. Ambao hamjaisikiliza mjue nyie ni tatizo ambalo litakuja kutatuka!
Timu nzima ya Vijana FM inamshukuru kwa muda wake, na tunachukua nafasi hii kumtakia kila la heri kwenye harakati zake kimuziki na kuamsha Taifa letu kwa ujumla.
Sikiliza baadhi ya nyimbo zake kwenye playlist ya Michael “Mx” Mlingwa:
Makala zinazohusiana na haya mahojiano:
Ngosha umefunguka vizuri, kama naona muvi hivi ya hiyo story. dah. ki ukweli since day nliposikia ‘huyu na yule’ hadi ‘propaganda’ hakika ni mtiririko wa ukuaji wa kifikra ambao umeuonesha — ni mkubwa mno.
najua wabongo wengi ni wavivu kukaa na kusikiliza lyrics, ndio maana nyimbo nyingi hupendwa kwa chorus zake tu. lakini naamini wakitafutwa watu watatu wanaosikiliza lyrics neno kwa neno, nami nimo. ndio maana leo angalau nawezajua nani ‘mkibaki na nani ni raila odinga’… kwa kifupi niseme: endelea kufanya kazi nzuri kwa ajili ya jamii ya wa-tz. ipo cku lengo litatimia. ni hayo tu!
Kazi nzuri mkubwa kiukweli nyimbo zako ni za kuelimisha, kufundisha, kukanya na kufurahisha jamii pia! Hongera kwa hilo pia mtegemee Mola kwa kila jambo unalo lifanya na utakalo lifanya big up man!
Hivi, mkisikiliza wimbo ‘Propaganda’ mnapata mawazo gani? Kwasababu, kama mnavyojua, wengi hawanunui kazi za wasanii, si ingekuwa fresh kama Fid Q angetoa ule wimbo kabla ya Uchaguzi Mkuu?
Aisee Fid Q and Vijana FM asanteni sana… hii ni fresh material!
Mimi ni mwandishi wa lyrics, lakini kama wanasema kula ‘marekani, mimi ni “ghost writer”. At the moment, nawasaidia rafiki zangu… wanajaribu ku-rap kama wewe sehemu fulani fulani, including hapo bongo. Sitaki kuingilia kwenye politics za Labels, Record Brands, etc, lakini napenda kuandika sana.
Je, unafikiri hii culture ya ghost writing inawezekana bongo? Nafikiri – kama unachosema na kama Vijana FM wamesema kwenye previous makalas – tunayo politics za copyright nyingi… I’m hoping nitaweza ku-submit lyrics kwa rappers, lakini at this rate, nafikiri better to stick with my boys. Au vipi?
@Anon, umeleta hoja nzuri sana hiyo ya ghost writing. Bongo nimeshawahi kusikia kuna baadhi ya majina makubwa kwenye bongo hip hop wakiwa wanaandikiwa, na hata ku-copy na ku-paste mashairi ya wengine.
Tatizo bongo kuna ukiritimba wa “aahh jamaa anaandikiwa”, hivyo msanii inakushushia credibility fulani, pamoja na kuwa, states wasanii wakubwa wanaandikiwa, sio kitu cha ajabu.
Mimi naunga mkono ghost writing, hasa kwa wale wenye kipaji cha sauti nzuri ya kughani lakini hawana uwezo mzuri wa kuandika, sasa mtu kama huyo akiungana na ghost writer mkali si itakuwa balaa, sema sasa politics za ukiritimba ndio hapo, na ndio hapo kila mtu anang’ang’ania kuandika pamoja uwezo ni mdogo.
Tunataka kuanzisha jamvi la wasanii, na ninadhani wewe kama ghost writer unaweza kuwa mdau wa muhimu katika “libeneke” hilo kwa ku-share uandishi na mawazo katika uwandishi, kitu ambacho kinaweza saidia wengine, wewe unaonaje wazo hilo?
@Ngowo umetoa hoja nzuri ya watu kutokupenda kusikiliza mashairi. Sasa swali langu unadhani radio stations na watangazaji wao na wanachangia kwenye hilo?
Kwani, unadhani tungekuwa na vipindi kwenye redio ya kuhakiki na kujadili tungo za wasanii, unadhani hilo lingesaidia, kwanza kufanya watu wapende kuwa watafiti wa nini kimeandikwa humo, halafu pili, itasaidia wanamziki kukaza buti kwenye kuandika wasije aibika hadharani, wewe unaonaje kwenye hilo au kuna njia nyingine inayoweza kuleta changamoto ya kupenda kusikiliza tungo badala ya chorus…
Manake ukisikiliza Propaganda, mashairi yake yametulia yenye metaphors za maana, sasa watu wakiwa wanasikiliza chorus, ningekuwa mimi ni Fid Q ingeniuma, kwani ninakaa na kukuna kichwa kujaribu kuwaletea jua kwenye giza, halafu watu wanazidi kujigubika na mablanketi wakilitafuta giza panapo mwanga wa jua.
Kuna mtu kwenye makala zilizopita alichambua nyimbo ya One The Incredible, aiseee hata mimi nilichoka manake jamaa alivyochambua mashairi ya hiyo nyimbo, hata mimi nilijishtukia kwani nilidhani nimemwelewa The Incredible, kumbe kidogo tu na uchambuzi wa mshkaji ulinifumbua macho…
Mwisho, wazo la kualika wasanii na kuchambua nyimbo zao wenyewe nalo ni kitu ambacho tunaweza kuwa moja ya vitu katika mjadala wa kuanzisha project mpya na wasanii wa aina mbalimbali….hilo ni wazo tu…
Naungana na wazo la Fid Q la kuanzisha somo la Kitaaolojia vyuoni. Hajatuelezea kiundani somo hili litakuwa linagusia nini, ila I am up for the surprise.
On another note, ile mixtape (Kitaa-Olojia) iko njiani? Tutegemee lini?
Wadau wa Hip Hop wanaipitia ile makala ya One The Incredible na wanatoa maoni yao. Mi nimewajibu kama ifuatavyo (nimeona niweke maoni yangu hapa pia kwasababu mijadala inafanana):
Unayosema yana ukweli. Lakini sioni sababu ya msingi wasanii kuandika nyimbo rahisi ili tu kupata wasikilizaji/mashabiki wengi. Hoja yangu ni kama ifuatavyo:
Wahusika kama kina One, Stereo, Fid Q, Nikki Mbishi wakiendelea kama wanavyofanya sasa hivi, basi Hip Hop itakua tu.
1. Wasanii wengine itabidi wawe makini zaidi kwenye uandishi, kwasababu wanajua kila nyimbo itakayotoka itakuwa inalinganishwa na classics za hao nilowataja na wengineo kama wao.
Nadhani mtakubaliana na mimi kuwa nyimbo ikitoka, lazima watu (wanaofuatilia Bongo Hip Hop) watakumbushia Ngangari, Hili Gemu, Bila Sanaa, Chemsha Bongo au Vina Utata. Mbona Hili Gemu ilikuwa ngumu — na bado watu hawaielewi! — lakini watu waliikubali? Sikumbuki kama kuna mtu yoyote au Juma Nature mwenyewe aliichambua…
Uzuri ni kwamba, sasa hivi tuna nyimbo nyingine ambazo ni fasihi; ushairi, vipaji, maisha, siasa, vijana, elimu… Rafiki, Propaganda ndio zangu sasa hivi.
2. Tusiseme kuwa mashabiki hatupendi vitu vigumu. Cheza Pure Namba mara mbili mfululizo halafu utaona kitakachotokea. Isizimwe tu kwasababu ni ngumu. Nyimbo kama ile inatakiwa kusikilizwa kwa makini zaidi ya mara moja.
Pia, zinaweza zikafumbua watu macho kwa kuwataarifu kuwa kuna mafumbo mule ndani. Au zikachambuliwa.
Mfano: Propaganda ni wimbo ambao unaweza ukaonekana ni wa kawaida tu. Lakini ukimuelewa Fid Q, unaweza ukaandamana kupinga mambo fulani kwenye jamii.
Mi’ binafsi nimemuuliza Fid Q, kwanini hakutoa ule wimbo kabla ya Uchaguzi? Anayozungumza kwenye beti mbili ni UKWELI MTUPU, lakini yeye anaziita au anaita ushairi wake propaganda; ni paradox.
Kwa kifupi, ametumia sanaa kuiambia jamii kuwa mnachoamini kutoka kwa viongozi wa siasa mengi hayana ukweli. (Uulize maswali ili iweje!) Yaani, tunaamini propaganda na kuuzika ukweli — ndio tulichochagua.
Sidhani kama ni wazo la busara kumwambia “dumb down your flow”; bali tuwasaidie kuchambua ushairi wao…
Kwa kumalizia tu, tutaendelea kuchambua nyimbo kama hizo ili kufumbua watu macho. Watakaosoma na wasome. Wiki ijayo: Propaganda!
@ Bahati, ni wazo zuri na nimelifikiria sana tu. Itabidi tuanze wenyewe kulifanyia kazi na naamini makala zikiwa zimesimama, wadau watatuunga mkono. Wiki ijayo tutachambua Propaganda, na tutaomba mchango wa “Msangi” pia.
@Bahati… wazo la kuanzisha mijadala baada ya kuzama ndani ya tungo ili kudadisi kilichomo ni la msingi sana. Binafsi nililiona siku nyingi isipokuwa sikupata fursa ya kuweza kuwakamilishia zile project tatu pale ubaoni, lakini kwa haraka ningependa kuwaambia nina kitu kinaitwa ‘POET ADDICTION’; a form of literal art or artistic perfomance in which lyrics, poetry or stories are spoken rather than sung.
Nafikiria kuifanya hii kwasababu haitomuamsha msanii tu na tungo zake, pia hata msikilizaji atagundua kipi anapaswa kusikiliza kiasi cha kumfanya ajute kwanini hakuziba masikio kipindi chote alichokuwa akilishwa chakula kibovu cha fikra, (hili suala nililiona wakati niko Soweto kwenye battlefield moja hivi inaitwa ‘SLAGHUIS‘, ambayo kwa Kiingereza inamaanisha ‘Slaughter House’. Hicho nd’o kilinge kikubwa na kinachoheshimika pale kusini, na Mc mkali huwa anasainiwa na record label pale, kwasababu audience ya pale ni ya vichwa vitupu.
Hawa ni watu ambao hauwezi kuchakachua chochote masikioni mwao, kwasababu wanajua kila kitu kiasi kwamba unapo-freestyle huwa kuna watu wanaootea rhyme yako itadondokea kwenye mzani upi, kwahiyo wanakusaidia kuimalizia!
Mipango iko tayari mstarini na kama nilivyosisitiza hapo mwanzo, ushirikiano ni kitu muhimu sana katika kufanikisha jambo lolote lenye faida na hii jamii yetu. Pamoja sana.
Kuna mdau aliulizia KitaaOLOJIA hapo juu, well, Kitaa sio mixtape — ni jina la album yangu ya 3 baada ya Propaganda.
Nadhani swali langu la nyongeza kuhusiana na KitaaOLOJIA ni kama ifuatavyo. Baada ya kutengeneza Propaganda, unadhani ni jinsi gani uta au umehakikisha kuwa, project hizi mbili hazifanani?
Manake siku zote kunakuwaga na hiyo risk ya project moja na nyingine pamoja ni tofauti, lakini zikasound kama ni project part I na part II. Mimi nadhani shauku yangu kwa sasa ndio hipo hapo kuona utofauti wa Propaganda na KitaaOLOJIA
Labda kwa kumalizia, baada ya mapokezi mazuri ya Propaganda, je unaona kuwa kuna pressure zaidi na hii project ya KitaaOLOJIA, kwani wapenzi wanategemea project hii mpya kuwa kali zaidi ya Propaganda, je unasikia hiyo pressure kabisa, na unai-handle vipi kama msanii anayeangaliwa na wengi…
….nimeishiwa maneno….ila nimesoma na kusuuzika vinono….ni kuwa nimenyoosha tu mikono…..umahiri kukaribia ule wa kwenye Agano!
Yo intaview imetulia, kitaaolojia ndo study ya nini tena?
Nimependa tofauti ya Rap na Hip-hop wengi wanasahau, tungependa na Juma Nature arudi kundini.(Nini Chanzo? ni certified 5 mic Classic).
Nnamshikaji anayo hii album ya Propaganda kwenye gari lake kila nikipata ride naidumbukiza, sijapata chance ya kununua lakini nshaweka mental note nikutana nayo tu ntafanya hivyo, kwasababu naisikilizaga juu juu sana.
Fid Q ningependa kuparticipate kwenye project yako inayokuja nna beat mbili that i think utazifanyia justice, hata kama utazifanya bonus tracks.
@BM.. Kiukweli hiyo ni hoja ya msingi sana.. ambayo huwa ninaizingatia sana katika uandaaji wa project zangu, na uzuri ni kwamba mi’ huwa siogopi kukosea ndo maana huwa wananiita mbunifu. Kwenye KitaaOLOJIA kuna elimu nyingi ambazo nimezipata nikiwa mtaani, nisingependa kuzama sana kwenye hili, isipokuwa ningependa kutumia fursa kuwaomba wana Vijana FM wenzangu tuwe wavumilivu — mambo mazuri yako njiani!
@Mugi.. asante kwa kunifikiria kwenye ufalme wako, binafsi ningependa kuzisikiliza hizo beats so unaweza kunitumia kwenye cheusidawa@gmail.com
pamoja sana
Daaaa!! Ebwana wana m binafsi nimewasoma kwa uzuli sana!
Kubwa zaidi namkubali saaana Fareed kiukwel bado cjachukua wala kusikilza propa but naamin mmenifanya niitafute mapema sana
Fid heshima kwako endelea kukaza but 2tafika2 tunapokwenda hata kama kuna …… Wa kusini!!!!!
Dah, kiukweli fid q ni mkali ukimsikiliza kwa makini utagundua kwamba PROPAGANDA Ina ujumbe mzito sana katika jamii kama tafakari dunia now ukimwi inatesa alafu wala wasanii (vioo vya jamii) wanaendkeza mapenzi katika tungo zao, polisi anazimia gangster ili uhalifu uendelee kwani uongo? Bngo flava kuimba mapenzi itachangia ukimwi usepe? Yaani jamii yuko wazi namkubali sana yatupasa kumpa sapoti ili tuweze kuondokana na umasikini tulionao.
nimekisoma kipindi hiki kilicho rushwa mnamo january dizaini kama ndo kipo live nitakuwa mchoyo wafadhila endapo sito sema ukweli “kwamba niulithi Wa kalne saba mbeleni Kwa wajukuu zetu” hongera brother keep it up mungu yu pamoja nawe.