Uchambuzi: Fid Q – Propaganda (I)

na Bahati Mabala na Steven Nyabero

Sikiliza wimbo kwa makini. Pia unaweza ukasoma kile Fid Q anachosema: Fid Q Propaganda – Lyrics.

Propaganda ni aina ya mawasiliano ambayo lengo lake hasa ni kubadilisha au kufanya watu kwenye jamii kuwa na itikadi, msimamo au mtazamo fulani kuhusu jambo husika. Lakini, kwenye aina hii ya mawasiliano, vitu au mambo kadhaa tu “huchaguliwa” na mtoa propaganda na kuwasilishwa kwa hadhira; kinyume na kuwapa watu taarifa na hoja sahihi — kikamilifu — na kuwaacha wafanye maamuzi yao wenyewe.

Kwa kutumia mfano na lugha nyepesi: Wewe unajua kuwa binti fulani mtaani ana virusi vya Ukimwi, na labda aliambukizwa wakati anafanya biashara ya ngono ili kukidhi mahitaji yake na mtoto wake. Kwa sababu wewe unataka jamii inayomzunguka imnyanyapae yule binti, basi, kama mtoa propaganda, utawaambia watu, “Yule changu ana ngoma.” Utaficha ukweli kwa makusudi kuwa kuna uwezekano alipata Ukimwi kwa njia nyingine, na wala hautagusia vitu vilivyomsukuma yule binti awe changudoa.

Propaganda hutumiwa sana wakati wa "vita".

Propaganda, ambazo huhusishwa na siasa zaidi, mara nyingi hudhamiria kuamsha hisia za watu. Hivyo kutoupa nafasi ujengaji wa hoja. Matokeo yake wapokeaji propaganda hushindwa kufanya maamuzi sahihi, au kwa matakwa yao kama wangepewa au wangejenga hoja sahihi kikamilifu. Vita ya Kwanza ya Dunia ni mfano mzuri wa jinsi propaganda zinavyotumiwa na wanasiasa na watu wenye mamlaka kwenye jamii.

Nyimbo kama ‘Juhudi za Wasiojiweza’, ‘Nyota ya Mchezo’, ‘Hey Lord’, ‘Mwanamalundi’, ‘Tema Noleji’, ‘Utaua Gemu’, ‘Nilipotoka’ na ‘Propaganda’ — zinazopatikana kwenye albamu ‘Propaganda’ — zinakupa picha kamili ya uanaharakati wa Fareed Kubanda kama msanii wa Hip Hop na raia wa Tanzania. Kwa wale wavivu kusikiliza tungo kwa makini, kufikiria wenyewe na kujenga hoja, kwa kifupi, albamu ‘Propaganda’ ni juhudi za dhati kabisa kutenganisha ukweli na uongo. Kwenye Bongo Hip Hop na jamii ya Watanzania kwa ujumla.

Na wimbo ‘Propaganda’ hubeba mantiki thabiti ya albamu nzima, hasa nyimbo zilizotajwa awali. Tungo zinabeba na kuwasilisha ukweli kuhusu sanaa ya muziki, siasa na maisha kwa ujumla, ili hadhira iweze kupambanua kama walichokuwa wakiamini kabla ni uongo — yaani, propaganda tu (kwa mtazamo wa Fid Q).

Wimbo ‘Propaganda’ unaanza kwa midundo yenye utulivu ambao unamlazimisha msikilizaji kusikiliza kile ambacho Fid Q anaghani. Wengi watakubali kuwa Fid Q anaghani vizuri na sambamba na midundo iliyoundwa na Marco Chali.

Badala ya kuanza kwa kughani ubeti wa kwanza moja kwa moja, Fid Q anaamua kuweka msingi wa ushairi wake kwenye kiitikio:

"Yule ni Last King of Scotland, sio Idi Amin wa Uganda."

Mambo anayosema na kuhoji kwenye mistari minne ya kwanza tu yanaamsha fikra. Ukifiria kwa makini utagundua kuwa anaanza na propaganda, “Polisi wanasapoti gangsta rap; ‘Ili uhalifu uongezeke'”,  kisha inafuatiwa na kitu ambacho anajipa fursa ya kuhoji, “Wabana pua kuimba mapenzi; ‘Je, ifatafanya Ukimwi usepe?'”. Kwa hiyo, mstari wa pili sio propaganda. Ila anahoji jinsi jamii yetu inavyozipa kipaumbele nyimbo za watu ambao hawana vipaji vya kweli na zinazochochea anasa, huku tukitegemea matokeo tofauti kabisa. Je, unadhani watoto na vijana wakiendelea kusikiliza mambo ya anasa na nyimbo zisizo na nasaha za kujilinda na magonjwa ya zinaa, tutegemee janga kama la Ukimwi kutoweka? Hamfungi mawazo msikilizaji, bali anahoji.

Lakini msikilizaji anaweza akadhani anayosema kwenye mstari wa kwanza labda yana ukweli — uhalifu mwingi humaanisha kazi nyingi kwa polisi! Kwanza, Tanzania hakuna “gangsta rap”. Pili, baadhi ya Wamarekani ndio walianzisha hizo propaganda ili kuchafua muziki wa Hip Hop, ambao mara nyingi huusishwa na uhalifu (matumizi wa madawa ya kulevya, mauaji kwa kutumia silaha, vitendo vya ngono na anasa kwa ujumla); kinyume na kuchukulia kinachoimbwa na wasanii kama ukweli wa mambo yanayotokea kwenye mitaa yao. Kama umekuwa unafuatilia mauaji ya halaiki mashuleni nchini Marekani, mara kwa mara vyombo vya habari vimekuwa vikisema watuhumiwa walikuwa wanasikiliza nyimbo za wasanii wa Hip Hop. “Gangsta rap”. Hivyo, bila shaka kinachoimbwa kwenye tungo za wasanii husika kimechangia mauaji ya halaiki.

Kama ilivyojadiliwa mwanzoni, mtoa propaganda hudhamiria kukufunga kimawazo kwa kutokupa nafasi ya kuhoji. Kutoa majibu rahisi kwa maswali magumu. Watu wengine huweza kuita tabia hii determinism, kwasababu wanashindwa au hawataki kuzipa nafasi hoja mbadala.

Anarudi tena kwenye propaganda: “Media zinapromoti beef; ‘Wanadai zinakuza muziki.'” Kawaulize hao ma-DJ kama wanawajua wasanii wowote ambao ni ushahidi thabiti kwamba viwango vyao vya kuandika tungo bora, ubunifu, uwasilishaji wa kazi zao n.k. viliongezeka baada ya kuingia kwenye malumbano na wasanii wengine.  Ukiacha ushabiki na umbea wa malumbano, kuna lolote la maana? Kwanini hatuwabani wahusika wanapotupa upuuzi kama huu?… Ni kama tunameza chochote kile ma-DJ wanachotuambia. Hiyo ndio jamii yetu.

Baada ya hapo, anaamua kuhoji kitu kingine kwenye sanaa ya muziki Tanzania: “Wadau wana wasanii wabovu; ‘Nyie wakali mtatoka vipi?'” Ndio, ni swali gumu kwa wasanii wenye vipaji, kwani hawapewi kipaumbele na walioshika usukani wa gari moshi la muziki. Kama hili halitoshi, wanajamii nao wanaamini chochote kile kinachotoka kwenye midomo ya wadau wa muziki! Halafu, kama tunavyowapa vipaumbele “wabana pua”, tunategemea matokeo tofauti — Ukimwi usepe na sanaa ikue — kwani kila siku tunalalamika muziki wa Tanzania unakufa kifo cha mende.

Baada ya kusema na kuhoji hayo yote, hasa kuhusu sanaa, anakwambia, “Hizi ni propaganda.” Usiyatilie maanani aliyosema na haupewi nafasi ya kuuliza maswali na kujenga hoja zako binafsi. Wakoloni wetu wa mwisho wanaita hii kitu sarcasm. Anatucheka.

Wasanii wabunifu wa Hip Hop hupata sifa na kuheshimika kutokana na punch-lines. Tafsiri nyepesi inaweza ikawa ni [kama] mistari inayojumuisha aliyosema kwenye mistari kadhaa iliyopita kwa kutumia fumbo au kucheza na maneno na kuweka msisitizo. Kwa maneno mengine, anakupa vidokezo vya mambo aliyokuwa anazungumzia.

Na Fid Q anatumia punch-line ifuatayo: “Utaibiwa ukicheza blanda; ‘Yule ni Last King of Scotland, sio Idi Amin wa Uganda!'”

"The Last King of Scotland"

Hapa unahitaji hisabati na utundu. “Utakuwa umefanya makosa (makubwa sana) kama ukidhani Last King of Scotland ni Idi Amin wa Uganda!”

Kuna Idi Amin mmoja tu wa ukweli.

[The] Last King of Scotland ni filamu iliyoandikwa na Giles Foden. Ni hadithi ya kutunga. Alichofanya mwandishi wa filamu hii ni kutumia wasifu wa mhusika wa kubuni — Dr. Nicholas Garrigan — kujenga wasifu wa Idi Amin Dada. Kilichofanyika ni “kuchagua” matukio machache tu kutoka kwenye historia ya Uganda/Idi Amin na kuyapachika kwenye filamu.

Ukiacha hayo, kuna uongo wa hapa na pale. Kwa mfano, mke wa Amin, Kay Amin alipewa mimba na Dr. Garrigan. Lakini, ukweli ni kuwa Bi. Kay alipewa mimba na ‘mpenzi’ wake, Dr. Mbalu Mukasa. Pia, kadri filamu inavyoendelea, mambo yanayotokea kwenye filamu yanazidi “kutengana” na mambo halisi yaliyotokea kwenye historia ya Uganda.

Haya, tafuta kikokotozi na visoda kama umesahau kuhesabu…

Mstari wa kwanza na wa tatu kwenye kiitikio ni Last King of Scotland! Propaganda.

Mstari wa pili na wa nne (ambayo inahoji na kuruhusu ukweli kujulikana) ni Idi Amin wa Uganda! Na usishangae ukikutana na Waganda wanaomchukulia Idi Amin kama mzalendo.

Bado unaamini Last King of Scotland ni Idi Amin Dada?

Sehemu ya pili, ambayo itachambua ubeti wa pili, wiki ijayo!

Makala nyingine:

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 21 Comments

21
  1. Kwa maoni yangu naona mstari wa pili wa kiitikio,“Wabana pua kuimba mapenzi; ‘Je, ifatafanya Ukimwi usepe?’” unamaana zaidi ya moja au wanavyosema huko Ughaibuni ni “double/triple entendre”. Ukiufatilia huu wimbo unatambua Fiddy anatukanya kuyaangalia maswala ya kijamii kwa juu juu tu. Kwa hiyo kama ziada ya jinsi Bahati na Steve walivyochambua, mi naona tunakanywa kutafuta uhusiano wa moja kwa moja (correlation) kati ya sanaa (hasa ya Bongo flava) na maovu ya jamii. Yani hata kama “wabana pua” wasipo imba Ukimwi utaendelea kuua Waafrika kama hatutabadilisha tabia zetu. Mziki unaweza kuonya au kukanya lakini mabadiliko yanaletwa na watu binafsi. Mwisho ningependa kuwapongeza sana kwa kazi yenu nzuri, nasubiria kwa hamu sehemu ya pili.

  2. Ndio maana ya kuchambua fasihi, na michango kama hii ndio inahitajika — hii ni fasihi, na kila mtu anaruhusiwa kutafsiri jinsi anavyoelewa. Nimekusoma mkuu!!

    Kwa hiyo, huo mstari ni propaganda au? Kumbuka anahoji… 🙂 ndio maana ukaweza kujenga hiyo hoja. Tutaingia kwenye falsafa…

    Hata hivyo, nyimbo zinaweza kutumiwa kama chombo cha kuelimisha wanajamii?

    Kuna kitu kingine tulitaka kujadili (na inafanana na hayo uliyosema): “Polisi wanasapoti gangsta rap; ‘Ili uhalifu uongezeke’” Ni propaganda, lakini nadhani ingekuwa vizuri zaidi kama Fid Q angegusia ile ishu ya “Muziki wa ‘kufoka-foka’ unakuza uhuni.” Sidhani wengi wanamuelewa vizuri anavyotaja “Gangsta rap”. Ukiacha hayo, kama ulivyosema, kutoa majibu rahisi kwa maswali mazito, na kukwepa kujiangalia wenyewe kama jamii kwa ujumla.

    Najua Fid Q atapita hapa kuangalia tunachojadili… Tafadhali, tunakuomba usichangie lolote hadi tutapomaliza mjadala/uchambuzi wa mwisho.

    Shukrani.

  3. @SN sijui huo ujumbe wa kuchangia ni wa watu wote au Fid Q tu lakini nitajizuia hadi mmalize kuchambua.

  4. Ujumbe ni kwa Fid Q tu. Akianza kuchangia hapa hatatutendea haki kwenye uchambuzi na mjadala. Kwa hiyo, tafadhali, endelea (endeleeni) kuchangia…

  5. fid q, i’m a kenyan in kampala, and married to a tanzanian mama. so that means i’ve rubbed shoulders with all east african music artistes. for this i wanna tell you are one in a million. your songs are good to the ears, touches the soul and there are very educative, and even though people will not turn to you in large to tell you you are a great artist, just know they feel you inside. you are so hard to hate. THUMBS UP BRO, KEEP UP THA GUD WORK. hope to meet you someday!

  6. fid q propaganda ni wembo ambao msikilizaji ili awaze kuelewa nini unamaanisha lazima akae kitako kuusikiliza kwa makin..punch ya Last King of Scotland sio Idi Amin wa Uganda!”inavutia lakini watu wengi walikuwa hawajui nini unaanisha kwani wengi wetu hatuja icheck hiyo movie but kwa sasa nafurahi nimeelewa vyakutosha kaka

  7. kwenye huo mstari wa Idi Amin na hiyo movie ya Last King of Scotland, nadhani ni kweli mtunzi anataka kuweka sawa maana ya Propaganda kwa kutoa huo mfano..

    Lakini swali langu ni hili, je hiyo movie pamoja na mapungufu yake, tunaweza kusema vyote kuhusu character ya Amin ni propaganda?

    Sasa uwiano kati ya huo mstari na nia ya mtunzi kuutumia. Je Fid Q anataka tuchambue ipi ni Propaganda na yapi ni ukweli, kwani sidhani kila kitu ni Propaganda. Kwani hata stereotypes zimejengwa kwenye msingi ya ukweli fulani, sema sasa watu wanakuwa wanazidisha chumvi na sukari hapa na pale au exaggerate.

    Inamaana tunakubali kuwa yule sio Idi Amin kwenye movie, bali ni Last King of Scotland, yaani character aliyeundwa na mtunzi wa hadithi ya filamu hii. Au hapo Fid Q anafanya tu wordplay ambayo inamaana iliyojificha.

    Labda unachotakiwa kujiuliza, kwani Propaganda zote ni uongo 100%, kwani utakuja kugundua kuna a lot of kejeli/ sarcasm nyingi kwenye hii nyimbo..

    Ni kama mtu asema, Yule wa kampeni ya 2005 alikuwa Chaguo la mungu kwetu sote, bali sio huyu kiongozi wa leo…hihihihi nimemaliza

  8. Kama ile mantiki ya propaganda (yenye “negative tone”) ikiangaliwa kwa makini, basi kwa uelewa wangu mdogo nadhani ule wasifu uliojengwa na mwandishi ni propaganda.

    1. Amechagua matukio anayotaka yeye binafsi yanayoendana na anachotaka kusema kuhusu Idi Amin.

    2. Je, alikuwa na lengo la kuwaambia watu ukweli? Kwa nini aongezee vitu/visa vya kutunga wakati ukweli upo? Hadithi za ukweli hazivutii sana au hazikukaa vizuri kwenye mtitiriko wake (ambao bila shaka ulikusudia kuamsha hisia)?*

    3. Watu wengi, hasa wa nchi za Magharibi, hawajawahi hata kusoma vitabu na historia ya Uganda na Idi Amin, unadhani watakuwa na mawazo au mtazamo gani baada ya kuiona ile filamu?

    4. Baada ya kuangalia ile filamu na documentary hii kuhusu maisha yake (Idi Amin), unadhani utakuwa na mtazamo ule ule? Lipi limeongezeka kwenye hiyo documentary? (Hiyo documentary inaweza kuchukuliwa kama propaganda pia, kama unajua zaidi ya yaliyooneshwa humo ndani…).

    Bahati, najua unaelewa “lying by omission”…

    5. Kuhusu suala la word-play, unadhani Fid Q alishindwa kutumia nyingine? Yaani, katika metaphors zoooote, kwanini alichagua hiyo ya Last King of Scotland? Nadhani hilo ndilo swali unalouliza.

    Kumbuka, propaganda humfunga mtu mawazo na hivyo hadhira hupata hisia kama ilivyodhamiriwa na mtoa propaganda. Hakupi nafasi ya kujenga hoja yako binafsi na kufanya mambo/maamuzi kwa matakwa yako mwenyewe. (Of course, hapa tunazungumzia ile hadhira ambayo haijui kinachoendelea… tutaelewa vizuri baada ya kuzama kwenye zile beti mbili nzito!)

    Kwenye Vita ya Pili ya Dunia, mojawapo za propaganda ilikuwa ni kuwa Wayahudi wameshikilia vyombo vinavyoendesha uchumi wa Ujerumani na dunia nzima kwa ujumla kwa sababu chungu mbovu. Unadhani kama watu wangeambiwa kuwa elimu na misingi ya kusaidiana kwenye kueneza ujuzi ndio umechangia mafanikio yao kwa kiasi kikubwa, je matokeo yangekuwa tofauti? Nini kilichokuwa kinasemwa dhidi ya Waromani, walemavu na mashoga? Yalikuwa yana “ukweli” — labda kiasi — tu?

    Yaani baada ya kupewa ukweli na hali halisi kama ilivyo, unadhani watu wangeshika mtutu?

    * Kama mchangiaji wa kwanza na Bahati wanavyodai, labda tunapaswa kujiangalia sisi wenyewe; hatupendi ukweli na tunajali mambo yanayoamsha hisia zaidi, hivyo kushindwa kujinufaisha na kujiendeleza.

  9. Sijawahi sikia mtunzi akaandika msatari mmoja fact mstari mmoja uongo kisha wimbo ukaitwa jina lenye utata.

    Mwandishi akiandika kimtindo huo lazima wasikilizaji wasielewe, kwa hiyo sioni mantiki kwenye uandishi wa aina hiyo. (Na kwa vile hakuna mantiki basi haikuwa hivyo :))

    Yaliyoandikwa yote ni facts au tuseme ‘ukweli’ japo unaweza ukawa sio ‘the whole truth’

    Polisi wana sapoti gangstar rap; ili uhalifu uongezeke
    Wabana pua kuimba mapenzi; kutafanya ukwimwi usepe?
    Media zinapromoti beef; wanadai zinakuza mziki
    Wadau wana wasanii wabovu; nyie wakali mtatoka vipi?

    Hapo juu mkuu Bahati hakuna propaganda, wote ukweli mtupu. Gangstar rap ni hiphop inayo promote violance. Wewe utasema hakuna gangstar rap, but kwenye dictionary la polisi na watu wa kawaida zipo.

  10. @Sakura, asante kwa mchango wako. Mimi ningeomba utoe mfano hai wa gangsta rap inayo promote violence, ukianza kwa kuelezea gangstar rap maana yake ni nini..

    Pili, Tanzania hakuna gangstar rap, sasa hapo jiulize, kwanini Fid Q ameamua kuzungumzia hiyo kwenye hii nyimbo yake, wewe unadhani ni kwanini? ningependa kujua fact ya hilo suala.

    Tatu nitaku-quote “Sijawahi sikia mtunzi akaandika msatari mmoja fact mstari mmoja uongo kisha wimbo ukaitwa jina lenye utata”, sasa ukiniuliza mimi nitasema hiyo ndio Propaganda yenyewe au wewe unasemaje?…Propaganda siku zote huwa na utata kwasababu, sio ukweli, japokuwa kuna kuwaga na ukweli kiasi fulani..huo ni mtazamo wangu.

    Lakini cha msingi ningependa mfano wako wa gangsta rap inayo promote violence na maana ya gangsta rap ni nini, na je Tanzania ipo kweli?

  11. Actually huo ubeti rahisi kuuelewa ukiuchukua kaa ulivyo

    Polisi badala ya kuzuwia uhalifu wanapendelea vitu vinavyouchochea

    Waimbaji badala ya kusaidia jamii kupambana na Ukimwi, wanaimba nyimbo zinazochochea 

    Media badala ya kusaidia kukuza vipaji vya wambaji kwa kutafuta ushirikiano, zinachochea mifarakano

    Wadau badala ya kupokea wasanii wakali tayari weshazongwa na wasanii wabovu

    Gangsta rap (kwa mujibu wa official media) ni hiphop iliyoanza east coast marekani ambayo ina ‘promote’ violence , profanity, drug abuse, sex, vandalism and other whatnots (japokuwa waimbaji wenyewe husema kuwa wanaakisi tu maisha ya vijana waliowazunguka na sio Kama wanakubaliana na vitendo hivyo)

    Kwa hiyo lazima tukubali kuwa gangster rap ipo na nyimbo zinazozungumzia kwa mfano wa kusifia vitu hivyo zipo tele kwa mujibu wa international media.

    Jee gangster rappers wapo Tanzania? Suala gumu kwangu kwa kuwa simsikilizaji wa muziki wa kufokafoka as a hobby but kuna mheshimiwa mmoja alisikika akijinadi “I want to kill right now”, sijui wengine.

    Hata hivyo, hata ikiwa hao gangsta rappers hawapo, haimzuwii muandishi kutumia mfano huo hata for a want of a better parody tu. (besides ametumia mfano wa Iddi Amini with no relation to Tanzania either)

    Akitaka kuonyesha kuwa polisi hawafanyi kazi yao inavyotakiwa na wakipata chance ya kuchochea uvunjaji wa sheria watafanya hivyo ili kujiomgezea chances za kula, nafikiri ni mfano mwepesi kueleweka.

  12. Sakura unasema: “Yaliyoandikwa yote ni facts au tuseme ‘ukweli’ japo unaweza ukawa sio ‘the whole truth’.”

    Narudia, “Facts” au “ukweli”, japokuwa zinaweza zikawa sio the whole truth…

    Halafu: “Hapo juu mkuu Bahati hakuna propaganda, wote ukweli mtupu.”

    Google neno “propaganda” au kaangalie kwenye vitabu maktaba kama hukubaliani na maelezo na mifano iliyotolewa kwenye makala. Ingawa kwa upande mwingine, wewe mwenyewe umesha-define propaganda, ila kwa kijichanganya kidogo: “Facts” au “ukweli”, japokuwa zinaweza zikawa sio the whole truth… No one can refute facts. Facts are facts.

    Usiulize ni nani? Ni yupi? Saa ngapi? Ilikuwaje? Na nani? Ili iweje? Nadhani wewe ndio unachofanya. Kumbuka, Fid Q ni mwana-Hip Hop.

    Mbona hizo media hazisemi chochote kuhusu Rock Music? Kina Eric Harris and Dylan Klebold si “wanadai” walikuwa influenced by Marilyn Manson’s music (kasome kuhusu Columbine Massacre)… Si polisi walikuta tapes za DMX na Eminem pia? Vipi, mbona “gangsta rap” tu ndio imejaa kwenye vinywa vya waandishi wa habari?

    Wao walianza na Hip Hop, waliokuja kuichafua wakaanza kuiita “Gangsta Rap”. Kuna wimbo mmoja wa Common unaitwa “I used to love HER”, nadhani labda utaongeza mwanga kidogo.

    Kwa kumalizia tu, kama mpenzi wa “Gangsta Rap” au Hip Hop akifanya uhalifu ina maana hicho tu ndio kimemsukuma (kufanya uhalifu). Yaani matatizo yote ya kiakili, kiafya, kifamilia n.k. yanapigwa pingu?

    Nakushauri umsikilize T.I. kwa makini sana kwenye hii clip:

    http://www.youtube.com/watch?v=YgOeuhoJAzs

    Ndio yale yale, mtu anadai ataandika Katiba Mpya ndani ya siku 100 na sisi hata hatusumbuki kuhoji.

  13. @Sakura, umetoa maelezo mazuri, ni kweli ukiangalia hiyo mistari na kuisoma kama ilivyo sio migumu kuielewa, lakini sasa, mashairi kama kazi ya fasihi, itakuwa ni sahihi tukisema fikra za mwandishi hapo zilikuwa tu ni black and white au alikuwa anabeba ujumbe uliojificha, kama kazi za fasihi zilivyo kawaida yake… hapo sasa, mimi sina uhakika, lakini tutasaidiana hivyo hivyo mpaka kujua nia hasa ya Fid Q.

    Pili, gangsta rap haikuanzia East Coast, hiyo source imekosea juu ya chimbuko halisi la gangsta rap. Ukiangalia gang violence Marekani ilianzia na kushamiri west coast au pwani ya magharibi. Huko ndio kitovu cha Bloods & Crips, lakini si muda mrefu sana ndio wakaanza ku-spread katika vitongoji vingine, hadi kutapakaa East Coast pia.

    NWA walikuwa wanaogopwa sana kwa mashairi yao ambayo nadhani yalikuwa makali kama hotuba za Malcolm X ambaye aliogopwa sana, na kuwa labelled kama mtu anayechochea uhasama na fujo, lakini sikiliza hotuba zake na interviews utachoka mwenyewe jinsi anavyovunja-vunja hizo hoja dhidi yake kuhusiana na kuwa violent.

    Sasa basi, kama Crips & Bloods chimbuko lao kuu lilikuwa West Coast na mwanzo wa Gangsta rap ulitokea huko, unadhani all that is just a coincidence? mimi binafsi sidhani.

    Kama tunakubaliana na Afande Sele kuwa sanaa ni kioo cha jamii, hivyo tutakubali ya kuwa, wasanii wa hip hop kutoka West Coast wasingeweza kuzungumzia kitu kingine chochote zaidi ya mambo yaliyowazunguka, na hilo ni gang violence iliyotapakaa katika mitaa yao.

    Tupac alisema hivi, nitatafsiri na ku-paraphrase: Wao kama wasanii wataendelea kutengeneza music videos ambazo zina images za kusisimua kuhusu gang violence mpaka watu washtuke na kuanza to do something about it. Yeye akatoa mfano wa jinsi media ilivyosaidia kufanikisha vita ya Vietnam kusitishwa. Kwani, Wamarekani wlaipoanza kuona picha za vita ya huko, na jinsi wanajeshi wao walivyokuwa wakitesekana na kufa kwa wingi, protests zinachachamaa Marekani kila kona dhidi ya vita hiyo.

    Sasa, ni vipi mimi ninayekaa uswazi ku-rap kuhusu mambo ya Masaki? Kama kila wiki naona mwizi akichomwa moto, unadhani ni nini nitazungumzia kwenye nyimbo yangu, si lingine bali hilo.

    Inashangaza kuwa, ni sawa watu kuishi kwenye extreme conditions, lakini we get offended hizo extreme conditions zinapozunguzwa na kuonyeshwa hadharani, mfano mzuri kipindi cha Hurricane Katrina… Marekani didnt like the images zilizokuwa zinatoka huko, maana’ke iliacha wengi wakijiuliza, hii sio Marekani tunayoijua, siyo ile ya MTV tunayoishobokea kila kukicha.

    Pia umesema, Fid Q alitumia mfano wa Idd Amin pasipo na uhusiano wowote na Tanzania, hilo ni kweli tukiangalia kijuu-juu, lakini unadhani alifanya hivyo by accident? Ukiniuliza mimi nitasema hapana, nadhani alifanya hivyo makusudi kutumia huo mfano kujaribu kuelezea zaidi maana ya neno Propaganda, na hapo hapo kuacha watu wakijadili hiyo filamu kama je, ilimtendea haki Idd Amin au ilijawa na Propaganda dhidi yake kama Fid Q anavyoonekana ku-suggest. Sasa hapo ndipo ninapomsifu Fid Q, kwani anagusia halafu anaacha hadhira ijitafutie jibu, kuliko ile style ya kutafuniwa na kumezewa.

    Mwisho, nadhani hapo juu umegusia nyimbo ya Sugu katika mixtape yake ya Anti Virus. Hiyo line ya “I want to Kill right now” sina uhakika inaingia vipi kwenye kuwa gansta rap, kwani kama khadija kopa kipindi kile taarab ilikuwa taarab angesema maneno hayo dhidi ya wapinzani wake, tungesema taarab ghafla imekuwa gangsta rap?

    Nadhani kuna nyimbo ya Hasheem inaitwa ”Saa za Kazi”, nadhani tukipata muda tutabidi tuujadili huo halafu tuone kama ni gangsta rap, kwa kuwa watu wanaweza kusema kuwa, anachochea maovu, kama ile bendi waliotupa nyimbo ya masikini mtaji wake ni nguvu zake mwenyewe, ambao ulikuwa ukiimbwa na majambazi wanapokuwa katika kazi… hapo sasa… sijui tuilaumu bendi kwa kutunga hiyo nyimbo, au majambazi kwa kuigeuza kuwa soundtrack to their action movie… hah!!

  14. Vijana mbona mnataka kuwa na double standards! 

    Tunakataa kuwa gangster rap hazipromote violence wakati tunakubali kuwa wabana pua kuimba mapenzi wanapromote ngono and consequently Ukimwi!

    Mnataka kunirudisha kwenye the theory of cause and actions naona. Hivi nyimbo ikisifia violence haimuathiri msikilizaji kweli? Why do we say msanii ana jukumu la kuelimisha jamii iwapo kumbe kazi zake hazisababishi actions kwa hadhira?

    Papo kwa papo kamba hukata jiwe, ukiimbiwa uchukue sheria mkononi kila siku mwisho utafuata tu. 

    @Bahati, Khadijah Koppa akiimba anataka kuuwa mtu tutamtafutia jina linalokwenda na sifa hiyo (since haimbi hip hop, hatakuwa gangsta rapper) kama sasa kwa wajuzi wa Taarab walivyomwita ‘Malkia Wa Mipasho’ (and I believe not in a good way)

    Hatusemi wala hatutaki wa Manzese kuimba kama wa Masaki, lkn akiimba ‘usihofu kuchomwa moto, pora japo mtoto’ tutasema ana promote violence na sio ana reflect maisha ya vibaka anaowaona.

    @Bahati, my bad, zilianza West coast you are very right.

    Hebu twende logically tu na huo mstari wa kwanza 

    “Polisi wana sapoti gangsta rap; ili uhalifu uongezeke”

    If this sentence is a propaganda then it means:

    Polisi wanasapoti gangsta rap lakini sio kwa sababu ya kutaka kuongeza uhalifu
     
    Or

    Polisi hawasapoti gangsta rap, wanazuliwa tu kuambiwa wanasapoti ili kuendeleza uhalifu.

    Tukisema mwandishi anataka kusema kuwa gangsta rap is just a propaganda hai-make sense logically kwenye sentensi hiyo and the whole sentence collapses. 

    Nitakupa mfano huu:

    Wanawake wa pwani wanapenda kujipamba kwa hinna ili kuburudisha waume zao.

    Nikiambiwa hiyo ni propaganda basi nitaangalia sentensi as a whole na sio kumega vipande niseme hapa ndo kuna propaganda.

    Ama wanawake wa pwani hujipamba kwa sababu nyengine na sio kupendezeshea waume zao au wanawake hao hawapendi kujipamba kwa hinna. Sentensi hainipi Mimi nafasi ya kuanza kuhoji uhalisia kuhusu hinna.

  15. “Tunakataa kuwa gangster rap hazipromote violence wakati tunakubali kuwa wabana pua kuimba mapenzi wanapromote ngono and consequently Ukimwi!”

    Wapi tumesema hivyo Sakura?

    Kilichoandikwa ni hiki:

    … ANAHOJI jinsi jamii yetu inavyozipa kipaumbele nyimbo za watu ambao hawana vipaji vya kweli na inayochochea anasa, huku tukitegemea matokeo tofauti kabisa. Je, unadhani watoto na vijana wakiendelea kusikiliza mambo ya anasa na nyimbo zisizo na nasaha za kujilinda na magonjwa ya zinaa, tutegemee janga kama la Ukimwi kutoweka? Hamfungi mawazo msikilizaji, bali ANAHOJI.

    Kwa mantiki hiyo, wewe msikilizaji unaruhusiwa kujenga HOJA yako, kwa matakwa yako na kuamua upi uwe mtazamo wako. Tofauti na lugha inayotumiwa kwenye propaganda.

    Mnataka kunirudisha kwenye the theory of cause and actions naona. Hivi nyimbo ikisifia violence haimuathiri msikilizaji kweli? Why do we say msanii ana jukumu la kuelimisha jamii iwapo kumbe kazi zake hazisababishi actions kwa hadhira?

    Kitakachoimbwa, kiwe kibaya au kizuri, hakimaanishi lazima msikilizaji atakifuata. Unachosikia kwenye kazi ya sanaa ni sehemu ndogo sana ya vitu vinavyokupa mwongozo wa maisha yako wewe binafsi. Nilihoji pale juu lakini hakuna mtu aliyejibu — labda kwasababu huo mjadala upo kwenye “positive tone”…

    Kama ingekuwa hivyo, mbona maisha yangekuwa marahisi. Just buying a couple of CDs from some “informative” smart artist who talks about positive things… Then, the parents’/society’s job is done.

    Mjadala na hoja nzuri @ Sakura. Lakini, ulivyomalizia ndio imenifanya niumize kichwa zaidi:

    Wanawake wa pwani wanapenda kujipamba kwa hinna ili kuburudisha waume zao.

    Nikiambiwa hiyo ni propaganda basi nitaangalia sentensi as a whole na sio kumega vipande niseme hapa ndo kuna propaganda.

    Ama wanawake wa pwani hujipamba kwa sababu nyengine na sio kupendezeshea waume zao au wanawake hao hawapendi kujipamba kwa hinna. Sentensi hainipi mimi nafasi ya kuanza kuhoji uhalisia kuhusu hinna.

    Huoni labda hapo ndipo kwenye tatizo kwenye jamii yetu. Kwani, watoa propaganda ‘hawapachiki’ vitu? Yaani kama Wahutu walivyoanzisha propaganda dhidi ya Watutsi, na kuwaita “cockroaches”… Ku-refute hizo propaganda kwa kusema tu “Watutsi sio mende, (au) kwasababu mende sio Watutsi” inatosha ku-reverse the effects of propaganda? Unadhani wakielewa ‘mantiki’ hasa ya kutumia neno “cockroaches” dhidi ya ndugu zao na kupembua kwa kina tofauti za ubinadamu na unyama au wadudu (mende), labda inaweza ikaleta matunda mazuri zaidi?

    Mfano mwingine kwenye makala ume-refute kuwa [The] Last King of Scotland ni Idi Amin wa Uganda kwa kuonesha kuwa kuna vitu vilivyopachikwa, ambavyo ni vya kubuni. Je, mimi binafsi kama nikitaka kujua ile hadithi ni ya kweli au uongo/propaganda, sina nafasi ya kuhoji uhalisia wa yaliyomo kwenye hiyo filamu? Kuna “formula” ya ku-refute propaganda?

    Kama mtu akiambiwa filamu ‘Last King of Scotland’ NI propaganda, ataanzia wapi kama hapewi nafasi ya kuhoji uhalisia wa mambo?

    Tuache mifano ya kubuni ambayo ni rahisi kupinga au kuelezea unavyotaka wewe au ninavyotaka mimi… ukipata muda soma hii makala — ni juhudi za kueleweshana hoja za pande mbili zinazosigishana. Halafu amua, hiyo ya kumtumia Einstein ilikuwa ni propaganda au la.

    Sakura, unaona, sisemi ipi ni sahihi, ila nahoji tu. Utaamua mwenyewe kutokana na mtazamamo wako. Sidhani ni jambo la busara kuchukulia lugha au aina za mawasiliano kama hisabati au logic. Labda makala ya tatu ya huu uchambuzi itakupa jibu litakaloridhisha fikra zako.

  16. @Sakura..hahaha nimependa mfano wako wa hinna, hao mabinti lazima watakuwa wanapaka ili wapendeze, na sababu kuu ya kupendeza mara nyingi huwa, either kuvutia wanaume (kama wao ni single) au kuvutia waume zao, si unajua tena mpango wa nje unaweza ukakukuta mwanamke kama hujiweki mrembo mara kwa mara..hah!!..mtazamo tu..

    “Polisi wana sapoti gangsta rap; ili uhalifu uongezeke”… hapa mimi mwenyewe sina uhakika kama ni propaganda au la, hasa tukiiweka kwenye context ya Tanzania, hili halitaleta maana sana tukisoma huo mstari kama ulivyo. Ndio maana mimi nikasema, ninahisi mwandishi anaweza akawa ametumia hiyo kama metaphor kuzungumzia kitu kingine, au maana hiyo hiyo lakini akituficha kitu. Hapo sasa ndipo itabidi tusaidiane kuweza kuelewa.

    Mimi nimependa hii “Tunakataa kuwa gangster rap hazipromote violence wakati tunakubali kuwa wabana pua kuimba mapenzi wanapromote ngono and consequently Ukimwi”. Hili ni swali zuri kabisa, nadhani double standard uliyoisema ndio inaingia hapa.

    Nadhani ndio maana makala ilichofanya ni kuuliza swali, na sio ku-draw conclusion kwenye hilo suala. I guess tunaweza kuangalia tafiti za wana-sosholojia na kuona takwimu kama wapo watu waliofanya maovu kwa kusukumwa na nyimbo au kufanya zinaa kwasababu ya nyimbo, lakini hapo hapo zipo nyimbo zinazo hamasisha watu kuvaa mipira, je zimefanikiwa au ni hadithi tu baada ya habari? Mimi sina jibu la moja kwa moja hapo, sijui nyinyi..

    Au je, inawezekana tunaangalia yasiyopo, yaani tumeng’ang’ania kusoma polisi kama polisi, bila kuhoji hao polisi ni akina nani, ni polisi wenye magwanda au hilo neno polisi limetumika tu kuzungumzia authority na wala sio polisi kama tunavyofikiria.

    Kama Kikwete atatumia wana-bongo flava kwenye kampeni zake, ina maana he cares for the youth? Yaani anataka kuonesha kuwa ana-support muziki huu wa Hip Hop, na hapo hapo, na yeye ni kijana kwa kuwa anafungamana na vijana, ili mwisho wa siku, tukiwaangalia hivyo, basi vijana na sisi tutoke kwa makundi kwenda kumpigia kura yeye kwani tayari tumeshamwona kama kijana mwenzetu, kwani anazungukwa na vijana wenzetu na anasikiliza nyimbo tunazozisikiliza. Sijui kama nimefanikiwa kuonyesha connection ya mfano huu na kilichosemwa na mwandishi wa shairi.

  17. Propaganda seems to be something we are all engaged with in some way or another. In presenting ourselves at a job interview, for example, we leave out things that would harm the chances of landing a gig; isn’t this propaganda, lest on a different level?

    So I’m with Fid Q on instigating the habit of asking questions; ni yupi, saa ngapi, ilikwaje, etc. But I would humbly extend this further than what we hear/watch on commercial media, and into our daily lives. In other words, I think Fid Q’s lyrics, especially the hook/chorus, tell us (everyone, young and old) to stop taking things for granted. Baas.

  18. KAKA POLE NA SAFARI NZITO YA KUIKOMBOA JAMII YETU! NAZIDI KUKUFUATILIA KIUNDANI ZAIDI, NA PIA NAOMBEA KAZI NJEMA YENYE MAFANIKIO, kiufupi kaka PROPAGANDA mzigo nimeukubali sana man, duh dude lipo salama kinoma

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend