Five Questions with Sule Mudi… aka Dowans

Kuhoji wanasiasa au watu wanaohusishwa na siasa nchini sio desturi ya tovuti hii. Ila ilitubidi tuvunje mwiko huu wiki iliyopita, kwa sababu tuliona kuwa ni wajibu wetu kusaidia kuwasilisha ujumbe kwa Watanzania.

Nilipokea simu majira ya saa sita mchana, siku ya Ijumaa, kutoka kwa mtu ambaye simfahamu. Alijitambulisha, “Mimi ni rubani wa Brigedia Sule kutoka Oman.”

Lafudhi yake ya Kiasia ilizaa maswali mengi. Lakini kabla sijafungua kinywa na kuanza kumhoji, rubani akaendelea, “Tafadhali njoo haraka Julius Kambarage Nyerere International Airport. Kuna ujumbe mzito kutoka Oman.” Kama hiyo haitoshi, akapaza sauti: “Usije na kamera ya aina yoyote ile!”

Haraka-haraka akili yangu ikaunganisha mambo — milipuko ya mabomu Gongo la Mboto, Uwanja wa Ndege… ; bila shaka Brigedia Sule amekuja kuwajulia hali wahanga na kutoa msaada wa aina fulani. Pia, ni mtu ambaye labda hapendi kujulikana ndio maana akaamua kunipigia simu mimi, mhariri wa tovuti inayotembelewa na mamia ya watu tu kila siku.

Nikaona haina nongwa. Akili kumkichwe; ili kukwepa adha ya foleni mjini nikaamua kuchukua bajaji kutoka ofisini hadi Njia Panda ya Ulaya. Baada ya dakika takribani 45 hivi nikawasili kwenye malango ya Uwanja wa Ndege, ambapo nililakiwa na mtu aliyejitambulisha kuwa ni rubani wa Brigedia Sule. “Mimi nd’o niliyekupigia simu muda mfupi uliopita. Usiwe na wasiwasi, nimeshakuona sehemu.”

Rubani akaniongoza njia hadi tulipofika kwenye VIP Lounge. Akafungua mlango na kuashiria niingine ndani, yeye akabaki nje mlangoni. Taratibu nikajongea ndani huku nikifaidi kiyoyozi maridhawa.

“Karibu mhariri wa Vijana FM! Tafadhali, keti chini,” mmoja wa watu watatu niliowakuta akanikaribisha. “Bila kupoteza muda, tunataka wewe umuhoji Brigedia Sule. Tunajua fika jinsi mnavofanya mahojiano kwenye tovuti yenu… Huwa mnauliza maswali matano tu kama sikosei. Kwa hiyo, ukumbi ni wako. Ratiba ya Brigedia ni nzito sana, hivyo fanya haraka kadri unavyoweza!”

Wakati naandaa kalamu na karatasi kwa ajili ya kunakili kile ambacho Brigedia atasema, nikahoji, “Hivi, naongea na nani? Brigedia ni nani hasa? Awali ya yote ningependa kujua wasifu wa Brigedia Sule.

Yule jamaa aliyenikaribisha akaniambia, “Hilo litakuwa swali lako la kwanza!” Akageuka kwa jamaa aliyevaa miwani (inayomfanya arandane na Muammar Gaddafi kwa kiasi fulani) na kumwambia, “Mzee, unaweza ukaanza mahojiano.”

‘Mzee’ akaanza:

Mimi ndio Brigedia Sule Mudi Dowans kutoka Oman. Ni mfanyabiashara na muwekezaji. Lakini sipendi hulka ya ufanyabiashara au uwekezaji initawale au kunitangulia kila ninapokwenda. Napenda kuishi maisha ya kawaida kama binadamu wengine.

2. Na Tanzania umekuja kufanya nini? Bila shaka utakuwa umeguswa na yaliyotokea Gongo la Mboto siku chache zilizopita.

Kama nilivyosema, sipendi hulka ya utajiri initangulie. Naishi maisha ya kawaida kabisa. Hata wewe mhariri, nadhani unaishi maisha ya kifahari kuliko mimi. Kwa mfano, sasa hivi nimetoka Bangladesh ambapo nilikuwa nazurura tu kwenye mji wa Dhaka…

Naipenda Tanzania sana. Hasa maisha ya Watanzania wa kawaida. Niliamua kujifunza Kiswahili na Uswahili miaka ya mwanzoni ya 2000! Lengo hasa la safari zangu ni kuja hapa na kufanya yale ambayo vijana walalahoi wanafanya.

Safari hii nilikuwa nataka kuja na kujaribu kufanya umachinga pale Ilala. Yaani, nichanganyike kabisa na vijana wa pale Karume. Lakini kuna kitu kilinipa ghadhabu nilipowasili tu hapa!

3. Nini hasa? Adha za uwanja wetu wa ndege, hasa baada ya milipuko ya mabomu?

Hapana. Kila kitu kilikuwa shwari ndugu mhariri. Ndege yangu ilitua bila matatizo ya aina yoyote ile. (Akageuka na kuangalia sehemu ambapo nadhani ndege yake imeegeshwa.)

Safari hii nilipanga kuja kujaribu kuuza mitumba kwa wiki moja hivi ili nijifunze na kuona maisha halisi ya mtu wa kawaida wa Tanzania… Yaani, nina hasira hadi machozi yanaanza kunilenga!

Baada ya kutoka tu kwenye ndege rubani akanitaarifu kuwa jina langu limetapakaa kwenye magazeti ya hapa. Nilitaharuki kusema ukweli… kwa sababu siwezi kufanya kile kilichonileta hapa.

4. Kwani wewe ndio mmiliki wa Dowans? Au jina lako tu ndio linafanana na jina la ile kampuni, ndugu Brigedia?

Jina langu kamili ni Sule Mudi Al Nawadai Dowans. Dowans ni jina la ukoo wa Sultani ambapo mimi natokea pia.

Dowans ni jina la Kisultani. Lakini nimedokezwa kuwa kuna viongozi wawili-watatu wa Tanzania ambao wamepachikwa jina Dowans. Kuna “Azizi Dowans” na “Jay Kay Dowans”. Hawa watu siwafahamu na sijui wamelipataje hilo jina la Kisultani.

Kwa hiyo, ningependa Watanzania walitambue hilo: Mimi ndio Dowans! Hilo jina halina wingi wala umoja… I mean, it’s not like Azizi is a Dowan; or Jay Kay is a Dowan. And the three of us together make up Dowans.

Ni mambo ya ngeli tu ndugu mhariri… tehe-tehe-tehe!

5. Nadhani Watanzania wangependa kujua kama wewe ndio mmiliki pekee wa Dowans. Kwanini umejitokeza sasa hivi? Siku zote hizo wakati tunahoji wewe ulikuwa wapi?

Ebo! N’shakwambia mi’ ndio Dowans! Ukiendelea na huu upuuzi n’taanzisha varangati hapa halafu nchi nzima ikose umeme.

Kawaambie Watanzania kuwa nitatembelea mitambo ya kuzalisha umeme pale Ubungo, halafu nakipa. Nikiona upuuzi wowote ule kwenye tovuti yako mi’ nazima mitambo yote. Hadi ambayo siyo ya Dowans!

Kwa unyonge nikachukua makabrasha yangu na kurudi ofisini.

Tunamshukuru Brigedia kwa kutupa nafasi hii kutumika kama chombo cha kuwafumba macho Watanzania.

Makala zinazohusiana na haya mahojiano:

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 5 Comments

5
  1. Nimefurahia kusoma, walao imekuja kama “khadith” kuliko kudanganywa waziwazi.
    Hivi huyo Brigedia wamemlipa mahela mangapi tangu miaka hiyo ya 2009 ili akubali watumie anwani yake na jina la kampuni yake na kumhusisha yeye binafsi na kampuni yao? Maana akili yangu ya kipumbavu inanishuhudia kabisa kuwa mtu alitengeneza Kampuni Tanzania lakini ili kuifanya ikubalike na apunguze kelele, akatumia akili yake ya kusajili kwa jina la mtu mwingine ili apate faida kadha wa kadha alizokwishazipigia mahesabu, sasa mpango haukuenda kama ulivyopangwa, ndiyo anacheza “plan B” halafu si kwamba amemaliza, maana pepo la kutaka fedha na utajiri likikuingia, hutawaza kushindwa hata siku moja hata ikiwa unayofanya yatahatarisha uhai wa wengine, we lengo lako la utajiri tu ndilo unalotizama na kutaka litimie. Maandiko *Matakatifu* yanaposema “…shina la uovu ni kupenda fedha…”, hayaongopi, hata asiye mwamini anakubali!

  2. Subi, bahati mbaya mhusika alikuwa tayari kujibu maswali MATANO tu — kama kawaida kwa kujichanganya, kurudia-rudia mambo na kutuongepea waziwazi.

    Itatubidi tuchunguze wenyewe na kutengua mambo ambayo Brigedia ametuambia.

    1. Hyperkei, kila mtu nadhani ana mtazamo wake (?). Wengine tunamchukulia Brigedia Sule kama litmus paper tu; yaani, anatusaidia kufahamu kama hiki kimiminika tunachotaka kunywa kina tindikali au la.

      Wale wanaotaka kuelewa nini hasa mchangiaji wa kwanza anachozungumzia, basi mkipata muda peruzi kwenye hii makala ya Mwanahalisi iliyochapishwa tarehe 18 Machi, 2009:

      http://www.mwanahalisi.co.tz/mpango_kununua_dowans_waiva

      NB: Wakati yote haya yanaendelea, “pilot” amesizi nje kibarazani akipunga upepo… Pia, kwa wale ambao hawajaelewa: mhariri wa tovuti hii hakupata bahati ya kualikwa kwenye huo mkutano! Ni “satire” tu.

  3. Hofu yangu iko katika kuhamishia lawama na wajibu kwa Bwana huyo mgeni na tukawaacha wenyeji waliotupandisha mkenge wakipeta.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend