Nestory Fedeliko — wengi wetu tunamfahamu kwa jina “FeDë” — ni mchoraji katuni chipukizi kiumri. Lakini kwa upande wa kazi, utasamehewa ukidhani ni mtu ambaye labda mvi zimeanza kuota utosini!
Tulipata nafasi ya kumuhoji; kama ilivyo desturi yetu, tulimuuliza maswali matano tu. Tulichopata ni majibu mazuri na ya kina — tafadhali, usiruhusu uvivu ukuingie kwasababu mahojiano yanaonekana ni marefu. Kuna hadithi na visa vya hapa na pale vitakavyokufanya utabasamu na ucheke. Majibu mengine yatakukumbusha mbali. Mengine yatakushangaza. Bila kusahau, FeDë ameamua kutoa nasaha kuhusu fani ya uchoraji wa katuni na maisha kwa ujumla.
Nitakachokuomba ndugu msomaji ni kuwatumia marafiki zako haya mahojiano.
1. Tulipata nafasi ya kumuhoji Bw. Mkuki ambaye anadhani alianza fani yake ya designing wakati anachora-chora kwenye daftari la mazoezi wakati yupo shule. Wewe safari yako unadhani ilianzia wapi?
Awali ya yote nawapa pongezi Vijana FM kwa kazi yenu makini yenye lundo la manufaa kwa jamii nzima na hasa zaidi kwetu vijana.
Tukirudi kwangu; safari yangu ya sanaa… Nilianza uchoraji kabla hata sijawa na ufahamu wa kujitambua kuwa mimi ni nani katika hii dunia. Nilijitambua kuwa mimi ni FeDë — msanii, mchoraji — nikiwa tayari nimekwishaanza uchoraji kabla hata sijaanza ‘vidudu’ (chekechea).
Shughuli ramsi za uchoraji/usanii zilianza pale nilipokabidhiwa karatasi kubwa za “manila” na “marker pen” ili nitengeneze michoro ya kufundishia madarasani — wakati nipo darasa la tatu katika shule ya msingi Mianzini, Mburahati, Dar. Baadae nikahamia shule ya Nansio, Ukerekewe, Mwanza. Huko nako ‘kazi’ ya kuwachorea walimu iliendelea, ila kilichoongezeka ni ‘madili’ ya kuwachorea wanafunzi wenzangu ramani (kwenye somo la jiografia) na michoro mengine ya sayansi… kwenye madaftari yao; huku wakinilipa!
Rafiki yangu wa karibu zaidi, Yuda Magafu, alikuwa akitafuta ‘madili’ kwa wanafunzi wanaohitaji kuchorewa na kuniletea kazi; ninazichapa, tunapata pesa ya kununua mihogo n.k.
Sio kuchora tu. Pia wakati huo nilikuwa nina-rap na kucheza (dance). Rafiki na jirani yangu Godfrey Msilanga (yuko UDSM) nilimuacha Ukerewe akiendelea na kukata mauno kwenye kumbi na sherehe mbalimbali.
Mi’ nikaenda zangu Dar kuendelea na masomo ya sekondari.
Nilijiunga na shule ya jeshi Makongo, chini ya Mh. Kipingu enzi hizo, na hapo ndipo kwa mara ya kwanza nikakutana na somo la “Fine Arts” linafundishwa darasani! Nikawa najitahidi kutokosa hata kipindi kimoja cha “Fine Arts”.
Wakati huo huo, nilikuwa nikifanya sign writting (uchoraji wa alama na mabango) uswahilini. Hii nilikuwa nafanya kabla ya kwenda au baada ya kutoka shule… ili niweze kupata nauli ya kwenda ‘skonga’… maana wazazi ‘hawakuwa njema sana’ kipesa.
Katika pilikapilka hizi nikakutana na Salma Ndomi na Nathan Mpangala, ambao walinisaidia kwenye masuala ya uchoraji wa katuni. Kwa upande wa michoro halisia, nilikutana na walimu Dede Maeda na Stephen Ndibalema wa UDSM, kitivo cha Fine and Performing Arts (FPA); walinipa msaada mkubwa sana na nitaendelea kuhitaji na kuthamini msaada wa hawa wote!
Baada ya maisha ya shule nd’o nikajitosa rasmi katika kazi hii. Kwa huku Kenya namshukuru sana Gado! Huwa najifunza vitu vipya kila ninapopata nafasi ya kuonana naye.
2. Unaonekana bado bwa’ mdogo sana. Uko Nairobi sasa hivi; kwanini ulikimbilia huko? Nafasi zinazopatikana huko hazipatikani Tanzania?
Ndio. Kimuonekano na kiumbo ni bwa’ mdogo, ila kikazi ni bwa’ mkubwa!
Nimekimbilia Nairobi kwa sababu za kimaslahi zaidi, na kujiendeleza kisanaa pia. Nafasi zinazopatikana huku zipo Tanzania pia, ila tofauti kubwa ipo kwenye maslahi.
Na kuja kwangu huku… nilichukuliwa na kampuni yenye ‘maskani’ (makao makuu) huku (Nairobi). Waliamua kunihamishia Nairobi ili nifanye nao kazi kwa karibu zaidi. Bila shaka hii ni baada ya kuzipigia saluti kazi zangu za uchoraji!
3. Kama sikosei, nimeshawahi kuona sehemu ukijadili mipango yako ya kuingia kwenye “vikaragosi”. Unadhani vikaragosi hufikisha ujumbe kirahisi zaidi? Au ni changamoto tu ambayo unataka ujaribu…
Unajua kaka, katika maisha… ama mwili wako, usitegemee mkono wa kulia tu kwa kufanya kazi zako siku zote. Uwezeshe mkono wa kushoto pia, ili pale wa kulia utakapochoka, ama kupata jeraha na kushindwa kufanya kazi, basi wa kushoto uendelee; ili usikwame.
Nia ya kuingia kwenye vikaragosi (animation cartoons) ni kujikuza kisanaa na kuuwezesha mkono wangu wa kushoto. Na si kwamba vikaragosi vinafikisha ujumbe kuliko katuni ama viponzo. La hasha. Bali ni kutaka kufikisha ujumbe kwa njia tofauti na kwa walengwa wengine.
Kuna wanaopenda kupata habari kwa maandishi magazetini, vitabuni n.k. Kwa upande mwingine, kuna wasiopenda kusoma; wao hupenda kutazama runinga au kusikiliza redio. Hivyo, baada ya kuwa na hadhira ya watu wanaopenda kusoma kupitia magazeti na mtandao, sasa nataka niende kwenye kundi la pili la wanaopenda kuona na kusikiliza; na wao wapate kazi zangu kwenye runinga zao!
4. Katuni zako — hasa zile za Kiraka — zinavunja mbavu. Lakini mara nyingine katuni zako hugusia/hugusa siasa na wanasiasa. Nini changamoto zake? Umeshawahi kupata ujumbe wa kukutisha au vitu kama hivyo?
Sio siri, katuni za Kiraka… kila anayepata kuziona zinamshawishi kurudi kuzisoma tena na tena. Kuna shabiki wangu mmoja nikuwa na-chat naye, akaniambia katuni zangu zote nilizoweka kwenye blog yangu — hasa za Kiraka — amezihifadhi kwenye kompyuta yake. Ili siku asipokuwa na “internate” asikose kuzisoma na kuburudika!
Kwa upande wa katuni zinazogusia siasa, zina changamoto kubwa na si za kukurupukia tu. Kwanza inabidi ujue undani wa tukio lenyewe unaloenda kulifanyia mchoro. Ili uweze kukabiliana na chochote kitakachoweza kutokea.
Na ukichora bila kujua undani wa tukio basi utakuwa unaongopa na unapotosha jamii — na kazi ya msanii ni kuiokoa na si kuipotosha jamii.
Pia, uchoraji wake inabidi uwe na mbinu ama namna ya jinsi ya kujilinda au kujitoa katika uhusika kwenye mada zenye utata. Ni vizuri kujadiliana na wahariri kwanza juu ya kazi unayotaka kuifanya; endapo unakuwa na wasiwasi na kitu unachotaka kufanya.
Vitisho vipo na sidhani kama vitakoma. Ukikubali kufanya katuni za siasa jua umekubali kuingia vitani kwa hiari! Kwa hiyo hutakiwi kuogopa vitisho. Kama hujiamini ni bora usifanye kabisa katuni za namna hii. Cha muhimu ni kujua na kutambua mipaka na wajibu wako kama msanii. Kwa mfano, kesi ikiwa mahakamani hutakiwi kuchora, kwa maana utakuwa umefanya kazi ya hakimu. Kama utaichora basi itabidi iwe kwenye mwelekeo ambao hautaeta athari kwa
pande husika.
5. Hebu tupe mtiririko mzima wa jinsi unavyotengeneza/unavyochora katuni… kuanzia unapopata wazo, hadi unapoona hii itanisaidia kuwasilisha kile kilichopo kichwani kwangu.
Uandaaji upo wa namna tofauti kulingana na aina ya katuni inayoandaliwa. Kuna katuni za vituko; ingawa zina ujumbe, huwa nachukua matukio yanayotokea miongoni mwetu na kuyawekea ucheshi ndani yake. Kwa upande mwingine, kuna katuni kama zile za ‘Muungwana ni Vitendo’. Hizi huwa nachukua matukio halisi ambayo sio ya kiungwana.
Sasa, ‘Baba lao’… katuni za siasa, maoni na uchambuzi: Hapa, kama ni habari au makala, lazima nisome kwa undani na ikibidi nijue chanzo chake. Kisha nabadilisha yale maandishi, habari au makala na kuwa katika mchoro.
Sio lazima nipate habari mpya nd’o niandae katuni. Naweza kuchukua mlolongo wa matukio ambayo yalitokea kitambo na yana athari mpaka sasa, halafu nikayatengenezea katuni moja tu ya nguvu.
Kwa mfano, katuni ifuatayo:
Kwanza, inafaa ujue Mungu kaumba vitu viwili-viwili duniani; binadamu mume na mke, mikono kulia na kushoto, mwanga na giza, hatari na amani, n.k. Hivyo ukikosa kimoja lazima utapata kingine. Kama ukikosa mwanga, basi utapata giza n.k. Hivi ndivyo vitu nilivyofikiria wakati naandaa hii katuni. Je, nitaliwasilisha vipi hili katika mchoro na kugusa mwenendo wa maisha halisi ya wananchi na viongozi wake?
Nikapata jibu kwamba mwanannchi ni kama msafiri na kiongozi ni kama dereva/chombo chake cha kusafiria. Kwa hiyo, kazi yake ni kuchagua dereva wake na chombo kinachomfaa. Nilichofanya mimi ni kumwonesha kuwa huku kuna hatari na huku kuna amani. Sasa chaguo ni lake, achague moja: hatari au ama amani; kushoto au kulia. Kwa kuwa nauli ni yake, halazimishwi na mtu, na kelele za wapiga debe si hoja; muhimu ni usafiri.
Na ninaposema viongozi, naongelea viongozi wa aina nyingi; chama, jumuiya, mashirika, vilabu n.k.
Kama ulivyoona, maswali magumu raha yake ni kupata majibu ya kina. Tunamshukuru Bw. Nestory kwa kuchukua muda wake kutujuza mengi kuhusu fani yake na maisha yake binafsi. Tunamtakia kila la heri kwenye kazi zake, aendelee kufanya kazi kwa bidii ili afike mbali zaidi! Baada ya kufahamiana tutajaribu kuendeleza ushirikiano wa hapa na pale.
Pia, tunamuomba da’ Subi awe anatuwekea vituko vya Kiraka kama zamani.
Tovuti na makala nyingine:
Nimefurahi sana Vijana, nimejifunza kuwa Mbunifu, maana mmetumia ubunifu wa hali ya juu katika mahijiano haya pamoja na picha zilizomo.
Asanteni sana.
Hongereni wana VIJANA FM. 120%
BRODA UKO HOT MBAYA. JARIBU KUFANYA CARTOON MOVIES, ZINAZLIPA MBAYA. EAST AFRICA SIJAONA NANI ANAFANYA. KEEP IT UP BRO.
hongera kaka kazi zako nazikubali kaza buti kaka
Let me start with thanks to you guys finally I can say i know fede, Though I were expecting more on personal stuff
kijana upo juu,naamini miaka mitatu ijayo utakuwa level fulani nzuri kimaisha,plz keep it up.
Nimekupata kaka majibu yamekaa kwenye mstari, kazana, usichoke, kazi zimesimama. Poa 2ko pamoja….!!
upo swafi sana, kazi nzuri sana
kama kijana mwenzako, nakuunga mkono sana, nimefarijika.
piga kazi.umetulia.ila angalia hao wanasiasa wanaweza kukupoteza,ikibidi sana ipe kisogo, umri bado mdogo.wazee hawajatulia.kaza buti, kama alivyosema mkubwa hapo juu,baada ya aka zako kama tatu unaweza kuwa level nyingine…big up sana!
safiii kijana napenda sana katuni broooo keep it up
keep it up broo
bro uko mbele na ni mtu unaestahili kuwa mfano wa kuigwa kwa wanao chipukia kisanaa…kaza buti na timiza malengo yako kwa wakati kama ulivyopanga…bt ma advise ni kushirikiana na wasanii wenzako k.m masood wa kipanya na wengine, wakati mkono wakushoto ukiuzoesha kufanya kazi mbadala…keeep it up jombaaaa.(here UDOM)
pongezi kwako kijana kwa ajiliya ujuzi ambao ume uonyesha kwani hivyo ni vipaji hadimu hasa kwenye dunia yaleo. hi ni kutokana na vijana wengi kuwa wavivu kujifunza, kwahiyo wewe ni mfano wa kuigwa na watu wote hasa vijana kwamba wasibweteke wa kazane kujifunza fani mbalimbali. na waache kusifia wenzaotu na wenyewe wakazane.
kaka upo juu!,kweli fanya cartoon movies kama za wenzetu………..dah!,kip it up brodaa!
nalo wazo