Ni uchawi, nguvu za asili ama sayansi isiyoonekana?

Na Churchill Shakim | Julai 5, 2011.

Muda unazidi kwenda lakini bado tunaendelea kuvuta subira. Nimekaa chini ya mwembe pamoja na watafiti wenzangu, masaa takribani matatu yameshapita na hakuna dalili wale tunaotarajia kufanya nao kazi kutokea. Tunasubiri kikundi cha wanaume na vijana wa kiume kwa kuwa siku iliyopita tulikuwa na maongezi mazuri na wakina mama na wasichana mahali hapa hapa. Leo ni zamu ya kuongea na wakinababa wa jamii hii.

Chini ya mwembe tukisimuliwa mkasa.

Nipo nje kidogo ya mji wa Makeni katika kijiji cha Panlap, umbali wa Kilometa mia moja hivi kutoka Freetown, mji mkuu wa Sierra Leone. Mji wa Makeni upo katika wilaya ya Bombali ambayo inapakana na nchi ya Guinea, uwanda wa Kaskazini usio na milima kama ilivyo kwa mji mkuu.

Hali ya kungoja hainipi subira hata kidogo, bado nafikiria namna ambavyo tutamaliza zoezi letu maana siku ni chache na bado tutalazimika kusafiri tena kwenye maeneo mengine. Mara inakuja taarifa kuwa wanaume wamesusia kuja kushiriki mjadala. Kwanini? Hawaoni haja ya kuja kuongelea jambo lolote kwa kuwa hawashirikishwi katika vikao vyovyote vya maamuzi vinavyofanyika. Nasikitika lakini naelewa kuwa wana haki ya kufanya hivyo. Hata nilipomtazama Chifu wa kijiji akihangaika kutafuta watu, sikuona dalili yoyote kama kweli wanaume wangekuja. Alionesha kukata tamaa na hakuwa na nguvu ya kuwashawishi. Hata taarifa iliyotolewa awali na tarishi wa kijiji ‘town crier, haikutiliwa maanani.

Suala la wanaume kususia mkutano wala halikunishtua sana, japo lingefanya zoezi letu kuwa gumu. Lakini sio kwamba wanaume walisusa kuja kwenye mkutano, la hasha. Kulikuwa na jambo jingine zaidi.  Kilichoniacha na mshtuko hata kunisukuma kuandika haya ni hii habari iliyokuja baadaye. Si tu ilinishitua, lakini pia ilinitia uwoga uliochanganyika na udadisi. Nimesikia mengi kuhusu uchawi na nguvu za asili lakini hii, kwangu mimi ilikuwa ni ya aina yake.

Wiki moja kabla ya ujio wetu katika eneo hili palikuwa na msiba. Kifo cha mwanamama, ni sawa kusema ni msichana maana alikuwa kwenye umri wa miaka 30 na ushee hivi. Kiafrika bado ni kijana. Alifariki na kuzikwa Alhamisi ya wiki iliyopita. Leo yapata siku ya tano ambapo ndipo hasa patashika ilipoanza. Hii ni kwa masimulizi ya wenyeji, huku wakisisitiza kuwa jambo hili ni kweli, tena ni kweli hata kama sitaki kuamini.

Mzuka (spirit) wa mwanamke aliyekufa na kuzikwa umetoka kaburini na sasa unarandaranda hapo kijijini ukipiga kila mtu mbaya. Tayari watu kadhaa wamesharipoti kutokewa na marehemu, na wengine wamekiri kupigwa au kukabwa na kufanyiwa kila aina ya ukorofi ambao unasemekana kuwa ni malipizi hasa kwa watu wabaya au ambao walikuwa na ugomvi naye siku za uhai wake.

Hivyo, hali ya kijiji leo haijatulia maana kila mtu ana hofu ya kutokewa na kusumbuliwa. Mwanzo wenyeji wakisimuliana kwa lugha ya kwao Temne ambayo siielewi, kisha watafiti wenzangu Isatu na binamu yake wakibadili lugha na kuongea Krio, lugha kuu ya Sierra Leone ambayo pia siielewi. Lakini mvuto wa mshangao wa rafiki yangu Jeremiah ambaye pia haongei Temne, unanifanya na mimi kutaka kujua habari gani hii ambayo imeletwa na bibi mmoja mzee ambaye ametukuta tukiwa tumepumzika hapa chini ya mwembe katika uwanja wa kituo cha afya cha kijiji.

Baada ya maongezi yao, wananipa nafasi ya kufahamu kinachoendelea kwa Kiingereza. Wananiambia, hili ni jambo la kawaida kutokea hasa sehemu hizi. Si mara moja kusikia mtu aliyekufa amerudi tena na kufanya mambo ya aina hii.

But you can’t see this unless you have four eyes my friend,” anasema Jerry, napenda matamshi ya Kiingereza chake kilichochanganyika na Krio. Ananikumbusha Liberia. Lakini yeye ni rahisi kumwelewa.

Churchill, are you scared?

No, I’m just curious…

Nataka kujua nini kitatokea kama mzuka huo utaendelea kufanya vurugu.

Muda si mrefu, ndugu wa marehemu watawaomba viongozi wa ‘jadi’, ‘The Powerful People’, kuchukua hatua ili kuuondoa mzuka huo. The Powerful People wakiambatana na wanakijiji wanamwendea Chifu Mkuu ambaye anajulikana kwa Kiingereza kama ‘Paramount Chief’ na kumwomba ruhusa ili waweze kufanya kazi yao. Chifu anaridhia na msafara unaanza kuelekea makaburini ambapo kila mmoja anaruhusiwa kushuhudia. Nyimbo maalum zinaimbwa ili kuivuta roho ya marehemu aweze kurudi kaburini kabla ya kufanyika kwa tambiko linalojulikana kama Oburuteh kwa lugha ta Temne, ikiwa na maana ya kukamata ama kuondoa mzuka kutoka katika kaburi.

Shughuli inaweza kusitishwa kwa siku kadhaa kama mzuka hatakubali kurudi. Mara nyingine mzuka unajua kuwa unatakiwa kurudi na hivyo unaweza kugoma na kusumbua zaidi. Unaweza hata kwenda mji wa mbali na hata nje ya nchi. Tambiko lazima lifanyike ili kuomba mzuka uweze kurudi kaburini ndio kazi ianze. Mzuka ukirejea mtu mmoja ataweka mti upande wa kichwa juu ya kaburi kuuzuia usitoke.

Baada ya kufika kaburini, The Powerful People wanachimbua kaburi na kuutoa mwili huku watu wote wakishuhudia. La kustaajabisha ni kuwa, iwapo mtu huyo alikufa katika kifo ambacho hakupangiwa, hasa kutokana na sababu za kichawi ambayo ndio mara nyingi hufanya mzuka wake kurudi duniani, basi maiti yake itakutwa ikiwa katika hali nzuri.

Mwili wake unatolewa ukiwa haujaharibika isipokuwa kucha za vidole gumba vya miguu tu ndio zinaweza kuwa zimeoza, lakini vinginevyo mwili unatolewa kaburini kama alivyo mtu hai, isipokuwa haupumui na hata mavazi aliyovikwa siku ya kuzikwa hubaki bila kuharibika. Hata kama mwili huo utakuwa umekaa kaburini kwa muda mrefu bado haukutakuwa umeharibika.

Mwili unatolewa na The Powerful People wanafanya tambiko kwa kuukatakata vipande vipande huku wakitenganisha viungo. Cha kustaajabisha ni kuwa, mwili huo unatoa damu kama alivyo mtu hai, jambo ambalo si la kawaida. Haya yote hufanyika huku umati ukishuhudia.

Baada ya hapo vipande vya mwili huo huzikwa katika makaburi tofauti ili kuzuia usiweze kujiunga tena ama huchomwa moto na majivu yake hutawanywa.

Ajabu nyingine…

Majivu hununuliwa na wale wanaotaka kupata nguvu katika jamii, hasa wanasiasa na wafanyabishara wakubwa. Majivu huwaongezea nguvu na uwezo mkubwa wa kushinda katika siasa ama biashara. Hali kadhalika machifu hutumia majivu hayo kujiongezea nguvu katika himaya zao.

Simulizi zinanisisimua, na kadri ninavyouliza maswali ndivyo ninavyopata kujua mengine zaidi. Ni jambo la “kawaida” kusikia habari za mtu aliyekufa akiwa ameonekana kwenye kijiji kingine. Anaishi na kuendeleza maisha huko.

Habari ya mtu aliyehamia kijijini na kuishi kwa miaka kadhaa, lakini akiwa amekufa mahali pengine hadi siku alipoonwa na watu walioshiriki mazishi yake — ndipo alipopotea bila kujulikana amekwenda wapi.

Simulizi ya msichana wa Freetown aliyekuwa akitumiwa fedha na nguo na baba yake aliyefariki. Mtu mmoja kutoka Guinea, dereva, alikuwa akija kuleta barua na zawadi kila mara kutoka kwa baba. Hata siku msichana alipoomba aletewe picha ili aamini, ni kweli aliipata kama alivyoagiza ikimuonesha baba yake katika maisha mapya baada ya kifo.

Mwili unasisimka, nataka kujua zaidi.

Lakini kuna vijana nane na wanaume watano wamefika. Wanatosha kutufanya tuendelee na zoezi letu la utafiti. Tunataka kujua kuhusu vile wanavyoshiriki katika jamii yao. Ndicho kilichotuleta hapa.

Kabla ya kuondoka hapa, tutaenda tena kumuona Chifu Mkuu Massayeli Tham II wa himaya ya Makarie Gbanti, mahali anapotokea raisi mtawala wa sasa wa Sierra Leone, Ernest Koroma. Mtu mcheshi ambaye nilifurahi kuongea naye — anayesisitiza umuhimu wa elimu kwa wasichana. Lakini nikifikiria kile nilichoambiwa kuwa utawala wa Chifu una kikomo, na ni yeye na kundi la waliomwapisha cabal ndio wanajua siku ya mwisho ya utawala wake. Ikifika siku hiyo lazima ‘afe’. Anatembea, anatawala lakini anajua siku yake ya mwisho.

Narudi hotelini jioni ili niweze kuandika hadithi hii kabla sijasahau. Inanilazimu kusubiri mpaka saa moja wakati jenereta itakapowashwa hapa katika hoteli yangu ya Buya, 25 Lady’s Mile, Makeni. Lakini kwanza nampigia simu Edwinah kumpasha habari hizi. Yupo Bo, mji wa Kusini kwenye kazi kama yangu. Anashtuka, anakata simu na kunipigia tena lakini mimi nacheka sababu nafurahia Becks baridi. Loh! Jenereta imeishiwa mafuta…

Makala Nyingine:

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 7 Comments

7
  1. Hii kitu bado inaniumiza kichwa..hasa hapo kwenye suala la kamera ya kawaida haiwezi kukamata picha mpaka wataalamu waifantie sayansi yao. Kuna suala zito zaidi hapa, na hilo ni suala la tamaduni za nje na hizi zetu. Nadhani tukifanya utafiti, tutakuja kugundua kuna mambo mengi ambayo watu walishafanya, lakini tunakuja kuyashangalia leo hii wana teknolojia wa nje wakifanya.

    Hili pia linaweza kuamsha mjadala wa dini na maandiko yake matakatifu. Nadhani makama ya Mbwa wa Pavlov II iliamsha hili kwa kiasi kikubwa.

    Mfano, yesu aliyoyafanya hayakuwa mazingaombwe?, na je mtu mwingine leo hii akifanya aliyofanya yesu, si ataitwa mchawi au? haya ni mambo machache tu. Kila mtu na imani yake, lakini waafrika mmezidi kushabikia tamaduni za watu. Mtafiti kutoka nje anakuja kufanya reserach za tamaduni za kiafrika, anarudi kwao, anaandika kitabu, alafu anakuja kuwauzia, kweli baadhi yetu tumepotea.

  2. Ili uwe na uwezo wa nguvu za kichawi kwanza uwe na imani hiyo moyoni mwako.uamini matukio ya nguvu za giza.Mashetani. Lakini ukiwa na imani mbili huku unamwabudu mungu huku unatukuza uchawi.Basi utafanikiwa sehemu moja ya uchawi.Na kama utachoma matunguli na kumuludia mungu.utapata nguvu za ajabu..Mungu wa ajabu ana mambo mawili ukitubu na kumwamini yesu aliye hai atakusaidia katka maisha yako.Yesu anawapokea wenye dhambi.Biblia inasema hivi mwenye kufanya uchawi au uaguzi ishara za bahati au ulozi. au anayefunga wengine kwa kuwatakia maovu.au yeyote anaye wasiliana na pepo..au mjuzi wa kubashiri matukio.au anaye uliza habari kutoka kwa wafu.kwa maana mtu anaye fanya mambo hayo ni chukizo kwa mungu(KUMBU KUMBU LA TORATI 18:10-12) Sheria ya mungu ilipinga kabisa kuwasiliana na pepo.ALBOGAST NKOMEZI.MZA TZ

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend