Na Frederick Fussi
Je, vijana wana ajenda katika mchakato wa uandishi wa katiba mpya? Kuna hoja gani zinazoweza kuwasukuma kuona ulazima, uhalali na utayari wa mchakato huo sasa zaidi kuliko kipindi kingine chochote? Nitachambua…
Ushiriki wa vijana katika mchakato wa uandishi wa katiba mpya ya Tanzania unapaswa kuzingatia mambo makuu matatu. Jambo la kwanza ni kuwa, sio tu ushiriki wa vijana katika hili, isipokuwa vijana wanapaswa kuwa na ushiriki wa kimkakati.
Jambo la pili ni kuwa ushiriki wa vijana katika mchakato huu unazingatia ukweli kuwa tangu kuundwa kwa taifa hili la Tanzania, licha ya kuwa na katiba tano kwa vipindi tofauti, hatujawahi kuandika katiba mpya yenye kukusanya maoni na mahitaji toka kwa wananchi (vijana wakiwemo). Hivyo huu ndio wakati muafaka wa kubadilisha historia ya taifa.
Jambo la tatu ni kuwa, japokuwa jukumu la uandishi wa katiba mpya ni la makundi yote katika jamii na kwa upana wake linahusu vijana wa sasa, tusitegemee kuneemeka sana na katiba hii isipokuwa tu kama uandishi wake utalenga zaidi kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
Mambo haya matatu kwa upana wake ndio muhimu sana katika kuelezea ulazima, uhalali na utayari wa uwepo wa ajenda ya vijana katika mchakato wa katiba mpya.
Msingi wa ajenda ya vijana haupaswi kuangalia mahitaji ya sasa ya vijana tu, bali uangalie mahitaji ya muda mrefu ya taifa hili bila kusahau maboresho ya katiba ya sasa ambayo hayategemei sana na yasingesubiri uwepo wa katiba mpya. Kwani kuna namna na taratibu ambazo zina uwezo wa kufuatwa kutimiza maboresho hayo.
Uhalali wa ushiriki wa vijana katika uandishi wa katiba mpya haujengwi na dhana kwamba lazima vijana washiriki ati kwa kuwa wao ni wengi kwa idadi ukilinganisha na makundi mengine, kwa mfano wazee na watu wazima. La hasha!
Uhalali wa ushiriki wa vijana katika uandikwaji wa katiba mpya utajengwa na utayari wa vijana katika kuainisha na kuweka bayana mtazamo wao juu ya maendeleo endelevu.
Mkakati wa ushiriki wa vijana unapaswa kuweka bayana ajenda ya vijana kwa Tanzania ya sasa na ile ijayo — Tanzania ambayo inatamaniwa na kundi la vijana lakini sambamba na makundi mengine yote.
Lakini yote yatafaulu ikiwa vijana watafaulu kuzungumza lugha moja ya kimaendeleo katika kusaidia kufikia utambuzi wa mambo ya msingi ya kuwekwa katika katiba mpya.
Mkakati wa ushiriki wa vijana unatakiwa kuzingatia mabadiliko chanya ya moja kwa moja, bila kutazamia faida za haraka haraka. Kwa mfano, mabadiliko ya moja kwa moja ni yale yatakayoleta tumaini jipya katika fursa sawa ya utoaji wa elimu kwa kila Mtanzania kisheria.
Katiba mpya itakuwa jibu pale ambapo katiba hiyo itahakikisha elimu inatoa mwanga kwa Watanzania kutoka katika giza nene la ujinga; tofauti na ilivyo hivi sasa. Elimu ambayo itatoa suluhu kwa zaidi ya vizazi vinne vijavyo vya Watanzania tofauti na hali ilivyo hivi sasa.
Elimu sahihi kwa watoto wa Taifa hili na ile iliyo bora kwa upana wa neno hili na maana yake halisi kama ikishikiwa bango na vijana ni moja kati ya sehemu ya ajenda ambazo zitabadilisha historia ya taifa hili. Na historia hii sharti ianze kubadilishwa sasa na sio wakati mwingine.
Ajenda sahihi ya vijana katika afya kwa mfano; ndio msingi wa mambo yote katika ustawi wa jamii inayojitambua vyema. Afya kwa ujumla wake inagusa sehemu nyeti za maisha ya kila siku ya wananchi mathalani, chakula na lishe bora, malazi na mavazi.
Mambo hayo matatu — chakula bora, malazi na mavazi — yakipatikana kwa wingi na ubora wake, husaidia kujenga jamii yenye afya tele. Jamii ambayo itatumia sehemu kubwa ya muda wake katika uzalishaji wenye tija.
Maradhi ni sehemu ndogo ya afya isipokuwa inakuwa nyeti pale afya ya wananchi inapokuwa duni na watu walio wengi kushindwa kupata chakula bora, malazi bora na mavazi bora. Ukiachilia mbali ajenda ya elimu bora na afya bora, yapo maeneo mengine nyeti kwa ajili ya mustakabali wa maisha ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Asasi ya TYVA ikiwa moja ya asasi za kiraia za vijana hapa nchini ilipata kuratibu zoezi la kuandaa Ajenda ya Vijana 2010, ikishirikiana na asasi nyingine za vijana. Juhudi hizi zilianza tangu mwaka 2004, pale TYVA iliposhiriki katika kukusanya maoni ya vijana ili yaingie katika MKUKUTA I mwaka ule wa 2005.
Juhudi hizi ni pamoja na ushiriki wa TYVA katika kutoa maoni ya mabadiliko ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977).
Ajenda ya Vijana 2010 iliyotolewa katika uchaguzi mkuu mwaka 2010 na kubainisha maeneo ya ajenda kumi yaliyofanyiwa tafiti ikilenga kuishawishi serikali kuzingatia ustawi wa vijana hapa nchini.
Ajenda ya Vijana 2010 inaweza ikawa ndio msingi imara wa kuibua hoja na maufaka wa nini ndio iwe ajenda ya vijana katika uandishi wa katiba mpya.
Malengo kumi ya ajenda ya vijana 2010 ni pamoja na madai ya vijana kutaka uanzishwaji wa baraza huru la Taifa la Vijana na utekelezwaji wa sera ya vijana.
Lengo la pili la madai ya vijana ni ongezeko la ajira kwa vijana na uboreshwaji wa mazingira ya kazi. Baadhi ya nchi kama Rwanda, Kenya na Uganda zimetaja bayana mifumo ramsi ya taasisi za kuwaunganisha vijana kama baraza la vijana ambalo kwa muda mrefu limeombwa pasipo mafanikio.
Lengo la tatu ni kuidai serikali iboreshe utoaji wa elimu bora na kuwezesha mabadiliko ya mfumo wa elimu. Katika lengo nambari nne, ajenda ni kudai ongezeko la ushiriki wa vijana katika vyombo vya maamuzi na michakato mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Wakati lengo la tano ni kuidai serikali kuchochea maendeleo ya michezo na utamaduni wa Tanzania kuanzia ngazi ya wilaya. Lengo la sita ni kuitaka serikali iboreshe na kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa vijana. Lengo la saba ni kuitaka serikali kujenga utawala bora na uwajibikaji.
Lengo la nane la ajenda linaitaka serikali itakayo hakikisha umasikini unapungua na kipato cha kila kaya kinapanda. Pia katika lengo la tisa serikali itakayowekwa na wananchi sharti iweze kuboresha ustawi wa vijana wenye ulemavu. Lengo la kumi ni kuitaka serikali kuwa na sera ya kimataifa yenye ufanisi na kuhusisha jamii kwa upana wake.
Malengo haya yaliainishwa baada ya utafiti wa hali ya vijana nchini tangu mwaka 2004 mpaka 2010 yakizingatia mahitaji na matarajio ya vijana ndani ya kipindi cha miaka 5 na zaidi kupitia uwezeshaji wa serikali iliyochaguliwa mwaka 2010.
Naona huu ndio wakati muafaka wa kurejea na kutafakari yaliyomo katika ajenda hii ya vijana na kuamua kuwa na muafaka wa kitaifa kama vijana juu ya ajenda ya kuisimamima iwe ipi hasa katika katiba mpya ya Tanzania. Mijadala inaweza kuendelea na tukapata suluhu ya ajenda yetu ndani ya katiba mpya ya Tanzania.
Wakati ni sasa. Ni muhimu sana kwa vijana kuweka tofauti zao pembeni — mathalani tofauti za kiitikadi za kisiasa — na kuungana pamoja kuhakikisha wanang’amua ajenda zao kama kundi na kuzisimamia ipasavyo katika mchakato unaoendelea kuelekea uandikaji wa katiba mpya nchini.
Makala nyingine iliyoandikwa na F. Fusi:
Frederick Fussi ni Katibu Mtendaji katika Shirika lisilo la kiserikali la TYVA. Baruapepe: frdmbimbi (at) yahoo (dot) ca; Blogu: www.frederick-fussi.blogspot.com