Na Frederick Fussi | Imeandikwa tarehe 14 Januari, 2011
Mwaka 2010 siku ya tarehe 26 Juni kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, nilikutana na marehemu Regia Mtema katika Mjadala wa Vijana (Dira Dialogue) ulioandaliwa na asasi ya Vijana Tanzania Youth Vision Association (TYVA) katika hoteli ya Peacock iliyopo maeneo ya Mnazi Mmoja katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Mjadala huo ulizaa maazimio ya kuwa asasi ya TYVA iratibu mchakato wa kuaanda ilani ya uchaguzi ya vijana, maarufu kama Ajenda ya Vijana 2010. Ilani hii ilijumuisha uchambuzi wa hali ya vijana Tanzania, na kuorodhesha matakwa ya vijana hapa nchini ili Serikali itakayoshinda uchaguzi mkuu mwaka 2010 iyatekeleze.
Marehemu Regia, alishiriki mjadala huu kama kijana shupavu wa Kitanzania, akiwakilisha kundi la vijana wenye ulemavu kupitia taasisi ya CHAWATA (Chama cha Walemavu Tanzania). Kipindi hiki nakumbuka Regia alikuwa mmoja kati ya viongozi wa CHAWATA.
Hivyo nilimfahamu marehemu Regia kama kijana mwanaharakati na mpambanaji asiyechoka kupigania kile anachokiamini. Kipindi hiki harakati nyingi alizokuwa akizifanya, alizifanya kupitia harakati za kudai haki za msingi za vijana wa Tanzania, hususan haki za makundi maalumu wakiwamo watu wenye ulemavu, watoto, wanawake na vijana kwa ujumla.
Harakati za kupigania haki alizofanya marehemu Regia zilizidi kudhihirika pale ambapo, baada ya mjadala wa Vijana, aliendelea kufuatilia utekelezaji wa maazimio ya mjadala ule. Jambo la ufuatiliaji wa utekelezaji wa maazimio ya mkusanyiko wowote ule hufanyika kwa nadra sana ila Regia alihakikisha utekelezaji unafanyika.
Nikiwa kiongozi wa TYVA, nilishirikiana na Regia na baadhi ya viongozi wengine wa Taasisi za vijana kama PHATA (Philosophy Association of Tanzania), SAVITA (Sauti ya Vijana Tanzania), UNA (United Nations Association) na JUVITA (Jukwaa la Vijana Tanzania) kutengeneza Ajenda ya Vijana 2010 iliyotokana na maoni na maazimio ya vijana katika mjadala ule.
Sehemu kubwa ya Ajenda ya Vijana 2010 iliegemea katika kuainisha haki na matakwa ya vijana hasa wa makundi maalumu mathalani walemavu ilifanywa na Regia Mtema. Hivyo ndiyo kusema kuwa ushiriki wa Regia katika kuandaa Ajenda ya Vijana 2010 ulikuwa mkubwa sana na wa kipekee.
Binafsi kama mwanaharakati, wakati tukiandaa Ajenda ya Vijana 2010, nilijifunza mengi sana kutoka kwa Regia. Moja kati ya mambo makubwa niliyojifunza kwake ni moyo wa ajabu wa kujitolea; kufanya kazi bila kujali kama atarudishiwa gharama zozote zile, moyo ambao vijana wengi wa Kitanzania hawana.
Alipopata fursa ya kuwa muwakilishi Bungeni, kupita Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema (CHADEMA), nimwambia sasa moja kati ya madai ya Ajenda ya Vijana 2010 imetimia kwa yeye kwenda kuongeza idadi ya Wabunge vijana Bungeni.
Ongezeko la wawakilishi vijana Bungeni, kama chombo cha maamuzi, ni jambo la msingi sana katika taifa changa kama Tanzania. Maendeleo ya Taifa lolote duniani yanategemea matumizi ya rasilimali watu, watu ambao sehemu kubwa ya wao hapa Tanzania ni vijana kati ya umri wa miaka 18 na 35, kundi ambalo Marehemu Regia alikuwa ndani yake. Nilimshauri Regia kuendelea na mapambano ya kusimamia utekelezaji wa Ajenda ya Vijana 2010 pindi awapo Bungeni, kazi ambayo aliendelea kuifanya vyema mpaka mauti ilipomkuta.
Ama kwa hakika, Tanzania kama Taifa limepoteza kijana shupavu, kijana shujaa na mpambanaji, kijana asiyelala, anawaza maendeleo wa watu wake. Wangapi kati yetu tuna moyo wa kuamua kujikana na kuamua kuwatumikia watu wengine? Regia alikuwa mmoja wa hawa watu.
Pamoja na harakati za kugombea na kushinda uchaguzi mkuu jimbo la Kilombero kutofanikiwa, alipatiwa fursa kwa kupitia chama alichoamini siasa zake na kuwa Mbunge wa Viti Maalumu. Nafasi ambayo alistahili kuipata kama mpambanaji hodari. Hapa naipongeza sana CHADEMA kuwa kutokosea katika maamuzi yake ya kumteua Regia kama mbunge wa Viti Maalumu.
Sitasahau harakati za kuanzisha taasisi ya maendeleo ya watu wa Kilombero, Kilombero for Change (K4C). Taasisi hii wewe mwenyewe Regia ulisema unataka iwe kwa ajili ya kuwakomboa wananchi wa Kilombero katika kona zote za maendeleo.
Ninapenda kutoa rai kwa familia ya Marehemu Regia, chama cha siasa CHADEMA, marafiki wa Regia, wapenzi wote, Watanzania wote na hasa wananchi wa Kilombero, kukuenzi kwa kuendeleza ndoto yako katika kuanzisha K4C, kuisimamia na kuiweka katika hali endelevu. K4C iwe ndio taasisi ya kumbukumbu yake marehemu Regia.
Binafsi nilishiriki baadhi ya michakato wa kuandaa taasisi hii. Nikiwa kama mwanaharakati kijana, nitaendelea kukuenzi kwa kusukuma mafanikio ya K4C, hii itakuwa ni njia sahihi ya kuendeleza jitihada zako Regia.
Ayubu katika Biblia Takatifu alipata kusema maneno haya, “Mtu ni mtoto tu wa mwanamke, huishi siku chache tena zilizojaa taabu, huchanua kama ua na kisha kunyauka, hukimbia kama kivuli na kutoweka. Siku za kuishi binadamu zimepimwa. Lakini mtu hufa na huo ndio mwisho wake, akishatoa roho yake anabakiwa na nini tena? Ee Mungu umeipanga idadi ya miezi yake hawezi kupita kikomo ulichomwekea.” (Ayubu 14: 1, 2, 10, 5)
Upumzike kwa amani rafiki yangu Regia…