Je wafahamu maneno asilia ya Kiswahili ambayo ni mbadala ya haya: damu, maiti, harusi, karibu, tafadhali? Ukiombwa utaje neno la Kiswahili lenye kumaanisha vinyweleo vilivyomo chini ya midomo ya wanaume, utasema nini? Matumizi yapi ya maneno ya Kiswahili ni sahihi? Fazaa au fadhaha? Huzuni au hudhuni?
Haya ni machache tu ambayo msomi wa lugha ya Kiswahili, hayati Salim Ali Kibao, aliyaeleza katika maongezi yake na wanahistoria yaliyorekodiwa mwaka 1995. Chondechonde msikilize.
Kila wakati huwa ninastaajabu nikisikiliza mawaidha kama haya. Mara nyingi yananifanya nisite kujieleza kwa wengine kuwa Kiswahili ni lugha yangu mama. Cha kusikitisha ni kwamba lugha hii inazidi kutenguliwa kadiri miaka inavyoenda. Katika uwanja na wakati huu tunalilia Kiswahili, ingali tunafahamu kuwa lugha kadhaa za kikabila katika ukanda huu wa Afrika nazo zinazidi kufa kila dakika. Lugha ndogo zinakufa kwasababu ya Kiswahili. Kiswahili halisi nacho kinakufa kwasababu ya matumizi mapya ya kurahisisha semi (pindi lugha inaposambaa, ikijumuishwa ukuaji wa matumizi ya Kiingereza na lugha ngeni nyingine). Mwisho wa siku mzungumzaji anayechimbuka katika maeneo haya angali mtu mzima atafahamu salamu za lugha ya kabila tu, ataongea Kiswahili hafifu (Swanglish), na kwenye Kiingereza matumizi yake nayo yatakuwa duni. Majanga matatu kwa mpigo! Jiulize, kizazi kitakachomfuata kitatumia lugha ipi?
Makala na kurasa nyingine:
Ningependa kukipendekeza kipindi cha ‘Ulimwengu wa Kiswahili’ kinachorushwa na TBC1 kila Jumanne saa saba mchana kwa wale wanaopenda kupiga msasa Kiswahili chao