Miongo mitano, uongo mtamu,
Uhuru ni wa mawazo, bila kumwaga damu.
Sura zetu bado vinyago, utumwa ndio adhabu.
Sisi twalima mahindi, wao wavuna almasi,
Rasilimali kwetu hadhi, yetu kimakaratasi.
Tumepangisha hadi ardhi, na hatuna hata samani.
Hapa kwetu tu watalii, chetu hakina thamani.
Hili shamba ni la babu, mimi bado kibarua.
Samahani kukukwaza,
Nipe nafasi tu kuwaza…
Tumepanda maembe, machungwa, na mananasi
Lakini miaka hamsini, bado hatuna nafasi
Kila tunda lina ukakasi.
Hili shamba la babu, matunda mbona hayaivi?
Tunanunua ujuzi, mashuzi, hadi maudhi.
Wanahamia kwa kasi,
Kushinda hata farasi.
Lugha zao mashuhuri,
Ya kwetu ni ya mihuri tu!
Tena kuonekana mahiri,
Tunasahau hata asili…
“Mimi hapana Swahili”
Twajivuna kwa ujasiri!
Tunajivunia ngao,
eti tulishinda ukoloni.
Twavumilia mgao,
maji yameisha mtoni.
Tunapanga maendeleo,
kwa msaada toka mbeleni.
Twawashukuru kwa senti,
Ukoloni mamboleo.
Tumelima, tumepanda,
wamemwagilia, wamevuna.
Tunasubiri bado mvua,
uchumi wasuasua.
Watendaji tupo likizo,
tunakula bila kupika.
Uzalendo sasa maigizo,
umaarufu kwenye luninga.
Lakini hadi lini
tutadanganyika kwa hotuba?
Shamba letu mashuhuri,
tunaibiwa bila bunduki.
Tumejaliwa rutuba
na rasilimali lukuki.
Kalamu yao mkuki,
watuchoma kwa maandishi.
Mikataba yao unafiki,
Watulaghai kwa pipi.
Tunalala usingizi,
tunasahau kudadisi;
Hili shamba la babu, matunda nani hufaidi?
Dah bonge la ujumbe shamba la babu mjukuu sina hisa