By Rebeca Gyumi (Si Mchezo magazine)
Kwenye Wizara Ya Vijana Utamaduni Na Michezo, kuna fungu linalotolewa kila mwaka wa fedha, lenye lengo la kuendeleza vijana chini ya “mfuko wa maendeleo ya vijana”.
Pesa hizi hupelekwa wilayani kama ruzuku kutoka serikalini kupitia kitengo cha maendeleo ya vijana, hutolewa kwa vijana kama mkopo, wenye masharti nafuu. Sio pesa nyingi kusema ukweli, kwa muda sasa wanasiasa, wanaharakati na mashirika mbalimbali wamekuwa wakilalamikia ufinyu wa pesa hizi ambazo kiukweli bado hazijaweza kupunguza ukali wa matatizo makubwa yanayowakabili vijana hivi sasa, nchini Tanzania.
Hili fungu lina shilingi ngapi?
- Ni jukumu la kila mkoa kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwenye mfuko wa maendeleo ya vijana.
- Kila mkoa unatakiwa kukusanya mapato kwa ajili ya kuendeleza shughuli mbalimbali za mkoa.
- Mapato haya hutokana na vyanzo vya ndani ya mkoa.
- Pia kuna fungu (ruzuku) ambayo hutoka serikalini kwenye wizara mama ya vijana, ambayo hutangazwa kila mwaka wa fedha. Fungu hili huwasilishwa kwenye mkoa husika kisha kupelekwa katika kila wilaya, kitengo cha maendeleo ya vijana.
Kazi ya fungu hili ni ipi?
- Kusaidia vijana au vikundi vya vijana ili waweze kujiajiri kupitia shughuli za uzalishaji mali na miradi ya kiuchumi.
- Kupunguza ukali wa maisha kwa vijana ili kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira.
Masharti ya fungu hili
- Spesho kwa ajili ya wanawake na vijana.
- Hutolewa kwa vijana kwenye vikundi lakini hata kijana mmoja mmoja anaweza kupewa ilimradi atimize masharti.
Ushauri
- Usikate tamaa, tembelea ofisi ya maendeleo ya vijana, zipo kwenye kila wilaya na tafuta taarifa sahihi kuhusu mfuko huu.
- Ukifanikiwa kupata pesa hizo kuwa mwaaminifu hasa katika kutumia fedha hii kwenye kujikwamua na ugumu wa maisha.
- Pendelea kutembelea ofisi za vijana, hakuna malipo.
- Nidhamu na uadilifu katika kutumia mikopo hiyo likiwemo suala la kurejesha kwa wakati mikopo hiyo.
Swali: Je, unadhani pesa inayotolewa inaweza ikakidhi mahitaji ya vijana ? Jibu ndio au hapana na kwanini.
This article was originally published in Femina HIP’s Si Mchezo magazine (May-June 2013, No. 66, page 28). Download the issue here.