Makala ya Kiingereza imeandikwa na Chimamanda Adichie na kutafsiriwa na Bahati.
Mwandishi maarufu wa riwaya kutoka Nigeria Chimamanda Adichie amekuwa mwandishi mwingine mkubwa kutoka Afrika kuzungumzia hili suala la sheria zinazopinga haki za mashoga. Nigeria anapotoka Adichie wamepitisha sheria kali inayopiga marufuku ushoga. Hapa Tanzania mjadala wa kupinga haki za mashoga ulilipuka tena majuzi baada ya mahojiano ya rais Kikwete na Christian Anampour aliyemuuliza rais kama Tanzania ipo tayari kukubali kuwapa mashoga haki zao.
Chimamanda amelizungumzia suala hili kwa kutoa mtazamo mwingine, tofauti na mitazamo mingi ambayo imejaa jazba na mihemko. Chimamanda anajenga hoja muhimu, hoja zinazochokoza fikra zetu. Adichie anataka tuangalie mitazamo mingine. Jamii yoyote inayoshikilia mtazamo mmoja bila kupanua mawazo kwa kuangalia mitazamo mingine, ni jamii itakayobaki hapo hapo ilipo kama maji yaliyotuwama na tunajua athari ya maji yaliyotuwama.
Nitajaribu kutafsiri alichokiandika Adichie kwa kadri ya uwezo wangu, kama ifuatavyo:
Sheria mpya inayofanya ushoga kuwa ni kosa kisheria inaungwa mkono na Wanigeria wengi. Lakini sheria hii inaonyesha kufeli kwa demokrasia yetu, kwasababu kielelezo kimoja cha demokrasia ya kweli si uongozaji wake wa walio wengi bali ulindaji wa wachache – au la sivyo uchukuliaji sheria mkononi utachukuliwa kama ni demokrasia. Hiyo sheria ipo kinyume na katiba, na haipo wazi, na inatoa kipaumbele kwa suala moja kwenye nchi ambayo ina matatizo mengi makubwa zaidi. Kati ya yote si sheria ya haki. Hata kama hii haikuwa nchi yenye matatizo ya umeme, nchi yenye wanachuo wanaomaliza masomo bila kuweza kuandika na kusoma vizuri na nchi isiyo na wananchi wanaofariki kwa magonjwa ambayo yanaweza kutibiwa kirahisi au isiyo na kundi la kigaidi la Boko Haram linalo uuwa halaiki ya watu, hii sheria bado ingekuwa sio ya haki. Hatuwezi kuwa jamii ya haki, mpaka tutakapoweza kukubali tofauti zetu. Tunaweza kutoelewa ushoga, tunaweza kuona ushoga ni kinyaa lakini hatuwezi kukabiliana nao kwa kufanya ushoga ni uvunjaji wa sheria.
Uhalifu (crime) ni uhalifu kwa sababu fulani. Uhalifu una mwathirika. Uhalifu hudhuru jamii. Hivyo, ni kwa vipi ushoga ni uhalifu? Watu wazima hawadhuru jamii jinsi wanavyopenda na wanaowapenda. Hii sio sheria ambayo itazuia uhalifu, lakini itakayochochea ukatili, na tayari, katika sehemu tofauti za Nigeria, kumetokea kushambuliwa kwa watu wanaoshutumiwa kuwa mashoga. Jamii yetu ni jamii ambayo wanaume wanaonyeshana wazi mapendo baina yao. Wanaume wanashikana mikono. Wanaume wanakumbatiana. Sasa tuanze kuwafunga marafiki wanaotumia chumba kimoja cha hoteli, au wanaotembea pamoja karibu karibu? Tuna amua vipi haya kwenye sheri?
Wanigeria wengi wanaunga mkono sheria hii kwasababu wanaamini Biblia inapinga ushoga. Biblia inaweza kuwa msingi wa namna tunavyochagua kuishi maisha yetu, lakini haiwezi kuwa msingi wa upitishwaji sheria, sio tu kwasababu vitabu vitakatifu vya dini mbalimbali havina maana kwa Wanigeria wote, lakini kwasababu tafsiri ya maandiko ya vitabu vitakatifu hueleweka na kutafsiriwa tofauti na watu tofauti. Biblia kwa mfano inapinga uasherati, uzinzi na talaka, lakini hivi vyote sio uhalifu.
Kwa waunga mkono wa sheria hiyo, inaonekana ni kama kuna kitu kinachotofautisha ushoga na kila kitu kingine. Hisia ya ushoga kutokuwa ni kitu cha kawaida. Kama sisi ni kundi la watu wengi, tunatabia ya kufikiri wengine waliokuwa kwenye kundi la wachache si wakawaida, sio kwasababu kuna kosa wamefanya, lakini ni kwasababu tumefafanua ‘kawaida’ kuwa sisi tulivyo na kilichokuwa tofauti na sisi ni kisicho cha kawaida. Lakini hatuwezi kutunga sheria ya dunia ambayo haipo: ukweli ni kuwa sisi binadamu tupo tofauti,viumbe vyenye mchanganyiko mbalimbali. Moja kati ya kipimo cha ubinadamu wetu, ni jinsi tunavyowafikiria wale waliotofauti na sisi. Hatuwezi – na tusifanye – kuhurumia wale tu walio kama sisi.
Baadhi ya waunga mkono wa hii sheria wameuliza – ni nini kinafuata, ndoa baina ya binadamu na mbwa? Au umeona wanyama wakiwa mashoga?’ (kuna tafiti zinazo onyesha kuwepo na tabia za kishoga baina ya wanyama.) Lakini, watu sio mbwa, na kukubaliana na hilo – kuwa mtu shoga anafanana na mnyama – ni unyama. Hatuwezi kupunguza ubinadamu wa binadamu wenzetu, wanaume na wanawake kwasababu ya namna na jinsi wanavyopenda. Baadhi ya wanyama wanakulana wenyewe kwa wenyewe, wengine wanatelekeza watoto wao. Hivyo, na sisi tufuate mifano hiyo pia?
Wengine wanaounga mkono wanasema kuwa wanaume mashoga wanalawiti watoto wa kiume. Lakini pedophilia na ushoga ni vitu viwili tofauti kabisa. Kuna wanaume wanaobaka wasichana wadogo na wanawake wanaofanya hivyo kwa wavulana wadogo, lakini hatuwadhanii kuwa wanafanya hivyo kwakuwa wao ni lijali. Ubakwaji wa watoto ni uhalifu mkubwa sana ambao hufanywa na wote, watu wazima walio lijali na walio mashoga (ndio maana huu ni uhalifu; kwani watoto wanahitaji ulinzi na hawajafikia umri wa kuweza kutoa ridhaa ya ngono).
Pia kumekuwa na misimamo ya kizalendo baina ya waunga mkono wa sheria hiyo. Ushoga sio Uafrika, wanasema, na hatutakuwa kama nchi za Magharibi. Lakini hata Magharibi pia sio sehemu salama kwa mashoga; tabia za kibaguzi dhidi ya matendo ya kishoga yapo sana huko Marekani na Ulaya. Lakini ni hili wazo la sio Uafrika ndio ambalo ni hatari. Wazazi wa Sochukwuma walikuwa wa kabila la Igbo, na alikuwa na bibi na babu ambao na wao walikuwa wa Igbo. Alizaliwa kama mtu anayevutiwa kimapenzi na wanaume. Wanaigeria wengi wanamfahamu mtu kama Sochukwuma. Mvulana aliyekuwa na tabia kama za kike. Msichana aliyekuwa na tabia za kivulana. Hawa ni watu tuliowafahamu, watu kama sisi, waliozaliwa na kukulia Afrika. Sasa ni vipi wao sio Waafrika?
Kama ni kitu chochote, ni sheria yenyewe ambayo sio ya Kiafrika. Inakwenda kinyume na maadili ya uvumilivu ambayo ndio sehemu kubwa ya tamaduni za Kiafrika. (Mwaka 1970 katika ardhi yaw a Igbo, Area Scatter alikuwa mwanamuziki mashuhuru, mwanaume aliyevaa kama mwanamke, aliyejipamba, na kusuka nywele zake. Hatujui kama alikuwa shoga – pamoja nadhani alikuwa – lakini kama angetumbuiza leo, angehukumiwa miaka kumi na nne jela, kwa kuamua kuishi jinsi alivyo). Huu mjadala sio mjadala ulioanza nyumbani (Afrika) lakini ni mjadala wa kijinga ulioanzimwa: tunafungulia CNN na kusikia nchi za magharibi wakijadili ndoa ya jinsia moja na sisi pia tukaamua, tutapitisha sheria ya kupiga marufuku ndoa ya jinsia moja. Nchi kama Nigeria ambapo katiba ipo wazi kuwa ndoa ni baina ya mwanamke na mwanaume, ni lini mashoga waliomba ndoa ya jinsia moja?
Mwisho wa kutafsiri.
Mijadala hii katika jamii yetu kama nilivyosema mwanzoni, imeonyesha kuegemea zaidi kwenye mihemko. Hili la kuhemka halinishangazi sana, kwani ni sisi hao hao ambao huemka na kuuwa mtu tunayesikia kaitwa mwizi, bila kuuliza, na kujua kama kweli ana hatia au la. Kwani katika mjadala huu mzima wa ushoga, tumejiuliza, upingaji wetu wa ushoga umetokana na tamaduni zetu, au dini zetu?
Kama ni dini zetu, je, Uislamu na Ukristo ulianzia Afrika au uliletwa tu kwetu wa wageni? Kama uliletwa na wageni, ni vipi leo tuseme ushoga ni tamaduni ya wageni, wakati wao hao hao ndio waliotuletea dini hizo tunazozitumia kupinga ushoga huu? Tamaduni zetu za Kiafrika zilichukulia vipi suala la ushoga kabla ya wageni kuja barani Afrika?
Haya ni baadhi tu ya maswali ambayo lazima sio tu tujiulize kwenye mjadala huu, lakini nadhani ni vizuri tukiwa tunajiuliza maswali kabla ya kuhemka. Rais Kikwete aliulizwa kuhusu haki za mashoga, na sio haki ya ndoa ya jinsia moja, sasa hamaki yetu kuhusu ndoa ya jinsia moja imetoka wapi? Lakini kati ya yote, mwenye ushahidi kuwa tamaduni yake ya Kiafrika (kabila) inasema mashoga wanyanyaswe, kupigwa na hata kuuwawa, tungependa kusikia kutoka kwake, na kama yupo baina yetu, basi aankaribishwa kurusha jiwe la kwanza.
Habari zaidi:
- Arizona, Marekani na muswada wa kuwanyanyapaa mashoga (CNN)
- “Chimamanda, are our differences not enough already?“(The Scoop)
- “Why the Nigerian anti-gay law will lead to the rise and acceptance of gay relations” (The Scoop)
- “Is Africa homophobic?” (Vijana FM)