Kadiri siku zinavyosonga, moyo wangu mweusi unasongwa na chuki na huzuni. Maumivu ya historia yetu bado ni kidonda kilichoanza kupona kwa juu, lakini chini linatunga usaha. Mateso ya kusaka uhuru ni mithili ya donda ndugu lisilo na tiba. Mustakabali wetu upo juu ya nani?
Nauona ukoloni unarudi. Kila siku natamani niwe kama Mandela, baada ya maumivu nitoe tu msamaha na kuanza upya. Lakini dharau za watu wengine zinachoma kama mkuki wa mmasai. Utamaduni wetu unaonekana duni, hafifu, haufai mbele ya macho yao. Akili zetu zinaonekana pungufu, eti kudidimia uchumi ni sababu ya rangi ya ngozi yetu! Umoja wetu unaonekana ni udhaifu, kama vile Imani yetu ina mapungufu. Ni kweli inawezekana kuwa pamoja na yote ya kale, binadamu tuwe wamoja, bila ya kujali rangi zetu?
Sifurahishwi na mengi. Uzalendo umepotea baina yetu wakazi. Ushabiki wa mambo ya nje umezidi. Ubaguzi wa rangi upo bado mioyoni mwa watu. Inakera sana kuona mzungu anathaminiwa zaidi yangu mimi ndani ya nchi yangu, eti ni mwekezaje apate likizo ya kodi!!! Nikizungumza Lugha ngeni naonekana mwerevu zaidi ya jirani yangu, na matakataka feki yanaonekana bora zaidi ya utamaduni wangu.
Hivi ni nani aliyetutumbukiza katika shimo hili? Sisi waafrika kweli tunajitambua? Na je tukijikubali, mstakabali wetu utabadilika?
Natamani ujasiri wa Mandela, na kujiwekea uhuru wa mawazo na akili zaidi ya ule wa mwili. Natamani fikra zetu za kitumwa zichomwe moto kwa kuvishwa matairi ya gari kama mkufu. Natamani nimwamini Nyerere, kua uhuru wetu ni wa kweli bila ya kumwaga damu. Na kua hatukua vibaraka vya mkoloni, uhuru wetu si wa bendera tu. Natamani mali zingekua za mwafrika kweli, hebu nioneshe ni nani anayemiliki mashamba makubwa ya chai huko njombe, au migodi ya almasi na uranium.
Tumedharauliwa kwa muda mrefu. Tumetemewa mate na tumeyafuta, lakini leo hii tunadiriki kusahau. Tunaacha watu wamwite Mandela gaidi, kisa amepigana na ubaguzi kugombania uhuru wa nchi yake! Tunadiriki kuwapa ardhi yenye madini bila kodi, mikataba ya miaka 99, bila hata kusutwa na nafsi zetu juu ya damu iliyomwagika juu ya ardhi hiyo, wazee walionyongwa kutetea nchi yetu na kupinga utumwa, tunadiriki kuwasahau na kuuza vizazi vyetu? Hivi kweli!! Tunadiriki kuwafundisha watoto wetu historia isiyo na mantiki, kua vita vya majimaji ni “rebellion against german government”, UASI! UASI! Katika ardhi yetu? Au ni kupigania uhuru ndani ya nchi yetu wenyewe. Kwani ni dhambi kudai uhuru wetu wa halali?
Natamani kupona makovu haya ya ukoloni. Natamani kuutukuza uzuri wa ngozi yangu, na ugumu wa nywele zangu. Kila siku roho yangu inapigana vita, ili ibaki kua nyeusi. Wengi tumekua pundamilia, ustaarabu umekua utumwa, sababu ya ukoloni mamboleo. Tunafikiri uhuru ni kujenga maghorofa, kuendesha range rover, na kubonga kingereza? Mwenge umezimwa na upepo wa rushwa na ubinafsi juu ya kilele cha Kilimanjaro, tamaa imemaliza ubinadamu wetu wote. Tumesahau tulipotoka. Tunatukuza wageni na kudharau wenyeji. Tunasubiri wafadhili waje kuijenga nchi yetu. Tunasubiri misaada ilipe mishahara yetu, na vitabu vyao vieleze historia yetu. Tutalala hadi lini?
Moyo wangu mweusi unazongwa na chuki na simanzi, chuki dhidi ya ukoloni na ukoloni mamboleo. Ukoloni endelevu uliopo chini ya mwavuli wa misaada, wahisani, wabia na wadau wa maendeleo.Lakini chuki kamwe haijengi. Ndugu zangu nifanyeje? Nikimuona Mugabe na vikwazo vyote nchini mwake, SANCTIONS. SANCTIONS! Suction – Unyonyaji tu! Mchezo wa nani mbabe, wa magharibi au sisi vinchi vidogo. Nimejawa na simanzi, simanzi kwa sababu dua yangu ya kuku haimpati mwewe, anafaidi tu vifaranga.
Lakini sikati tamaa. Mstakabali wa nchi yetu upo juu yetu. Tusisahau historia yetu, ubora wa nchi yetu kabla ya ukoloni. Na kiu yetu ya kujikomboa hadi tukapata uhuru. Tusisahau sababu ya mapinduzi yetu, ujasiri wetu hadi kuondoa utumwa nchini mwetu. Tusisaha mateso waliyopata babu zetu. Tusamehe, tena bila kinyongo, lakini hata siku moja tusidiriki kusahau, ili tusifanye makosa. Mstakabali wetu upo juu yetu. Uhuru wa watoto wetu upo ndani ya mikono yetu. Tusisubiri msaada, hisani ya watu wa nchi Fulani ije kutuletea maendeleo endelevu.
Eti tunasubiri atupe samaki, au atufundishe kuvua samaki ili tusilale njaa; tunachosahau ni kwamba hili bwawa ni la kwetu, tutege nyavu, kamwe hatutakufa njaa.
Very mooving piece, I love the way it flows especially on the structure of your ideas. But most of all, the message was the peak of the work. Keep writing and sharing dear, change always begin with a single step and it begins with you and me. (Interesting Bio) hope to read your book someday. Keep inspiring young artists. God bless you. Zu.
Napenda jinsi unavyouliza maswali ya msingi ndani ya hii makala.
Yamenipa changamoto ya kuyafikiria kiundani zaidi. Asante sana Neema.
Thats a very interesting piece of education…! Hakika inasikitisha kuona sasa sio kuomba tu bali tumeanza kulilia misaada kwa kuwa tumefungwa minyororo ya ukoloni na hatuamini kama tunaweza kujitegemea kwa kuvuna kutoka katika ardhi yetu na kutumia rasilimali zetu tulizopewa na Mungu katika ardhi yetu na kujitegemea. Hongera Neema kwa kutupa elimu nzuri