Barua ya wazi kwa wahitimu wa chuo

Salamu kwa wahitimu wote mliofanikiwa kumaliza chuo mwaka huu.

Kwanza poleni kwa kazi kubwa mlioifanya, hakika kumaliza chuo kwa kiwango cha degree ni ndoto ya vijana wengi, kwa juhudi zenu na kwa baraka za Mola mmeweza kumaliza salama.

Ila kuna kitu kidogo ningependa kuongea na nyinyi, ni kuhusu maisha mapya ya huku mtaani.


Huku mtaani mnapoingia ni tofauti na chuo, maisha ya mtaa kamwe usifananishe na chuo.

Downtown Dar-es-Salaam. Picha na Peter Mitchell (Unsplash).

Huku mambo magumu kidogo zaidi ya chuo, huku unatakiwa kuishi kwa busara na hekima zaidi ili uweze kutimiza malengo yako uliyotoka nayo chuoni.

Acha kuishi yale maisha ya nadharia uliyokuwa unayaota kipindi upo chuo. Sasa ni wakati wa kuishi uhalisia, uhalisia ambao unaweza kuwa mchungu. Usishangae mambo mengi yakienda tofauti na ulivyodhania au kupanga kipindi upo chuo.

Yule mjomba aliyekwambia mtumie CV ukimaliza chuo tu anakuajiri, usishangae akikuzimia simu. Wale marafiki uliokuwa unakula nao raha, usishangae usipowaona tena. Utakuwa nyumbani na bibi yako, akiwa na matumaini kesho unaingia kazini ili uweze kununua yule ng’ombe aliyemuuza ili kukusomesha.

Utakuwa wewe na familia yako, huku wakitegemea makubwa kutoka kwako. Kwa bahati mbaya huku mtaani ni gombania goli, kila mtu anatafuta nafasi ya kuajiriwa ili aweze kusaidia familia yake.

Achana na yale maneno ya “bila milioni sifanyi kazi”. Labda nikwambie tu, huku kuna watu wana degree kama yako na wana miaka mitatu hawana ajira.

Ogopa sana kukaa nyumbani bila kufanya kazi au chochote kile. Jitolee maofisini, jiajiri, fanya biashara au kitu kile ambacho kitakuwa msaada kwako na familia yako.

Fanya kile kilicho mbele yako, huu ndio utakuwa mwanzo wako mpya. Katika shughuli utazozifanya ndio zitakupa connection na kukutanisha na watu, ukifanya kazi nzuri, watu watakuona na kutambua uwezo wako.

Kila utakapo pata nafasi, tumia nafasi hiyo, hata kwa mshahara mdogo. Jaribu kuonyesha uwezo wako, kazi nzuri inajiuza. Ikitokea nafasi yoyote, hakika utakuwa wa kwanza kupigiwa simu na watu wanaojua uwezo wako.

Kamwe usifiche kile unachoweza kufanya. Onyesha uwezo wako, hakikisha kila mtu anajua kile unaweza kufanya, ili ikitokea nafasi uwe wa kwanza kufikiliwa.

Jaribu kuwa msaada kwa familia kwa kipindi hiki unasubiri ajira. Usiwe mzigo nyumbani. Umiza akili, fikiria, epuka kukaa nyumbani bila kazi yoyote ile, ikitokea umekaa nyumbani, basi kaa kwa faida.

Kwa bahati mbaya kaa ukijua, ukituma CV ni “only shortlisted candidates will be contacted”. Na hili pia lisikuvunje moyo.

Previous ArticleNext Article
Leonce Godfrey has been in the field of Digital media and digital marketing with more than 3 years experience working in various capacities with highly reputable companies and organizations. He is writer, storyteller, content creator, photographer and journalist by professional. He simply amazing.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend