Richard Nchimbi, kwa jina la sanaa anajulikana kama Mucho Flows ni msanii wa muziki wa kizazi kipya akiwa tayari na “Extended Play (EP)” album moja ambayo inapatikana mitandaoni kote.
Nilipata muda wa kuongea nae na kumuuliza mswali machache vile anatumia mitandao ya kijamii na mitandao mingine ya digitali katika kazi zake za sanaa;
1. Mitandao ya kijamii imekusaidia vipi?
Mitandao ya kijamii imenisaidia kuweza kuwafikia na kunikutanisha na watu mbalimbali, kama vile mashabiki, wasanii wakubwa na wadau wa mziki wengine ambao walivutiwa baada ya kuona kazi zangu katika mitandao ya kijamii.
Pia nimeweza kutangaza kazi zangu kwa kutumia mitandao ya kijamii. YouTube, Instagram na WhatsApp ni kati ya mitandao ambayo imenifanya niwezekusambaza kazi zangu bila mipaka na kwa gharama nafuu. Hivyo kutumia mitandao hii imenifanya niweze kuwafikia watu wengi sana.
2. Challenge gani kubwa ya mtandaoni ambayo umewahi kushiriki na ikakupa mafanikio makubwa?
“Da Vinci Code Freestyle Challenge” chini ya msanii mkubwa wa HipHop, Nikki Mbishi, na Wanene Tv ni kati ya challenge ambazo nimewahi kushiriki na kunipa mafanikio makubwa baada ya kuwa kati ya wasanii tano bora tuliofanya vizuri katika ile challenge.
Challenge ile ilienda na hashtag #DaVinciCodeFreestyleChallenge ilinipa nafasi ya kufanya kazi na Nikki Mbishi pamoja na Wanene Tv.
3. Changamoto gani unayoipitia kama msanii katika matumizi ya mitandao kijamii na digitali kwa ujumla?
Kuna changamoto kwenye sera za nchi juu ya matumizi ya mitandao kama vile ya kutakiwa kusajiri YouTube Channel kwa 500,000 ambayo ni ada kubwa kwa sisi wasanii wachanga.
Gharama za vifurushi vya internet ya mitandao ya simu na kasi yake, ingawa sio kikwazo kikubwa kinachoweza kufanya kazi isifanyike.
Pia kuna watu wengine huko mtandaoni huwa hawachukulii mambo kwa uzito, wanadharau kazi zetu na muda mwingine unaweza kupokea jumbe zinazokatisha tamaa.
4. Una malengo gani na matumizi ya kidigitali katika kukuza sanaa na mziki wako?
Lengo kubwa moja ni kuhakikisha natumia mitandao ya kijamii kukuza sanaa yangu kwa kuwafikia watu wengi zaidi.
Nataka kuwekeza sana kwenye “Branding” ya kurasa zangu za mitandaoni na kuhakikisha kazi zangu zote zinapatikana katika mitandao yote ya muziki kama vile YouTube, Audiomack na Boom Play.
5. Unawashauri nini vijana na wasanii wengine wa sanaa kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii?
Watumie vizuri mitandao ya kijamii kuleta matokeo chanya kwenye mambo wanayofanya. Mitandao ya kijamii inafaida sana kama ukiamua kuitumia katika kutangaza kazi zako.
Inaweza kukutanisha na watu wengi, pia kukupa soko la bidhaa yako kwa kukutanisha na wateja. Ni njia nzuri sababu inatumia gharama nafuu katika kufikia watu ukilinganisha na aina nyingine za matangazo, ni muhumu tu kuwa na njia sahihi na utaalamu wa kufanya mambo yako kwa uweledi na ufasa.
Unaweza kumpata Mucho Flows kupitia mitandao ya kijamii Instagram na kusikiliza kazi kupitia Audiomack na YouTube.