Adui yako ni yule unayemuona ukitazama kioo
Hakuna vita ngumu kupigana kama ile ambayo humjui adui yako, kila anayekuja maishani mwako unaweza kuona ndio kikwazo cha wewe kufanikiwa. Utawalaumu walimu waliokufundisha, utamaliza. Utawalaumu wazazi wako waliokulea, utamaliza. Utailaumu serikali pia, utamaliza.
Lawama hizi zote zinakuja sababu humjui adui yako wa kweli anayekukwamisha katika maendeleo yako.
Ukikaa na kutafakari kwa kina na kumjua adui yako wa kweli, utakuwa umepiga hatua kubwa kuelea mafanikio na malengo ya maisha yako.
Wengi wetu adui yetu mkubwa ni sisi wenyewe, ndio vijana wengi tunajichanganya sisi wenyewe. Kwa bahati mbaya hatujui wapi tunakosea na tunaishia kulalamikia watu na ndugu.
Naomba nikwambie hili: Uvivu wako ndio adui yako, kusubiri kwako kuchangamkia fursa ndio adui yako, kutojifunza vitu vipya na kushindwa kujiongeza kwenye taaluma yako ndio adui yako.
Ni nani alaumiwe kwa haya?
Usipojiongeza utamshika kila mtu uchawi kwa kuhisi unarogwa, utalalamikia watu kwa kuhisi unabaniwa kupewa nafasi, utahisi unaonewa.
Ila ukweli tatizo ni kutojua udhaifu uliopo ndani yako na kuufanyia kazi. Ni nani ambaye hana udhaifu ndani yake?
“KUJITATHIMINI” ni neno ndogo ambalo limebeba herufi chache zenye maana kubwa kwenye maisha yetu ya kila siku.
Kutojijua ni kitu kibaya sana. Ni adui mdogo kama sindano lakini maumivu yake ni makali mno apenyapo mwilini.
Mjue kwanza adui wa maisha yako halafu taratibu panga mipango ya kumwangamiza kwa kujijengea mazoea na akili mpya ya ushindi. Kila siku jifunze, ondoa uvivu kwa kufanya kazi, kwenye fursa jiamini na jiongeze usibaki nyuma.
Pale utakapojijua madhaifu yako ndipo utajua adui yako aliyopo ndani yako. Kila mtu ana yule adui ambaye anaishi nae, huyu adui anaweza kuwa vivu wako, uoga wako, ulevi wako, mazoea yako mabaya, na vitu vingine vinavyokurudisha nyuma kushindwa kutimiza malengo yako.
Swali, ni nani adui wa maisha yako?.
Ili upige hatua, unahitaji kumkwepa na kumkabiri adui yako. Niambie mdau wangu, adui yako ni nani? Umechukua hatua gani kumkataa?
Amka jiangalie kwenye kioo, aliyesimama mbele yako anaweza kuwa adui mkubwa wa maendeleo yako.
Usinyooshe kidole kwa serikali, watu au ndugu zako kuwa wanakubania usifanikiwe maana inawezekana adui yako ni yule unayemuona ukijitazama kwenye kioo.
Baada ya kujitazama kwenye kioo, moyoni unaweza jisemea “Mimi adui yangu mkubwa ni usingizi na uvivu wangu mwenyewe” na usishangae baada ya hapo ukarudi kulala huku ukiwaza ni nani anakubania mpaka hufanikiwi. Hivyo ndivyo tulivyoamua kuishi na adui zetu.
Picha na Denny Müller kwa kupitia Unsplash