Kitu rahisi unachoweza kufundishwa na waliofanikiwa ni kujikubali. Kuwa na imani na wewe mwenyewe kwanza, kwa kupenda unachofanya na kukithamini.
Hata kama hakuna anayekufuata nyuma, haimaanishi kuwa njia uliyochagua si sahihi. Kila mtu ni shujaa wa maisha yake mwenyewe.
Ni kwenye matatizo pekee ndipo mwanadamu hufahamu nguvu na uwezo ulio ndani yake. Usiyachukie.
Mungu hajawahi kumpa mja wake mzigo asioweza kuubeba. Linapokuja tatizo, furahi. Maana, wakati wako wa kuijua nguvu iliyo ndani yako umewadia.
Katika maisha kila mtu ana matatizo yake. Usisononeke na ukadhani Mungu wako amekuacha pekee yako kwa misukosuko ya maisha.
Katika maisha kila mtu ana matatizo yake.
Dhahabu ili ing’ae inahitaji kupita kwenye moto. Na sisi ili tufanikiwe tutapita kwenye moto huo. Tunahitaji kupita kwenye matatizo, tunahitaji kujaribiwa ili tushinde vita kuelekea mafanikio.
Ukidharauliwa, kuchekwa, kukataliwa na kutengwa basi jua unapitia kwenye moto ili uwe imara katika mafanikio yako.
Ukiona giza nene ujue asubuhi imekaribia kufika. Ukiona matatizo yanazidi ujue unakaribia “kukomaa” kuelekea kwenye mafanikio. Binadamu tuna tabia ya kumkwamisha yule mtu ambaye yupo kwenye njia sahihi, hivyo usisumbuke na kutingishwa na matatizo wala maneno ya watu.
Angani kuna jua na mwezi, vyote vina ng’aa kwa wakati wake. Unaweza usifanikiwe leo, usifanikiwe kesho na usione kabisa dalili ya kufanikiwa. Ila haimaanishi uache kufanya kile unachokiamini.
Shikilia hapo hapo, wakati wako wa kung’aa utafika na hakuna mtu atakayeweza kukuzuia. Amini katika unachokifanya na usikate tamaa juu ya ndoto zako ulizojiwekea.
Mafanikio ya marafiki na watu wako wa karibu yasikupe presha. Wao leo ndio jua na ni zamu yao kung’aa, usikate tamaa maana usiku utaingia na wewe utakuwa mwezi na utang’aa kama nyota angani.
Mimi naamini, kufanikiwa ni suala la muda tu. Kila mtu ana muda wake wa kufanikiwa endapo utajiamini na kusimamia zile ndoto zako ulizojiwekea.
Pia, usichoke kumuomba Mungu abariki kazi za akili na mikono yako. Asante.
Picha na Sebastien Gabriel kwa kupitia Unsplash