Maswali matano na Joseph Taifa

Joseph Taifa Sanga ni mhandisi na mwanzilishi wa Taifa Innovations ambao ni wavumbuzi na watengenezaji wa vifaa mbalimbali vya kibunifu vya teknolojia.

Tulipata nafasi ya kumuuliza maswali na haya ndio aliyotuambia kuhusu ubunifu, uhandisi na jinsi ya kuwa mtatuaji wa changamoto za jamii.

  1. Tuambie kidogo kuhusu Taifa Innovations

Taifa Innovations ni kampuni ambayo imeanza rasmi mwaka 2020 mwezi wa kwanza ikiwa imeanzishwa na kijana mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shahada ya kwanza ya uhandisi mitambo (2019).

Ni kampuni ambayo inajihusisha na ubunifu hasa kenye upande wa teknolojia, kwahiyo changamoto zote ambazo zinaisumbua jamii ambazo zinahitaji suluhisho la kiteknolojia basi Taifa Innovations ipo kwaajili ya kuzitatua changamoto hizo.

Kuna baadhi ya bidhaa ambazo Taifa Innovations wamehusika kuzifikiria (buni), kuzitengeneza na kuzipeleka kwa jamii ili kuweza kutumika mfano mashine za kunawia mikono, mashine za kukanda unga wa ngano, mashine za kusukuma chapati, kuna mashine kwa ajili ya mafunzo ya udereva lakini pia kuna vifaa mbavyo vinafugwa kwenye gari ili kuwawezesha watu wenye ulemavu wa miguu au watu wasiokuwa na miguu kuweza kuendesha magari, hivi vyote vinapatikana Taifa Innovations.

Pia Taifa Innovations tunafanya mafunzo ya namna ya kutumia softwares za design (kama Solidworks na AutoCAD) hasa kwa wahandisi mitambo, softwares hizo zinafundishwa hapa na kijana anafundishwa na ataweza kwenda kufanya kazi hizi za design vizuri baada ya mafunzo sehemu yoyote ya kazi.

Simulator, kwaajili ya mafunzo ya udereva wa magari. Mwanafunzi anajifunza huku akiwa amekaa na kuiona gari kwenye screen ila anaiocontrol kama gari.

2. Unapata wapi msukumo / hamasa ya kufanya ubunifu?

Msukumo wa kufanya ubunifu ulianza toka nipo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na hapo ndipo nilipoanzia kufanya ubunifu, changamoto ambazo zilikuwa zinatusumbua tukiwa chuo basi nilikuwa naweza kuzitatua ambazo zilikuwepo chini ya uwezo wangu.

Kwa mfano, kulikuwa na changamoto ya wizi wa nguo. Changamoto hii niliweza kuitatua kwa kutengeneza kifaa kwaajili ya kudhibiti wizi wa nguo kambani, kilifanikiwa kwa asilimia zote na sikuwahi kuibiwa tena nguo baada ya kutengeneza kile kifaa. Lakini pia nilitengeeza vifaa kadhaa ambavyo vilikuwa vinatatua changamoto ambazo zilikuwepo mazingira ya chuo.

Msukumo haswa wa kufanya ubunifu unaanzia darasani, namna ambavyo walimu wanatufundisha, namna ya kutatua changamoto mbalimbali, pamoja na kujiongeza mwenyewe kichwani basi unaweza ukatengeneza vitu ambavyo vinatatua changamoto.

3. Je unafikiri pesa ni changamoto kwenye ubunifu?

Pesa si tatizo kubwa kwenye ubunifu, ila ni kitu ambacho kinahitajika sana kwenye maswala ya innovations.

Kwa maana kitu cha kwanza unapofanya ubunifu tunasema kwamba kuna pesa ambayo unaichoma, inapotea ile pesa ya mwanzo huwa hairudi.

Sasa utahitaji uwe na pesa, ila sio pesa kiasi kikubwa ili uanzishe wazo. Ishu kubwa huwa ni wazo, je limekaa sawa? Lina tija? Ila pesa huwa ni kukuinua kwamba hicho kitu unachotaka kukitengeneza kitaonekanaje, mwanzoni unaweza toa pesa ya kutengenezea prototype lakini kama kifaa kinajiuza unaweza kupata pesa kwa wepesi.

Jambo kubwa ni tija ya hilo wazo maana unaweza pata hata watu watakaoweka pesa zao kwenye wazo lako, kikubwa tu ataangalia tija ya wazo na sio gharama za matengenezo.

Pesa si tatizo kubwa sana kwenye stage ya kuanzia, ishu tu hiyo idea unayotaka kuifanyia kazi iwe na tija.

Pesa si tatizo kubwa sana kwenye stage ya kuanzia.

Ikiwa na tija, hata mteja anaweza akaweka pesa awe wa kwanza kutengenezewa hiyo bidhaa hata kama hajaiona. Kama tija hamna ndio innovators tunatumiaga nguvu kubwa kuwaaminisha watu pia, kwahiyo kunahitajika gharama.

Kwenye ubunifu pesa sio tatizo kubwa ila inahitajika ili kukusogeza kwenye ubunifu wako, ishu kubwa ni tija ya wazo (innovation for impact).

4. Una ushauri gani kwa future engineers?

Kwa future engineers ninachoshauri ni kuwa tukae katika ku-innovate for impact, tusibuni tu kwamba ili tupate sifa tu ya kuwa aliyetengeneza kitu fulani ni fulani lakini tuangalie impact ya kile ambacho tunaenda kukifanya.

Tuangalie impact ya kile ambacho tunaenda kukifanya.

Tusiangalie tu ukubwa, tuangalie impact yake, kinaweza kikawa kidogo lakini kinaimpact kubwa. Si tu kwenda kujenga ndege wakati huku kuna vitu vidogo ambavyo vina impact vingeweza kutusaidia, na ndio pale unaweza kuwa na wazo kubwa sana ukashindwa hata pesa ya kuweza kuweka ili utengeneze hiyo innovation yako na watu wakaogopa hata ile pesa ya kuwekeza kwa pale unapoanza, lakini kwa kuwa na  mawazo madogo madogo lakini impact yake ni kubwa basi ndio hata sasa tunaona innovators ambao anafanya innovation kwenye vitu vidogo ila vinamlipa vizuri.

Mfano kifaa nilichokitengeneza cha kuzuia wizi kwenye kamba, kilikuwa ni kidogo sana kile kifaa lakini nguo tulikuwa tunaibiana sana, na mimi ile tabia nilikuwa siipendi kwahiyo kwangu kile kifaa kilikuwa na impact lakini pia kuna wengine walitaka niwatengenzee ili na wao wazuie kuibiwa nguo. Impact tayari imeonekana kwao, ila ni kifaa fulani kidogo sana, kidogo mno, wazo dogo lakini linafanya kazi.

5. Una mipango gani ndani ya miaka 5-10 ijayo?

Miaka 5-10 ijayo tunaiona Taifa Innovations ikiwa kampuni nguli au kampuni inayotegemewa kwenye kutatua changamoto zinazoisumbua jamii kupitia teknolojia.

Tunaamini kwamba tutaaminisha watu kupitia bidhaa zetu ambazo tunazitoa kwa maana ni bidhaa za uhakika, bidhaa ambazo zinapatikana kwa wepesi na kwa bei ambayo ni affordable na reasonable kwa watu.

Baada ya miaka 5-10 tutakuwa ni kampuni ambyo ni tegemezi kwenye maswala ya teknolojia, kampuni ambayo tunaona hata serikali inaweza kuitegemea kwenye maswala ya kiteknolojia kwasababu tunajitahidi kuleta bidhaa ambazo zinahitajika kutumika kwenye jamii, tutaendelea kufanya innovation for impact, tutabuni vitu vyenye uhitaji ili maisha yaendelee katika jamii.

Swali la nyongeza: Unadhani mambo gani yatatusaidia kukuza viwanda na ubunifu zaidi Tanzania?

Nadhani ili kuvuka kwenda upande wa uchumi wa viwanda ni muhimu kuangalia nini ambacho tunacho kwa sasa, nacho ni wabunifu na bunifu zao.

Kitu ambacho bado sijaona kikifanyika vizuri ni namna ambavyo serikali inathamini wabunifu na bunifu zao, hapo hakuna nguvu nzuri katika kuwaweka sawa na kuwasaidia.

Kujali wabunifu na bunifu zao ni jambo ambalo litatusaidia tusiwe na viwanda ambavyo havina ubunifu (yani viwanda vya ku-copy na ku-paste yale yanayofanywa nje).

Kwenye swala hili nafikiria kama kungekuwa kumetengwa eneo maalumu kwaajili ya wavumbuzi, kazi yao wao ni kufanya uvumbuzi kama vile timu ya mpira ilivyo kuhakikisha taifa linakuwa vizuri kwenye michezo, kwahiyo changamoto yoyote ikija eneo hilo lazima suluhisho lipatikane kwenye nyanja yoyote mitambo, umeme nk.

Kama ilivyo Sabasaba au Nanenane basi kungekuwa na kiwanja cha innovations, sehemu maalumu kwaajili ya wavumbuzi kukaa na kuumiza kichwa kuhusu ubunifu. Na pia hata akitokea mvumbuzi kwa sasa asipotee bila impact, bali Serikali isapoti wavumbuzi wakitanzania na vitu vyao wanavyobuni. Serikali iwekeze nguvu katika wavumbuzi wakitanzania, tuamini wavumbuzi na bidhaa za kiTanzania.

Lakini pia maonesho yawe mengi na yawe ya mara kwa mara, na maonesho yawe na impact, tukionesha vitu, basi baada ya maonesho kuna uwekezaji unatokea kwa wavumbuzi mfano kwenye kuiendeleza bidhaa nk. Kama tutafanya maonesho bila kuwa na matokeo chanya ya yale maonesho bado tunakuwa hatuendi mbele.


Taifa Innovations inapatikana Sido Dar es Salaam. Unaweza kuwapata kwa Instagram (@taifa_innovations), na Facebook (Joseph Taifa). Pia unaweza kuwapata kwa namba ya simu (0757 273 531) na email: (taifainnovations@gmail.com / josephtaifa@gmail.com)

Previous ArticleNext Article
Eunice is a multi-niche freelance writer with experience in writing health, lifestyle, finance, interviews, tech, travel, entrepreneurship, automotive, and mental health articles.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend