Tangu dunia iingine katika mfumo mpya wa sayansi na teknolojia, yapo mambo mbali mbali ambayo yamebadilika katika jamii yetu. Dunia hii sio ile ya miaka 20 iliyopita. Tena utandawazi umepanuka mno hivyo kuifanya dunia kuwa kama kijiji.
Kukua kwa utandawazi kumeleta mitandao mbali mbali ya kijamii na kuwaunganisha watu katika dunia hii ya leo. Lakini je unajua kuwa mitandao hiyo inafaida sana katika jamii inayotuzunguka? Mitandao kama vile Facebook, Instagram na Twitter, na Youtube imekuwa ikitumika katika maisha yetu ya kila siku. Mitandao hiyo imeleta manufaa sana katika jamii yetu. Ila tumekuwa tukiitumia mitandao hii kimazoea.
Kila siku tunafungua WhatsApp, halafu tunahamia Instagram. Tukiona hakuna mpya tunaenda Twitter halafu tunahamia Facebook. Tunazunguka katika mitandao hiyo pekee. Je wajua kuna mitandao mingi mizuri huko nje? Ndio, kuna mitandao ambayo unaweza kuitumia na kubadilisha kitu katika maisha yako.
Leo nimekuletea baadhi tu ya mitandao hii.
Mtandao wa medium umeanzishwa na Ivan Williams baada ya kufanikiwa kuwa mmoja wa watu waliounda Twitter. Akaja na wazo la kutengeneza mtandao wa kwake. Mtandao huu ukaitwa Medium, umetengenezwa mnamo mwaka 2012 ukiwa na malengo mbali mbali katika jamii.
Ni nini umuhimu wa Medium katika jamii? Mtandao wa Medium umejikita zaidi katika kuandika makala ya mambo ambayo yanaweza kukuletea mawazo mapya katika fikra zako. Mambo haya yanaweza kuwa halisi au sio halisi lakini yanalenga kukufundisha jambo fulani. Medium pia ni chanzo cha mapato kwa vijana kwani mtandao wa Medium ukiutumia vizuri utalipwa kila mwisho wa mwezi.
Ndani ya Medium utapata makala mbalimbali kutoka kwa watu wazoefu waliopitia au kusomea mambo mengi ambayo yanaweza kuwa msaada kwako. Pia kama unapenda kuandika makala na vitu vyako, basi Medium utakuwa mtandao wako.
Mtandao wa Quora umeanzishwa na Adam D’angelo pamoja na Charlie Cheever wakiwa na lengo moja, malengo ya mtandao wa Quora ni kuleta pamoja watu wenye matatizo mbali mbali ili wapate utatuzi wa matatizo yao, hivyo kupitia quora watu wengi kutoka jamii tofauti wanauliza maswali mbali mbali ili kupata majibu sahihi ya maswali yao.
Maswali hayo yanaweza kuwa kuhusu siasa, elimu, burudani, hata kuhusu maisha yako binafsi unaweza kuomba ushauri kutoka kwa watu mbali mbali. Hivyo Quora ni mtandao wenye manufaa chanya kwenye jamii zetu.
Je una swali lolote ambalo hujawahi kujibiwa? Je ungependa kupata mawazo tofauti tofauti juu ya maswali yako? Ndani ya Quora unaweza kupata majibu ya maswali yote unayojiuliza.
Mtandao huu umeanzishwa na Ben Silbermann ukiwa na malengo ya kuinufaisha jamii.
Mtandao wa Pinterest ni muhimu zaidi kwa wafanya biashara mbali mbali unaweza kuuza biadhaa yako kupitia Pinterest na kupata faida zaidi kwa kuweza kuvutia wateja wako waweze kutembelea website yako. Pia unaweza kukuza idadi ya watu ambao wanatembelea website yako kupitia Pinterest. Lakini pia kupitia mtandao huo unapata taarifa mbali mbali kutokana na chaguo na mapenzi yako kuhusu nini unataka kuona.
Vile vile Pinterest inaweza kukusaidia kupata taarifa mbalimbali kutoka kwnye websites nyingi zenye maarifa muhimu kuhusu vitu unavyovifuatilia.
Mtandao wa YouTube ulisajiliwa rasmi mnamo mwaka 2005 huku waanzilisha wakina Jawed Karim, Steve Chen, na Chad Hurley, wakiwa na malengo ya kuhifadhi video mbali mbali online.
Video hizo zina faida nyingi katika jamii ya leo. Kupitia videos hizo ndio unaweza kujifunza vitu vingi, mfano namna ya kutengeza na kupika vyakula, jinsi ya kufanya biashara, au mazoezi. Lakini pia mtandao wa YouTube umemwezesha mfanyabiashara kutangaza biashara yake kupitia matangao ya video hivyo hunufaisha soko lake kwa kupata wateja wapya.
Pia imekuwa msaada na chanzo kikubwa cha mapato kwa watengeneza maudhui. YouTube kila mwaka inalipa watu mamilioni ya pesa kutokana na matangazo yanayowekwa kwenye video zao. Wasanii, vyombo vya habari, wanamichezo, na wengineo wamekuwa wanufaika wakubwa na hela za matangazo ya YouTube.
Na wewe unaweza kuwa mmoja wao wa hawa watu wanaolipwa na YouTube. Ni rahisi sana, kila kitu kimeandikwa kwenye internet.
Mtandao wa linked unafaida kubwa kwa watumiaje wake, mtandao huo huwakutanisha watu wenye taaluma mbali mbali sehemu moja ili kushiriki katika mawazo na kujifunza taaluma mpya ambayo hauifahamu. Lakini pia LinkedIn ni mtandao ambao unatumika katika kutafuta ajira, watu huandika taaluma zao ambazo wana ujuzi nazo au wamesomea ili kupata ajira.
Hivyo LinkedIn ni chanzo sahihi kupata ajira na kukutana na kampuni mbalimbali zinazotoa nafasi za kazi. CV yako kuwa LinkedIn ni kitu kikubwa sana, hujui ni nani atakutafuta kule kuangalia uwezo na taaluma yako. Pia ni sehemu sahihi ya kuanzisha au kusoma midahalo mbalimbali ya kitaaluma.
Hiyo ni kati ya mitandao ambayo inatumika sana kujifunza na kupata maarifa ya vitu vingi mbalimbali. Ukitumia muda wako vizuri katika mitandao hii hakika utapata vitu na mambo mazuri. Ni muda wa kuacha kutumia mitandao kimazoea, ina vitu vingi inayoweza kukusaidia kimasomo, kimawazo na pia inaweza kuwa chanzo cha ajira pia. Ni vile tu unavyoamua wewe kuitumia.