Pamoja na yote, kadri dunia inavyozunguka katika mhimili wake kuna mambo mengi yanatokea. Yapo ya kujenga na kubomoa, mengine yanafurahisha na kuchukiza. Kila mmoja anaegemea anapoona sawa.
Ni kama ilivyo upweke na imani. Neno hofu pia limebeba herufi chache zenye maana kubwa kwenye maisha yetu ya kila siku. Hofu ni kitu kibaya sana. Nakiogopa. Ni adui mdogo kama sindano lakini maumivu yake ni makali mno apenyapo mwilini.
Wakati fulani niliwahi kumwambia mtu, ni heri yule abebaye moyo wenye upweke kuliko mwenye nafsi yenye hofu. Ukiwa na hofu utashindwa kula, utashindwa kulala na moyo wako hautakuwa na amani pia.
Ni katika kipindi hiki ambacho hofu imetawala kwa kiasi kikubwa. Dunia inaumwa, haijui itapona vipi. Ni wakati huu ambao kila nafsi imekumbwa na upweke. Hakuna tabasamu tena.
Imani imepotea. Upweke umechukua nafasi lakini kubwa zaidi hofu imezunguka katika nafsi zetu na kuifunga milango ambayo pengine ingetupa ufahamu wa kupambana nayo.
Ni kipindi hiki ambacho imekuwa haramu kushikana mikono, tunaogopana. Ni muda huu imekuwa ngumu kusalimiana kwa kukumbatiana. Tunaogopana.
Hatutembeleani kama zamani, tunaogopa hadi kusafiri kwenda kuwaona wapendwa wetu Bibi na Babu kijijini, ni sababu mioyo yetu imejaa hofu ya kuwapelekea Corona.
La hasha, kama tukiweza kuisha hofu iliyojaa katika mioyo yetu, tutakuwa na uhakika wa kuikimbiza na kuitokomeza corona. Akili yetu itakuwa na afya, na mawazo yetu hayataishia pale hofu ilipo, bali yatafika pale utaratibu wa afya unavyotaka ili kuiepuka Corona.
Hata hivyo, lazima tufuate njia stahiki zinazoweza kutufanya tupambane na adui tusiyemuona kwa macho. Ni vita ngumu, mapigano yanayohitaji utulivu wa akili na nafsi.
Kushinda dhidi yake hatuna budi kunawa mikono mara kwa mara kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya, kukaa umbali wa mita moja na zaidi wakati wa maongezi yetu.
Kuepuka kukaa kwenye mikusanyiko ya watu ambayo haina ulazima wa kufanya hivyo. Kuvaa barakoa na kuwa na ikiwezekana kutumia dawa maalumu ya kupaka katika mikono.
Ni kwenye matatizo pekee ndipo mwanadamu hufahamu nguvu na uwezo ulio ndani yake. Pongezi kwa madokta kwa manesi, hakika tumeiona nguvu yenu. Tungefanya nini bila nyinyi katika kipindi hiki kigumu.
Usiyachukie wala usichukie kwanini wewe umepata tatizo, Mungu hajawahi kumpa mja wake mzigo asioweza kuubeba. Linapokuja tatizo, furahi, kwa maana wakati wako wa kuigundua nguvu iliyo ndani yako umewadia na safari hii tumegundua nguvu iliyopo ndani ya wahudumu wetu wa afya.
Hakika kuna upweke na hofu, halafu kuna Corona. Kuishinda vita hii ya corona lazima tuishinde kwanza vita ya kuuondoa upweke na hofu iliyojaa katika nafsi zetu. Inabidi tuongozwe na akili katika kupambana na sio kuongozwa na hofu. Tufuate taratibu za afya kwa kutumia utashi na akili.