Maswali matano na Ally Ahmad Doo

Ally Ahmad Doo ni mkurugenzi wa Muungano Recovery Community Tanzania (MRC Tanzania), ambalo ni shirika lisilo la kiserikali linaloendeshwa na waraibu / wahanga wa tatizo la mihadarati kama pombe, unga na bangi.

Shirika hili lilisajiliwa mwaka 2016, na mwaka 2017, shirika lilianzisha mradi wa sober house. Mpaka sasa shirika lina vituo sita, kimoja kikiwa cha wanawake, ambapo toka shirika lianzishwe mpaka sasa wamesaidia vijana 600.

Ally Doo pia alikuwa mraibu na alishirikiana na waraibu wenzie katika kuanzisha na kuendesha shirika hili. Tulipata nafasi ya kumuuliza maswali matano ndugu Ally, na haya ndio aliyoyasema kuhusu uraibu, afya ya akili na MRC Tanzania.

1. Je uraibu (addiction) na matatizo ya akili yanaathari gani kwa mtu akiwa anateseka nayo kwa muda mrefu bila matibabu?

Uraibu na matatizo ya afya ya akili yana athari sana kwa mtu anayekuwa anateseka kwa kuwa anapoteza uwezo wa kujitambua, kufanya maamuzi sahihi, anakuwa kwenye hatari ya kupata maradhi mengine hatarishi kama HIV, TB nk, pia anakuwa kwenye hatari ya kushindwa kufanya maamuzi au kukabiliana na changamoto mbalimbali kipindi anapokuwa kwenye hali za uraibu.

Mfano mimi nilianza kutumia madawa ya kulevya miaka 20 iliyopita nikiwa askari wa jeshi la wananchi wa Tanzania, matumizi ya madawa yalipelekea kupoteza kazi, mke na vitu vingi katika maisha yangu. Mwaka 2013 nilianza safari mpya ya maisha yangu baada ya kuamua kwenda sober house kupata matibabu ya uraibu uliokuwa unanisumbua kwa muda mrefu, miaka mitatu baadae ndio tulishirikina na wenzangu niliowapokea sober house kuanzisha shirika la MRC.

2. Ni matatizo gani ya afya ya akili unaona vijana wengi wa Tanzania wanapitia na unashauri nini jamii na familia katika namna ya kuwasaidia vijana na matatizo ya akili majumbani?

Mtu anayetumia madawa ya kulevya lazima awe na tatizo la afya ya akili kama schizophrenia, bipolar nk, matumizi ya bangi ndio yanayoonyesha kwa zaidi tatizo la afya ya akili kwa wagonjwa wengi ninaowapokea MRC. Ushauri wangu kwa familia na jamii ni kuwa tusiwanyanyapae vijana, tuwasaidie kuwapa haki zao za msingi kama matibabu, haki za kisheria na upendo kwa kuwa ni wagonjwa kama wagonjwa wengine.

3. Kwanini unadhani kuna matangazo mengi sana ya vilevi, sigara nk ukilinganisha na matangazo ya jinsi ya kupona ukiwa mraibu?

Ni kweli kuwa kuna matangazo mengi sana ya pombe na sigara kuliko yale ya kupona ukiwa mraibu, matangazo ya ulevi kama pombe na sigara lazima yawepo kwa kuwa ni biashara halali na inayoingiza kipato kwa taifa.

4. Je mnapata msaada gani kwenye vituo vyenu kutoka kwa serikali na kama hapana mngependa serikali ihusike vipi au kuwasapoti vipi kwenye kazi zenu?

Serikali inatuaidia kwanza kwa kututambua, kwa kuweza kutupa vibali vya kufanya kazi, lakini pia tunaandika ripoti na kuweza kuzipeleka sehemu mbalimbali mfano wizarani, na pia tunapata miongozo ya kazi zetu za sober house kwa wakati kuanzia ngazi ya serikali ya mtaa, wilaya na mkoa ambao tunashirikiana nao vizuri sana. Kwa upande wa polisi wao wanatupa ushirikiano wa karibu pale tunapokuwa tunauhitaji wao.

Lakini pia ni muhimu kwa serikali kuwa na sera na mpango maalumu kwaajili ya mapambano dhidi ya madawa ya kulevya.

5. MRC inasaidiaje vijana katika kukabiliana na uraibu na maswala ya afya ya akili na je kazi mnayoifanya ina umuhimu gani kwenye jamii?

MRC Tanzania inatoa elimu kwa jamii kupitia redio, TV, mikutano ya wazi, mashuleni na vyuo kwa vijana ambao bado hawajajiingiza katika matumizi ya mihadarati.

Pia MRC inafanya ushawishi kwa vijana walioathirika kwenda kwenye matibabu na kupima afya zao kila wakati ili kama watakuwa na maradhi yoyote waweze kuanza tiba mara moja.

Kazi tunayoifanya ina umuhimu sana maana tunasaidia kupunguza ongezeko la watoto wa mitaani au ongezeko la watoto wasiopata malezi ya wazazi kwa vile wameathirika na uraibu, mbali na hilo, kazi tunayoifanya ina umuhimu pia kwa kuwa tunaepusha nguvu kazi ambayo itapotea kutokana na janga la madawa, lakini pia tunasaidia kupunguza maambukizi yasiyo ya lazima kwa vijana wanaotumia madawa ya kulevya na kufanya ngono zembe, na pia tunachangia kurudisha ndoto za vijana ambao wenye taaluma mbalimbali kuja kuwa wazalishaji katika jamii na kuwa wachangiaji wa kulipa kodi kutokana na shughuli zao.


Kama unahitaji msaada kuhusiana na swala la uraibu, una swali au unahitaji ushauri na sapoti, au kama ungependa kusapoti kazi za vituo vya MRC au ungependa kuwasiliana nao, mawasiliano yao ni haya;

Email: mrcsober@gmail.com

Namba: 0683620421

Na nyingine ni: 0769875623

Previous ArticleNext Article
Eunice is a multi-niche freelance writer with experience in writing health, lifestyle, finance, interviews, tech, travel, entrepreneurship, automotive, and mental health articles.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend