Jinsi wafanyabiashara wadogo wanavyoweza kutumia WhatsApp Business kuendesha biashara zao kidijitali
WhatsApp Business ni aina ya WhatsApp inayowasadia wafanyabiashara kufanya mawasiliano na wateja, kuonyesha biashara zao na kujibu maswali ya wateja wao kwa uharaka zaidi viganjani mwao.
Kama wewe ni mfanyabiashara basi nikushauri upakue WhatsApp Business ili uitumie ipasavyo kwaajili ya kuboresha muonekano wa biashara yako na huduma kwa wateja wako lakini pia kuitangaza biashara yako kwa watu wanaofungua namba yako.
Kwanza kabisa kupitia WhatsApp Business unaweza kutumia namba ya biashara yako, kama una namba ya matumizi yako binafsi na biashara basi kwenye WhatsApp hii unaweza kufungua akaunti kupitia ile ya biashara.
Ukishafungua akaunti bonyeza vile vidoti vitatu halafu chagua Setting halafu bonyeza Business Setting halafu bonyeza Profile, halafu sehemu ya jina, weka jina la biashara yako na sehemu ya ‘about’ andika biashara yako inahusu nini.
Mfano:
- Name – Ashura Mapishi
- About – Tunafurahisha tumbo lako kwa kila shughuli uliyonayo.
- Kwenye picha unaweza kuweka logo ya biashara yako, hii itakuwa ni utambulisho mwepesi wa biashara yako. Itapendeza zaidi kama logo hii itafanana na ile ya Instagram au uliyoiweka kwenye mitandao ya kijamii mingine, ili watu wanaotoa namba yako kwenye mitandao ya kijamii kwaajili ya mawasiliano wawe na uhakika ni wewe mnapowasiliana kwa vile logo ni ile ile.
Jambo lingine zuri kutoka kwa WhatsApp Business hasa kwa biashara ambazo zinaweka maudhui mtandaoni ni, kuna link maalumu unayoweza kuitengeneza ambapo mteja sio lazima aweke number yako kwenye simu ili kuwasiliana na wewe, anabonyeza tu ile link na anaweza kuwasiliana na wewe kiurahisi kabisa kupitia WhatsApp.
Kutengeneza link hiyo ambayo unaweza kuiweka kwenye mitandao yako ya kijamii ili wateja wako waibonyeze nakuja moja kwa moja kuwasiliana na wewe WhatsApp unabonyeza vidoti vitatu pale juu halafu unachagua Settings, halafu unabonyeza Business Tools halafu unaenda kwenye Short Link, hapo utaona link tayari iliyotengenezwa kwaajili yako kwa kutumia namba yako hiyo ya biashara utakachofanya ni kuikopi hiyo link na kuweka kwenye profile zako mitandaoni ili wateja wako wawasiliane na wewe kwakubonyeza link.
Unaweza kutumia link hii au kuweka mawasiliano yako ya WhatsApp kwenye Instagram na Facebook yako kwa njia nyingine. Unaweza kuunganishha hivi WhatsApp yako na mitandao mingine ya kijamii kwa kwenda kwenye vidoti vitatu halafu unachagua Business Tools halafu ubonyeze Facebook and Instagram pale chini kabisa sehemu iliyoandikwa Reach more customers. Njia hii inafanya namba yako hii ya WhatsApp ionekane kwenye profile yako sehemu ya mawasiliano.
Hapohapo unaweza kuweka ujumbe ambao wakiwasiliana na wewe ukiwa haupo online kwa wakati huo unawajibu wateja wako automatically ili wasubirie kuwasiliana na wewe ukiwa online. Ujumbe huu unaweza kutengeneza kwa kubonyeza vidoti vitatu halafu unachagua Business Tools halafu kwenye sehemu ya Messaging unachagua Greeting Message, na hapo unaandika ujumbe wako ambao mtu akiwasiliana na biashara yako itakuwa majibu ya kumkaribisha mpaka wewe utakapokuwa online. Wengine hutumia ujumbe huu kuorodhesha bidhaa na huduma wanazotoa, wengine hutumia kuwakaribisha ili wawe huru kuelezea tatizo au huduma wanayoitaka kwako.
Mfano mzuri wa jumbe hizi ni kama: Asante sana kwa kuwasiliana na Ashura Mapishi, karibu sana. Ungependa tukuandalie chakula kwa ajili ya shughuli gani?
Sehemu hiyo hiyo ya Messaging pia unaweza kuweka ujumbe kwa ajili ya wateja wako ambao wataupata ukiwa haupo, kama umesafiri kwasababu ya sikukuu nk, unaweka Away Message ambao ni ujumbe mfupi unaoweza kuelezea lini utarudi nakadhalika.
Kitu kingine kizuri kwenye WhatsApp Business chenye msaada kwenye biashara yako ni kuweka eneo ambalo biashara yako inapatikana, tovuti, masaa ambayo ofisi yako inakuwa wazi, email, mitandao ya kijamii unayopatikana, aina ya biashara unayofanya nakadhalika. Kuweka haya yote unaenda tena kwenye vidoti vitatu halafu unachagua Business Tools halafu unabonyeza Business Profile na unajaza haya yote.
Jambo lingine kuhusu WhatsApp Business lenye msaada mkubwa kwenye biashara yako ni Catalogue, ambayo ni sehemu unayoweza kuonyesha picha ya bidhaa na huduma zako lakini pia na gharama zake na wapi wateja wanunue kama unaziuza kwenye tovuti. Kuweka catalog ya bidhaa na huduma zako, bonyeza vile vidoti vitatu halafu chagua Business Tools halafu Catalog, baada ya hapo bonyeza Add New Item na ikifunguka unaweza kuweka picha hadi kumi, jina la hiyo bidhaa, bei ya hiyo bidhaa, maelezo kidogo ya hiyo bidhaa halafu na jinsi wanavyoweza kuinunua kama kwenye tovuti nk.
Hiyo ni namna fupi ya kutumia mtandao huu wa mawasiliano kuiweka biashara yako kwenye ulimwengu wa kidijitali, siku hizi mambo yamebadilika, kuwaleta wateja kwa ukaribu zaidi na kuwa na namba zao kwa ajili ya mawasiliano kupitia WhatsApp kunaweza kukusaidia kwenye mauzo.