Siku ya Ijumaa ina utamu wake jamani, we acha tu. Hasa ukiwa umeridhika na kazi nzito na murua ya wiki nzima. Unaweza ukajikuta unaingia kwenye mawazo ambayo sio ya kawaida. Mimi hapa nilipo nasubiri mvua ipungue ili nianze safari ya kwenda nyumbani…ghafla, nakiangalia kitasa cha mlango wa ofisini. Nakiangalia kwa makini na naanza kujiuliza, hivi nani aligundua kitasa (cha mlango)? Mtu au watu waliogundua vitasa na funguo walikuwa wanafikiria nini? Kitasa ni kitu kidogo tu lakini nadhani kina historia kubwa kuliko ukoo wangu.
Baada ya kuzoea ‘msisimuko’ wa mwanzo wa weekend, akili inatulia kidogo na naanza kutafakari mwelekeo wa maisha yangu – kama kijana wa kawaida. Nini kitafuata baada ya kumaliza hiki kinachokula ubongo wangu kila siku?
Napitia forum ya Wanabidii, ambayo ina mijadala mizuri, na mawazo ya kuingia kwenye Siasa naona yananinyemelea baada ya kusoma kwamba Wabunge wa Tanzania wanategemea kupata kiinua mgongo cha shilingi za Kitanzania 15.3/= bn. Sijachapia – bilioni 15.3! Sidhani kama nitaelewa kusema ukweli. Na nitashukuru sana kamati husika za Serikali zikitoa takwimu kama hizi, zitoe maelezo au sababu za viinua migongo kwa wananchi pia.
Nitoke vipi kwenye Siasa na mimi nithaminiwe zaidi kuliko kitasa cha mlango tu?
Naona mvua imepungua na safari ya kwenda nyumbani itaanza punde. Wakati huo huo ubinadamu au mawazo yangu ya kawaida yanarudi baada ya kukumbuka matokeo ya kidato cha sita yaliyopita. Labda hizi bilioni 15.3 zipelekwe kwenye sekta ya elimu?
Ngoja niache kufikiria mawazo ya Siasa ili nisitibue weekend yangu. Weekend njema Vijana!