Kuna wakati wasanii nyumbani walikuwa wanategemea vituo vikubwa vya redio – hasa Clouds FM – kuamua mafanikio ya kazi zao. Kwa maneno mengine, kama kazi yako ikikubaliwa na ikachezwa vya kutosha na Clouds FM basi unapata uhakika wa kupata shows. Wale ambao nyimbo zao zilikuwa zinatupwa kapuni ilibidi warudi wajipange upya au kuhamia kwenye fani nyingine.
Lakini kuna Vijana ambao wamefikiria na wakaona mbali zaidi.
Siku moja nilitumiwa nyimbo inayoitwa ‘Mshindi’ na mdogo wangu anayesoma India. Akaniambia tu, “msikilize mbongo huyo.” Nilikuwa natumia headphones uchwara, lakini baada ya beat kuanza ilinibidi nihamishie mambo kwenye spika kubwa! Nikarudia kuusikiliza mara kibao na nikaanza kufanya utafiti ili nijue nani hasa anayeghani…
Jina: Wakazi!…Nyumbani: Ukonga, Dar es Salaam!…Makazi: Chicago!
Kusema ukweli sikuamini jinsi ilivyokuwa rahisi kupata habari na taarifa zote za Wakazi aka Swagga Bovu; bila kusahau nyimbo nyingine nyingi nilizoweza kuzisikiliza kwenye mtandao.
Wakazi anajishughulisha na mambo mengine lakini ana mapenzi makubwa na Hip Hop. Ukiacha utundu wake wa kucheza na maneno ya lugha ya Kiswahili na Kiingereza, inaonekana amefikiria mbali. Ameona nini kinaendelea kwenye teknolojia (hasa mtandao) na akaamua kuelekeza juhudi zake zote kwa kujitangaza kupitia twitter, facebook na myspace. Na wiki hii amezindua tovuti yake. Idadi ya watu wanaofuatilia kazi zake za muziki inazidi kukua na hii inaasharia kuwa juhudi zake zinaanza kuzaa matunda.
Sitashangaa akianza ‘kuwapiga bao’ wasanii ambao tayari wako juu kwenye vituo vya redio Bongo pindi mtandao wa fibre optic utakapoanza kutumiwa na watu wengi Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Kama wahenga walivyosema, “Chema chajiuza, kibaya chajitembeza.”
Sasa hivi ana Mixtape ya Ukweli Vol. 1* ambayo imeanza kutapakaa kwenye mtandao (click here to download). Na yuko studio akirekodi mixtape yake ya pili na album yake ya kwanza.
Wale ambao wako Dallas, Texas, Wakazi atakuja kuwakonga nyoyo zenu kwenye weekend ya Pasaka. Kama unataka kujua mambo mengine zaidi…Just Google him! Au mwandikie e-mail: wakaziwavina (at) gmail (dot) com.
*Quote from the mixtape review: “If I start quoting his best punchlines or one-lines, then it won’t be an ending process as the whole mixtape got those, you can peep wordplay here ‘Kimziki wewe ni Cheater (Chettah), unafanana na duma!'”