Msimamo Wenu, Maendeleo Yetu

na Michael Dalali

Z. Kabwe

Ukurasa mpya umeandikwa katika vyombo vya kimaamuzi kwa ongezeko la vijana wawakilishi tofauti na chaguzi za awali. Kupata wabunge vijana wa kuchaguliwa takribani 15 (CCM (4), CHADEMA (8), NCCR-Mageuzi (3)), tofauti na awali katika chaguzi ya mwaka 2005 ambako kulikuwa na mbunge mmoja tu wa kuchaguliwa, Mhe. Zitto Kabwe toka Kigoma Kaskazini. Ikumbukwe kijana anayezingatiwa hapa ni kwa mujibu wa sera ya Taifa ya vijana inamtafsiri kijana kama mtu mwenye umri wa miaka kati ya 18-35.

Idadi hiyo ni zao la juhudi kubwa na za muda mrefu za wadau mbalimbali, mathalani asasi za kiraia hususan za vijana kupiga chapuo hitaji la ongezeko la uwakilishi wa vijana katika vyama.

Lakini hatuwezi kupuuza usikivu wa vyama vya kisiasa ambavyo viliweza kuona tunu ya wito wa kuwekeza katika vijana kwa kuwapa ridhaa vijana kusimama kama wagombea katika majimbo. Hakika imedhihirisha inawezekana!

Ushindi ambao vijana wengi wameweza kuupata ni taswira pana ya mabadiliko ya kimtazamo kuwa vijana si tu wasindikizaji ama wapambe wa wagombea, bali wao pia wanaweza kuwa wagombea na kuwa wawakilishi wa wananchi katika ngazi za maamuzi.

J. Mnyika

Imani ambayo Watanzania wamewekeza kwenu vijana wabunge kupitia kura zao mnapaswa mjitahidi kuishi kwa vitendo; mnapaswa muirejeshe imani hiyo kwa utumishi uliotukuka kwa kusimamia maslahi ya wananchi.

Vijana waliofaulu kuchaguliwa kuwa wabunge wasisahau wao ni sampuli ndogo miongoni mwa vijana wengi ambao wana uwezo na utashi wa kuwatumikia wananchi, hususan kwa kuwakilisha katika vyombo vya kimaamuzi, hivyo ni jukumu lao kuenenda na kuthibitisha vijana ni tunu na hazina katika mabadiliko.

Licha ya majukumu mazito ya wabunge vijana wa kuchaguliwa waliyonayo dhidi ya wananchi katika majimbo yao, kundi la vijana haliwezi kuacha kuwaangalia wao kama watetezi pekee wa ajenda na vipaumbele vya vijana.

Baadhi ya ajenda ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele kwa zaidi ya miaka mingi sana na vijana toka makundi mbalimbali kama asasi za kiraia za vijana, taasisi za kisiasa, taasisi za kitaaluma n.k. Tena baadhi ya vijana waliokuwa katika harakati hizo miongoni mwao sasa wamefaulu kuwa wabunge, tunatarajia wataendelea sasa kusimamiwa kidete katika ngazi ya juu na uwezo wa ushawishi wa kimaamuzi kwa Bunge na Serikali kwa ujumla.

Mwaka 2010, kama ilivyokuwa mnamo mwaka 2005, asasi za kiraia kadhaa zenye kujihusisha na masuala ya vijana zikiratibiwa na asasi ya TYVA, zimeweza kukusanya na kutathmini vipaumbele vya vijana na Taifa zima kwa ujumla. Vipaumbele ambavyo kwa asilimia kubwa ndivyo vilio vya vijana; hivyo tunapaswa kuwakumbusha tena na tena wabunge vijana ambao ni wawakilishi wa sampuli ya vijana katika vyombo vya kimaamuzi kuweza kuvitetea.

Ni kundi hili dogo la vijana wabunge ambao vijana wote wa Kitanzania wanaweka matumaini yao kuwasikia wakiwa mstari wa mbele kutetea uanzishwaji wa Baraza Huru la Vijana la Taifa na haswa kusimamia na kuhakikisha sera ya vijana ya Taifa inatekelezwa kwa mapana yake licha ya changamoto zake.

J. Lusinde

Ni vijana hawa wabunge ambao wanaujua uchungu wa ukosefu wa ajira, mazingira magumu yaliyopo katika kilimo — hususan kwa wakulima wadogo wadogo — ukosefu wa ujuzi na ukomavu wa fani na ujasiri wa kupambana katika soko la ndani na kimataifa. Na ni wabunge hawa vijana ambao wanajua hali na mazingira magumu ya upatikanaji wa mitaji na fursa za kuwekeza kwa vijana nchini. Tunaamini hawatatusaliti!

Ni wabunge hawa vijana ambao kwa asilimia kubwa wamepitia katika mifumo ya elimu nchini ambayo changamoto zake hakika naamini hawajazisahau, kama ilivyo kwa sekta ya afya. Naamini watapaza sauti sasa kusimamia mabadiliko yake.

Ninaamini mmeshuhudia ufu wa vipaji vya vijana wenzenu na wachache ambao walisimama kidete kutetea vipaji hivyo jinsi walivyokuwa na ugumu katika kufaidika; naamini mtahakikisha sera na usimamizi madhubuti wa ukuzwaji na mazingira bora ya uchocheaji vipaji nchini kama tunu ya mchango wenu kwa kundi hili kubwa.

Mazingira bora ya ukuzwaji wa vipaji, mathalani michezo; kwa kukomesha tabia ya ubinafsi ya kuuza viwanja vya wazi ambavyo baadhi vilikuwa vikitumiwa na vijana kucheza michezo mbalimbali. Naamini hamtakenua wakati haya yakitendeka, na hata kwenye baadhi ya maeneo mtarudi nyuma na kusawazisha mabonde.

Kwa msukumo wa ujana wa chachu ya fikra mpya, ubunifu, nguvu mpya na uwezo wa uthubutu, naamini mtakuwa na uthubutu wa kusukuma uwepo wa mchakato wa kufanyia mabadiliko Katiba ya Tanzania.

H. Mdee

Uundwaji wa katiba mpya imekuwa kilio cha muda mrefu cha makundi mbalimbali katika jamii ya Tanzania mathalani vyama vya kiraia, vyama vya siasa (ambavyo ndimo mnakotoka), wasomi na hata wananchi wote kwa ujumla. Hakika tunawapa jukumu la kusimamia uwepo wa mabadiliko! Kuhakikisha uundwaji wa katiba mpya.

Ni katiba mpya inayoweza kutoa fursa hata kwa kijana kushika nyadhifa ya juu ya kiuongozi nchini ya urais, ambayo kwa sasa kwa mujibu wa katiba yetu, kijana hawezi kuwa rais. Na kuhakikisha mabadiliko ya kigezo cha umri toka miaka 40 hadi japo miaka 35 yanafanyika.

Naamini mnatambua kuna vijana wengi wamekosa fursa kusimama kuwa wagombea kutokana na baadhi ya vyama kutotoa fursa kwa vijana. Ni mabadiliko ya kikatiba ambayo mkiyasimamia, mathalan kuruhusu mgombea binafsi, yanaweza kuwa suluhu kwao.

"Sugu"

Mmezunguka na kusikiliza wananchi, hakika wengi wana hali duni kiuchumi. Naamini hamtawasaliti na kusahau kuwa wameweka matumaini yao kwenu; mtawatoa katika mfumo ambao unapelekea kuwa na hali duni ya kiuchumi na kupunguza umaskini wa mtu mmoja mmoja.

Tumaini la vijana wenye ulemavu lipo mikononi mwenu. Naamini mnatambua hali duni inayowakabili katika upatikanaji wa huduma za kijamii mathalani elimu, mazingira duni katika sekta za kiafya, na hata wenye elimu kukabiliwa na changamoto ya kunyanyapaliwa katika fursa za ajira na vyombo vya kimaamuzi. Kuweni sauti yao!

Tunaamini mtakuwa wabunge wenye chachu na mwamko mpya katika kusimamia kuleta mabadiliko katika nchi yetu. Ni matumaini ya wananchi katika ujana ambao mnao, mtakuwa na nguvu na fikra mpya kuweza kuwa nuru kwa Taifa na kurejesha imani kubwa ya kusimamia maslahi ya nchi, hususan ya wanyonge na makundi yanayosahaulika ama kutengwa.

Kumbukeni daima maneno ya Frantz Fanon kwamba kila kizazi kinapaswa kung’amua utume wake na aidha kiutekeleze ama kiusaliti.

F. Mkosamali (24)

Hakika msimamo wenu ndiyo chachu ya maendeleo yetu. MUNGU awajaze hekima katika utumishi wenu!

*                    *                    *

Ukitaka kufahamu wasifu wa mwandishi, tembelea:

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 2 Comments

2
  1. Ngugu Michael,

    Ninashukuru na kufurahishwa sana na jitihada zako kama hizi. Nina amini kwamba kazi za ujenzi wa taifa sio mpaka uwe kwenye nafasi kubwa katika jamii ila ni msukumo wa ndani ya mtu binafsi unaotokana na uzalendo wake.

    Naomba nikupe pongezi kwa jitihada hizi na niungane na wewe katika kuhimiza yale uliyo yasema hapo kwenye makala! Sote tunawategemea viongozi wetu hawa vijana kwani wao ndo wanaoelewa mikiki mikiki inayotukabili sisi vijana na tumepiga hatua nyingine ya kuwapa kura zetu za ndiyo, hatujaishia hapo, tungali tunapatikana na kuunga jitihada zao katika kutekeleza majukumu mazito yanayowasubiri kitaifa.

    Ninaamini kwamba hakutakua na wasaliti miongoni mwao kutokana na imani yetu juu yao. Tunafahamu upepo mkali uliopo mbele yao ila ninaomba wasiogope kwa kusimamia haki! Nina kumbukumbu ndogo sana baada ya kuangalia movie ya Sarafina mwaka wa 1997 nilipata kitu kidogo tu kutoka pale aliposema Sarafina kwamba ” I rather die like him than stay like you” Sarafina aliamini kwamba baba yake mzazi alikufa kwa haki akipambana na udhalimu kwa hiyo ni jambo la kujivunia endapo maisha yako yatakatishwa na wenye nguvu ila ijulikane kwamba ulisimamia haki na manufaa ya umma!

    Twaungana nao!

    Mungu awape nguvu vijana hawa wenzetu katika haya majukumu mazito!

    Mark Okello

  2. Aisee, shukrani Michael kwa kutuletea hii makala. Ingawa michango kutoka kwa wasomaji imekauka kwenye hizi siku mbili tatu, ila bado nina duku duku kubwa sana la kusikia kutoka kwa hawa wabunge vijana.

    Nitawatafuta. Kwa hiyo, wahusika msishangae kupokea mwaliko wa mahojiano na VFM!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend