Talaka

Mke wangu Politiki,

Nimejaribu kukuvumilia kwa kipindi kirefu mno, lakini mwili na akili yangu imechoka sasa. Jazba, mifadhaiko na huzuni zimejaa pomoni.

Bado nakumbuka siku niliyokutia machoni kwa mara ya kwanza mwaka 1995 katika jimbo la Temeke. Nilikuwa bado mdogo — darasa la tano katika shule ya msingi Chang’ombe — ila nilianza kupata ufahamu wa uwepo wako kwenye mtaa wetu.

Nakumbuka siku tuliyokutana kama vile ilikuwa jana tu; wewe ulikuwa unatoka shuleni Kibasila na mimi nilikuwa natoka shule na kuelekea mpirani kabla ya kwenda nyumbani. Nina uhakika bado unakumbuka jinsi wote tulivyokuwa tumesimama pembezoni mwa barabara ya Uwanja wa Taifa, huku tukishuhudia umati mkubwa wa vijana ukimsindikiza mtu mmoja ambaye bila shaka alikuwa maarufu kwenye nji hii.

Baada ya muda mfupi tu tukazoeana kupita kiasi na tukawa tunacheza kombolela karibia kila jioni. Bahati mbaya mwenzangu ukanichoka mapema. Visa vikaanza. Labda ningekuwa nina akili ningejifunza kusoma alama za nyakati tokea kipindi kile… na haya matatizo yasingetokea.

Unakumbuka siku ile nilipokuja na cha ndimu ili kukuonesha naweza kupiga dana-dana kumi? Hukuonekana umefurahishwa hata kidogo. Nilipomaliza kupiga dana-dana zangu tu ukaniambia unataka kucheza rada; mchezo wa kike! Nani alikufundisha? Yule mtoto kibonge mwenye nywele kipilipili? Anayependa kuvaa cheni ya goldi?

Najua huwezi kukubali sasa hivi baada ya miaka mingi kupita. Mpenzi Politiki, majibu yako siku zote yamekuwa ni ya kunipiga chenge za mwili. Wakati mwingine naogopa hata kukuuliza maswali ya msingi kwa sababu unakuwa mkali bila sababu yoyote ile.

Miaka nenda rudi. Hujakubali kubadilisha nyendo zako. Kwa kiasi kikubwa, najilaumu nafsi yangu.

Jua fika kuwa sikupanga kukuoa. Ni upumbavu wangu tu ambao uliniingiza kwenye kadhaa hii inayoonekana haina mwisho. Ndoa yenyewe… mhh, nikifikiria jinsi ilivyotekea, nadhani ulinitega. Kila nikifikiria mtiririko wa matukio mwaka 2005, sipati picha kamili ya maana.

Sawa, tulikuwa likizo. Tukapanga tukutane usiku wakati unatoka kununua mkate kwa ajili ya kifungua kinywa siku inayofuata. Sikufichi, tabasamu lako lilinihadaa. Moyo wangu ukashindwa kusukuma damu kwenye ubongo wangu na nikaishia kukuvuta karibu nami ili nipate fursa ya kukubusu. Kwa ridhaa yako mwenyewe ukakubali na ukanisogelea. Kamwe sitakuja kuelewa kilichotokea baada ya hapo.

Hivi, nani aliandaa lile jopo zima lililotufungisha ndoa ya mkeka? Yaani, pale pale kichochoroni? Walimpata wapi yule Sheikh? Waliwazeje kutafuta na kupata ubani, mkeka na vifaa vyote ndani ya dakika mbili tu? Wewe ulikuwa unawafahamu wale wazee? Kumbuka, tulikuwa bado watoto wadogo tu.

Nina haiba ya kutopenda shari ndio maana sikuanzisha varangati. Hii tabia ni msingi niliopewa na baba yangu, ambaye hakuchoka kunisihi kuwa mpole na kuhakikisha ujamaa unadumu katika jamii yetu.

Lakini, mpenzi wangu Politiki, nasema nimekushindwa na sitajaribu kukuelewa tena. Visa ulivyonifanyia kwenye miezi sita iliyopita vimenikwaza na nimeamua kukupa talaka!

Nianzie wapi… Pigo la mwisho ni huyu kidume kutoka Oman! Yaani, jamaa amekuja kutalii kwa siku mbili tu lakini umefanikiwa kulala nae?

Kama hiyo haitoshi, shoga yako kaniambia ulinidanganya unakwenda kuwaona wazazi wako Dodoma wiki iliyopita, ili upate upenyo wa kwenda Loliondo. Unasumbuliwa na ugonjwa gani, Politiki? Najua hauna kisukari, pumu, saratani wala presha. Loliondo umeenda kufanya nini?

Huu ndio mwisho wetu. Mizigo yako hiyo hapo, nyumba imefungwa, na hii ni talaka rasmi! Usichukulie ninayosema kama sina uzalendo; mapenzi yamefika kikomo. Ingawa sina uwezo, ujuzi na maarifa kama ya Watunisia, nisikufiche, mawazo yangu yananituma kwenda Kaskazini ili nikaoe Mmisri.

Mtanzania.

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 12 Comments

12
  1. Ama kweli.Kwa mtiririko huu,nakuelewa unapoamua kutoyakoga maji ambayo ulikuwa ushayavulia nguo.Baridi imezidi…na kesho si ipo?Basi utaoga kesho.Politiki hakufai.Utaishia kwenda Loliondo kwa maradhi yasiyo yako.Kisa?Achana naye mapema.Ila weka milango wazi.Urudishie lakini usitie kufuli.Anaweza akaja akaomba msamaha.Jaribu kusamehe mara saba sabini kama alivyotuasa yule naniii wa kwenye kitabu cha Muumba.

    Amka sasa nenda kadai hela zako za mahari.Hata kama ulitoa nusu.Ni zako.Amka sasa,usiogope.

    Well written piece Brother.Loved it.Nimetia kizungu kuonyesha msisitizo

  2. Irony katika satire hii ni pale mfumodume unapotumika kumulika maovu ya kisiasa kwa kuyavika maovu hayo hali ya uke.

    Wanawake wanapata mapigo mara mbili, moja kwa sababu mfumo wa kisiasa Tanzania unaendana na mfumodume, kwa hiyo unawaumiza na kuwadhalili moja kwa moja. Lakini upande wa pili, tunaona hata hawa vijana wetu wanaharakati ambao ndio hasa wanatakiwa kuwa wakombozi wa mwanamke kwa maana ya kubadili mfumo wetu wa siasa (ambao unakumbatiana na mfumodume) nao wanatumia mfumodume kutuletea hadithi zinazomdhalili mwanamke kwa kufananisha mmomonyoko wa siasa na mpenzi wa kike.

    Labda ni kwa sababu waandishi wenyewe wengi ni wanaume wenye mfumodume kwenye DNA bila kujijua. Na wanaandika kwa kutumia “experiences” zao bila hata kutambua kwamba wanamdhalilisha mwanamke kwa kumfananisha na mmomonyoko wa siasa. Siwezi kuwalaumu.

    Ninachoweza kusema ni kuuliza tu, sauti za kkina dada zetu ziko wapi? Maana bila ya kutaka kuanzisha vita ya jinsia, siamini kama kinadada wangeweza kufananisha udhalili huu na mwanamke. Overanalysis?

    Otherwise kazi nzuri, hasa unapochomeka “kucheza rada” (At first I was like, typo?) then “chenge za mwili” made it sensible. Surprised I didn’t see anything about “ukapa”, or would that be vulgarly banal and overstretching the freshness of the technique ?

  3. @Buruda, ndugu hoja yako is on point, mimi binafsi nimeikubali. Ukiniuliza mimi sina uhakika kama mwandishi alifikiria mbali kote huko, manake upeo wako kweli uko makini. Nadhani mwandishi yeye alikuwa amezamia zaidi kwenye kutuletea ujumbe fulani, lakini nimefurahi safari moja imeanzisha nyingine, safi sana..

    Sasa tukiacha nililojadiliwa kwenye hii satire, na kuzungumzia hoja yako ya jinsia, nadhani tunaweza rejea kwenye makala moja iliyowekwaga humu wiki chache zilizopita. Makala hiyo iliibumua hili suala zima la wanawake wakiwezeshwa wanaweza. Hoja hiyo ikatupeleka moja kwa moja kwenye mjadala wa hawa wabunge wa viti maalumu, ambao wengi wao kama sio wote ni wanawake.

    Sasa basi, ingawa mwandishi hakulenga issue ya jinsia kwenye hii satire, mimi nitajaribu kuiweka kwa namna ifuatayo. Wanawake labda wasingependa kufananishwa na mmomonyoko wa siasa, kwani wengine watasema hiyo ni sexism. Mimi binafsi nitawaelewa wale watakaoleta hiyo hoja. Lakini the catch inakuja hapa, mbona wanawake hao hao wanachochea mfumo dume katika siasa. Kwa maana gani, kwa mfano huo wa wabunge wa viti maalumu, kwani kwa wao kukubali kupewa viti vya dezo, ni kama kukubali wao ni viumbe dhaifu, hivyo wanahitaji wanaume kuwafanyia kila kitu, kwani wa binafsi hawawezi kufanya kitu chochote. Kwa upande wa wanaume, sis tunaweza kusema, utaratibu wa viti maalumu ni sexism pia. Wanawake wenyewe wanajiangusha kwa kukubali huo mfumo wa dezo miaka nenda rudi.

    Hapo hapo, tuangalie mchango wa hawa wanawake walioshika hivi vitu maalumu katika siasa na maendeleo ya jamii kwa ujumla. Pamoja sina uhakika, lakini kuna hisia inaniambia hwafanyagi kitu, na mchango wao katika siasa ni mdogo au haupo kabisa. Sasa hapo unapata jibu lako, kuwa hao wanawake wanachangia mmomonyoka wa siasa katika jamii, kwani hakuna la maana wanalofanya, zaidi ya kupewa hivyo vyeo vya uheshimiwa na kupokea fungu lao kila mwisho wa kikao.

    Sasa ni vigezo gani ambavyo vinatumika katika kuchagua hao wanawake wa kupewa hivyo viti maalumu, uliza swali hilo na majibu yatakuwa mengi. Je, tunauhakika kuwa hao wanawake wanaochaguliwa wanapenda siasa, na wana huo uchungu na uwezo wa kushika hivyo vyeo?, hapo sasa

    Hivyo basi, pamoja ninaelewa hoja yako ambayo nina ikubali, lakini kwa mfano niliyokutolea nadhani tunaweza kuona ni vipi wanawake wanachangia mmomonyoko huo, na pia kuutumia mfumo dume huo to their advantage. Mimi nasubiri wanawake kusimama na kusema, hatutaki tena mfumo wa viti maalumu, na kuanza kupambana majimboni kama kila mtu…tusubiri tuone

    p.s la ukapa nalo lipo humo, rudia kusoma na utaona kidokezo kimoja la hilo unaloulizia, mimi sitataja, staki ushahidi..hahah!!..

  4. Buruda,

    Kusema ukweli nilikuwa nasubiri na kuombea mchango kama wako — honestly!

    Kuna dhana inayopendwa kutumiwa na Watanzania kuwa “sanaa au wasanii ni kioo cha jamii”… lakini bahati mbaya sisi tumeshindwa kuielewa vizuri. Tunataka wasanii, waandishi au watu kwenye fani fulani ya sanaa wawe ‘watakatifu’ au role models. Kioo cha jamii ina maana hadhira inapoangalia kazi ya sanaa, basi inajiona yenyewe, na si vinginevyo, na kumlaumu msanii.

    Leo nikiona video fulani ya Bongo Flava ya Dully Sykes ikiwa na wasichana waliovaa nguo ambazo zina utata fulani, njia rahisi ya kuiangalia ni kumlaumu Dully kwa kutengeneza video kama ile. Lakini, Dully ni sehemu ya jamii, na kazi yake inamaanisha tuna vijana kama yeye wanaopenda mambo anayofanya au anayoyaonesha n.k. Lakini mtihani utakuwa ni kuangalia uwiano uliopo kwenye jamii na kazi za sanaa zinazopewa nafasi kwenye vyombo vya habari.

    Kwenye hilo la mfumo dume, nimefanya makusudi. Ndio maana hata nilipotaja “rada” — nikimaanisha mchezo “rede” — nikaongeza “mchezo wa kike” kama kuweka msisitizo madhubuti. Umenielewa? Nilikuwa sina haja ya kusema “rede” ni mchezo wa kike. (Kuhusu “ukapa”.. kuna yule kibonge mwenye nywele kipilipili anayependa kuvaa cheni ya goldi….)

    Sitaki kukuchambulia kila kitu… kukwambia nini hasa kimenisukuma kuandika hii makala. Ila, kama unasoma vitabu, metaphors zinazotumia “wanawake” kwenye kazi maarufu za fasihi zinaonekana kuamsha fikra za watu kupita kiasi. Na zinafanikiwa kufikisha ujumbe (“Disgrace” by J. Cotzee). Kwanini? Basi tuiangalie jamii kwa ujumla. Na mimi kama mwandishi ni sehemu ya jamii na siko kwenye tabaka fulani ambalo ni tofauti na wengine wanaokumbwa na matatizo yanayotokana na mifumo mibovu ya siasa kwenye ‘nji hii’.

    Kwa kumalizia tu, mwandishi hajichukulii kama mwanaharakati… anatumia upeo wake mdogo kufumbua macho au kuwakumbusha watu mambo mbalimbali; ambayo inaonekana yanajirudia-rudia kila kukicha.

    Ukiangalia juu juu tu inachekesha, lakini…

  5. Nyongeza tu hasa kwa ndugu Buruda, kuna hadithi naziandika ambazo zinagusa masuala kama haya, na naziandika kwa mtindo huu huu. Humo ndani natumia nafsi ya kwanza ambayo ni sauti ya mwanamke (zaidi ya nusu ya kitabu). Mpaka leo sijui kwanini nilichagua kuandika kwenye mtindo huo. Ila kitabu kinatiririka vizuri tu, ingawa sio cha kusoma mara moja.

    Pia, kuna mambo mengine mengi tu. Kitu kingine ambacho kinasisitizwa hapa ni haiba na hulka fulani ya Politiki na sio Politiki kama mwanamke… Kwanini ametumiwa na watu fulani kutudanganya? Labda wahusika wanajua jinsi ya kumlaghai na kumtumia? Nani ni victim hapo, mume wa Politiki tu au Politiki naye yumo? Kivipi anadhalilishwa wakati yeye ni “victim”?

    Kuna vitu zaidi. Jaribu kuunganisha kila kitu, kila mhusika na kila “jina” halafu utanielewa. Kuna makala nyingine ipo jikoni na hiyo ni hadithi ya kweli (ambayo inatoka kwenye filamu fulani). Usishtuke utakapokuja kuisoma kwasababu itakuwa kinyume kabisa na hii… Nakutaarifu ili usije ukasema nilijisikia vibaya baada ya wewe kuweka maoni yako yenye changamoto. La hasha. Mtiririko umeshapatikana kilichobakia ni kutafuta muda tu.

    Kuhusu hilo suala la overanalysis, sikubali. We chukulia unavyotaka na fikra zako zikupeleke unapodhani ni sahihi (kwa mtazamo wako). Kwa sababu hakuna mtu anayejua kila kitu. Hata kama utachimba zaidi kuliko nilivyodhamiria, basi utaweza kukaribia kilichonisukuma kuandika hii makala…

  6. Hahaa @ SN, nimefurahi ulivyonitoa hofu yangu kwamba waandishi “wana mfumodume kwenye DNA”. Angalau hujaanguka katika kundi la chini kabisa katika uandishi, mwandishi asiyejua anachoandika.

    I am not saying that you subscribe to any of these, but it’s one thing if you say “art should be free of political correctness” na “art for art’s sake” ( nude paintings anyone ?. Look, Flaubert is revered despite the controversy of “Madame Bovary”) and quite another if you are an innocent/ unconscious chauvinist. Contrary to my original post I actually like the realism (as long as it is done consciously and not out of ignorance) and despise moralistic idealism. It just so happens that we have a plague of pungent chauvinism choking the lungs of our language and all the arteries of art.

    I was provoking a conversation to check whether your fountain is poisoned by this decadent spring. Turns out you are one of those somersaulting smart-aleck delibarate marauders using artistic license to the fullest in the name of “kioo cha jamii”.

    I am torn, complimenting you and damning you at the same time.

    But then again, damning you is so Tipper Gore fighting Hip Hop profanity. I would like to hear what the real feminist think.

  7. Hahahaha, Buruda… nadhani “tunafahamiana” vizuri tu. Feminists wanaokuja hapa wananifahamu vizuri sana, kuanzia nilivyolelewa hadi nimekuwa mtu mzima. Wengine wanajua hadi misimamo yangu.

    Tukirudi kwenye mjadala wa sexism, umenikumbusha mwalimu wangu mmoja (wa literature) ambaye alikuwa anajua kuuliza maswali mazuri yanayokupa muongozo wa kuchambua kazi za fasihi.

    Kwa mfano, atauliza:

    1. Lugha iliyotumiwa na mwandishi inaonesha jambo lolote kuhusu ubaguzi wa kijinsia? Ametumia lugha kali au…?

    2. Amemdhalilishe mwanamke? Hajatumia maneno makali kama malaya, kicheche n.k… Mtanzania anaonekana ana hasira ila bado anamuheshimu Politiki?

    3. Mbona bado anamuita Politiki mpenzi/mke? Unadhani bado ana ‘feelings’…? Au kuna uwezekano atamrudia mkewe?

    4. Do you feel any kind of sympathy for Politiki and Mtanzania at the same time? Why (not)?

    Ukiacha hilo la sexism kwenye hicho kipande, kuna suala lingine ambalo mtu akisoma haraka-haraka atadhani nazungumzia “udini”…

    Hoja zako (Buruda) zimenikumbusha kipande hiki cha ushairi wa Fareed Kubanda:

    Amenyaye kwa mdomo siku zote haishi kutema,
    Maisha ni kama kioo ukiyechekea nayo yanacheka,
    Hii mipaka bila uhuru wa fikra ni utumwa wa kifikra,
    Chagua ufe Kijerumani uanguke una tai shingoni,
    Au Mchagga anayeshinda njaa wakati anazo hela mfukoni,
    …Huu sio muda wa kujaribu WENZAKO WANAFANYA KWELI,
    Au hujui bahari tulivu haipimi nahodha wa meli,
    Ona! Wasio na hatia wanapelekwa gerezani…

    Mi’ namuelewa vizuri tu, bahati mbaya wengi wetu tunavutiwa na huu mstari “Mchagga anayeshinda njaa wakati anazo hela mfukoni”, bila kujaribu kuonganisha mambo… Halafu tunasema jamaa anaunganisha mistari tu ili kunogesha ngoma. Wengine watasema Fid Q ni ‘mkabila’. (Nampa jamaa heko zote kwa kuendelea kuandika vitu kama hivi bila kuchoka!)

    Kama ulivyosema, tusubiri mchango wa feminists…

  8. Kabla sijachangia hebu nikumbusheni feminists ni akina nani?

    Nipate kujijua naingia katika kundi gani 🙂

  9. Kibua; from Wiki:

    “Feminism is a collection of movements aimed at defining, establishing and defending equal political, economic, and social rights and equal opportunities for women.”

    http://en.wikipedia.org/wiki/Feminism

    Naona Buruda kaugeuza mjadala kutoka kwenye siasa zetu na kuuelekeza kwenye harakati za feminism. Hata hivyo michango inakaribishwa.

  10. Nikijiangalia kwa chap chap najiona wasfu wa huyo feminist unasadifu kwangu (au ni mie ninaesadifu wasfu wa feminist vile?!)

    Sijaona jambo mahsusi linalomdhalilisha mwanamke kwa ujumla wake kwenye satire hii kwa sababu hatutaki kuwanyima waandishi nafasi ya kutumia mifano wapendayo kwa kuwajaza hofu kuwa wataambiwa wana mfumodume. Kwangu binafsi naona mfumodume zaidi iwapo mwandishi ata attribute tabia za mwanamke mmoja kuwa ni za wanawake wote.

    Nafikiri ukigeuza kuwa msemaji ni mwanamke itakuwa tusi kubwa zaidi kwa mwananamme.

    “Nilipomaliza kupiga dana-dana zangu tu ukaniambia unataka kucheza rada; mchezo wa kike! Nani alikufundisha? ”

    Kama mwanamke kucheza mchezo wa kike ni jambo la kawaida, ingekuwa mwanamme na akaambiwa anacheza mchezo wa kike lingekuwa tusi.

    Labda penye mfumo dume kidogo ni pale panapozungumzia

    “Yaani, jamaa amekuja kutalii kwa siku mbili tu lakini umefanikiwa kulala nae?”

    Kwa mwanamke kulala na jamaa aliyekuja siku mbili inachukuliwa kama big deal lakini kwa mwanamme angefanya hivyo kwa sisi jamii ya kiswahili tusingeshangaa sana. Na sio kwa kuwa wanawake wako radhi kwa wanaume kufanya hivyo,hapana, ni kwa sababu wanawake ‘weshawatolea sadaka’ wanaume

    Ndimi Kibua cha kike

  11. Shukrani Kibua,

    Msiwe na wasiwasi kabisa kuhusu mwandishi kuwa na mawazo ya mfumo-dume.

    Kuhusu hii satire… kwa kifupi, unaweza ukafananisha siasa na mapenzi (ingawa kuna sehemu hapo juu ambapo Politiki anabadilika na kuvaa uhusika wa kiongozi fulani). Hasa ya Bongo; itakuletea visa kila kukicha, wakati mwingine unajua huu ni upuuzi kabisa na unasema sitafuatilia tena, lakini kesho yake au baada ya siku mbili tatu hivi unajikuta unatafuta magazeti yenye taarifa za mwenendo wa siasa.

    Ukiacha hayo, nadhani mmesikia kwamba sekretarieti nguli ya chama tawala imepewa talaka… Mi’ najiuliza hapa, wale walioenguliwa/waliojiengua watakaa mbali au bado wataendelea kuwa na mahusiano na sekretarieti mpya? Ili hali kwa mlango wa nyuma…

    Yaani, kama enzi zile wakati baba wa mwandishi (aliyethamini ujamaa) alivyokuwa anamuendesha mke wake Politiki.

  12. @SN [i]”Mi’ najiuliza hapa, wale walioenguliwa/waliojiengua watakaa mbali au bado wataendelea kuwa na mahusiano na sekretarieti mpya? Ili hali kwa mlango wa nyuma…”[/i]

    Ukiangalia Halmashauri Kuu, bado kuna kazee pale kameweka kuvuruga kura za vijana! Kamati Kuu ndio wamemua kujijaza pale! Kwa kisingizio cha kuwaweka vijana kwenye mstari! Wazee bado wanang’ang’ania madaraka, hawataki kung’atuka.

    Kujivua gamba kwao kwa kweli ni changa la macho kwa wananchi tu!

    nnn

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend