Uwakilishi wa wananchi unaporwa

Na Jenerali Ulimwengu

KATIKA kujadili michango ya watu na taasisi katika safari ya uboreshaji wa utawala na upanuzi wa demokrasia, wiki jana niligusia mchango wa Christopher Mtikila.

Nilieleza kwamba binafsi si shabiki mkubwa sana wa Mtikila, kwa sababu sikubaliani na baadhi ya matamko yake ambayo kwangu nayaona kama yanaudhi na wakati mwingine yanamharibia uwasilishaji wa hoja zake.

Lakini hatuwezi kutaraji kwamba mtu ye yote atakuwa na kila sifa njema na katika kila idara. Sote tunajijua kwamba tunazo kasoro zetu na hizo ndizo zinazotufanya tujue kwamba sisi sote tu wanadamu. Kwa hiyo, zile kasoro ninazoziona kwa Mtikila katika maeneo fulani ndizo zinazonifanya nikubali mchango wake mzuri katika  maeneo mengine, kama hili la upanuzi wa demokrasia.

Nimepata wasomaji wawili ambao hawakupenda Mtikila atajwe kama mtu mwenye mchango wo wote wa maana katika mchakato wa upanuzi wa demokrasia. Hawa wawili walikuwa na masuala waliyoyaibua, na ingekuwa vizuri iwapo wangeleta maoni yao kwa njia ya Barua kwa Mhariri au ingekuwa kupitia blog ambako watu wengi zaidi wangechangia.

Lakini mmoja wao amenisaidia kwa kunikumbusha umuhimu wa kuwa makini na watu ambao wanaweza kuwa chanzo cha vurugu na machafuko, hali inayoweza kutuumiza sote. Hakuna atakayepona iwapo machafuko kama hayo yatatokea, anasema.

Nakubaliana kabisa na msomaji huyo, na iwapo kuna msomaji mwingine mwenye mawazo kama hayo aliyoyatoa msomaji huyu, ningependa ajue kwamba nakubaliana naye moja kwa moja. Jambo ambalo siwezi kukubaliana nalo ni kusema kwamba wale wanaofanya kampeni ili kupanua demokrasia, pamoja na Mtikila, wanatishia amani au wanataka kusababisha machafuko ndani ya nchi.

Inawezekana yapo mambo ambayo yanaweza kuwa chanzo cha machafuko, na ni hayo mambo kwayo hatua za kisheria zinachukuliwa mara kwa mara dhidi ya Mtikila mwenyewe, na wala hapa mimi si mtetezi wake hata siku moja. Ama kwa hakika, nimekwisha kubainisha maoni yangu kuhusu masuala kama hayo.

Lakini nadhani kwamba ni kukataa kuona mantiki kama tutajiaminisha kwamba Mtikila (au mtu mwingine ye yote) anayetetea haki za msingi za raia, basi anataka kusababisha machafuko. Hiyo si kweli.

Ningependa kukariri kile nilichokisema mara kadhaa, nami sina sababu ya kukitilia shaka: machafuko ndani ya jamii hutokana ama na watawala wasioheshimu haki za watawaliwa, ama na uhasama baina ya makundi yanayotaka kutawala. Nafasi ya raia wa kawaida ni ile ya uhanga.

Ukweli ni kwamba Mtikila amesimama mbele na kujionyesha bila woga wowote wakati wengine wakisemea chini chini; amediriki kusema kwa sauti kuu wakati wengine wakinong’ona vijiweni. Lakini ni ukweli vile vile kwamba miongoni mwa wanademokrasia walio wengi, anachofanya Mtikila ni cha msingi, na kinastahili kupongezwa.

Katika mazingira mengine, na tungekuwa na jamii ya watu wanaodiriki kusema wanachokiamini, wala Mtikila asingepata nafasi ya kubeba mabango ya upanuzi wa demokrasia, kwa sababu kazi hiyo ingefanywa na watu ambao hiyo ndiyo kazi yao. Wangejitokeza wanasiasa ndani ya chama-tawala ambao wangewaambia wakuu wa chama chao kwamba ni upuuzi kuendelea kupinga dhana ambayo ni ya msingi kabisa katika haki za raia.

Wabunge wa chama-tawala wangewakumbusha viongozi wao jinsi walivyompoteza Dk. Wilbroad Slaa kwa kung’ang’ania dhana isiyo na maana yo yote isipokuwa kuwanyima raia haki yao. Wabunge wa Upinzani nao wangekuwa wakali zaidi kwa sababu ni jukumu lao pia kuikosoa Serikali pale inapoonyesha wazi kudharau haki za raia.

Endelea kusoma hapa…

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 2 Comments

2
  1. Mi naona ingeanza na kujaribu kubadili katiba ya nchi. Manake mahakama ya kuu ilipitisha ombi la Mtikila, ila serikali (..aka CCM….) ikabana. Manake naona wengi wao wanasema katiba ya nchi hairuhusu. Zaidi ya hapo sioni sababu za msingi wanazozitoa kwa kweli. Labda wenzangu waliofutilia pia hii ishu wanifahamishe. Kwahiyo wakibadili katiba sababu zao zitaisha mi naona.

    Ila last time katiba ilifanyiwa mabadiliko 2000. Sijui inabidi usubiri muda gani mpaka kufanya mabadiliko tena. Nitajaribu kucheki.

  2. Ili kupitisha mapendekezo ya kubadilisha kifungu fulani cha katiba kuna hatua ambazo muswada inabidi upitie. Sijui kama suala ni muda… Inategemea nini kinahitajika.

    Sasa kwenye mambo ya mgombea binafsi, sijui wahusika wanaogopa nini. Ila, kama Jenerali anavyodai, kama watu wangekuwa wanapiga “kelele za maana” labda watu wangeweza kumuvuzisha muswada.

    Of koz, watu ambao ni wahafidhina (maana yake ni ‘conservatives’ kwa nyie mliokimbia darasa la Kiswahili), kwasababu zao ambazo wanadhani ni za “msingi”, wanaogopa. Fikiria, mtu yoyote makini na mwenye mpangilio makini (hizi kampeni ni hela tu) anaweza kuchukua kile kiti nyeti.

    Sasa, swali ni hili: Tanzania iko tayari kwa mgombea binafsi? Kama jibu ni ndio, wa kujilaumu au kuwalaumu ni wapinzani; naungana na Jenerali… CCM kamwe haiwezi ikapendekeza huu muswada! Kwanini wapendekeze kitu kama hiki wakati wao ndio wanaoshikilia “nji hii”.

    Ndio maana Jenerali anasema, ingawa hamfagilii sana Mtikila kutokana na kauli zake matata mara nyingine, hatuwezi kudharau mchango wake ambao unaonekana ni mdogo sana (labda tunadhani Mtikila ni mwehu kutokana na mambo machache ambayo anayosema na tunapingana nayo, kwa mfano Tanganyika/Zanzibar).

    Hata saa ambayo haina betri inasema ukweli angalau mara mbili kila siku.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend