Kugombea uongozi ni kilevi kipya?

Na Kiranga

Mara ya mwisho niligusia umuhimu wa kufuata siasa za sera.Ili kufuata siasa za sera, inabidi kuwa walau na uongozi wenye werevu na haiba fulani unaoweza kwenda na sera. Uongozi unaoweza kuaminiwa kutupa mwongozo wenye mizizi katika sera, na sio kutawaliwa na tabiri za hali ya hewa za masaa ishirini na nne yajayo pamoja na mipasho.

Demokrasia kwa namna ilivyo inaruhusu hata viroja na kutoa uhuru wa mambo hata yale yasiyoyumkinika kutokea. Lakini kwa sababu tu demokrasia inatoa uhuru huu, haimaanishi kwamba yakitokea yasiyoyumkinika tukae kimya. Hususan kama vituko hivi vinatoka kwenye kuwa vituko tu na kuingia katika uvunjwaji wa maadili ya uongozi na sheria za nchi.

Tunashuhudia vituko katika maandalizi ya chaguzi zetu kwa jinsi ambayo hatujawahi kuona. Sidhani kwamba shuhuda hii imeweza kuonekana zaidi kutokana na kuboreka kwa njia za kupashana habari. Aghalabu mfumo wetu chini ya chama kimoja ulikuwa na nidhamu zaidi, ingawa naweza kusema ilikuwa nidhamu ya uwoga.

Hilo kando, najua kuna ongezeko la kujulikana vituko vya kutia aibu kwa mtu ye yote mwenye kufikiri. Baadhi ya wataka ugombea, hata baina ya chama kimoja, wameacha kupigana vijembe vya kisiasa, na kuanza kupigana ngumi (mfano Shyrose Bhanji). Ukisema hayo mambo ya ngumi ni nasibu za mjini tu, nitakwambia kuna kisa kingine cha huko Mwibara ambako Charles Kajege na Cyprian Musiba walirushiana ngumi pia. Tukubali tu visa hivi vinaonekana kuongezeka.

Hata kwa wengine wasio hulka ya ngumi, uwezo wao mdogo unaumiza kuliko pigo la ngumi ya Tyson enzi zake. Mgombea mmoja kasema mtu yeyote anaweza kuwa mbunge, pamoja na kukiri kwamba hajui vifungu vya msingi kabisa vya katiba yetu (Regia Mtema). Mwingine, anayesemekana kuwa msomi wa haja, kapita kujinadi na vyeti vya vyuo mikononi (Mpoki Mwambulukutu). Kuna vituko vingine vingi kama vya kufanya kugombea uongozi kuwa tiba ya kujenga kujiamini, Zamaradi Nketema wa Clouds FM, na bila shaka wengine wengi ambao hata hatuwasikii. Vingehitaji kitabu kizima kuviorodhesha kikamilifu tu. Almuradi kila mtu anakuja na kituko chake na kufanya uongozi wetu kuwa kama kile rais mstaafu Mwinyi alichokiita “kichwa cha mwendawazimu,” ambacho ye yote asiyejua kunyoa anaweza kujifunza bila matatizo.

Kuna wengine watapenda kuwa na maoni yanayotetea nafasi za raia kutumia haki zao za kikatiba, na kwa kweli sipendi kuonekana kama mpinga haki za kikatiba, napenda kujiona kama mtetea uhuru wa wananchi. Marekani walishawahi kuwa na chama ambacho kaulimbiu na itikadi yake ilikuwa ni “kutojua kitu” (The Know-Nothing Party).

Uingereza kuna watu mpaka leo wana chama kinachosimama katika mimbari na kupinga kanuni ya fizikia ya uvutano (anti-gravity platform, soma makala hapa). Ninachosema ni kwamba, yasiyoyumkinika yanaruhusiwa hata kwenye demokrasia zilizokomaa. Lakini napenda kusisitiza tena kuwa, haki hizo hizo zinazowapa watu uhuru wa kufanya kampeni za vituko, bila kutuambia kipya watakachofanya, ndizo zinazonipa uhuru wa kuumbua mtindo huu. Afadhali hata hao wenzetu washakubali kuwa wanatumia dhihaka kama sehemu ya kuyapa umaarufu maswala fulani; sisi tunachanganya dhihaka isiyo wazi na uongozi wazi wazi.

Nasaha
Nasaha za B. Russell.

Ingawa kuna wengine wanatetea kuzidisha kiwango cha elimu rasmi inayotakiwa katika uongozi, binafsi sipendelei hili. Naona hii ni kutafuta majibu rahisi kwa maswali magumu, pamoja na kuiminya demokrasia iliyo wazi. Nimeshawahi kutoa mfano kama wa rais anayemaliza muda wake wa Brazil, Luiz Inacio Lula Da Silva, kama mtu ambaye hajapata elimu rasmi, lakini amesoma katika chuo cha maisha. Ameweza kuendesha uchumi wa Brazil vizuri mpaka sasa inajulikana kama moja ya nchi zenye maendeleo makubwa kabisa za BRIC (Brazil, Russia, India na China).

Rais aliyemtangulia Lula alikuwa Fernando Henrique Cardoso, msomi aliyetambulika dunia nzima, lakini hakupata mafanikio kiuchumi kama Lula Da Silva. Baadhi ya walaghai wakubwa ni hawa walioenda shule maarufu kabisa duniani bila kuelimika (mfano Andrew Chenge, UDSM, Harvard). Ni muhimu kutofautisha elimu na elimu rasmi. Na ingawa naelewa umuhimu wa elimu rasmi — siipigi vita kwani inasaidia sana kumpa mtu upeo pamoja na kumfungulia milango — jinsi mtu atakavyoitumia si lazima iwe vizuri. Elimu rasmi ni kama moto, unaweza kuutumia kupikia chakula (vizuri) au kuunguzia nyumba (vibaya). Tuwapime watu kwa kazi zao, sio kwa vyeti vyao.

Kwa mfano mdogo tu, kuna wazee vijijini hawajasoma elimu rasmi lakini wana busara na maadili. Na kuna watu wana elimu rasmi lakini hawajaelimika kwa sababu wanaweza hata kuuza mama zao kwa vipande thelathini vya fedha. Kwa nini tusiwaache walaghai hawa na kusema kwamba hawa ni wachekeshaji tu ambao wana leseni ya demokrasia? Uongo na maigizo ya ulaghai yakirudiwa sana bila kukemewa yanaweza kuonekana kama ukweli. Katika rekodi zake kuhusu vita ya pili ya dunia, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Winston Churchill alieleza (WWII Vol. 1 “The Gathering Storm) ni jinsi gani Waingereza, hususan viongozi waliokuwa madarakani kabla ya vita vya pili, wangeweza kumshikisha adabu Adolf Hitler na kumzuia kukusanya nguvu za kijeshi baada ya mkataba wa Versailles; wangemjua huyu mtu ni kichaa aliyekubuhu hata kwa kusoma kitabu chake cha “Mein Kampf” tu. Badala yake wakampuuzia, wakaiacha kansa ambayo ingeweza kukatwa mapema ienee mwili mzima na kushindikana. Unaweza kusema hatuna Hitler, lakini kwa nini tukubali kungoja mpaka kansa ya kutaka uongozi kwa ulafi tu bila uwezo iote mizizi?

Tuikemee mapema. Kuna wengine wanaweza hata kusema kwamba hii kansa ishaota mizizi mirefu tayari. Hili hata kama ni kweli lisitukatishe tamaa, bali litupe shauku zaidi ya kukataa usanii.

Tumeshaona kwamba katika mfumo kama wetu ambao haujaimarika kiufuatiliaji na kuwa na mizani inayofaa, mara nyingine wachekeshaji kutosemwa kunawajengea kuaminika na wanaishia kwa nasibu kuwa viongozi wetu. Nikiweka pembeni ulimbwende wa soni na staha za kisiasa ambazo zinaweza kunitaka nisimhukumu mtu, napata maswali kama “Hivi hata huyu naye anataka uongozi? Hana hata aibu? Atatuongoza nini sasa?” Kuna watu ambao washajaribu madawa ya kulevya karibu yote, wameyachoka, na sasa wanaona kugombea uongozi ni sawa na dawa mpya ya kulevya. Wanaona raha kuhutubia watu hata kama hawana kipya cha kusema wala uzoefu wowote wa kutufanya tutake kuwasikiliza.

Mwanafalsafa wa Kiingereza, Bertrand Russell, katika miaka iliyofuatia karibu vita vikuu vya pili aliandika, “Jambo la msingi kabisa linalosababisha matatizo duniani leo ni kwamba wajinga wanajiamini sana wakati wenye maarifa wamejaa shaka.” Shaka hii na kiasi ni muhimu katika kuhakikisha mambo hayaendi bila kurejewa na kurejewa tena. Ndiyo maana jamii za kisayansi zinaamini katika kuchunguza na kuchunguza zaidi. Kwa hivyo sitaki kuishambulia kabisa. Lakini dozi gani ya shaka na kukaa pembeni kama mwanafalsafa wa Ugiriki wa kale, mwenye maongezi zaidi na matendo machache, itafaa wakati tunaona wasio uwezo wala uelewa wakiparamia mimbari za kisiasa bila hata staha wala haiba, sembuse uwezo na nia? Tukiwaachia, halafu kwa kuwa hakuna hamaki miongoni mwetu, wakiweza kupata uongozi na kuboronga mambo tutalalamika?

Sitasahau kauli ya mgombea mmoja wa ubunge miaka kadhaa iliyopita, akiwaelezea wapiga kura wa Tanzania kwa kutumia msemo, “Nzi milioni moja hawawezi kukosea wote katika uchaguzi wao wa kula kinyesi.” Kwa maana ya kwamba, wapiga kura ni kama nzi, na wananchi wanapochagua uongozi mbovu, huwezi kuwalaumu kwa chaguo lao dhati. Lakini vipi kama hili linatokana na ukosefu wa habari, uchambuzi, kupandisha vigezo vya uwajibikaji na utamaduni wa uwazi miongoni mwetu?

Inataka moyo kuweza kusema mambo fulani. Kwa mfano, katika jamii ambayo inaonekana kuwa na uwakilishi mdogo wa vijana na wanawake, unawezaje kuanza kuwashambulia wagombea wote wasio makini, pamoja na vijana na wanawake wasio uwezo na uelewa wa kutosha? Kwa watu wenye kufikiri kwa kutumia kigezo kimoja, wanawake na vijana hawa wanaweza kuwa hawasemeki, ukiwasema unaonekana mpinga wanawake au mpinga vijana.

Lakini kama ninavyokataa kuunga mkono upinzani kwa sababu ni upinzani tu, ingawa kifalsafa naweza kuwa naelekea kupenda upinzani kuliko chama tawala, vivyo hivyo ingawa kifalsafa mimi ni mpenzi wa kuona uwakilishi wa vijana na wanawake unaongezeka zaidi, lakini hili halinizuii kuuliza maswali, wagombea hawa vijana ni wa aina gani? Wanawake wa aina gani? Kumkubali kijana kwa sababu ni kijana tu, au mwanamke kwa sababu ni mwanamke tu, ni kutukana uwezo wa kufikiri wa vijana na wanawake.

Alexis de Tocqueville, yule Mfaransa aliyeandika kwa kirefu kuhusu demokrasia ya Marekani na vipi mafanikio yake yangeweza kuigwa sehemu nyingine, alionya kuhusu demokrasia kuwa na tabia ya “imla ya wengi.” Kwa kweli imla hii ni nzuri kama wengi hao wanaelewa kuitumia. Lakini vipi kama imla hii katika mfumo usio na elimu ya uraia wala utamaduni wa kuwajibishana inageuka kuwa hundi isiyojazwa, inayompa nafasi ye yote mwenye ujanja-ujanja wa kusema tu kuongoza? Hatuwezi kukaa kimya.

Tuchukulie mfano wa mbio za urais, ambazo nazo zimetupa rais msanii aliyeweza kupita vikingo vihunzi vyote kwa sababu hatukuwa na uchunguzi wa kutosha, na sasa hivi tunaona matokeo yake. Baada ya kutoa sifa za mgombea urais mzuri mwaka 1995 katika mkutano na waandishi wa habari Kilimanjaro Hotel, Mwalimu Nyerere aliulizwa swali na Eda Sanga wa Radio Tanzania (siku zile) kwamba, mbona hizo sifa zinaonekana kama hakuna mtu anayeweza kuzitimiza? Mwalimu alijibu kwa kusema katika nchi ya mamilioni ya watu haiyumkiniki kuwa hamna watu wenye uwezo. Na Mwalimu alikuwa sawa, haiyumkiniki kuwa hatuna watu wenye sifa za uongozi. Tatizo linakuja tukianza kuwatafuta, wako wapi? Hawaonekani, hata tukiamua kwamba hatutafuti malaika na tutakubali mawaa ya kibinadamu ya hapa na pale — nani asiye mawaa? — bado tunaona tunaangukia mbali sana na sifa za kiongozi bora.

Ni kama vile wale wenye sifa za uongozi, kutokana na werevu wao pamoja na kuelewa kwamba ili kupata uongozi inawabidi wajiingize katika maigizo ya kushusha utu wao, wameamua kukaa mbali na siasa. Katika huku kukaa mbali na siasa, wamewaachia watu wanaofikiri sifa pekee za uongozi ni kujiamini na ulafi wa madaraka unaokwenda kwenye ujivuni-kichaa (egomania). Chaguzi zetu zinazidi kuwa za fedha, sheria mpya ya gharama za chaguzi bado ina mianya mingi ya rushwa, na hata pale inapotoa mipaka ya kisheria, mipaka hii katika kutoa misaada ya kifedha kwa vyama vya siasa; kwa mfano inaruhusu kutoa pesa hata zaidi ya nchi tajiri kama Marekani zenye sheria kama hii. Kimsingi sheria inafanya mianya ya rushwa iwepo kisheria. Kuingia katika uongozi leo ni lazima uwe mtu wa makundi yaliyojikita katika kushinda chaguzi zaidi ya kuongoza; uuze utu wako kwa vyama vya siasa visivyo muelekeo, au uanzishe chako kutoka mwanzo na kuombea kwamba wajanja hawata ku-Mapalala ukishajenga chama imara.

Sasa unaweza kuuliza mtu mwenye uwezo, nia na sifa za kuongoza ana matumaini gani katika mfumo kama huu? Mimi naona ingawa ni muhimu kupata watu wenye sifa katika nafasi za uongozi rasmi (nawatia moyo kugombea nafasi), kama kuna staha na shaka za kisomi zinazowazuia watu hawa kujiingiza katika maigizo haya yasiyo kichwa wala mguu, basi wasisite pia kujiingiza katika vikundi visivyo vya kijamii katika kujaribu kubadilisha mfumo ili uruhusu wenye sifa za kweli kushiriki kikamilifu.

Wasitupe kaa na gando. Hivi tuna vikundi gani vya kusaidia wananchi kuwasiliana na wabunge wao? Wangapi wanawaandikia wabunge wao?

Badala ya kuendelea kidemokrasia, kuna ushahidi kwamba tunarudi nyuma. Huhitaji kuangalia mizani kama ya Mo Ibrahim, Transparency International, Freedom House na REDET kuona kwamba demokrasia yetu inapoteza maana; inageuzwa kuwa dawa mpya ya kulevya kwa walevi sugu wachache waliokubuhu kila kilevi, na sasa wanaotafuta kilevi cha jukwaa la kuhutubia watu, kuandikwa magazetini na kujisikia kwenye redio.

Je tunaweza kumudu kuwaachia wale wanaoona uongozi ni zawadi ya mchezo? Uongozi ambao lengo lake pekee ni kushinda na kushinda tu, bila ya kujali utafanya nini baada ya kushinda? CCM wanatumia kaulimbiu “Ushindi ni lazima” kwa sana sasa, tunashuhudia unazi na ushabiki unaingia katika chama kwa namna ya rasmi sasa. Badala ya chama kutuomba wananchi tukishindishe kwa taadhima na heshima, tunaambiwa kwamba lazima chama kitashinda. Je chama hiki kinaweza kuwalaumu watu wakisema kwamba kishaandaa mpango wa kuiba kura kama kitashindwa kwa kura? Kishasema “ushindi lazima” ati, vipi watu wakikikataa?

Demokrasia ni jungu kuu lisilokosa ukoko, na mara nyingine hususan pasipo wali, ukoko unaweza kufaa. Lakini hili halimaanishi tuache jungu lote liungue na wali kuwa masizi kwa kisingizio cha “Jungu kuu halikosi ukoko.” Ni wakati wa kuchukua hatua za dhati kuhakikisha tuna uongozi bora zaidi; kutoruhusu walaghai waliokosa shughuli kuvamia uongozi, na kufanya kazi kwa vitendo ili kuboresha siasa na uchumi wetu, hata kama ni kwa hatua za mtoto anaejifunza kutembea kwa kuanzia. Kila mmoja wetu ajiulize leo, nimefanya nini kuendeleza hatua hizi?

*      *      *

Makala za awali zinazohusu mada hii ya uongozi:

Hatuna Kiongozi

On colloquialism, the genesis of an incoherent non-policy politics (I)

On colloquialism, the genesis of an incoherent non-policy politics (II)

Previous ArticleNext Article
Joji was born and grew up in Dar es Salaam, Tanzania. He graduated with a B.Sc in Biochemistry in Germany, and is now pursuing a Masters degree in Microbiology & Immunology at the Swiss Federal Institute of Technology (ETH) in Zurich, Switzerland . Joji is particularly interested in matters related to global health, and basic science research that tackles public health challenges. He is engaged in mentoring Tanzanian students in higher education issues, most notably at the Kibaha High School. In this capacity, Joji blogs with Vijana FM about scientific research and development, and how youth can gain greater access to higher learning.

This post has 9 Comments

9
  1. Unajua kuna viongozi wengine tulio nao huwa ninajiuliza tunawaruhusu vipi waje mbele na kudai kura? Mtu kama Aden Rage, ambaye alipata kufungwa kwa kosa la wizi wa mamilioni ya shirikisho la soka Tanzania. Leo hii anaomba kura za ubunge kule Tabora, halafu watu wanamshangilia kwa vigelegele.

    Je, tukipata viongozi kama wale mwanafalsafa Plato aliowasimulia kwenye the Republic haitakuwa safi? Yaani kiongozi atakayefaa lazima awe philosopher?

    Pia, kama ulivyogusia, sioni umuhimu wa kushikilia kauli mbiu ya vijana wawe viongozi kisa tu tunataka kijana. Siko tayari kwa mtu kama Nakaaya awe kiongozi wangu, kwasababu tu ni kijana, na eti kuwa ameimba nyimbo kuwaponda wanasiasa. Tutafute uwezo kwanza, na hizi category za elimu, umri na jinsia vifuate.

  2. Natumaini tukiongeza kiwango cha elimu rasmi pamoja na namba ya watu wanaoelimika na elimu hii, tutaongeza uelewa wa wananchi kiujumla na kufanya uongozi uwajibishwe zaidi.

    Sasa hivi watu wanapelekwa pelekwa tu sanasana kwa sababu hawana elimu. Kweli elimu rasmi haina guarantee ya kutoa watu walio ethical, lakini wakielimika wengi angalau uongo uongo wa kijinga na propaganda mbuzi itakuwa kazi kuupa nafasi. Tutakuwa na ma watchdog kama hii site wengi watakaofuatilia vitu na wananchi watapata picha kamili zaidi. Ni vigumu kufanya yote haya kama kiwango cha elimu nchini bado ni kidogo na mwanafunzi wa chuo kikuu mwaka wa kwanza anaitwa “msomi” .

  3. Kiranga, makala imeenda shule!

    Sasa, mimi naamini kuna watu ambao wanaweza kuwa viongozi wazuri tu Tanzania. Je, kutojitokeza kwao ni uwoga wa kuingia kwenye “tope”, au kutopenda kujishushia hadhi zao? Hii ni sababu ya msingi kweli?

    Kama ulivyosema, nadhani wengi tunafikiri kiongozi lazima awe mwanasiasa tu. Hapo wengi ndipo tunapopotoka na matokeo yake tunawaachia vitu vyote wanasiasa. Kibaya zaidi, ni kwamba tunataka, tunategemea au tunatumaini maendeleo au mabadiliko yatatokea (tu).

    Lakini kuna shughuli nyingi sana za kijamii ambazo vijana wanaweza kufanya; hili ndilo wengi hatulifikirii… Ukiacha hayo, tukubali ukweli kwamba “kuamsha” Watanzania ni kazi nzito mzee (hapa namaanisha, watu kukaa chini na kubadilishana mawazo, halafu mwishowe kila mtu akaondoka na ujuzi zaidi). Mpaka siku ambapo wengi wetu tutaanza kukubali kukosolewa na kujifunza kutoka kwa watu wengine, ndipo tutaanza kuona mabadiliko — huo ndio mtazamo wangu.

    Pia, ningependa kuuliza: nimeona nchi nyingi watu wakifundwa kuwa viongozi. Unadhani hii inawezekana au inahitajika Tanzania? Yaani vijana waanze kufundishwa majukumu yao na kupewa mzigo wa kuwa viongozi — kwenye nyanja mbalimbali — huko baadae?

  4. Ningependa kuwakumbusha wagombea wanaojinadi kwa kutumia ‘ujana’ wao kuwa kundi la vijana linaanzia kwa raia wenye umri wa miaka 18 (umri wa mpiga kura).

    Ili kumvutia kijana huyu mdogo kwenye harakati za siasa na uongozi kwa jumla, muonekano wa mgombea na namna anavyojiweka (appearance and attitude) vinachukua nafasi kubwa kwa kwa vile bado vijana chipukizi hawajakomaa kuvutiwa na misimamo pekee au maono ya mgombea.

    Hatuwezi kutarajia kuwavutia vijana wadogo iwapo wagombea vijana hawaonekani kuwa watanashati* au iwapo wataruhusu kuonekana kama watu wazima** wa kulingana umri wa mama/baba nyumbani wa hao vijana chipukizi.

    * Tumeona video za mgombea mmoja kijana akiwa ameroa jasho na kikwapa mpaka kitovuni kabla ya kuanza kuwahutubia wananchi jimboni, tumeona wagombea wengine walioenda kwenye midahalo inayorushwa nchi nzima wakiwa na fulana za mistari, cap ya chama, na mwengine pinafore ya kitambaa cha mpira ya mchanganyiko wa rangi)
    Iwapo huwezi kuwa kwenye muonekano huo kwenye mkutano wa kunadi bidhaa tu za kampuni yako kwa wadau ofisini, inakuwaje uonekane hivyo kwenye kazi ya kugombea ubunge?!

    ** Kuna wagombea ‘vijana’ ambao kimuonekano wamejiweka kama watu wazima sana kiasi cha kuwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 hawawezi kuamini kuwa mgombea anaweza kufahamu matatizo yake kama kijana.

    🙁

  5. Utirio uliomo katika hii makala unaelimisha. Unajua mazingira na historia ya nchi yetu ni ya kipekee, ila kuna umuhimu wa kupata chambuzi kama hizi zinazolinganisha yanayotokea nchi nyingine na hapa kwetu, bila kuondoa uhalisi wa hoja.

    Kuhusu mada. Mara nyingi mitaani kwa juu juu tukiongelea uongozi wengi tayari wanapata picha ya kuwa kiongozi mwanasiasa. Mi ninadhani kiongozi ni yeyote mwenye uwezo wa kuwavuta wengi wajiunge naye kwa kutumia hoja zinazokidhi. Kuna mtu hapa alisema awali, ujanja ujanja wa viongozi wetu, ndio taswira ya jamii yetu wenyewe. Kwakuwa wengi wetu hatupo makini kufuatilia mambo ya kitaifa, kuuliza maswali, kupigania haki, na kupendelea njia za mkato basi viongozi wetu tunaowachagua nao huwa na sifa hizo hizo tulizonazo. Our leaders reflect part of our mental make-up.

  6. Kuna usemi unasema usiseme jambo kabla ya kufanya utafiti,jamani mimi Cyprian Musiba sikupigana na Kajege kama ambavyo watu walivyokuwa wanapotosha wakati ule wa kura za maoni CCM. Kilichotokea tulitofautiana sera na mitazamo.

    Tatizo kubwa lililopo kwa sisi waandishi wa Tanzania tumekuwa tunaandika makala ama habari bila utafiti wa kutosha, ama kumuuliza muhusika ama wahusika, tunakurupuka tu tumesikia jambo mwaandishi anaandika bila hata kujua kiini ama chanzo cha habari yenyewe pengine kasikia ama kusoma katika magazeti. Waandishi wa Tanzania tubadilike coz kama sheria ya habari itatumika kisawasawa vyombo vingi vya habari vitafungiwa kwa kuandika habari ama makala bila utafiti.

  7. Bw. Musiba,

    Habari hizo zilipatikana katika magazeti ya nyumbani, na kwa kadri tunavyojua hazijawahi kupingwa mpaka leo. Usipopinga tuhuma mbaya moja kwa moja unakubali tuhuma hizo kuchukuliwa kama za kweli.

    Hii habari tayari ilikuwa katika public domain. Uliona Gazeti la Mwananchi? Umefanya nini mpaka sasa? Mfano wako ni sehemu ndogo tu ya mmomonyoko wa maadili ya uongozi nchini mwetu. Hata kwa kukubali habari potofu — kama kweli ni potofu — ziandikwe juu yako bila kusahihisha, unatuonyesha kwamba si mtu wa kufuatilia mambo.

    http://www.mwananchi.co.tz/news/5-habari-za-siasa/3526-takukuru-ccm-wacheza-kombolela.html

    “Habari hizo zilifafanua kwamba, Kajege alizuiliwa na wasimamizi kabla ya kurushiana ngumi, hali hiyo ambayo ilikuwa inatishia amani kwenye mkutano huo.

    “Inadaiwa kwamba, Musiba kila alipopanda jukwaani alikuwa akimrushia tuhuma Kajege kuwa si mwadilifu, hafai kuchaguliwa tena na amekuwa akitumia fedha za jamii kwa maslahi yake ikiwa ni pamoja na zile za jimbo.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend