Uchaguzi 2010: Vyombo na vyanzo vya habari

Leo hii Msajili wa Vyama akitangaza chama kipya cha siasa kinachoundwa na kabila fulani moja tu Tanzania, wengi tutashtuka, kisha wachache wataanza kuhoji. Kama hiyo haitoshi, wachache sana wataweza kuliangalia suala zima kwa ‘jicho la tatu’, kulichambua na hata kujaribu kutabiri mwelekeo wa nchi iwapo makabila mengine yatafuata mkumbo na kuunda vyama vyao.

Ngoja kwanza. Kama aya iliyopita imekufanya uanze kujiuliza maswali mengi, basi jua fika kuwa hilo ndilo lengo hasa la hii tovuti; kuwakutanisha watu — hasa vijana — na kubadilishana mawazo, kwa maana hatuamini mtu au kundi la watu fulani linajua kila kitu.

Tanzania, kama jamii nyingine yoyote ulimwenguni, ina mazuri na mapungufu yake. Hivyo itakuwa jambo la busara kuangalia nini kilitokea kwa majirani zetu ili kujifunza mawili matatu. Hii itatusaidia kuzuia maafa yoyote yanayoweza kutokea huko mbele.

Kama unadhani jamii yetu ni “takatifu” na haiwezi kukumbwa na majanga yaliyowakumba majirani zetu, nakusihi ujaribu kupembua mambo kwa kina ili uujue ukweli.

Kabla ya kuzama kwenye mjadala wa matumizi ya vyombo na vyanzo vya habari kwenye mchakato mzima wa Uchaguzi, itakuwa vema ukisoma makala ifuatayo ili tuweze kuelewana vizuri: Spreading the word of hate (Kenya). (Usiwe mvivu kwasababu tu makala ni ‘ndefu’; uzito wa haya mambo huhitaji mijadala ya kina!)

Taarifa au kampeni?

Kampeni zilianza kwa mwamko wa aina yake, ambao nadhani haujawahi kushuhudiwa katika historia ya Tanzania. Lakini, kwa mtazamo wangu, kulikuwa kuna walakini jinsi matukio mbalimbali yalivyokuwa yakiripotiwa.

Baada ya kuwa mtu mzima na kupevuka kifikra nimeondokana na ile dhana ya “kuamini” kila taarifa ninayopokea. Nafikiria mambo mara mbili-mbili na kuhakiki kwa kutafuta taarifa zaidi (au nyingine) kwenye vyanzo vingine vya habari.

Ingawa nilikuwa ughaibuni, nilikuwa nina shauku kubwa mno ya kutaka kujua na kupata picha halisi ya mambo yanayojiri kwenye majimbo mbalimbali. Kuna wakati nilikuwa natembelea tovuti na blogs zaidi ya kumi kwa siku ili kupata picha halisi.

Labda unajiuliza, nini kilinisukuma kutembelea vyanzo vingi vya habari? Si kupoteza muda tu?

Baada ya vyama mbalimbali kuzindua kampeni zao, watu wengi, hasa wa vyama vya upinzani, walilalamika kutotendewa haki kwenye taarifa za habari. Na baadhi ya watu hawakusita kuanzisha vyombo ambavyo vilikuwa vinafuatilia kila chama kinapewa muda gani kwenye taarifa za habari.

Ingawa suala la muda ni muhimu, mimi niliamua kufuatilia jinsi matukio yalivyokuwa yakiripotiwa. Kimantiki ni kama ilivyokuwa inafanyika hapa. Kwa mtazamo wangu, kitu ambacho niliona na kinapaswa kuangaliwa kwa ‘jicho la tatu’ ni ile hali ya “utengano” (namaanisha polarization) wa maoni na mawazo ya watu, na hata matumizi ya lugha kwenye habari na mijadala mbalimbali. Kibaya zaidi, maoni ya wasomaji wengi yalikuwa hayana hoja, kitu ambacho kinakufanya ujiulize maswali mengi.

Siku chache kabla na wakati wa Uchaguzi

Bahati nzuri nilirudi nyumbani, Dar es Salaam, wiki moja kabla ya Uchaguzi na kushuhudia kilichokuwa kinaendelea. Hali halisi ilikuwa sio tofauti sana na ile picha niliyokuwa nayo. Kumbuka ya kuwa nilikuwa ninatembelea vyanzo lukuki vya habari; kinyume na kwenda kwa Michuzi au Jamii Forums tu na kuridhika na nilichoona pale.

Hali ilikuwa shwari, ila mwamko wa vijana ulikuwa ni wa kipekee sana! Kila kijiwe, kila sehemu, kila mtu alikuwa anazungumzia Uchaguzi. Cha kufurahisha zaidi ni kwamba baadhi yao walikuwa wana hoja, tofauti kabisa na makelele niliyokuwa nayaona kwenye blogs.

Siku yenyewe ya Uchaguzi ilikuwa na matukio mengi. Sasa, hapo ndipo ile “jinsi” ya kuripoti mambo ilipochukua kiti cha mbele kabisa kwenye hafla. Maneno “kasoro ndogo ndogo” yalikuwa yamejaa kwenye vinywa vya wana-habari wengi sana. Ila wachache mno walikuwa na kiburi cha kukemea hizo “kasoro ndogo ndogo.”

Vinyonga

Nitakuwa sijatenda haki kama nisipogusia vitendo vya wana-habari na waandishi wa TBC 1. Vituo mbalimbali vya runinga vilianza kutanganza matokeo ya awali, yakiwemo ya Urais, kutoka kwenye kata mbalimbali. Na tarehe 1 Novemba, wakati naangalia TBC, nilidhani naangalia kituo tofauti cha habari! Kwa mara ya kwanza walialika mgeni ambaye alikuwa anakosoa mwenendo mbaya wa uongozi, na kueleza labda hiyo ndio ilichangia kambi ya upinzani kuelekea kupata viti vingi Bungeni.

Nikashindwa kujizuia kuhoji: je, ule mjadala ungekuwepo kama upinzani usingeelekea kushinda majimbo kadhaa? Walikuwa wapi kabla ya Uchaguzi?

Pia, kama ulikuwa makini, utagundua kulikuwa na mabadiliko ya mwenendo wa blogs fulani maarufu kwenye utoaji taarifa. Yaani, ghafla kulikuwa na taarifa kutoka kambi ya upinzani!

Chanzo cha matokeo na taarifa za matukio

Sijui kama ilikuwa ni busara au la kusitisha zoezi la utangazwaji wa kura za Urais kutoka kwenye kata mbalimbali. Ila nina uhakika unapata picha tete kama matokeo ya awali yangetofautiana kabisa na yale ya Tume ya Uchaguzi.

Bahati mbaya au nzuri, wote tukaishia kwenda Jamii Forums ili kupata taarifa za matokeo na matukio mbalimbali haraka zaidi. Bahati mbaya,  mambo yalikuwa kishabiki zaidi na nilisikitishwa na kitendo cha viongozi kuacha watu waandike chochote kile wanachotaka; kiwe na lugha za kukashifu, kusifia, kukosoa, kuelemishana au hata kutoa taarifa tu.

Labda unaweza ukanipinga kwa kusema hiyo ndio ‘demokrasia’ ya kweli, kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni na mawazo yake.

Kumbuka, hivi vyombo vya habari vinakuja na dhamana, hasa pale watu wengi wanapovitegemea kupata taarifa nyeti. Visipotumiwa ipasavyo ndio hapo tunashuhudia majukwaa muhimu yakigeuzwa kuwa vyombo vya propaganda; na kushindwa kutupa picha halisi.

Lakini kulikuwa na watu wachache ambao hawakuchoka kuulizia “data” au “namba” kila mtu alipoleta taarifa. Jiulize, hao ni sehemu gani ya jamii yetu? Watu wangapi hupenda kuhakiki taarifa au habari fulani?

Mwishowe, kwasababu wengi wetu hatuwezi kufikiri wenyewe na kuuliza maswali ya msingi, tunaishia kwenda kwenye vyombo ambavyo vinaakisi mawazo yetu tu. Hatupendi kusikia mawazo mbadala ambayo hayatufurahishi. Yaani, kwa maneno mengine, tunapenda kwenda sehemu ambazo zina watu wenye mawazo kama yetu tu.

Hebu fikiria, tuwe na majukwaa mawili ambayo yana wachangiaji wenye fikra na mawazo (namaanisha porojo) yanayokinzana kabisa. Kila kundi litaamini wanachojadili kila siku kwa dhati. Itakuwaje hawa watu wa makundi husika wakikutanishwa mitaani?

Naamini Uchaguzi wa mwaka 2015 utakuwa una mwamko zaidi. Na kama hatutarekebisha kasoro zilizojitokeza — hususan jinsi ya kuripoti — basi tutaishia pabaya.

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 6 Comments

6
  1. Kwahiyo ndio kusema msisimko ulio kwenye blogs nyingi hauna reflection ya vitu vilivyopo kwenye main street au? Ila ukweli ni kwamba nadhani kuna exaggeration nyingi sana kwenye blogs hasa kwa kuwa ni rahisi kuna na fake IDs na kusema chochote utakacho. Information goes viral but the authenticity is questionable… Angalau hapa VFM sijaona watu wakiweka points zisizo na kichwa wala miguu, references are quite important.

  2. Mwamko na msisimuko upo, ila ukiwa unasoma maoni kwenye baadhi ya tovuti unaweza ukadhani Tanzania kuna na machafuko makubwa — ingawa kulikuwa na fujo za hapa na pale kwenye sehemu chache. Naelewa yule jamaa ambaye gari lake lilichomwa moto Mwanza atakuwa na mtazamo tofauti kabisa (Unaona; nimejifunza kuwa na uwiano unaoakisi hali halisi).

    Kwa mtazamo wangu, blogs nyingi (hasa maoni ya watu) zilikuwa na bado zipo far too polarized. Sijui kuna tovuti gani ilikuwa inafanya kazi vizuri kuliko wavuti.com — kwenye kuripoti matukio mbalimbali ipasavyo bila ushabiki (na huyu hakusomea uandishi wa habari).

    Kuna tofauti kati ya “Mongela aangushwa” na “Mongela chali!” Sijui umenielewa?

    Lakini hata sehemu ambapo mtu alijitahidi kuripoti ipasavyo (kwenye tovuti za magazeti), bado maoni ya watu yalikuwa na utengano sana kama nilivyosema — maoni ni ya kishabiki zaidi, kitu ambacho kinaleta mashaka sana. Na sehemu nyingine inaonekana kama vile watu wa chama fulani hawaruhusiwi; au watu wa CCM au ambao hawashabikii CHADEMA/CUF hawatumii mtandao??

    Cha kusikitisha, ingawa kulikuwa na mwamko mkubwa, idadi ya waliojitokeza kupiga kura ilikuwa ndogo mno (milioni 8; najua suala la majina ya wapiga kura kukosekana kwenye vitabu vya wapiga kura limechingia kwa kiasi fulani). Nina uhakika wale ambao waliamua wenyewe kutokwenda kupiga kura wanajuta sasa hivi na lazima watajitokeza mwaka 2015.

    Mtazamo wangu: hatujaweza kutumia majukwaa ya kubadilishana taarifa ipasavyo na tusipobadilika tunaweza kuishia pabaya.

    Au ndio yale ya “Simba kumla mtu ni hadithi; lakini mtu kumla simba ni hadithi ya kusisimua”? [Fid Q]

  3. Mimi sidhani kama ni jambo baya kuona kundi la wafuasi wa mtazamo fulani kutumia chombo chochote kile kuweka mawazo yao bayana, ili mradi tu mtoa hoja awe na facts, na awe na uelewa wa hoja zinazoweza kupingana na za kwake.

    JF inaonekana kushabikia upinzani kwa kuwa tu hakuna chombo chochote mbadala kama hicho chenye kuwapa watu hao fursa ya kutoa maoni anonymously, in real-time, back-to-back, in aggregated form. In actual fact wapo wachangiaji mule walio’critical na pande zote, ila ndio, ni wachache mno.

    Umeona mwenyewe TZ, kuanzia televisheni, radio, na mpaka magazeti media houses zote ni pro-establishment (remember onyo la serikali kwa Mwananchi?), sasa wananchi wenye mtazamo tofauti wakimbilie wapi kujadili hoja zinazopinga utawala?

    Lisilofaa kwa mtazamo wangu ni chombo kujiita cha ‘umma’ na wakati huohuo kupendelea upande mmoja, hasa kuhusu masuala haya ya kisiasa. (TBC, Blogu ya jamii etc)

    Jambo lingine all this may boild down to human psychology. Do most people want to change the TV channel from that providing credible news source to another where news is news but always in exaggerated form, just for the sake of a second opinion?

    Sidhani kama JF ni chombo cha habari, ule ni uwanja wa mjadala.

  4. Naelewa kabisa hoja zako. Na hata watu Tanzania walikuwa wanajadili mambo kama hayo. Kwamba, ili uweze kuelewa vizuri kinachoendelea, ulikuwa hauna budi kuwa na akili inayoweza kuchuja taarifa. Hapa naongelea:

    1. Hata kama unatumia JF kupata taarifa, basi uwe na uwezo wa kutafuta maoni ya hao wachache ambao wanaonekana wako “critical”.

    2. Ukishazipata, tafuta taarifa zaidi ili kuhakiki ulichosoma pale.

    Sasa, unadhani Watanzania wangapi wanaweza kufanya hivyo? Kumbuka, hii ni ishu nzito mno; taarifa fulani zinaweza zikazaa maandamano na ghasia, au hata kuchafua/kuharibu shughuli za mchakato mzima wa uchaguzi.

    Wale watoto walioanzisha fujo Tandika unadhani ilikuwaje? Mpaka polisi wakaamua kuwaachia; kulikuwa na watoto wa mpaka darasa la pili. Walikuwa wanafanya nini pale?

    Majimbo mangapi yalikuwa yanajadiliwa JF? Yanazidi 80? Kati ya 293.

    Je, uliona taarifa zozote kuhusu vituo vya uchaguzi Kurasini ambapo wasimamizi walikuwa wanasinzia? Kwenda kuulizwa, kumbe wao walianza shughuli mapema na wapiga kura walikuwa wachache sana. Ilipofika saa saba mchana wakaamua kupumzika tu.

    Habari kama hiyo inaweza kutafsiriwa tofauti na majukwaa tofauti. Nina uhakika unaweza ukaotea jukwaa gani litasema nini.

    Pia, wangapi wanaelewa kuwa JF ni jukwaa la mjadala tu? Wakati mule kulikuwa na watu ambao walikuwa kwenye vituo kadhaa wakilinda kura. Huyu mtu aliyekuwa kwenye kituo cha kupiga kura si ni chanzo cha taarifa? Au ni chanzo cha mjadala tu?

    Ukiwa na blog au chanzo cha taarifa kinachotembelewa na watu 10 – 100, sawa. Lakini ukiwa unatembelewa na watu 10,000 kwa wakati mmoja, ujue tayari una dhamana. That’s all I am trying to say.

    Ukiwa nje ya nchi halafu ukawa unachagua kuangalia taarifa/habari kwenye chombo fulani, utakuwa unapotoshwa sana. Hicho ndicho ninachosema.

    Siku ya Uchaguzi watu walienda viwanja, na kesho yake karibia watu wote waliendelea na shughuli zao kama kawaida. Kitu ambacho labda watu waliokuwa kwenye mtandao muda wote wakifuatilia matokeo hawawezi kuelewa.

    Waliojiandikisha kupiga kura ni takribani milioni 20. Waliopiga kura ni kama milioni 8. Tanzania ina watu zaidi ya milioni 40. Watanzania — waishio Tanzania — ambao wanatumia mtandao hawafiki hata laki 8 (hiyo takwimu inajumuisha hata wale wanatumia mtandao mara moja kwa mwezi).

    Kuhusu vyombo vya habari, ITV (Radio One), DTV na StarTV walijitahidi. Lakini ITV walikuwa wana wageni ambao walikuwa wanakosoa Tume ya Uchaguzi ipasavyo; kwa kutumia data na vielelezo kikamilifu. Na hawa walifanya vizuri kuliko hao wachache waliokuwa wanaripoti kwenye majukwaa ya mijadala.

    Kuhusu magazeti, Mwananchi na Raia Mwema walikuwa wanafanya vizuri. Lakini, unajua Mwananchi huuza nakala ngapi kwa siku? Niliulizia, nikaambiwa siku ambapo wanauza kuliko kawaida idadi ya magazeti haizidi 36,000 (Chanzo: Mwananchi) Unaweza ukazidisha hiyo namba mara 10-20 ili kujumuisha wale wanaoazimana, au mara 100 kujumuisha wanaobadilishana taarifa kwa njia ya maongezi… Taarifa kwa njia ya maongezi itakuwa inapoteza ule ukweli au ukamilifu…

    Kwahiyo, ninachosema ni hiki: 2015, mkonge mpya wa mtandao utakuwa unafanya kazi, watumiaji wa mtandao Tanzania wataongezeka labda zaidi ya maradufu. Kwa mwelekeo huu, tusipobadilika, tutafikishana pabaya kwa kuwa kuna vielelezo kuwa Watanzania wanaweza kulishwa propaganda kiurahisi.

  5. Nimekupata SN, umesisitiza hasa utafutaji, uhakiki na jinsi ripoti za uchaguzi zilivyokuwa zikiripotiwa, nakubaliana nawe, vichwa vya habari ni vya kushabikia sana , magazeti yetu mengi yanafuata mtandao wa udaku (cha kusikitisha hata Habari Leo na Daily News nao wameingia humo!).

    Magazeti na website ya IPP Media, kidogo wanajitahidi kuwa partial. Hii yote ni kama ulivyoona ndugu yetu, bado tuko nyuma kweli kweli, ni rahisi wachache bongo kujidanganya bongo New York, labda sababu ya kuwa na DSTV, internet na kusafiri nje ya nchi mara kwa mara. Lakini ukweli unatisha, ni wahusika hasa viongozi waende back to basic, yaani kumsaidia mwananchi wa chini kwa shida zake za kila siku. Baada ya hapo ndipo kuendelea na level ya juu zaidi, hasa za technology.

    Utauliza kama tutafika, mie nasema tunaweza kufika hasa pale tutakapodhamiria, washauri wapo, ni viongozi kutega masikio tu.

    Nadhani by 2015 media reporting itakua tofauti na sasa, labda wa akina SN, Joji, AK na wengineo watakua wamerudi nyumbani, na kuchangia mawazo yao kwa nchi yetu.

    Mie nilisumbuka kidogo kupata taarifa za uchaguzi, hata nilipowatumia sms washkaj nyumbani, ilionekana hata wao hawakuwa na taarifa za uhakika kuhusu matokeo ya uchaguzi. Bado wananchi hawajajua umuhimu wa kura, na ndio mwamko unatakiwa uendelezwe ili wananchi waelewe umuhimu wake. Wengi wao ndio maana hata hawaelewi kwanini CHADEMA wanamsusa raisi wetu, wanailani CHADEMA bila kuwasikia sababu zao, ama wanawaona CHADEMA kama wabishi tu, labda wananchi wataelewa kama katiba yetu ikisomwa na wengi, maana kwa kweli, kama kweli wewe ni msomi huwezi kuikubali kabisa.

  6. Kitu kimoja ambacho inabidi tukubali ni kwamba vyombo vya habari duniani kote vinakuwa vinaunga mkono upande fulani. Hili pia linatokea kwenye nchi zilizoendelea japokuwa wanakuwa hawaonyeshi wazi kama wanaunga mkono upande upi.

    Kwa mfano, nilifuatilia kwa makini uchaguzi uliopita Uingereza. Vyombo vya habari vya huko vinavyomilikwa na kampuni ya New Corporation, kama Sky News, The Sun, n.k. vilionyesha dhahiri kuwa vilikuwa vinaunga mkono chama cha Conservative. Vyombo vya habari kama vile BBC News, na gazeti la The Mirror vilionyesha kuunga mkono chama cha Labour.

    Ninachojaribu kusema ni kuwa linapokuja suala la uchaguzi sio tuu wapiga kura bali pia hata vyombo vya habari navyo vinakuwa vinaunga mkono chama fulani. Kwenye uchaguzi wetu tuliona wazi JamiiForum na baadhi ya blogu mbalimbali zikiunga mkono Chadema. Pia tuliona baashi ya vyombo vya habari kama Michuzi Blogu vikiunga mkono CCM.

    Hili limeendelea hata baada ya uchaguzi. Kwa mfano ukisoma maoni ya wachangiaji juu ya kitendo cha wabunge wa Chadema kutoka bungeni juzi kwenye Michuzi Blog na Jamii Forums, utafikiri wachangiaji wanatoka Northern Sudan and Southern Sudan. Pili watoa maoni wanaendekeza ushabiki zaidi.

    Ninafikiri mambo yatakuwa hivi hivi kwenye uchaguzi ujao. Sidhani kama kutakuwa na mabadiliko makubwa pamoja na kuwa watu wengi watakuwa na access ya internet.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend