Five Questions with M-Lab’s Patrick Gondwe

Sauti nyororo na utulivu wa midundo kwenye wimbo ‘Free Soul’ wa Grace Matata unaweza ukafanya hata “wagumu” wasiopenda R&B wavutiwe. Video yake imetulia… Naomba niishie hapa kwasababu nikiendelea kusifia kilichomo humo, mwenzenu naweza nikaambiwa nilale nje!

Ukiacha huyo, kuna dogo Ben Pol, ambaye ukiambiwa kuwa alianza sanaa kama rapper, unaweza usiamini. Msomaji, sikushauri umuache mwandani wako aimbiwe ‘Nikikupata’ na Ben; ukirudi unaweza ukakuta mtoto si wako! Au unaweza ukajaribu halafu urudi hapa kutupa matokeo.

Nikianza kuzungumzia ‘Punch Lines’ za Nikki Mbishi na beats za DukeTachez, nadhani naweza nikaandika kitabu…

One the Incredible na Stereo walishatambulishwa vizuri hapa.

Binafsi, navutiwa na kazi za watu niliowataja hapo juu; kuanzia vipaji, ufanisi na bila shaka nidhamu katika kazi zao. Na timu ya Vijana FM iliamua kumtafuta Patrick Gondwe, ambaye ni meneja wa wasanii na studio ya Music Lab (aka M-Lab au Media Kings Tanzania Ltd.). Ni matumaini yetu wasanii chipukizi, mashabiki na wadau wengine wa muziki watajifunza vitu kadhaa kutoka kwenye mahojiano yafuatayo:

1. Ukiangalia juu juu tu, utagundua kuwa M-Lab mnafanya kitu tofauti. Tafadhali tupe undani wa mradi mzima wa M-Lab kwa ujumla.

Mradi mzima wa Mlab ulianzia mbali sana, lakini ulibaki vichwani mwetu kwa muda mrefu kutokana na kutokuwa na ‘access’ ya vifaa vya studio, na pia tulikuwa bado wanafunzi. Kuanzia mwaka 1997 hadi 2003, maeneo ya Mwenge, kulikuwa na ‘movement’ moja kubwa iliyozaa vipaji vingi sana, ambavyo sasa hivi vipo fani ya muziki. Kulikuwa na mashindano ya u-Dj, uchezaji wa muziki, na pia production katika kiwango hafifu.

Upande wa u-Dj kulikuwa na changamoto sana; na hapo ndipo chimbuko la Dj PQ, Dj Stevie B, Dj Chilli, Dj Tama, Dj Snow, Dj Marc na wengineo. Upande wa ‘production’ na ‘graphics’ nilikuwepo mimi, kaka yangu Godwin na wengineo. Na kwa upande wa ‘rappers’ na ‘singers’, lilikuwepo kundi kubwa la Sewa Side —  lililokuwa na watu kama Daz Nundaz, DukeTachez, Pablo na wengineo wengi. Ukiacha hao, Unique Sistaz na kaka yao Dj Ibrah (wa Bils) walikuwa katika mitaa hiyo pia.

Tukiwa katika pilika hizi, ndipo Duke alipoanza kubadilisha mapenzi ya u-rapper na kwenda kwenye production. Nyumbani nilikuwa na ‘kiji-computer’ kimoja kilichokuwa maarufu sana… kilikuwa na Fruity Loops program ambayo Duke alianza kufanya nao kazi.

Baada ya muda na kuhama-hama kutokana na masomo, karibia watu wote tukapoteana. Niliporudi kutoka masomoni, mimi na kaka yangu tuliamua kuanziasha Media House Company. Tukiwa katika pilika za kupeleka matangazo studioni, tukaingia Tongwe Records… ndipo nilipokutana tena na mtu mzima Duke. Tukakumbushana zile ndoto za kuja kuwa na studio yetu na movements kwa ujumla kwenye masuala ya muziki. Kimasihara tu, tukaulizana: “Why not?”

Lilikuwa ni zoezi la miezi miwili tu [na] tukawa tayari tunameshaagiza vifaa na kupata eneo (premises).

Ndipo Music Lab ilivyozaliwa; ikiwa chini ya umiliki wa watu wanne, mimi (upande wa operation), Duke (production) na Godwin — Double G —  na Musa (promotion). Mara nyingine huwa tunaingiliana kazi kutegemeana na majukumu yanayotukabili.

2. Bongo vipaji vipo vingi tu; je, mnavimbuaje (vipaji) na kuvilea vipi?

Tumepata bahati kubwa sana ya kutembelewa na watu wenye vipaji kwenye studio yetu wakati tunaanza!

Sera yetu ilikuwa kuanza na vipaji vichanga, kuvilea, na pia kujenga tabia ya nidhamu kuanzia chini. Tuliogopa kufanya kazi na wasanii wakubwa kwa kuwa sisi wenyewe tulikuwa ni wageni; na mara nyingi wasanii wakubwa ni “Mr. I know everything”. Ingekuwa taabu sana kukaa na kuelewa kile tunachotaka kufanikisha.

Utaratibu wetu ni rahisi sana, kuna njia mbili:  kwanza, tuna watu (scouts) ambao wakinusa kipaji tu, basi hutuletea taarifa na sisi huanza kufuatilia; pili, ni kupokea ‘demo’ moja kwa moja kutoka kwa wasanii na kuwaalika studio.

Njia zote hizi mbili ni lazima zipitie hatua ya ‘audition’, ambayo husimamiwa zaidi na Godwin aka Double G, Duke pamoja na production crew nzima. Hapa msanii huanza kwa kuambiwa aimbe ‘copy’ studioni bila vikorombwezo vyovyote (reverbs au effects ). Halafu hupewa maada ili aitungie wimbo. Baada ya hapo, anapangiwa siku nyingine ya kuuwasilisha wimbo wake studioni.

Kama akifaulu basi moja kwa moja anapewa mkataba na kupewa wiki mbili aende kutafakari kama una manufaa kwake. Na baada ya hapo ni aidha kusaini ama kutosaini, kutegemeana na matakwa yake. Nidhamu pia ni jambo linaloangaliwa katika mchakato nzima.

3. Nadhani mmewekeza juhudi zenu kwenye kutangaza wasanii wenu kwenye mtandao (blogs, tovuti, n.k.), kwanini mnafanya hivyo?

Kila kitu kina gharama yake. Ukweli ni kwamba internet ndio njia rahisi isiyo na gharama kubwa kutangaza bidhaa yako; ingawa pia inafaa kuangaliwa kwa umakini sana maana kwa soko la ndani sidhani kama ina ‘impact’ kubwa (1% ya Watanzania ndio wana-access ya internet). Hivyo mara nyingi hii inasaidia sana kupromoti nje  ya Tanzania zaidi. Hapa namaanisha nchi nyingine za Afrika, Ulaya na Amerika…

Bado promosheni za redio na televisheni zina nafasi yake kubwa tu, ila kuna vikwazo vya hapa na pale. Kuna msemo unaosema, “Kama wewe upo kwa hii industry basi you cannot afford to mess with a Radio Dj ama presenter!”

Wapo wachache wanaoharibu sifa za wengine, lakini niseme tu kuwa hali kwa sasa imebadilika sana kutokana na ushindani mkubwa wa vyombo vya habari. Ma-Dj wengi wamekuwa wakiwasaidia wasanii. Changamoto na matatizo binafsi bado yapo japo kwa kiasi kidogo.

Kwa upande wetu, bado tuna tunategemea blogs, social networks sites na pia ‘movement’ kama Vijana FM katika kusambaza habari za wasanii na studio yetu, pamoja na huduma nyingine tunazotoa pale.

4. Wewe kama meneja wa wasanii, unafanya nini tofauti na mameneja wengine tuliowazoea?

Kutoa mwongozo au ku-manage msanii ni jambo gumu sana hasa katika mazingira haya ya Kitanzania. Ukusanyaji wa mapato ya msanii ni kitu ambacho ni changamoto kubwa sana kwa ‘labels’ na mameneja kwa ujumla. Tunajaribu sana kulinda haki za msanii, na wakati huo huo kumjenga msanii kwa promosheni, “PR” na pia kutafuta, kujadili na kufanya makubaliano kwenye mikataba iliyo na manufaa kwa msanii.

Kwa bahati mbaya mfumo huu wa ‘management’ umekuwa haueleweki kwa mapromota wengi sana, na pia watangazaji wa vipindi.

Mathalani, tunapenda kuhakikisha mahojiano yote yanayohusisha wasanii wetu yanakuwa ‘well-controlled’. Kwa maana ya kwamba, msanii anapewa muda wa kutosha kabla ya mahojiano, anathaminiwa anapokuwa katika vituo vya redio, na sio anakwenda (kwenye mahojiano) saa nne halafu anakalishwa hadi saa saba.

Kwa kusimamia mambo haya unapata changamoto za kuambiwa mnajidai n.k. Ni mfumo wa Kimagharibi zaidi lakini wenye manufaa siku watakapoja kuulewa.

Pia kuna mambo ya ubabaishaji mkubwa sana katika ‘shows’, malipo na mpangilio unavurugwa sana na mapromota. Unapokuwa makini kama sisi basi unakuwa adui wa hawa watu, kwa hiyo mwisho wa siku wasanii wanakosa ‘shows’ kwa sababu mapromota feki wanakuwa wamekosa mianya ya kuwaonea wasanii wetu.

Kwa kuona hivyo, tukabuni mkakati ambao bado haujaanza kuzaa matunda maana bado upo katika hatua za awali sana za kujitangaza. Tumeunda bendi itakayosaidia wasanii wetu na tumenunua “PA system”. Tunawahimiza wasanii wetu kujibunia ‘shows’ mbalimbali, wao wenyewe wanaenda wakijua kabisa thamani ya kukodisha bendi au “PA system” ya ‘label’ ni kiasi gani.

Tunaamini kwa kufanya hivi basi wataweza kujikimu na kuuza kazi zao katika ‘shows’ husika.

Bendi yetu inapiga kila Alhamisi maeneo ya Mikocheni; lengo kubwa ni ku-manage ‘shows’ zetu wenyewe Dar es Salaam na mikoani. Nje ya Tanzania, tunajaribu kufanya kazi na kampuni ambazo zimeshajikita katika kupeleka wasanii nje. Tunakaribia kusaini mkataba na Unity Entertainment chini ya Ambwene Yessaya (A.Y.). Pia kuna mazungumzo mawili matatu na Trinity Promotions.

5. Tupe mtazamo wako wa mwelekeo wa muziki kwa ujumla.

Nilishawahi kumwambia rafiki yangu mmoja kuwa ajaribu kufanya jaribio dogo: ajaribu kutopiga aina yoyote ya muziki akiwa kwenye gari lake, akifika nyumbani asiwashe redio wala TV. Na kwenye harusi na msiba kusiwepo na aina yoyote ya muziki.

Je, maisha yangekuwaje? Bila shaka ni ngumu sana.

Naamini muziki haufi na bado utabaki kuwa kiungo kikubwa sana katika jamii. Hivyo basi muziki hauwezi kukosa soko.

Tatizo sugu tulilonalo ni mfumo na udhibiti. Hapa tuaanzia toka kwenye uandaaji wa msanii, uzalishaji, usambazaji hadi stadi za jukwaani. Kumekuwa na juhudi nyingi sana za makundi tofauti-tofauti lakini tumekosa sauti moja.

Serikali ina wajibu mkubwa sana katika kulisimamia hili na si kumpa kazi hii mtu mmoja… tuna “regulatory authorities” chungu nzima katika sekta tofauti tofauti, ‘why not showbiz area?’ Sidhani kama tunahitaji hisani ya rais katika hili, bali nadhani Serikali ina wajibu kulichukulia suala hili kwa uzito unaostahili. Hii ni moja ya sekta isiyo rasmi inayoweza kupunguza tatizo la ajira kwa kiasi kikubwa sana kama ikithaminiwa.

Pia kuongeza somo la muziki katika mitaala vyuoni hasa yale masomo ya ujasiriamali. Naona juhudi za BASATA za hivi karibuni, na pia kuteuliwa waziri mpya kama faraja fulani. Ngoja tuone kama mambo haya yatabadilika. Bado nina mashaka sana na mfumo mzima wa COSOTA katika udhibiti wa haki za msanii; ni eneo jingine linalohitaji sana msukumo na mabadiliko.

Bila shaka umepata mwangaza na kuelewa nini kinaendelea nyuma ya kazi nzuri tunazosikia kutoka kwa wasanii wa Music Lab. Naelewa ni kazi ngumu sana, hasa mwanzoni, ila tunawaomba wasivunjwe moyo na changamoto wanazokutana nazo kila kukicha. Mwanzo mara nyingi huwa mgumu sana, hasa kwenye fani hii.

Sisi tutaendelea kuwapa mawazo na kuendelea kuwasaidia kila tutakapoweza. Mwisho wa siku, vipaji vya ukweli vitaendelea kusimama; na heshima ni kitu muhimu zaidi.

Timu ya Vijana FM inawaombea kudra zote. Mwishoni mwa mwaka huu tuna uhakika tutakuwa tunajadili mambo mengine kabisa tofauti na haya.

Sikiliza nyimbo 10 za wasanii wa M-Lab kisha uamue mwenyewe. Usisahau kumdokeza na mwenzako! Kuna mawe mazito mapya kutoka kwa Stereo (Rafiki) na Ben Pol (Maumivu)…

Kama hiyo player hapo juu inakusumbua, basi bofya hapa ili kujaribu kutumia nyingine. Quantcast

Makala na tovuti zinazohusiana na haya mahojiano:

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 9 Comments

9
  1. Hongera sana kwa VFM kwa kutumulikia watu muhimu kama hawa ili kwa wale ambao wanasikia tu au kama SN ulivyosema wanaona “vyaelea” tu basi watapata nafasi ya kusoma fikra za waundaji wenyewe.

    Mimi binafsi nazikubali kazi zinazotoka mLab kwani naamini kuwa ni kampuni ambayo inauchukulia muziki sio kama kazi tu bali sanaa tofauti na baadhi ya kampuni nyingine ninazozifahamu. Na kwa hilo nadhani wako katika nafasi ya kubadili mwelekeo wa muziki wa Tanzania kutoka kwenye msingi.

    Nilikutana na Patrick na Duke kwa bahati tu kupitia rafiki yangu ambaye aliniambia “ebwana kwa sababu wewe ni mpenzi wa muziki kama sanaa nadhani utafurahi kukutana na jamaa mmoja ana studio anaitwa Patrick…” Na kweli baada ya kukaa na kubadilishana mawazo mbalimbali na kusikiliza muziki uliokuwa unatokota kwenye chungu cha Duke mwenyewe nikakubali kuwa hapa kuna hazina ambayo nadhani wengi watakuja kuithamini.

    Napenda sana watu ambao wanawekeza katika muda wa R&D maana ni kawaida sana hapa bongo kulipua mambo au kutaka kuvuna kabla hata mbegu hazijanunuliwa. Kwa muda mfupi ambao nimewafahamu hawa jamaa nadhani hiyo ndio tofauti yao kubwa (bila kusahau kipaji kina cha Duke)

    Nimefurahiswa sana na mchakato mzima wa kumsaini msanii ambao wanautumia kwani ndio njia pekee ya wao kuhakikisha kuwa kiwango chao kinaendelea kupanda. Hii quality control ndio mhimili mkuu kama hauna pesa nyingi za kujitangaza kwani mara zote word of mouth ina nguvu zaidi, lakini njia hiyo inafanya kazi pale tu ambapo unaweza kuhakikisha kiwango chako kiko juu na kinaendelea kuongezeka ubora.

    So far nadhani mLab wamekuwa consistent na pongezi ziende kwao kwani hapo ndio kampuni nyingi zinafeli.
    @SN ukipata nafasi nadhani itakuwa vizuri ukimpata Duke nae atupe mawili matatu kuhusu upande wake wa kazi

  2. Mkuki, nakuonea donge kwasababu umeona wenzetu wanavyofanya kazi. Na majibu ya Patrick yanadhihirisha kuwa Bongo tuna vipaji vingi tu (vya aina tofauti; sio lazima muziki), ila tu wenye uwezo wa kuvisaka, kuvilea na kuvikuza ndicho pekee kinachotuangusha. Bahati mbaya wengi hupenda “kuwatumia” watu tu kwa manufaa yao wenyewe — hivyo kuwakatisha vijana tamaa na kudumaza vipawa vyao.

    DukeTachez atatafutwa, ila subira itahitajika kidogo kwasababu makala yake itabidi iwe tofauti kidogo… kama kila kitu kikienda vizuri.

  3. Maelezo mazuri sana toka kwa Patrick. Safi. Nimecheka sana kwenye hiyo seheme ya kijicomputer kdg ha ha ha! I guess Patrick alikuwa akigonga pia beat zake pale!

  4. Interview nzuri, sema sijaelewa hili la bendi. Bendi hii ni kwa ajili ya live performance kwa ajili ya wasanii wenu, au hii bendi ni kitu tofauti na wasanii tunao wafahamu..

    Mziki pamoja ni sanaa pia ni biashara, hivyo je, mna-control ubunifu wa msanii kwa kiasi fulani, kama mnaona amekuwa extreme kidogo hivyo hawezi kufanya vizuri kwenye soko, kitu kama hicho.

    Nadhani kama umepata nafasi ya kufuatilia kasheshe ya Lupe Fiasco na his upcoming album ya Lasers na kwanini imechelewa sana kutoka, utaelewa swali langu vizuri, kama sio, nitafafanua kasheshe hilo lililomkuta mzee mzima Lupe..

  5. Bahati sijapata bahati ya kufuatilia saga la lupe fiasco lkn nitaelezea kwa upande wetu! nikisema tumeanzisha band na ununuzi wa PA SYSTEM tupo kwenye mtizamo wa kibiashara zaidi na kama management tunawajibika na udhibiti wa viwango vya ubunifu wa msanii. Tumetoa uhuru wa ubunifu kwa wasanii lkn kwa misingi ya taratibu zetu,biashara,na sheria za nchi. Na si kwamba tumefunga milango ya kufanya kazi na promoters! Bado tunafanya kazi kama kawaida ila hz njia nyingine ni njia ongezeko za kibunifu za kuongeza pato…band ni separate entity na wanapiga bila kuhusisha artist wa lebel kila wiki..ila endapo msanii atatakuwa na show yenye hitaji la band ama PA SYSTEM peke yake basi atakuwa na masharti nafuu sana ya kutumia resources hz

  6. Lupe album yake ya lasers imechelewa kwasababu record company yake walitaka afanye mambo mawili. Kwanza, asaini mkataba wa 360 deal, kwa maana kila kitu atakachofanya Lupe, record kampani watachukua asilimia fulani ya mapato, Lupe akawakatalia. Lakini sidhani hili ni tatizo kwa wasanii wa bongo.

    Pili, record company yake walikuwa wanataka waingilie uwezo na ubunifu wake kama msanii, kwani hawakupenda alichokuwa amesharekodi. Nadhani walitaka atoe nyimbo ambazo zitauzika zaidi, kama hawa akina Souljah Boy, hivyo wakamtengenezea chorus na mambo mengine wakampa. Sasa hapo ndipo kiini cha swali langu, je na nyinyi mnaangalia uwezo wa msanii lakini hapo hapo mnahakikisha anatengeneza nyimbo ambazo zitauzika, hata kama itabidi kumiliki uwezo wake kama msanii na ubunifu wake, na u-unique wake ili mwisho wa siku atoe kitu amacho kinauzika, kupata manufaa kama msanii na nyinyi kama label.

    Au hili kwenu halipo, msanii yupo free kufanya anachotaka kisanii/ kibunifu that is..

  7. Bahati! Labda nianze kwa kusema kuwa soko la muziki la Marekani lina tofauti kubwa sana na la kwetu… hivyo basi hakuna presha kubwa kwa wasanii kutoka katika labels zao!Kwa upande wetu, si’ tunaamini msanii anatakiwa kupewa uhuru wa kile anachotunga lakini bado tutashauriana nae na kumuelewesha wapi kavuka mipaka, wapi ana strength ya ujuzi na wapi labda anapaswa ku-twist! Ila mwisho wa siku ni yeye mwenyewe.

    Sisi mwisho wa siku huwa na headache tu ya kuamua nyimbo gani ya msanii husika iende redioni. Lakini pia ni muhimu kwa labels kuwa makini na kile kinachotungwa na kuangalia kama kina maadili na hakijavuka mipaka ya nchi.

    Nikupe mfano: ROMA kabla hajasaini na Tongwe Records tulibahatika kuwa nae, na niseme tu katika watu ambao tunasikitika kuwakosa kuwa-sign wakati tumekaa nae zaidi ya miezi miwili basi ni huyu msanii. Original ya mwimbo wa “Mr. President” upo M-Lab, sasa baada ya wimbo kuisha Duke akatuita studioni — plan ilikuwa Mrisho Mpoto akae kwenye chorus! Tukaanza kuusikiliza, mimi, Godwin, Musa na Mpoto! Mwanzo tuliogopa, lakini likaja wazo kukaa na Roma na kumshauri kutumia tasfida nyingi (metophors) kuliko kuyaweka kwa uwazi vile masuala mazito kama yale!

    Jamaa alielewa akafanya edit na kuirudia ngoma! Likaja wazo la kuweka speech za nyerere kwenye chorus. Musa aka download speech tukampatia Roma achague kipande cha sample. Kwa bahati mbaya Roma bado alikuwa haja-sign as tulikuwa tunamu-assess tujiridhishe! Tukiwa tunajiandaa ku-release nyimbo, mara tukaisikia kwenye radio ikiwa na beat na chorus! Tukajua tumeshazidiwa ujanja… but we respect his decision, coz it was a pure busines move. Tunajutia kumkosa lakini hatujutii taratibu zetu za ku-recruit wasanii.

    Ukiangalia huo mfano utagundua kuwa hatuingilii ubunifu wa msanii bali tunatoa ushauri tu.

    SN — Sikiliza ‘Mr. President’ ulioimbwa na Roma:

  8. Mkuki thanx a lot brother! Nakumbuka sana jinsi ulivyofurahia kazi za Musa vipaji vingi (yule dogo wa traditionals music) ulivyopita studio! Album ya dogo ni kali sana ila headache ipo kwenye marketing yake. Aina ya muziki wake hauna support kwenye media yetu! Tunatafuta njia sahihi…

    skywalker, mie nilikuwa nagonga sana beats na ndio nilikuwa mwalimu wa kwanza wa Duke, japo ilikuwa at preliminary stage. Kwa sasa yupo kwenye sayari nyingine kabisa! Ni aibu hata kujisema kama nilikuwa mwalimu wake..enzi hizo wengi sana tulikuwa na dreams hizo. Succes kubwa ya u-producer wangu uchwara ilikuwa kumtengenezea demo MB DOGG apeleke studio kubwa! Ilikuwa zamani sana sidhani hata kama ana kumbukumbu hizi! Miaka mitatu baadae ndio MB Dogg akatoka na “Latifa”… pia nilishafanya kazi na Gazzab Mob..kundi lililokuwa linasimamiwa na marehemu Moses Justine (Papaa Mo RIP)! At least uzoefu huu mdogo wa production umenisaidia upande wa artists management.

  9. @Gondwe, dah asante sana kwa kuzidi kutufumbua macho tuliokuwa tunaangalia industry kwa nje. Hiyo track ya Roma mimi mwenyewe nilisikia, na kusoma lyrics nilishtuka. NIlishtuka manake mashairi yako so bold.

    Nadhani kuna haja ya kumtafuta Roma ajadili hii track manake, duh!!…

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend