Mbwa wa Pavlov II

Shule ya msingi ya mazoezi Chang’ombe, iliyopo kwenye wilaya ya Temeke, ilikuwa na desturi ya kualika mwanamazingaombwe karibu kila siku tuliyokuwa tunafunga shule kwa ajili ya likizo fupi. Ijumaa moja ya mwezi Aprili mwaka 1994, wakati nipo darasa la nne, baada ya kufanya usafi siku nzima, wanafunzi kama 80-100 tuliokuwa na shilingi 50 tuliamua kubaki ili kumuona mhusika aliyealikwa.

Mbele ya darasa lililotumiwa kama ukumbi kulikuwa na nyungo kadhaa zilizokuwa na tunguli, visu, vibuyu na vitu kama hivyo. Mwanamazingaombwe hakupoteza muda. Baada ya darasa kujaa tu akaingia kwa vitisho, akiwa amevaa hirizi na vitu vingine ambavyo ni kama mavazi yetu ya kijadi. Kama kumbukumbu zangu hazinihadai, kitu cha kwanza alichofanya ni kuweka kikombe juu ya kichwa cha mwanafunzi mwenzetu. Akakifunika kwa magazeti. Akafanya madubwasha yake huku akizunguka-zunguka, halafu ghafla akakibonda kwa nguvu kwa kutumia mikono yake! Kile kikombe kikapotea! Yule mwanafunzi hakuonekana kama ameumia.

Kitu cha pili alichofanya kilinishangaza zaidi. Alichukua papai, akacheza nalo kwa muda mrefu tu. Sasa, ikafika muda wa kulikata ili tuone kilichomo ndani. Kiini macho; badala ya kukuta mbegu nyeusi, tukaona bigi jii kibao zikiwa bado na maganda yake mekundu. Akazichukua na kuanza kuturushia. Sikuwa nafikiria kudaka angalau moja na kuitafuna, ila moja iliangukia kwenye shati langu jeupe ikiwa na chembe chembe za papai. Nilijawa na hofu kubwa kwasababu nyingi tu, nikaitupa ile bigi jii chini na kuamua kwenda nyumbani huku nikiacha “burudani” ikiendelea.

Jioni yake kulikuwa na mkesha wa Pasaka katika kanisa la Kilutheri (Keko Juu) karibu na sehemu tuliyokuwa tunaishi. Baada ya kupata mlo wa usiku, dada yetu aliambatana nasi — mimi na watoto wengine majirani wa rika langu — kwenda kutazama filamu ya Yesu. Ilikuwa imetafsiriwa kwa hiyo tulikuwa “tunajua” kinachoendelea. Kwa sababu hii hufanyika kila mwaka, ilikuwa ni kawaida kusikia watu wa wakimalizia kauli za waigizaji kwenye filamu.

Kama unaifahamu filamu ninayoingelea, nadhani watu wengi huangua vicheko pale Yesu anapomponya yule kipofu omba-omba kwenye mji wa Yeriko (au Jericho; kasome Marko 10). Unakumbuka pale Bartimeo anapoamka na kuanza kusema, huku akipaza sauti, “Nimeona! Ninaonaaa…!”

Siku iliyofuata ilikuwa ni Jumamosi, na kama kawaida yangu saa tatu asubuhi nilikuwa kanisani. Kama kijana niliyekuwa nahudhuria madarasa maalumu ya Biblia, nilikuwa nakariri mafungu mengi sana! Tulikuwa na programu ya kila mwezi ambapo tulikuwa tunapewa nafasi ya kukariri mafungu ya vitabu vya Biblia mbele ya kanisa.

Hadithi haiishii hapa… Sehemu niliyokuwa naishi kulikuwa na watu wenye imani nyingi tofauti, kitu ambacho kimenijenga na kujifunza kuhoji. Kuna wakati nilipokuwa kwenye mizunguko yangu (soma ‘kuzurura’) nilikuwa nakutana na mihadhara ya dini mbalimbali na madhehebu mengine tofauti. Kitu kilichokuwa kinasisimua ubongo wangu kilikuwa ni kusikia watu wakitumia mafungu yale yale niliyokariri kuhubiri au kuwasilisha ujumbe tofauti kabisa na kile nilichodhania. Wengine walikuwa hata hawamalizii mafungu husika.

Propaganda? Nilikuwa sijui hilo neno. Nilikuwa bado mwanafunzi wa shule ya msingi. Maneno yangu yanakufanya uanze kuhoji vitu fulani unavyoamini; imani yako kwenye kitu fulani? Unajua historia ya dini yako? Unafahamu jinsi imani ya dini yako ilipoanzia? Ungezaliwa Jerusalem, kama Muafrika na haufungamani na imani yoyote, je, ungekuwa Muislamu, Mkristo au ungefuata imani ya Wayahudi? Au ungeamua kutafuta dini au imani nyingine ambayo inakubaliana na mwenendo wa maisha yako au jinsi unavyotaka uwe? Ungetafuta vitabu vya imani mbalimbali kutoka kwa Wamaya, Wahindu, Ismailia, Buddha, Mormons na imani asilia za Afrika? Unadhani kuna tofauti kubwa kati ya imani ya madhehebu makubwa ya Kikristo na Mormons? Unajua tofauti kati ya Quran na Hadith?

Labda unajiuliza, nini kimenisukuma kuandika haya makala? Kuna kitabu kinaitwa “Diary of a Bad Year”…

Wengi wetu wa kizazi hiki tunabeza mifumo ya utawala ya mababu zetu au falme za kale. Tuna kitu kipya na cha ukweli kinachoitwa “demokrasia”. Wengi tunaamini kuwa demokrasia ndio mfumo sahihi.

Vizazi vingi vya kale vilikuwa vina mifumo ya ‘ufalme’ au ‘uchifu’. Wengine bado wanaendelea kufuata hiyo mifumo. Na jamii nyingi zilikuwa zina familia teule ambapo viongozi wa jamii husika walikuwa wanatoka. Kitu kilichofanyika ni kufunda kiongozi atakayefuata, muda wote. Kila mtu alikuwa anajua fulani au kijana yule ndio alikuwa anafuata baada ya mfalme au chifu wetu wa sasa. Hivyo, iliwapa nafasi ya kuandaa mtu mwenye sifa ya uongozi. Walikuwa wana uhakika — au, imani? — kuwa mtu atayekuja kuwaongoza, baada ya huyu mfalme au chifu wa sasa, atakuwa ana vigezo, sifa na hulka ya uongozi.

Ukiacha rasilimali, mazingira na mazingara, hii ndio ilikuwa sababu kubwa ya msingi baadhi ya jamii zilikuwa zinakua na kupanuka, na mwishowe kujijengea himaya madhubuti.  Ndio maana katika historia ukisoma kuhusu himaya fulani kubwa kutoka Afrika, Ulaya au Mashariki ya Kati, basi lazima iambatanishwe na jina la kiongozi wao; ambaye alikuwa anafikiria mbali… moja ya hulka ya kiongozi!

Najua fika kuwa baadhi ya nchi zetu zililazimishwa kufuata mfumo wa “demokrasia”. Ila sizungumzii Tanzania tu. Nauangalia ulimwengu kwa ujumla na mfumo wa kisiasa ambao umepitishwa bila wengi wetu kukaa kitako na kuhoji kwa kina mambo ya msingi.

Je, demokrasia humaanisha nini? Sehemu ambapo kuna “demokrasia ya kweli” (kama unaamini hivyo) inamaanisha tu kwamba watu wengi “zaidi” wanampendekeza mtu au chama fulani kiongoze nchi. Basi.

Demokrasia haikuhakikishii kiongozi bora. Au, demokrasia haikupi kiongozi. Demokrasia haiwezi kufunda watu wawe viongozi bora, hasa kwenye nchi ambazo watu hawasomi vitabu na kuzipa bongo zao changamoto. Kama unadhani mfumo wa demokrasia unafanya kazi kwa njia ya ushirikishaji au uwajibishaji, unadhani ni sahihi mtu kujifunza kuhusu uongozi wakati tayari amekalia kiti?

Vipi kuhusu nchi ambazo zipo kwenye wakati mgumu kiuchumi, nchi zinazohitaji mtu wa kuongoza kwenye majanga, je, demokrasia inawatendea haki?

Sisemi kuwa demokrasia haifai, lakini ukiangalia mazingara halisi, hatupaswi kubeza jamii ambazo waliweka imani zao juu ya familia za kifalme au kichifu. Na tunapaswa kuwa na watu wanaohoji aina zote za mifumo ya kisiasa.

Vivyo hivyo kwenye imani, kuwa na imani tofauti, au kutokuwa na imani. Wale wasio na imani kabisa hawapaswi kuhoji na kujifunza kuhusu imani au dini tofauti? Suala imani kama lilivyo — kimantiki, kuamini bila ‘kuona’ au ‘kuhoji’ — tofauti kubwa kati ya ushirikina na dini tulizonazo ni nini? Kwani, mwisho wa siku, tafsiri ya vitu tunavyokumbana navyo maishani ndivyo vinatupa maana ya “kuishi”.

Kizazi chetu kipo kwenye kipindi chenye changamoto nyingi mno sasa hivi. Kila kukicha unasikia jambo jipya, ambalo linakufanya uhoji. Kuanzia ukiukwaji wa haki za watoto na binadamu, watoto wadogo wanabakwa, watu wananyofoa nyeti za wenza wao, nchi mpya zinazaliwa, propaganda za kipuuzi, vijana wanachomwa moto, watoto wanamaliza shule huku hawajui kusoma, mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, vijana kuendekeza udaku, Loliondo, n.k.

Ndio, ni kutaka kuelewa tu mantiki ya “maisha”. Wewe unatumiaje kura yako kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa. Ni sahihi kwenda kupiga kura kwa kufuata mkumbo? Kama ukiona wagombea wote hawafai kuongoza, ni sawa kwenda kumpigia kura mmoja wapo tu, hata kama unaona hafai?

Kwa kumalizia tu, naelewa kuwa hoja za kifalsafa hutumia logic. Na mara chache logic huzaa paradoxes. Lakini, tusitupie mbali kila hoja kwa kisingizio cha paradox na kuendelea kushtuka na kushangaa pale tunapoona jamii yetu ikizidi kuwa na watu wanaoamini mambo ya kishirikina — wakati watoto na wadogo zetu wanaoneshwa “mazingaombwe” mitaani na mashuleni.

Makala Iliyopita:

Makala Nyingine:

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 5 Comments

5
  1. Du aisee, thanks for sharing such deep thoughts SN. Would love to read more like this (the first article was a good read as well!).

    If I’ve understood you correctly, I agree that bandwagoning the “democracy train” without proper/full understanding is useless for the improvement of people’s quality of life. I think if people understand and agree on the cause of a government – if they truly all concur – then it can be called whatever, even a dictocracy (??), but it would lead people down a happy path.

    Now, having said that, a lot of our politics in Tanzania seem to be religion-faction based, which is why its ridiculous that our country seems to bandwagon on the whole “separation of religion and state” mentality. Do we really think our politics are separate from people’s religious beliefs? I’m very glad you brought up questions about knowing one’s own faith, because rarely do we appreciate (today, at least) the significance of these belief systems on our day to day lives.

  2. …Kweli ninaona uhusiano kati ya mazingaombwe shuleni na taifa linaloamini sana uchawi au ushirikina na the fact that tumeambiwa kuwa demokrasia is the way to go kwahio twafikiria kuwa it should always be the way to go…hebu cheki mambo yanavyoenda vema Rwanda ingawa naweza kusema kuwa hakuna demokrasia kiukweli…Kagame ni mtu ngangari anayejua nchi au wananchi wake wanataka nini ili ku-survive kama nchi…nimependa makala za ‘Mbwa wa Pavlov’…

  3. napendekeza mbinu tofauti ya demokrasia. Imagination. Pengine ndio kitu kinachopungua mara nyingi katika maamuzi yetu, malengo yatu, maono yetu, kama watu binafsi, na kama jamii husika. Na hapa ndipo linapokuja swala lingine, taarifa. Taarifa zinabidi kuanza kisha ndipo imagination ianze.

    Iwapo watu hawana utamaduni wa kusoma, basi wamefunga milango ya kupokea taarifa. Na iwapo wanasikiliza na kusoma kilichoandikwa na copy cats(taarifa za habari na habari za magazeti) zenye maudhui yanayonukuu hotuba za viongozi na presentations za semina na vikao), na kama zaidi ya nusu ya data zilizopo zina makosa, ama ni za zamani basi imagination inazidi kufungwa. Na iwapo hakuna imagination, basi maamuzi yatatoka (kwa vile ni lazima yatoke) lakini hayatampeleka muhusika ambako angekwenda. Na atajua tu kuwa amekosea pindi akikutwa na tatizo lililozaliwa na ufumbuzi aliouchukua.

    Unaweza ku apply hiyo theory kwa mambo mengi yanayotokea hapa kwetu. Solutions nyingi ziliundwa toka kwenye misinformed imaginations, na matokeo yake ni matatizo yanayojengwa ndani ya mfumo. Na sasa tumefika tunapoona kuwa tufumue mfumo mzima. Pengine hiyo ni solution, lakini sivyo. Naomba nitoe utabiri.

    Si mabadiliko ya mfumo wa demokrasia(kwa taifa), ama dini(kwa mtu binafsi) ambayo yatatulea ufumbuzi wa matatizo yetu. Lakini mabadiliko ya mfumo, lazima kwanza yaanze kwa mabadiliko ya fikra za watu walio katika mfumo. Iwapo, watanzania hawataona umuhimu wa profesionalism,(ambayo ndani yake ina utafiti na kujifunza-kusoma), hata katiba ingebadilishwa kuwa kama ya ahera ama peponi, au mbinguni, wao wenyewe hawataweza kutekeleza matakwa yake, na hivyo hawatastahili kufaidi matunda yake. Kitakachowastahili ni kile walichochagua, toka mioyoni mwao. Simaanishi uchaguzi wa rais wala mbunge(tu). Namaanisha uchaguzi anaofanya mtu kila siku wa kufanya wajibu wake ama kuboronga makusudi. Hivi mtu akila ice cream kisha akatupa mfuko wake barabarani; akienda field work kwa ajili ya allowance, akifagia uwanja wa nyumba yake akaacha mtaa mchafu, tumtegemee atoe maamuzi yenye fanaka kwa mustakabali wake? Pengine kwa kunakili mahali.

  4. nimependa mwanzo wa makala haya, unavutia kusoma.
    Jambo moja najifunza hapa na ambalo naamini ni kuhusu uhuru wa kuamini, na kuwa na hakika ya kile tunachokiamini baada ya kukitafakari na kujiridhisha. Imani kuhusu dini na imani kuhusu mifumo ya maisha tunayoitaka.
    Mazingaombwe tunayoyaona yanaweza kutafsiriwa kwa namna tofauti, aghalabu wanadini husema hata shetani anaweza kufanya miujiza. ‘Ila miujiza ya kiMungu ndiyo sahihi.’ sijui pia kama usahihi wa demokrasia yetu umeteuliwa na nani?
    hatuna muda wa kutafakari wala kukubali mifumo tunayoitaka maana kuna mungu wa kutuamulia kuhusu kuamini, itikadi na mungu wa kutuamulia demokrasia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend