Na Mkereketwa
Unategemea kuona jinsi utawandazi unavyoathiri matendo na mawazo ya watu, hasa vijana wa Tanzania, ili kuleta mabadiliko kwenye jamii. Lakini ninachokishuhudia kila siku kinanipa hofu na mashaka.
Nimeanza kufuatilia kwa karibu sana mambo yanayofuatiliwa na vijana takribani miezi nane iliyopita; aina ya mijadala tunayopenda kuchangia kwa kina na hoja zetu (kwenye tovuti mbalimbali). Kusema ule ukweli, inasikitisha sana na ninadiriki kusema: Vijana wa Tanzania hatuna dira na hatujui tunapokwenda. Na kwa mwendo huu, sitashangaa tusipokuwa na mabadiliko yoyote ya kifikra, matendo na jamii kwa ujumla kwenye miaka 15 – 20 ijayo!
Najiuliza, sisi kama vijana, takribani 70% ya idadi ya watu Tanzania, hivi tunajua tunachofanya? Mbona hatujui hata kuuliza viongozi wetu maswali ya msingi? Au jambo linalogusa Taifa linapotokea, mbona tunanywea na kujificha? Au muda mwingine, mbona tunakuwa kama majuha na kutetea upumbavu?
Walahi! Ningekuwa fisadi, sijui kama mikwara ninayoiona kwenye blogs na vijiwe vyetu ingenitisha! Kwasababu, najua fika kuwa baada ya siku mbili tatu, watu watasahau na maisha yatarudi kwenye hali ya kawaida — nitakuwa kaunta kwenye kiti changu kirefu huku nikipata moja baridi moja moto kwa mrija na kiti moto. Matawi ya juu.
Nitakupa mifano michache.
Miezi michache iliyopita, wasanii kadhaa wa Bongo Flava walijitosa kwenye vyama mbalimbali, iwe CCM, CHADEMA, TLP, CUF… Hiyo sio hoja. Kama tungekuwa angalau tunajua katiba au sheria vizuri, tusingewatukana; kwasababu wao kama wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wana haki ya kukipigia debe chama chochote kile cha siasa.
Kwa taarifa yako, Prof. Jay hakutuasi kwasababu tu aliimba “Ndio Mzee.”
Lakini, kwasababu wao wamekubali kutumiwa kama nyenzo ya kuwahimiza vijana kufuatilia, kukichangia au kukipigia kura chama fulani, si wajibu wetu ungekuwa kuwauliza maswali kuhusu sera za vyama walivyochagua? Mi’ namfagilia Nakaaya kwa sana tu (usiulize kwanini!), ila kamwe hautaniona namchagua mgombea fulani wa CHADEMA kwasababu tu Nakaaya yuko CHADEMA. Tungepaswa kuwabana ili watupe sera za CHADEMA au CCM! Je, wanazijua katiba za vyama husika? (Nilitembelea JF mara moja na kushangazwa na mmoja wa wachangiaji na mshabiki mkubwa wa CHADEMA aliyekuwa hajui hata kirefu cha neno “CHADEMA”! True story… Watu walimshambulia!)
Ni upumbavu – kwa maoni yangu – kushabikia chama fulani, eti kisa ulimuona Juma Nature kwenye bango! Fanya utafiti; sikiliza sera za wagombea, halafu amua yupi atakidhi mahitaji yako kama kijana. Hiyo ndio maana ya demokrasia.
Mfano wa pili: Kuna mijadala ambayo kila kijana anapaswa kuifuatilia na ikiwezekana kujaribu kujifunza vitu viwili vitatu. Hata kama hupendi kufuatilia mambo ya uchumi au siasa, chama fulani kikitangaza mgombea wa Urais, unapaswa kupandisha nyusi zako ili uone yanayoendelea.
Hata kama wewe hupendi wanyama au hujui mambo ya mbuga za wanyama, kelele kama hizi kutoka nchi za Magharibi zinapotua kwenye ngoma za masikio yako, unapaswa kuuliza maswali mpaka majibu yanayoeleweka yapatikane.
Nadhani unauliza kwanini; mimi sio vegeterian na napenda sana nyama ya nyati, mbogo, nyumbu na pundamilia! Halafu, wanyama wa Serengeti wanapenda sana kwenda Kenya kuzurura, eneweiz.
Fikiria tena. Serikali inasema itajenga Barabara ya Serengeti kama walivyopanga, lakini, “the feasibility studies are still under way.” Mtu unatoa tamko rasmi la kujenga kitu fulani kabla ya kumaliza utafiti? Ok, kwa sasa hivi sahau mambo yanayosemwa na watu kutoka Unyamwezini. Angalia ripoti ya TANROADS kuhusu mpango wa kujenga ile barabara halafu amua mwenyewe. Usisahau kuilinganisha na ripoti ya Frankfurt Zoological Society.
Binafsi, nimetoka sasa hivi kuisoma (ya TANROADS) na ikanikumbusha lile sakata la uchafuzi wa mazingira Mara lililokufa kibudu. Unakumbuka wataalamu wetu wa Wizara ya Nishati na Madini walioenda Mto Tighithe na litmus papers tu? Karne hii?
Nina uhakika kuna vijana wengi wapiganaji wenye machungu na Tanzania. Lakini wanasita kutoka kwasababu kelele zao zitakuwa ni kama kumpigia mbuzi gitaa. Nani ajitoe mhanga, halafu ‘akishindwa’ watu watasema tu, “Oh, alipigania haki za wasio na sauti.” Nukta. Yaani huo ndio mwisho wa upiganaji? Kugombea haki? Mtu katolewa kafara, halafu watu wanaleta upuuzi wa kujibu tu kwa sentensi moja. Kisha wanazima tarakilishi na kwenda kulala?
Mfano wa tatu: Tembelea ukurasa (facebook) wa Chama cha Vijana Tanzania? Nini kinatokea pale? Mbona porojo tu zisizokuwa na mbele hata nyuma? Kuna mzee (wa maana anayeheshimika Tanzania) alijitolea kutoa mwongozo na kuuliza maswali ya msingi. Unadhani kuna jibu la maana tuliloliona? Mzee akala kona. Sijamuona tena akichangia!
Halafu linganisha na ukurasa huu ambao unaendesha mijadala inayohusu Afrika – siasa, uchumi, utamaduni na maisha ya Waafrika kwenye kona mbalimbali duniani. Unajua wachangiaji wazuri wanatoka wapi? K-E-N-Y-A! Tunawaita Watani wa Jadi.
Wewe kama kijana, unajua hili Soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki linamaanisha nini? Utaathirika vipi? Je, ulishafikiria labda kuna njia ambazo unaweza ukazitumia ili ufaidike? Tuling’ang’ania tu, “Watakuja kuchukua kazi na ardhi yetu!” Mi’ mwenzenu nimeshaanza kupiga msasa ngeli yangu. Baada ya mwezi natia timu Nairobi.
Wakati wewe unafikiria kujibu haya, wenzako walishaanza kutuma CVs kwenye makampuni yanayopanga kuwekeza Afrika Mashariki…
Nitaishia hapa kwa leo. Nitaanika mambo mengine yanayonikereketa wiki ijayo. Kabla sijakuacha ili urudie kuisoma hii makala, napenda kusema nina ghadhabu kwasababu nina uhakika baadhi yenu – nyinyi vijana – ndio mtakaoshika usukani wa Serikali baada ya miaka kadhaa. Na sasa hivi kuna dalili inayoashiria kuwa tunayoshuhudia sasa hivi yataendelea kujirudia kutokana na uvivu wenu wa kusoma na kujifunza.
Kwa maneno mengine, zile kesi za Richmond, EPA, BoT, Uharibifu wa Mazingira Mara na Ujio wa Brazil zitajirudia. Majina tu ya wahusika ndio yatabadilika!
Kwaheri!
Nyerere sema, sema usiogope se…, sore, soore sana, ngoja nianze upa.
SN sema, sema…. hapana, hii hai-ryme vizuri, ajua, anza upya…
Vijana sema, Semaaa usiogope SEMA. Sisi vijana, hatuogopi vibaraka SEMA!
Nimeipenda sana posti hii, naperuzi linki ulizoweka humo kati ambazo sikuwa nazifahamu. Ila nachelea kusema, haya maneno hayavutii ‘wengi walengwa’ wao wanataka utume ‘msanii’ gani ana bifu na nani, na nani anatoka na nani na nani anatarajia kuoana na nani na nani kafumaniwa na nani…. si kwamba hizo si habari, bali zinapopewa kipaumbele kabla ya habari za msingi za kusimamia mustakabali wa nchi yetu, yaani tunapowaza aina ya ‘bling bling’ ya rim za LandCruiser wakati hata ‘bajaj’ hatuna uwezo nayo, ujue jamii hiyo ina walakini na mashaka makubwa, ukitaka kuthibitisha hili, chunguza kiwango na uwezo wao wa kujadili mada ngumu. Mi nlishachoka kuziandika, ni kama kuzungumza mwenyewe wanaopita njiani wanakuona mwehu, unazungumza mambo magumu teh teh, aliyesema maisha ni rahisi ni nani? Baada ya muda, wanaanza kulalamika tumeuzwa, tumetawaliwa… wakati wakistuliwa yanayoendelea sasa hivi, wanasema ‘unaandika sana’ au ‘acha kuchonga kihivyo’…!
Utavuna upandacho… tatizo, hawataki mavuno hayo! (Jamaa anakokota toroli kubeba Alizeti wakati alisia Ulezi)… lazima asingizie ‘mchawi kaloga shamba lake’.
Ni kweli kabisa,wengi wetu hatujui tufanyavyo wala hatujali kesho itakuaje.Ukitafakari mambo yanayoendelea nchini kwetu ni aibu tupu kwasababu hakuna dalili ya mabadiliko yoyote kutokea,vijana tumezubaa sana na tumekubali kuwa warithi wa matatizo yanayoikumba nchi yetu.Tumevipa vipaumbele vitu visivyokuwa na msingi,majungu,umbea na starehe vitatufikisha wapi??!@!Tusipobadili mitazamo ya maisha yetu,kamwe tusitegemee kuvuna yaliyo bora kwetu na jamii zetu.
Mwaka jana nilifanyiwa mahojiano na mwandishi wa habari na vitabu wa siku nyingi,Freddy Macha,mwenye makazi yake makuu huko nchini Uingereza.
Katika mahojiano yale,nilisema jambo moja ambalo liliwachukiza baadhi ya watu.Nilisema tatizo kubwa linalowakabili vijana wa leo ni uvivu,uvivu hata wa kufikiri!Vijana wa leo,tunapenda mambo mepesi mepesi.Tunataka yale mambo ambayo kimsingi hayahitaji kuumiza kichwa.Kama ni kitu kinachohitaji matokeo,tunataka matokeo ya haraka haraka.Hatutaki kujenga msingi,kujenga kuta na kisha kuezeka bati au vigae.Tunachotaka sisi ni nyumba.Ndio maana habari za kwamba fulani anatembea na fulani,zina washabiki wengi.Zinachangamsha genge na haziumizi kichwa.
Sasa tumefikaje hapa? Tatizo la uvivu wa kufikiri,lina misingi yake.Misingi hiyo ina historia ndefu.Ili kubadili jinsi vijana wanavyofikiri,ni muhimu kuzichunguza kwanza sababu zake.Kwanini vijana wa leo hawapendi kitu “siasa”?Kwanini wapo tayari kumtundika tairi shingoni mtu aliyeiba kuku na wasiwe tayari kusimama barabarani kumsubiri aliyeiba mabilioni ya fedha za kodi za wananchi?Kwanini wengi wapo tayari kununuliwa kwa vijisenti kidogo tu?
Ipo misingi ambayo iliwekwa na waasisi wa taifa letu.Nazungumzia zile habari za “zidumu fikra za fulani”.Fikra za mtu au watu wachache sana ndizo zilizohitajiwa.Kazi ya kufikiri na kuwaza ikawa sio ya kila mtu bali wachache tu.Kwa bahati mbaya kile kitu kikageuka na kuwa tamaduni.Tukawa watu wa “Ndio Mzee”.Hatuhoji.Ukihoji unaambiwa huna adabu au mpinzani.Unapachikwa majina ambayo msingi wake ni kukupotezea malengo na kukulainisha.Ukizidi kupinga zaidi na zaidi,itabidi uishi uhamishoni kama sio futi sita chini ya ardhi.
Na tatizo hili sio kwa vijana wa ki-Tanzania pekee.Limetapakaa duniani kote hivi sasa.Of course,viwango vinatofautiana.Inawezekana Tanzania tumezidi kidogo kwa sababu ya misingi niliyoielezea hapo juu.Lakini pia tukumbuke kwamba vijana wengi wa leo hawana pa kuigia miongoni mwa viongozi wetu(lack of role models).Kwani viongozi wetu wa leo wana muda wa kuwaza na kuwazua?Kama hawana muda wa kuisoma kwa makini mikataba,watapata wapi muda wa kufikiri kwa undani namna ambavyo watamkomboa mwananchi?Kwanini wamkomboe?Nani amtumikie nani?
Kwa hiyo,cha msingi tunachotakiwa kufanya ni kuikabili misingi yetu.Ilikuwa mizuri kwa wakati ule lakini haifai kwa sasa.Inahitaji mabadiliko.Tubuni mbinu mpya ya kushirikiana katika kufikiri.Ni kazi ya ziada.Natambua hilo.Lakini ni lazima tuanze kuijenga.Sisi wenyewe vijana.Tuwe wabunifu.Kama vijana wengi wa leo wanapenda habari nyepesi nyepesi,tufanyeje ili kutumia mwanya huo huo kuingiza chachu ya mabadiliko?Tuwakaripie?Tuwaburuze maktaba ili wasome japo vitabu viwili kwa mwezi?Enewei,hilo ni gumu.Maktaba hakuna vitabu.Kama vipo ni vya misaada kutoka nje(reject za ughaibuni)havijaandikwa kutokana na mazingira yetu.Ndio maana mtu anakuwa na degree ya uchumi lakini anachokielewa zaidi ni jinsi uchumi wa Marekani ulivyo.Ukimuuliza kuhusu Tanzania,mtakosana.Utamlaumu?Si kirahisi,baba zetu,wazee wetu hawakuandika.Najiuliza,si ungependa kusoma kitabu cha Mkapa kuhusu maisha yake na jinsi alivyofanya kazi zake wakati akiwa Rais?Kiko wapi?
Tunaoyaona matatizo hayo,tuna wajibu wa kubuni mbinu mpya.Tutumie sanaa?Tutumie hadithi?Tutumie video games?Tutumie mashairi?Ngonjera?Tunao wajibu.
Nimetembea lakini sijawahi kuona taifa lenye vijana wenye mtazamo finyu wa mawazo kama TZ. Tanzania imesharidhia soko la pamoja la Afrika mashariki, hatuwezi kuendelea kupoteza muda kwa kulalamika kuwa wenzetu ni wajuzi kuliko sisi, hayo mawazo ni mfu kwa sasa. Kila Mtazania anatakiwa aanze kujifunza ni jinsi gani atakavyo nufaika na soko hilo kwani wakati tunapiga kelele za kijinga wenzetu wanachangamkia fursa hiyo.
Lazima Watanzania tuanze kufuatilia kuna fursa gani kwenye mataifa ya wenzetu. Wizara yetu ya afrika Mashariki, mabalozi wetu katika nchio hizo, vyombo vyetu vya habari ni wakati wa kuwaelimisha watanzania na kuwajulisha watanzani fursa zilizopa katika nchi za wenzetu ili tuweze kuziwahi mapema. Vyombo vya habari visitumike kuwakatisha tamaa watanzania kuwa hatuwezi kushinda na wenzetu wakati mikataba ilishasainiwa na sasa watu wapo kwenye utekelezaji.
Vyombo hivyo vitumike kuelimisha jamii juu ya fursa zilizopo kwenye mataifa ya wenzetu. Tukumbuke kuwa sehemu kubwa ya Afrika Mashariki watu wanaongea Kiswahili, kwahiyo watu wenye uwezo wa kufanya biashara wanaweza kuelimishwa fursa ziko wapi. Watanzania wenzangu, tuache kulalamika tuingie uwanja tupambane na wenzetu kipenga kimeshapulizwa tuanze kucheza tukizubaa tutafungwa magoli mengi.
Shukrani kwa maoni ya kina. Nadhani mjadala unaelekea kuzuri — kujua chanzo na labda wachache wataamka na kufungua macho.
Jeff, nimeamua kuwakumbushia watu yale mahojiano uliyofanya na Macha: Sehemu ya kwanza na ya pili (bofya; hapa mpaka kila kitu kieleweke!).
Pia, ndio maana nikafungua huu mjadala kwa kudokezea matokeo ya utandawazi, bila kusahau athari au matokeo ya kuwa na mtandao. Sasa, hawa vijana ambao hata hawakumbuki zile hotuba maarufu za Mwalimu, inakuwaje leo bado wanakuwa wabishi kufungua mawazo na kujenga tabia ya kuhoji?
Mmegusia masuala muhimu sana ambayo ninaombea wahusika wayashughulikie… Kwanza, suala la vitabu; si viongozi wetu walipendekeza ile sera ya kitabu kimoja tu kwa kila somo nchi nzima? Pili, nadhani vitabu vya siasa vipo. Sijui mara ngapi nimepitia blog ya Udadisi nikaona hafla kibao za uzinduzi wa vitabu. Kama haitoshi, kuna hii tovuti: Marafiki wa Vitabu. Wanaandika hadithi fupi fupi, mambo ya siasa ya Tanzania (na Afrika kwa ujumla) na historia za watu maarufu Tanzania/Afrika.
Unadhani vijana wangapi wanajua hata Soma Book Café ilipo? Mi’ – kwa mtazamo wangu – nadhani ni visingizio tu. Na kama unaona haya yote niliyoyataja ni miyeyusho tu, fikiria mara mbili kwa makini sana. Kama unajua wapi pa kuzipata kwa urahisi habari za umbea, muziki na starehe nyingine, kwanini ushindwe kutafuta taarifa muhimu? Google wanabania searches za vitabu, siasa au mambo yanayokugusa?
Kusema ukweli, kuna wakati namuonea huruma Prof. Mbele, kwasababu juhudi zake ni kubwa mno. Lakini nadhani watu wanamuona kama amechanganyikiwa (Kusoma vitabu Bongo?).
Kijana mwenzangu, kama ulikuwa hujui dunia hii inapoelekea, basi itabidi ujiandae. Kwasababu muda si mrefu utakuwa unapigana vikumbo na watu kutoka kila kona ya dunia kitaani kwako! Sasa, kama unashindwa kuanzisha mjadala wa maana kuhusu maendeleo, uchumi, siasa n.k. basi ujue utapata shida. Sikutishi; ni hali halisi.
Uvivu wa vijana wa Tanzania ni kitu ambacho tumerithi tokea enzi za siasa ya ujamaa na kujitegemea. Hiyo siasa iliwafanya wengi kudhani kuwa maisha ni laini, kwahiyo watu wengi ambao ndio wazazi wetu wakazubaa kidogo. Kwahiyo, hatukupata urithi ambao ulitakiwa utufanye tuwe wachapakazi sababu tulitegemea Serikali kwa kila kitu. Kwa ujumla, siasa ya ujamaa na ukomunisti ililemaza pembe zote za kimaendeleo nchini mwetu.
Ingawa wengine wanasema kuwa Kiswahili kilisaidia sana kuiunganisha nchi yetu kwa kupunguza tofauti ya lugha kati ya makabila, naweza sema kilikuwa kichocheo au chachu iliyozuia mawasiliano ya idadi kubwa ya Watanzania na nchi zinazotuzunguka na dunia kwa ujumla. Magazeti yaliyokuwepo yalikuwa yanaandika habari zisizozipingana na siasa ya nchi kwahiyo wananchi hawakuweza kuelimishwa vya kutosha.
Mtu mwingine anaweza akapingana nami kwa kutoa mfano wa nchi zilizoendelea ingawa hawatumii Kiingereza, mfano Korea Kusini, Indonesia na Iran. Ninachoweza sema kuhusu hizi nchi ni kwamba hawakuwa na siasa ya Ujamaa bali waliwaacha wananchi wawe na maamuzi jinsi ya kufanya biashara na kuwasiliana na nchi nyingine ila wasivunje sheria. Ndio maana kukawa na mageuzi ya uchumi Korea Kusini na Indonesia na pia serikali ya Kiislamu ya Irani ikachukua nafasi kwa mapinduzi mwaka 1979.
Ukichukua mfano wa nchi kama Korea Kaskazini iliyoficha watu wake wasiweze wasiliana na dunia, utakuta kuwa uelewa wa watu ni mdogo. Nchi kama hio inaongozwa na wababe wachache. Hii haina tofauti na nchi yetu Tanzania. Kitu ambacho siwezi kukataa na ninakifurahia sana ni kuona jinsi Watanzania walivyoanza kuhangaika kutafuta elimu na maisha pande zote za dunia. Hii inaonesha kuwa baada ya miaka kama ishirini au thelatini hazina kubwa ya elimu na mtandao wa utaalamu utakuwa kila kona ya dunia na utaweza kufika na kutumika Tanzania bila wasiwasi. Kinachohitajika sasa ni kutoa elimu mbadala kwa Watanzania wote ili kuhakikisha kuwa wanajua haki zao za msingi. Mwamko wa vijana wa Kitanzania kwa sasa unafurahisha ingawa idadi ya hao vijana bado ni ndogo sana. Wacha muda uwe hakimu. Lakini tunapaswa kusubiri mpaka lini? Ngoja ngoja huumiza matumbo.
This was a very moving article. As a Tanzanian, I am proud to have someone like you who opens our eyes and let us know whats going on in Tanzania at present. Its sad to say the country isnt serious in any way possible..From the elderly to the young. I am sometimes ashamed of being part of the community of lazy people who only care about themselves…
I support all you have said and will stand and fight with you. Eti litmus paper was used…Are they serious?? Na akili zao zote wakaenda na litmus paper? What were they expecting to get out of that?? I have no words.. But I plan to start acting on this.. We are a very rich country. All we need is the right leadership to guide us in the right direction. I wasnt thinkin about voting since you already know who is going to win. Even though they say people have rights to choose their leaders corruption takes control of the country. We need to adopt to the freedom of speech policy as other countries. As we all know all those who have said anything have either disappeared or died miraculously.
Hii kitu si mchezo, yaani imeni-inspire mpaka nimeona nianzishe facebook group kwajili ya kujaribu kuamsha vijana: Campaign for Presidential Debate in Tanzania 2010 is on Facebook.
Dah. nakupa tano SN kwa kuinua mjadala huu muhimu. What the heck, nakupa 5 x 10^(infinity).
Mliochangia hapo juu mmeeleza ya maana – kuzubaa kwa wengi wetu chanzo chake ni tokea miaka ya 60 na tumeendelea kurithishwa tabia hii mpaka leo hii. Ila hili lisiwe sababu ya kuwa hatuwezi kubadili mwelekeo huu – hasa vijana wa sasa.
Kuna wakati ninajiuliza kichwani mwangu kuwa; je, ni kwasababu tuliupata uhuru wa kupewa tu na wakoloni ndio maana hatuna tabia ya kuwa wachangamkaji/wadadisi/wauliza maswali? Ninakaa na kujiuliza, je wazazi/mababu zetu nao wangeingia msituni kupigania uhuru, je taifa letu si lingekuwa na wananchi wenye uchungu na nchi yao – wasio tayari kukubali ufisadi wa nje nje? Tungekaa kimya tusikiapo wanaoiba mabilioni wanapewa nafasi ya kurudisha fedha? Ndio maana nikasema Tanzania ni nchi ya wapole, na hili sio jambo la kujisifia.
Tazama documentary Storyville. Cuba! Africa! Revolution!” (google for torrent or youtube)
Angalau basi nasisi tuwe wachangamkaji – aggressive kidogo (without arrogance), wenye kutaka kuwauliza viongozi wetu ‘kwanini’ ‘kivipi’ ‘lini’! Ukitaka kuona jinsi gani tulivyozubaa na kupenda ushabiki ushabiki usiokuwa na mantiki wewe tazama bunge letu au mikutano yetu ya kisiasa. mf. Umeshagundua ni mara ngapi watu wanapiga makofi kila mara mwanasiasa akiweka ‘punch-line’ kwenye hotuba bila hata ya kutoa ‘point’? Wakati mwingine inakuwa ni ‘punch-line’ ya kawaida tu, isiyo na mbele wala nyuma – ila utasikia makofi pwa pwa pwa. Bungeni ndio usiseme. Katika kila hotuba inayosomwa, ‘mheshimiwa’ na ‘kupeana shukrani’ nyiiingi. Ukihesabu ‘mheshimiwa’ na ‘napenda kutoa shukrani kwa’ zinaweza kuchukua 5-10% ya hotuba nzima. Huku ni kupoteza muda na kuwaleweza tu wasikilizaji ili tu waelemee upande wako pale unatoa hotuba ya kisiasa. Haya yote ndio tunayoyaona katika surrounding zetu.
Turudi kwa vijana. Binafsi sidhani hapa SN anahimiza vijana wafuatilie masuala ya siasa. No way. Tuwe angalau na motisha ya kutaka kujua au kuwa concerned na masuala ya nchi yako. Kwanini uogope? Kuogopa kwetu ndio hao mafisadi na viongozi feki wanautumia kwa faida zao. Kuna ubaya gani ukikataa Tisheti ya bure ya chama fulani unayoipata pindi mbunge akija kufanya kampeni tu? Uko tayari kupokea tisheti ya bure na wakati hujui mbunge huyo ameleta mabadiliko gani kifikra au kimaendeleo katika jimbo lako? Au hata kabla ya kusikia ‘manifesto’ yake?
Tuamke.
Ahsante kwa makala nzuri.
Kwanza kabisa ningependa tujiulize sababu zinazopelekea vijana wengi Tanzania kukosa mwamko katika kushiriki mambo ya msingi ya maendeleo ya taifa letu. Kwa maoni yangu, sababu ziko nyingi ambazo zinatokana na mabadiliko ya kimifumo ambayo taifa letu linayapitia. Tanzania ilipobadili mfumo wa kiuchumi kuelekea ubepari, hatukufanya maandilizi ya kutosha kuendana na matakwa ya ubepari, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha tunawaandaa vijana wetu kikamilifu kuzikabili changamoto za ubepari. Matokeo yake tulifungua milango kwa tamaduni za kigeni ambazo ziliwanyima nafasi vijana wetu kujifunza tamaduni zetu na kukumbatia tamaduni za kigeni (sio zote ni mbaya), ambazo kwa kiasi kikubwa haziendani na hali halisi ya matakwa ya nchi yetu. Lakini pili, vyuo vyetu vimejikita zaidi katika kuwaandaa vijana kuwa washiriki wazuri kwenye uchumi wa soko huria, vyuo vingi vinatoa shahada/stashahada za masomo ya kushiriki katika sekta binafsi ambayo mara nyingi hayawaandai wanafunzi kuzingatia majukumu ya serikali na siasa kwa ujumla, hapa namaanisha kuwa vijana wengi wanaufinyu wa uelewa wa majukumu ya serikali, jumuiya za kiraia na hata sekta binafsi, na ni jinsi gani wanaweza kushiriki kupungunza umasikini.
Mifumo yetu ya kiutawala pia ni kikwazo kikubwa sana katika maendeleo ya vijana nchini, mifumo iliyopo inawanyima vijana fursa za kushiriki maamuzi muhimu yanayohusu nchi yao. Maofisini, vijana wanakabiliana na changamoto nyingi za kunyanyapaliwa kwa hofu ya kuchukua nafasi za juu, mifumo yetu huwanyima vijana kuwapa kazi zinazoendana na taauluma zao (tuzingatie kuwa sekta binafsi bado ni ndogo hivyo ajira nyingi ni za umma), vijana wanakabiliana na ukosefu wa waelekezi (mentors) n.k. Mifumo mibovu inayolinda ufisadi serikalini na hata kwenye sekta binafsi pia imekuwa ni kikwazo kwa maendeleo ya vijana, vijana wanakabiliana na upinzani wa khali ya juu na vitisho pale wanapokataa kushiriki ufisadi.
Ukosefu wa elimu kwa vijana walio wengi nchini pamoja na ukosefu wa ajira kwa waliohitimu masomo, pamoja na hayo niliyoyahaainisha hapo juu ya ubovu wa kimifumo na kukosa ushirikishwaji, kwa pamoja huwanyima vijana moyo (incetives) wa kushiriki mambo ya kisiasa, ikiwa ni pamoja na kufuatilia sera mbali mbali za nchi na vyama vya upinzani. Vijana wakijua kuwa mchango wao hautathaminiwa, na hawapewi nafasi katika jamii, basi huamua kusema kwamba siasa ni mchezo mchafu na kubakia kushiriki mambo ambayo wanaona yanawaongezea faraja kama mapenzi, starehe n.k.
Ziko changamoto nyingi katika taifa letu ambazo zinawahusu vijana na utatuzi wake unahitaji umakini mkubwa ikiwa ni pamoja na ushiriki wa pamoja. Ushirikiano baina ya serikali, vyama vya kiraia, mashule na vyuo, sekta binafsi, na jamii kwa ujumla ni wa muhimu sana katika kukuza maendeleo ya vijana.
Mawazo mazuri sana. Na mengi nakubaliana nayo. Ila, kama mzee aliyekulia miaka ya sabini ningependa kupinga kwamba ujamaa na kujitegemea ni kosa la kimsingi. nadhani mambo hayo ya zidumu fikra sahihi zilikuja miaka ya themanini lakini miaka ya sabini vijana walichangamka kupita kiasi. Wanafunzi wangu, akina hayati Mwaikusa, Mwakyembe, Kabudi, Kajubi na wengineo wengi walikuwa wabishi kupita kiasi na wanaharakati kuanzia uanafunzi wao. Silabasi za Tanzania zilikuwa za kipekee na zilizolenga kukuza kufikiri.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam usiseme. Watu walikuwa wanakesha si kuandika assignment ya kupata maksi tu bali katika kubishana kuhusu mambo ya msingi. Na mara nyingi walienda kinyume cha au mbele zaidi ya viongozi wa nchi. Kulikuwa na intellectual excitement and intellectual debates, na naamini hali hii ilikuza sana uwezo wa kufikiri wa vijana.
Kwangu mimi, itikadi ni muhimu, itikadi ni mwongozo unaotulazimisha tuache kufikiria watu, mavazi yao, majisifu yao na kadhalika. Lakini mtu anafuata itikadi fulani kwa sababu amechambua kwa kina na kuielewa. Ametumia akili.
Kwahiyo sipendi kuchukua muda mrefu, lakini nadhani uvivu wa fikra umeenda sambamba na kuporomoka kwa elimu yetu, na kupotea kwa itikadi na/au dira ya aina yoyote.
Mzee Mabala, nilikuwa nimeshaanza kuandika notes (kwa ajili ya makala ijayo) ili kuwajibu watu wanaodhani sera za Ujamaa ndizo chanzo kikubwa. Kwasababu wewe ulikuwepo na umesema mwenyewe, mi’ nitaongezea tu:
Rafiki wa mama na baba yangu wamewahi kurudishwa vijijini kwasababu tu walikuwa “wanajadili” mambo ya siasa; kuipa motisha Serikali ya wakati ule. Kumbuka enzi zile kulikuwa hakuna hizi simu za mikononi wala nini.
Kwahiyo, Serikali ilichokuwa inafanya ni kuwapandisha wanafunzi wa Chuo Kikuu kwenye yale mabasi ya UDA na kuwarudisha vijijini. Muulize mzazi wako atakupa hadithi zote…
Baada ya hapo, wakirudi baada ya miezi sita au mwaka mzima, wanaanza upya! Halafu basi, kuna baadhi hawakuishia hapo. Vijana wangapi wanajua kuwa kulikuwa na wanafunzi “watukutu” waliowahi kumchora Mzee Ruksa kwenye kuta za majengo ya vyuo?? Sisemi ile ilikuwa sahihi, lakini msisimuko wa kufuatilia mambo muhimu nchini ulikuwa mkubwa sana. Kinyume kabisa na sasa hivi… Na wakati ule kumbuka kulikuwa na magazeti ya Serikali tu – Uhuru na Mzalendo.
Nadhani wengi mnaosoma hapa kuna sehemu ya akili yenu ambayo bado “inam’misi” Ze Utamu… Oooh, nimesahau; Mange anajitahidi kuendeleza libeneke.
Yaani kuna wakati ghadhabu zinazidi kwasababu ya visingizio visivyokuwa na maana! Wakati naandika hii almanusura nitumie matusi ya nguoni.. kwasababu hiyo ndio lugha itakayoeleweka zaidi!!!
Basi kwa kuwa vijana hawataki kufutilia mambo ya msingi kwenye vitabu, mijadala au vijarida, basi tusikilize basi nyimbo zenye mashairi yenye mambo ya msingi:
http://www.eastafricantube.com/media/20005/Roma_-_Tanzania/
Heshima mbele Mabala Sr. Tunashukuru kwa maelezo yako kwani wengi wetu hapa tuna’hypothesize masuala mengi kuhusiana kipindi hicho cha nyuma. Uwanja huu ni kwa vijana wa leo na wakipindi cha nyuma, kwahiyo binafsi ningefurahi kusikia mawaidha yako hapa mara moja moja.
@Bahati. The song is now ‘on repeat’ in my itunes. Asante!
Very articulate intelligent arguments. Sadly…Good intentions are not enough; the more i think about it the more I realise labda vijana tujitahidi kugombania uongozi. Watu kama sisi tungekuwa wabunge, its obvious majimbo yetu yangekuwa na maendeleo.
Maybe a lot of tanzanians have potential, but they never get a chance or are struggling to fulfill that potential…:-(
[Edited]
This is very inspiring, I have just realized that my complaining is not gonna bring change; it all begins with me!!!
Asante sana.
Makala hii imenigusa sana — inaelimisha, inakemea na inafundisha pia! Ahsante sana mdau.
ASANTE.
Ndilo ninaloweza kusema kwa sasa.
Kakangu nikushukuru kwa kutunza na kuoanisha matukio na makala. Kuweka “marejeo” ni kitu chema saana. Na hiki ni kati ya mengi tunayokosa kwenye blogu nyingi. Blogu makini za wanaosoma mambo makini (na waweza kuwaona na kuwasoma humu wakichangia) hufanya hivyo.
Tunaendeshwa na kile tunachofikiri watu wanataka (hata kama watakao wamelewa na wawazalo si lao wala wao)
Hatuoni mstari mwembamba saana ulio kati ya Umaarufu na Ubora. Na hilo latufanya TUJIPOTEZE KATIKA HARAKATI ZA KUJITAFUTA.
Kama nilivyosema, nitaanza ku-link makala hizi kwenye yale niandikayo (japo najua wengi watafanya kama ulivyotabiri hapo juu….KUTOSOMA KWA KUWA NI NDEFU) lakini mwisho wa siku tutafika
ASANTE KWA UCHAMBUZI MAKINI.
I wish hata vyombo vyenye dhamana (kama TBC) vingekuwa na makala kama hizi.
Baraka kwako
“Maneno yenye kubamba mfano wa miba Bamba” ~Wanaume TMK
Watanzania wengi tumekuwa na nidhamu ya woga na hiyo ndiyo inayopelekea mambo mengi kufa ama kubaki kama yalivyo. Vijana kuwa hivi inatokana na mifumo mibovu tuliyopokea kwa shinikizo la misaada kutoka nje. Mathalan suala la vijana kumomonyoka kimaadili sio kwamba halikuwapo katika miaka ya zamani, hasha isipokuwa kwa sasa limezidi.
Jaribu kuangalia vijana ambao walipitia National Service ya wakati ule na sisi wa dot.com utaiona tofauti.
Suala lingine linalotutatiza ni kwamba watu wamekuwa na tabia ya kuongea na kuwa na nadharia nyingi lakini hakuna utendaji. Hakuna mtu mwenye guts ya kufanya kitu fulani na hii inatokana na woga kama nilivyosema hapo mwanzo. Na kama mtu akijaribu na kufanikiwa utaona utitiri wa marafiki ambao hapo mwanzo walimwona kama mzandiki tu.
Suala lililopo kwa vijana ni kuamua kati ya pumba ama mchele. kwa sababu mustakabali wa nchi hii upo mikononi mwao. Napendekeza mkazo utiliwe kwenye Elimu,National Service irudi, Miiko yetu izingatiwe,tufanye kazi tuache kukaa vijiweni na kuweka visingizio ati serikali yetu haifanyi kazi, Watendaji wabovu serikalini waadhibiwe kwa adhabu kali ikiwamo kifo kama wanavyofanya China. Halafu tuone
Mada nzuri ndugu Baraka, sema mimi nilikuwa na maswali kadhaa. Umesema National Service irudi, kwanini National Service ilisitishwa kipindi kile, sababu zilikuwa ni nini hasa?
Pia umesema vijana waache kukaa vijiweni, ni kweli. Pamoja najua hatuna hulka ya kuchakarika, lakini watu wafanye nini kama kazi zenyewe ndio hizo za kubahatisha.
Tatu, sidhani itakuwa vyema tukiwafuata wachina na mambo yao ya ukiukwaji wa haki za binadamu, lakini kuna haja ya kuwawajibisha viongozi, au wachapwe kama Nyerere alivyokuwa akiwachapa…hahah!!…
Ikumbukwe katika miaka ya 80 Tanzania ilikuwa katika hali mbaya sana kiuchumi. Kutokana na hilo Nchi pamoja na wananchi wake iliwalazimu kufunga mikanda. Lakini hata hivyo, kulikuwa na ulazima wa kukopa kutoka kwenye Taasisi za kimataifa ikiwamo Benki ya Dunia na IMF ambao walipinga Sera ya Ujamaa na kujitegemea.
Ni hawa hawa IMF na benki ya dunia walioleta mkanganyiko wa mawasiliano baina ya Waziri wa fedha na Ikulu. Na kupelekea kwa Waziri wa fedha wakati huo E.Mtei kujiuzulu.
Katika kipindi hicho hao wahisani walikuja na pepa yao ilyokuwa na mapendekezo yao ambayo ilibidi tuyachukue bila kuchambua kama yalivyo ili tuweze kupata hiyo fedha vinginevyo nchi ingekuwa kaputi na ni baada ya Mwalimu kung’atuka mambo hayo yakaanza kutekelezwa.
Mapendekezo hayo yaliitwa “Structral Adjustment Programme” ambayo yalipendekeza kuwe na mfumo wa vyama Vingi, Soko huria, Ubinafsishaji, Uhuru wa maoni na kuabudu, Mageuzi ya kiuchumi pamoja na mambo mengine ambayo siwezi kuyaelezea. Wakati huo suala la National Service kwa vijana ilikuwa ni suala la lazima na huwezi kuajiriwa kama hujapitia huko. Lakini hawa jamaa watoa misaada kutokana na akili zao wakawashauri viongozi wetu waliondoe.
Sasa hivi athari zake tunaziona
Suala la vijiweni liko tu na litabaki kuwepo kutokana na kukosekana kwa ubunifu na serikali kuendelea kutafuna kodi za wananchi. Suala la wamachinga halitaisha kwa sababu Serikali kwa kutumia makucha yake imeua mfumo wa kilimo cha biashara ambacho kilikuwa kinawalipa watu kiasi kwamba wengi wao wamesomeshwa ama kwa pesa ya pamba, Kahawa, Korosho ama Mkonge.
Viwanda vingi vya uzalishaji vimekufa na taasisi kubaki magofu ukianza kutaja list haitaisha na kupelekea ajira kufa. Nitakupa mfano mdogo tu. Hapo Ubungo kulikuwa na viwanda vya nyuzi za Samaki, Zana Za Kilimo, Maziwa, Urafiki tujiulize viko wapi.
Katika mazao haya ya kilimo cha biashara kulikuwa pa na taasisi ambazo mbali na kuwaongezea ujuzi wakulima viliwaongezea pia namna ya kuweza kujiajiri na kuongeza kipato.Nikutajie Chuo cha Mkonge, Chuo cha Ushirika
Mifumo mizuri iliwekwa ili kwamba kusiwe na sehemu ambayo tuatukuja kujilaumu wenyewe. Tujiulize mchawi wetu ni nani?
Ukienda kwenye mashirika ya serikali ni hivyo hivyo kila shirika ama idara ilikuwa na taasisi yake kwa ajili ya kuwaongezea ujuzi watu wake.
Reli – Chuo cha reli, Simu – Chuo cha simu kijitonyama, Umeme- Chuo cha Umeme, Mapato- Chuo cha Mapato nk nk
Sasa suala la vijana kukaa vijiweni na kuanza kulaumu ninaliongelea kwa namna ile ile ya woga mtu anaweza kusema mimi nimesoma mpaka kidato cha sita siwezi kuzibua mitaro ya maji machafu ili nipate pesa. Wakati huo huo anapiga kelele maisha magumu. Hatuna guts.
Tunahitaji kiongozi mwenye guts za kurudisha vyote hivyo na sio peke yake kwa support ya watanzania wote kwa vitendo.
Asante sana kwa maelezo yako, nadhani leo nimejifunza mawili matatu, hasa hilo la nyuzi za samaki, sijawahi kusikia hiyo..kila siku mtu unajifunza.
Nadhani kwa ufupi, tunaweza kusema mchawi wetu utandawazi/ uwekezaji?..hiyo itakuwa sahihi?…
Napenda kurudi tena kwenye swala la vijana. Nimekubaliana na wewe sehemu kubwa, lakini nadhani tutatofautiana kidogo kwenye swala la vijana. Umesema kuwa vijana kwanini wasichimbe mitaro ya maji machafu ili wapate pesa, kuliko kukaa na kupiga kelele tu..mhh!!..mada kali hiyo. Hivi kweli leo hii tupiganie kuzibua maji machafu kama njia ya ujasiliamali? Tatizo langu ni hili, wanaofanya hiyo kazi wanalipwa shilingi ngapi? Je, malipo ya kuzibua maji machafu yanakidhi gharama za maisha ya Tanzania ya leo?….
Mimi kwakweli sidhani, kama mwalimu analipwa chini ya laki mbili, sitapenda kujua mzibua maji machafu analipwa shilingi ngapi. Hata kama mtu atasema, bora uzibue mitaro ya maji machafu ujipatie shilingi elfu mbili, kuliko upige domo kijiweni, sidhani hiyo ni realistic. Bora mtu akae kijiweni amkabe mtu, aibe au atafute sugar dady, (kama ni msichana).
Maisha bado yatakuwa equally hard, hata kama mtu ukizibua maji machafu na maisha yalivyo bongo sasa hivi.
Baraka, shukrani sana kwa mchango wako. Bila shaka ulikuwa makini wakati mambo uliyoyataja yakiendelea miaka ile ya 80 mwishoni na 90 mwanzoni; vitu ambavyo vijana wengi hawavijui kwa kina (Ni kujiuliza tu, kwanini 80% walikuwa hawataki mfumo wa vyama vingi, lakini mwishowe Serikali ikabadilisha katiba?).
Hilo la kiongozi mwenye guts, linaakisi mambo tuliyojadili (hapa) miezi michache iliyopita. Natamani ungeona ule mjadala na ukatupa mawazo yako. Nisingependa kurudia niliyosema.
Pia, kwa mtazamo wangu nadhani ni tatizo letu, vijana, kutokuwa na ule mwito wa kuwajibika; iwe kulitumikia Taifa au jamii inayotuzunguka. Sababu? Kila mtu ana mawazo yake.
Hivyo basi, nadhani hatuna budi kuanza kufikiria njia za kurudisha yale mawazo ya kuwajibika kwenye vichwa vyetu. Elimu? National Service irudishwe? Au National Service “mbadala” iingizwe kwenye mitaala ya elimu?
Kwa mfano, wakati wa likizo kila kijana awe anafundisha watoto wadogo mashuleni, kutembelea vituo vya watoto yatima, kusaidia kusafisha majengo ya hospitali na shughuli nyingine ambazo zina manufaa kwa jamii na kujenga fikra za vijana.
Kwanza shukrani kwa makala nzuri na elekezi, nakubaliana na wachangiaji wenzangu kwa mambo mengi tu.
Lazima tukumbuke kuwa uwajibikaji umepungua sana nchini kwetu na tabaka zima vijana kwa wazee hakuna anayejali Taifa kwa ujumla kila mtu anajijali mwenyewe.
Hili ni tatizo kubwa sana ingawa mnaweza mkaona kama ni kidogo, mtu unaposhindwa kujali mustakabali wa Taifa lako hapo ndipo utaona vijana hawana hata mda wa kuuliza… Kwanini? Au, mbona hivi? Sababu anajua hata akiuliza halitamsaidia kitu.
Ndo tunaona urasimu kila ofisi na imekuwa ni sehemu ya maisha yetu kutoa na kupokea rushwa, vijana hatuulizi wala hatufikirii na kama ukijaribu kuuliza na kuwaeleza watakuambia unapoteza mda tu wewe hii yote inaonyesha ni jinsi gani vijana wengi wameshakata tamaa kuhusiana na Taifa lao.
Wanaona mfumo umeoza na taifa linaelekea kuanguka kama mabadiliko hayajafanyika, lakini watu bado tupo “lazy” kama kawaida; kulaaumu viongozi kila siku. Jamani, viongozi au serikali itakufanyia kila kitu? Kuna nafasi ya Serikali kama kujenga mashule,hospitali and other infrastructures; au kusaidia uchumi lakini mengine [ni] ya wewe binafsi, si [sahihi] kulaumu kila kitu Serikali.
Baraka umejaribu kuongelea China kuhusu sheria kali, pia naunga mkono kwa hilo. Jamani ifikie mahali sisi kama vijana tuwe wawazi na bila unafiki. Hivi unavyoiona nchi yetu hii kweli inahitaji uongozi wa lelemama?
Kunatakiwa kuwe na viongozi watakao kuwa na nguvu ya kusema kitu fulani na kinafanyika kweli. Sio Serikali za kishikaji kishikaji halafu manasingizia Haki za Binadamu, Haki za Binadamu zipi? Umeshafikiria ni wangapi hawapati hata mlo kwa siku TZ? Ni wangapi wanafia magerezani bila hata makosa? Ni wangapi hawawezi hata kupata basic needs? Je hizo sio Hakio za Binadamu? Tukisema hao mafisadi wanyongwe mara moja mnasingizia Haki za Binadamu, hivi kweli tunafikiria sisi Watanzania? Ana haki gani ya kuishi mtu asiyethamini Taifa na maisha ya mamilion ya Watanzania? Kwanini hufikirii leo hii wewe unateseka/anateseka kwa sababu ya hao viongozi wasiotahamini Taifa?
Watu kama hao kwa mimi wala sioni ajabu kama wangenyongwa na kupotelea mbali halafu tuone kama wataendelea kufanya madudu. Hii yote ni kwa sababu ya sheria zetu [ambazo] haziabani; ndio maana wanafanya wanavyoona,na sisi vijana kama hatutabadilika basi ndio Taifa hili linaelekea kuwa hivyohivyo — mambumbumbu, wazembe, wavivu na wasiojituma wakisubiri wafanyiwe kila kitu na Serikali yao. Serikali ya China ukileta uzembe lazima wakunyonge mara moja [kwasababu] inajali sana wananchi wake. Hivyo ni bora kumtoa mmoja na kubakiza 99 kuliko kumwacha na kuwapoteza wote 100.
[Edited]
Former Beijing mayor gets suspended death sentence: [bofya]
Watanzania na hasa vijana tunapaswa kujua kuwa tukitana mafanikio ya taifa letu lazima [tuzalishe]. Hakuna taifa lolote lililopata maendeleo kwa kufanya biashara za kichuuzi. Biasha ya kununua na kuuza hazina mchango wowote kwenye uchumi kwa upana wake. Hebu tujiulize Tazania tunazalisha nini? mazao ya biashara ni kama yote yamekufa, viwanda vya kusindika mazao vimekufa, viwanda vya kuzalishia zana za kilimo vimekufa, hivi kweli kuna mtu atakayeona kilimo kama mkombozi ?. Hebu tuangalie bei ya mazao yanako limwa kweli inavutia kiasi ambacho vijana watapenda kuwekeza na kupata mafanikio.
Watanzania wenzangu wakati nchi yetu ikitamba duniani kwa kuzalisha mazao ya biashara miaka ya nyuma serikali ilikuwa na mchango mkubwa sana kwa wakulima kuazia mbegu, pembejeo, masoko etc.
Serikali haiwezi kukwepa jukumu lake la kutengeneza mazingi yatakayo wezesha nguvukazi (watu) kuzalisha. Kwa mfano kama ni kilimo ihakikishe kunakuwepo na miundo mbinu ya umwagiliaji, wataalamu wa kilimo kwaajili ya kuelimisha wakulima, pembejeo, masoko, miundombinu ya kusafirishia mazao, viwanda vya kushindika mzao ili yaweze kuongezeka thamani etc. Kilimo lazima kiwe ni kivutio kwa kuwekeza na sio kimbilio la mwisho ili kukidhi mahitaji ya chakula. Ili kilimo kiwe kivutio lazima serikali itengeneze mazingira hayo.
Serikali ya Tanzania imeamua kuachia sekta binafsi jukumu la uzalisha huku ikidai yenyewe kazi yake ni kukusanya kodi. Ukumbukwe kuwa sekata ya uzalisha ndio yenye uwezo wa kutoa ajira nyingi ya mtu mmoja mmoja au makundi, pia ndio yenye mchango mkubwa kwenye uchumi. Kwa Taifa lenye watu masikini kama Tanzania ,watu hawawezi kubeba mzingo mkubwa wa gharama unaohitajika katika sekta ya uzalishaji kwa upana wake. Watanzani wengi wamebaki kuzalisha kwa kiwango cha kukidhi sehemu ya mahitaji binafsi tu, kutokana na hali halisi ya mazingira wanayozalishia.
Mimi nipo Ulaya kwa sasa, serikali za huku zimetengeneza mazingira katika nyanja zote ( kilimo, viwanda, biashara, elimu, etc) amabayo yanavutia uwekezaji kutoka ndani na Nje ya mataifa yao, ambapo uwekeza umezalisha ajira nyingi kuliko hata raia wa mataifa haya ndio maana na hata sisi wageni tunaweza kuajiri japo tupo wengi.
Ni kweli Vijana wa Watanzinia ni waoga na wavivu wa kufikiri, lakini haya tumerithishwa na wazazi wetu walio tulea na kutukuza hivyo. Lakini hata Ulaya hakuna mtu mwenye uwezo wa kujitafutia ajira mwenywe, ila ni serikali zimetengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji ambapo ajira zinazalishwa kwa mamilioni.
Lazima serikali ya Tanzani ibebe jukumu la kutengeneza mazingira ambayo yatazalisha ajiri kwa vijana wetu. Vinginevyo tutabaki tuanapiga “Vuvuzela” huku tukiangamia kwa umasiki ulio tukuka.
Kaka we mkali natamani hata nikuone uko na mtazamo chanya kwa nchi yetu hii ya wadanganyika, yote uliyosema kweli ni tatizo kubwa vijana wa Tanzania zaidi ya asilimia 99. Kwa upande wangu inaniuma sana nikiona mambo ktk nchi yetu yanakwenda mrama na vijana tumekaa kimya, lakini kwanini tumekuwa hivi? ndo swali la msingi la kujiuliza, nimejitahidi kufuatilia mijadala mingi kwenye vipindi mbalimbi kwenye luninga kuhusu sisi vijana nikagundua tatizo kubwa ni malezi tuliyopata pamoja na mazingira tuliyoyakuta ktk nchi yetu. Ukweli ni kwamba hatukuandaliwa na wala hatuandaliwi kupambana na maisha kwa sasa na kwa baadae, yaani mambo mengi ni ilimradi tu siku zimeenda watu wanajifanya wako busy kila kukicha hawajali wala kuheshimu waliowachagua kuongoza nchi yetu.
Mi naamini kabisa kama tutajengewa mazingira mazuri hilo suala la uvivu halitakuwepo kwa vijana wa Kitanzania, tunawasifia jirani zetu kwasabu viongozi waliowapa jukumu la kuwaongoza wako na mlengo wa kuongoza nchi na si kuchukua chao mapema. Viongozi wetu hawana uchungu na nchi yetu wala maendeleo ya wananchi wanaowaongoza tukiwemo vijana.
Mtazamo wangu ni kwamba vijana tulioamka tuwaamshe na wenzetu umefika wakati tuwe na sauti ya pamoja kuhusu nchi yetu. Tuachane na mambo ya ushabiki tuangalie uhalisia wa mambo na tusome alama za nyakati, wakati ndo huu bado hatujachelewa sana. Tuachane na mambo ya nchi zilizoendelea hasa ya starehe tuikomboe nchi yetu. Vijana tumekuwa busy na vipindi visivyo na maana kwenye luninga na tunategemea mabadiliko kwenye nchi yetu. Nchi yetu iko na mapungufu mengi sana kama matumizi mabaya ya fedha, usalama wa vyombo vya usafiri mdogo, maisha mazuri kwa tabaka fulani, mishahara midogo kwa wafanyakazi, kodi kubwa kwa wafanyakazi, matatizo ya fedha kwa vyuo vya elimu ya juu, na mengine mengi sana.
Pamoja na yote niliyoyataja hapo juu lakini vijana tumekuwa kimya na wengine kuendelea kushabikia viongozi waliotufikisha hapa tulipo. Kinachonikera zaidi ni pale mtu anaposimama jukwaani na kuanza kunadi mambo fulani wanayodai kuyafanya ktk nchi hii, hivi kama umefanya mambo mazuri wananchi si wanaona kwani mpaka utuambie ina maana hujiamini ya uongozi wako.
Naomba niishie hapa ma’ke naona kichwa changu kiko na mambo mengi sana kuhusu nchi yetu, vijana tuungane tufanye kitu kipya na cha muhimu kwa nchi yetu mpaka washangae wenyewe, tuache kulaumiana bali tuambiane, tufundishane na tuongozane katika kipindi hiki tunachotaka mabadiliko kwa nchi yetu. Nawapenda sana.
TUWE NA KAULI MBIU YETU VIJANA, VIJANA TUSIDANGANYIKE, TUAMKE SASA TUIKOMBOE NCHI YETU.
Kim, shukrani kwa mchango wako. Inatia moyo.. Unajua unaweza ukadhani mjadala umeshafungwa; lakini mzee umeamua kusoma makala yote na kutoka maoni yako kwa kirefu. Heko kwa hilo!
Hapa tunajaribu kuwaamsha wenzetu kwa njia tofauti. Ila kama ulivyosena, hatujachelewa sana. Safari ndio imeeanza.
Its all true,vijana wa Kitanzania haya tunayoyaona leo tujifunze sana tusije tukayarudia watoto watoto wetu watatushangaa.
Ninayo furaha kufahamu forum hii kupitia jamii forum.
Napenda kuchangia mada kuwa vijana wengi hasa wa tanzania wanasumbuliwa na tatizo la kuishi maisha yaliyopita badala kuelewa kuwa tuko katika karne hii tofauti na enzi ya wazazi wetu. Tuko katika karne ya habari na mawasiliano. Hivyo ni muhimu vijana kufuatilia habari na taarifa kuhusu nchi yao na dunia kwa ujumla. Tatizo vijana wanaangalia nyuma na kuanza kulalamika.
Tuko kwenye kipindi cha kutengeneza ajira badala ya kutafuta ajira, kipindi cha ubunifu wa miradi binafsi sio ya umma. Ni wakati wa kubadilisha matatizo kuwa fursa za kibiashara, Ni wakati wa kujenga mitandao ya biashara, siasa nk.