Siku 33 zimepita tangu Watanzania watumbukize kwenye masanduku yale makaratasi yaliyokuwa na picha za watu ambao walitangaza nia ya kutuongoza; katika ngazi ya kata, jimbo na nchi nzima.
Mengi yamesemwa, mengi yamejadiliwa na yataendelea kukumbukwa kwa kipindi kirefu. Ila kuna mambo, au niseme visa, ambavyo vilinigusa. Sina uhakika kama vinatuambia kitu fulani kuhusu mwelekeo wa nchi yetu, lakini nimeamua kuviweka kwenye maandishi.
Timu ya Makame imetuangusha. Na mpaka sasa hivi bado nasubiri hicho kibali cha kuandamana kwenda NEC kudai muda niliopokonywa siku ya Jumanne, tarehe 2 Novemba, mwaka 2010. Najipanga kuwasiliana na Mh. Tundu Lissu ili tuone kama kuna uwezekano wa kuunganisha nguvu zetu na kudai haki zetu za msingi kwa pamoja.
Ukiangalia upande wa pili wa sarafu, kutokana na mizengwe ambayo machoni mwa wengi ilikuwa ni “kasoro ndogo ndogo,” watu waliona hawana budi kulinda kura zao. Hiyo ilihitaji kujipanga vizuri, uvumilivu na wakati mwingine ubunifu wa ziada ulitumika.
Ngara – Mpaka wa Tanzania na nchi za Rwanda na Burundi
Inasemekana majirani zetu walikuwa wanatumiwa na wagombea fulani kwenye chaguzi zilizopita. Kilichokuwa kinafanyika ni kuwapa vitambulisho vya kupiga kura Wanyarwanda na Warundi wanaoishi kwenye vijiji karibu na mpaka. Kwa hiyo unashtukia tu siku ya uchaguzi unapanga mstari na sura ngeni kabisa, ambazo hujawahi kuziona kwenye kata yako au maeneo yanayozunguka kituo chako cha kupiga kura.
Wanavijiji wa Ngara wakapewa semina kadhaa ili kuwafundisha njia za kuzuia huu upuuzi. Lakini zoezi lao lilikumbwa na kizingiti kikubwa; tofauti kabisa na walivyotegemea, baada ya kupiga kura, wananchi waliamrishwa kuondoka na kukaa mbali kabisa na vituo vya kupiga kura.
Badala yake, walichofanya ni kujipanga kwenye njia inayoelekea kwenye vijiji vilivyopo upande wa Rwanda na Burundi. Na kila aliyekuwa anatoka Rwanda au Burundi (kwa nia ya kuingia Tanzania na kupiga kura) alirudishwa alipotoka!
Dawa ya mabomu ya machozi
Wale waliokuwa wameganda kwenye runinga (ITV), bila shaka watakuwa wanakumbuka zile vurumai za Mwananyamala. Askari wa FFU hawakuwaruhusu vijana kukesha kwenye vituo na kulinda kura zao. Fujo za hapa na pale zilitokea. FFU wakawa wanatumia mabomu ya machozi kuwatawanya wale vijana.
Hii ni taswira iliyokuwa inaonekana sehemu kadhaa Tanzania kwa siku mbili hadi nne mfululizo — kwenye vituo vya kupiga/kuhesabu kura Mwanza, Mbeya, Arusha, Mara na mikoa mingine.
Walichofanya vijana wa Mwananyamala ni kutembea na chupa za maji. FFU wanawapiga mabomu, vijana wanatawanyika, wanaenda kunawa nyuso, halafu wanarudi na zoezi la kulinda kura linaendelea; kufuatilia kila mtu anayeiingia kwenye vituo ambavyo kura zilikuwa zinahesabiwa, kama ana mihuri, makaratasi ya kura na kadhalika. (Kuna dogo muuza mihogo alikamatwa Ubungo na mihuri inayotumiwa kuidhinisha matokeo!)
Sasa, waliokuja na ubunifu wa aina yake ni watu kutoka Tarime. Ukiacha mbinu ya kutumia maji tu kupunguza makali ya mabomu ya machozi, wao walikuwa na mtihani mwingine — FFU walikuwa wanatumia maji yanayowasha kuwatawanya walinda kura. Hivyo wakaamua kujipaka mafuta machafu (sina uhakika kama ilikuwa crude oil au oili chafu); basi maji yale ya FFU yakawa yanateleza tu bila kugusa ngozi.
Shughuli nzito – Nyamagana na Arusha Mjini
Ukiacha visa vilivyokuwa vinajiri sehemu nyingi Tanzania, nadhani yaliyotokea kwenye majimbo ya Nyamagana na Arusha Mjini yataendelea kuwa kwenye vinywa vya Watanzania wengi.
Kama “tetesi” za sababu ya kucheleweshwa kwa matokeo kutangazwa ni za kweli, basi hatuna budi kujiuliza maswali mengi.
Kwa kifupi tu: kwenye hayo majimbo mawili, wagombea wa upinzani (CHADEMA) walijizolea kura nyingi kuliko wapinzani wao. Wagombea wa chama tawala wakaja na ‘ofa’ ili washindi waachie majimbo. Lakini “msukumo” wa wananchi waliokuwa nje ya halmashauri husika uliwalazimu wahusika kutangaza matokeo halali kama yalivyo.
Binafsi, nawapa heko wananchi waliojitokeza kufanya waliyofanya; niliguswa mno. Nitakuja kuwahadithia wajukuu zangu hapo baadae. Ni vitu vidogo machoni mwa wengi, lakini ukiwa katikati au karibu na kushuhudia haya yote, na kunusa ile hali ya utete, kuna kitu kitakufanya ufikirie sana.
Ningependa kusikia maoni yenu:
- Wale ambao walijiandikisha lakini hawakwenda kupiga kura kwasababu walidhani kura zao zitaibwa, wanajisikiaje sasa hivi? Kuna sehemu za mioyo yao inajuta?
- Mwamko wa Uchaguzi Mkuu na siasa kwa ujumla utaongezeka tunapoelekea mwaka 2015?
- Ni wazi kuwa wananchi hawana imani na Tume ya Uchaguzi. Je, hii ndio njia pekee iliyobakia “kulinda kura”?
- Je, kama Katiba na mfumo wa kuteua watu wa NEC usipobadilishwa, haya matukio yatabaki kwenye hayo majimbo tu, au mikoa mingine “itaambukizwa” mbinu za kulinda kura?
Wabunge wa upinzani