Hivi tunakielewa Kiswahili

Dk. Slaa, "umepora" mke?

Kama wewe ni mfuatiliaji wa kampeni za uchaguzi, huwezi kuwa umepitwa na  mjadala huu wa Dr. Slaa “kupora” mke wa mtu. Lakini baada ya kusoma sehemu mbalimbali juu ya hili suala, nimekuja kugundua vitu vikuu viwili. Kitu cha kwanza, hatujui Kiswahili, pamoja ya kuwa hii ni lugha yetu ya taifa. Pili, ni mwamko wetu katika masuala ya udaku, kitu ambacho si kigeni miongoni mwetu.

Mambo haya mawili yanatosha kuakisi taswira ya jamii yetu, kuwa ni jamii ya aina gani. Pamoja na kuwa tunaweza kuangalia haya mambo mawili kwa haraka haraka bila kufikiria mara mbili, lakini kuna siri kubwa iliyojificha. Tuanze na hili la lugha, kabla ya kugusia suala la mapenzi yetu na mambo ya udaku.

Lugha ni nyenzo muhimu sana katika jamii ye yote ile, na kwenye jamii ya watu wenye akili timamu hilo linafahamika. Kwani lugha hutunza mila na desturi zetu, historia yetu, huonesha ukuaji wa jamii, mwenendo wa jamii  na mambo mengine. Hivyo utunzaji wa lugha ni jambo la muhimu, pamoja na kuiheshimu.

Leo hii Kiswahili, kama Kiingereza, kimekua kwa uzuri na ubaya. Ukuaji wa lugha umechangiwa na vitu mbalimbali, kama teknolojia, mabadiliko ya maisha na kadhalika. Kwa mfano kwenye katuni hii, tunaweza kuona ni jinsi gani teknolojia ya sms ilivyobadili utumiaji wetu wa maneno na lugha kwa ujumla.

"ttyl"

Utumiaji wa lugha wa namna hii unaweza kuangaliwa au kutafsiriwa kama ushahidi wa ongezeko la umomokaji wa maadili. Pia, kuonesha ni jinsi gani jamii yetu ilivyobadilika haraka — kutoka kuwa jamii makini mpaka jamii inayochukulia mambo kirahi-rahisi. Ukweli huu usichukuliwe kama ni sifa, bali fedheha kubwa.

Sasa tukirudi kwenye matumizi ya lugha, na leo nitajadili matumizi ya maneno haya mawili, kuporwa na kuiba au kuibiwa. Nimeona nijadili kwani yametumika sana siku mbili hizi kwenye vyombo vya habari mbalimbali. Hofu yangu ni kuwa wengi wetu hatujui matumizi fasaha ya maneno hayo; labda yametumika makusudi, ili kuamsha hisia badala ya fikra. Pamoja na kuchochea udaku badala ya busara.

Ndugu Daniel Mahimbo, amelalamika kuwa “ameporwa” mke na mgombea urais wa Chadema, huku wengine wakitumia neno “kuiba”. Lakini, je, neno “ameporwa” au “kupora” ni sahihi? Uelewa wangu mdogo wa neno kuporwa au kupora linahusihwa na uwizi, hivyo huweza kuamsha hisia za kifedhuli kirahisi na haraka. Na hilo ni kweli, kwani leo hii tunaona mawazo mengi ya kifedhuli katika mijadala mbalimbali kuhusiana na hili suala.

Pili, mtu ukiporwa, inamaana umeibiwa, na kwa kawaida katika taratibu za kijamii, unatakiwa kupeleka hilo suala polisi. Hapo hapo inaleta picha ya unyang’anyi, tena wa kutumia nguvu. Lakini, je, hilo ndilo lililotokea kwenye hili tukio?

Pia, mtu kawaida unaporwa mali yako, kwa maana ya kitu, lakini unaposema umeporwa mke, hiyo inaleta hisia ya kuwa mke ni mali yako. Sasa mjadala huo unaweza kutupeleka kwenye mambo mazito ya kijinsia, hilo ningeomba tujadili siku nyingine tena.

Tatu, kuiba kwa kawaida ni tendo ambalo mtendewa hufanyiwa bila kujua. Sasa, je, ndugu Mahimbo hakujua kuwa mke wake haishi nyumbani kwao tangia mwezi wa tatu? Kama hivyo ndivyo ilivyo, nadhani na yeye inabidi atazamwe alikuwa mume wa aina gani. Pia na kama alikuwa baba wa aina gani, kama alikuwa anajali familia yake, au alikuwa na tabia kama za wanaume wengi ambao hutelekeza familia zao kilolela-holela.

Tatizo langu kuu juu ya habari hii ni ukosefu wa umakini. Kivipi?

Lugha za kirahisi-rahisi zikitumika kwenye vyombo vya udaku, inaeleweka, kwani lengo hasa ni kutumia lugha ambazo zitaamsha hisia na sio fikra. Vyombo hivyo hutengeneza pesa kwa kutumia lugha na picha kucheza na watu kisaikolojia.

Lakini vyombo vya habari visivyo vya udaku vinapotumia lugha nyepesi-nyepesi unabidi upatwe na wasiwasi juu ya mustakabali wa jamii yetu na huko tunapoelekea. Wasiwasi wangu zaidi ni kuwa taaluma ya uandishi wa habari imeanza kuingiliwa na mamluki na hadhi yake imeanza kupotea kwa kasi inayotisha.

Maneno fasaha yangetumika yangesaidia kutupa usahihi wa suala hili, na majadiliano ya kijinga yasingekuwa mengi. Kwani matumizi sahihi ya lugha huziba mianya ya uwezekano wa mawazo tata au ya kijinga kupenya na kutuathiri sisi sote. Hii si kwa habari hii tu, ipo mifano mingi.

Kwa mfano, sote tunajua kuwa Mheshimiwa Lowassa hakustahafu, bali alijiuzulu. Lakini kila atokeapo kwenye chombo cha habari, yeye huitwa Waziri Mkuu mstahafu. Kwanini? Neno kustahafu huficha ukweli wa hali halisi na kupotosha mantiki, na hata kulaghai historia ya kilichotokea kwa kizazi kijacho.

Jamani, mimi "sikustahafu!"

Hapo hapo, neno kustahafu humlinda mhusika na kunyamazisha watu ambao wangependa kuuliza maswali juu ya kitendo cha kujiuzulu. Kujiuzulu huleta picha ya kuwa kuna dhuluma fulani ilitokea, lakini neno kustahafu huhusishwa na busara. Hapo tunazidi kuona nguvu ya lugha jinsi ilivyo nyenzo muhimu sana katika jamii; si tu kama chombo cha kutuwezesha kuwasiliana peke yake.

Lakini kabla sijamalizia na aya ya mwisho, nimejaribu kujiuliza: Kwanini jamii yetu ina mwamko mkubwa wa mambo ya udaku? Je, hii ni ishara kuwa umakini wetu ndio huo unatutupa mkono? Je, utandwazi ndio wa kulaumu?

Lakini labda ya kutokana na maisha kuwa magumu, watu wanatumia habari za udaku kupunguza misongo ya maisha. Pia inawezekana habari nyingi kuhusu jamii zetu ni habari za kusikitisha au kuudhi, hivyo watu wamechoka na kuamua kupunguza mawazo na habari za udaku au ‘nyepesi.’ Hii labda inatokana na (ukweli kwamba) watu walio wengi wamepoteza imani ya mabadiliko yanayohitajika kutokea, hivyo kutojali tena.  Labda nimekosea kabisa? Sijui.

Mwisho ningependa kuwasihi, jamani tuwe makini na matumizi ya lugha, kwani matumizi yetu ya lugha yanaweza kutujenga au kutubomoa sisi na jamii yetu. Na hata kutuchochea kuwa watu wenye kutumia fikra au kutuhamasisha kuwa watu wajinga. Hili ni dhahiri, kwani tumehamasika kweli-kweli na hili suala la “uporwaji” wa mke, ikichangiwa na lugha inayotumiwa na vyombo vya habari. Bila kutilia maanani kuwa mpaka sasa hatujui ukweli na undani. Lakini baada ya kuona tu maneno, “kuporwa” na “kuiba,” basi tumepandwa na jazba, bila ya kufikiri. Kama jinsi ‘tunapovimba vichwa’ tuitwapo “wananchi wenye hasira kali.”  Na kuhalalisha matendo yetu ya kinyama. Hii si ishara nzuri, kwani tukiendekeza hii hali tutakuwa watu wa kuongozwa na hisia na sio fikra; tutafanya mambo mengi kwa papara na sio kwa busara.

Previous ArticleNext Article
Bahati was born and raised in Tanzania, and then moved to California to pursue his college education. He graduated in 2008 with a Bachelor’s Degree in Political Science and a minor in Sociology. Bahati expects to be doing his Masters in African Studies in the near future. He is currently working on starting a t-shirt business and a possible publication of some of his writings. One thing that Bahati cannot live without is music, specifically Hip Hop & Bongoflava which he argues are both the voice of the youth today, and is excited to look into how Bongoflava can be a source of further entrepreneurship among the youth in Tanzania. Bahati believes that Bongoflava can help to reduce poverty in Tanzania, as can a more collective effort among key players.

This post has 8 Comments

8
  1. Nimefurahishwa sana na hii makala. Hongera sana mwandishi kwa kuweza kuyaona makosa kama hayo katika matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili. Lugha inaendelea kubadilishwa na kizazi cha sasa kadri siku zinavyoenda na kile Kiswahili halisi kinapotea. Nini kifanyike?

  2. Upo kwenye ukweli mtupu,hili jambo la Dr.Slaa ni sawa na kuamsha hisia za watu wale waliolala tangu mwaka 2005 baada ya uchaguzi na hatimaye kuamka juzi tena wakitegemea kulala tena baada ya October 31.Pambanua African politics ni sawa na nchi yenye wasomi watatu na wananchi zaidi ya milioni 45.

  3. Nimefurahishwa sana na makala hii, nimekuwa nikijiuliza kwa muda mrefu juu ya swala hili, hivi kama mmeoana si ni wewe na mke wako ndio mpo kwenye mkataba wa ndoa, iweje mkeo kavunja mkataba wenu wewe uende kumshtaki dr slaa? haiingii akilini kabisa.

  4. Nakwambia lugha ya Kiswahili ni ngumu kweli kweli. Mfano mzuri ni mchangiaji aliyepita ambaye ametumia neno “swala” badala ya “suala”. Simlaumu kwasababu hata mimi nilikuwa nalitumia hilo neno mpaka juzi juzi nilivyogundua.

  5. Makala safi sana! Sasa, haya makosa tunayoyaona kwenye vyombo vya habari, ni vitendo vya makusudi au waandishi hawajui kama wanafanya makosa?.. Ambayo yanapotosha kama mwandishi alivyosema.

    Nadhani ni muhimu sana tukihimiza kufundisha wanataaluma ya uandishi wajibu wa kuwa waandishi wa habari; huwa unakuja na majukumu mengi sana…

  6. Nimesoma kaka, na nimeelewa sana.
    nguvu ya Lugha ni kubwa sana, inaweza kufanya mambo mengi yakaharibika. Na kinachoonekana hapa pia ni kwamba ilitakiwa itumike Lugha kama hiyo ili kuleta tafsiri iliyokusudiwa kwa wananchi, na ionekane kwamba Jamaa (Dr. Slaa) amepora, ameiba.
    Lakini sasa wengi wetu hata hvy, tumepata mwanga mwingine ambao hatukuwahi kufikiria kuwa lugha yetu haikutumia sawa sawa, pamoja na ukweli kuwa bado hatukukubaliana na hilo. Ila sasa tunajua kuwa kwa makusudi kabisa maana ninaamini kuwa wanafahamu walichoandika hakikuwa sawa ila tu kwa makusudio yao.
    Ahsante sana.

  7. Ninadhani Tanzania ndio nchi pekee mhitimu yuko tayari kusoma gazeti la udaku kuliko kununua “Raia Mwema” au “Rai”. Yaani mapenzi yetu ya udaku ndio yanasababisha haya yote. Ukitaka kuona jinsi hawa waandishi wanavyopotosha wengi pitia habari hizi mbili (kurasa za mbele!)

    Vichwa vya habari:
    1. DK SLAA AFIKISHWA MAHAKAMANI (bofya)
    2. WAFUMWA NA MADENTI (bofya) (picha haihusiani na makala)

    Ingawa sidhani magazeti haya yanatiliwa maanani na mtu yeyote makini, ukweli uliopo Watanzania wengi wanapenda kuyasoma – kuna kipindi niliona kibosile kwenye Prado yenye namba za usajili za STJ akisoma gazeti kama hilo.

    Waandishi wa habari kuweni makini. Mnapotosha vizazi.

  8. Kweli umeandika. Ni kweli kabisa lugha yetu inatumika vibaya sababu kubwa ni watu kupenda udaku kuliko ukweli wa mambo. Magazeti kwa issue hii ya Dr Slaa wameweka ushabiki mbele kwa maslahi ya wanaowatuma badala ya kutumia maneno yenye ujumbe halisi. Kuporwa ni neno lenye maana ya kutumia nguvu umchang’anya mtu kitu, badala ya kwenda mahakamani, anakuja kurudia rudia habari hii ya kuporwa mke wake. Police wapo, mahakama ipo.

    Vyombo vya habari visijidhalilishe kwa kutumia lugha yetu ya Kiswahili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend