Uchaguzi 2010: NEC nirudishieni muda wangu!

Acha haya mambo ya vyombo vya habari; tayari tunajua uozo wa waandishi wengi wa habari!

Siku mbili baada ya Uchaguzi niliamua kuganda mbele ya runinga nikitegemea Makame atakuja kutupa matokeo ya Urais ya angalau majimbo 50 – 70 kwa mpigo. Jana yake alitangaza matokeo ya majimbo 10 tu. Sikutoka nyumbani siku nzima. Baada ya kupata msosi wa mchana tu (msosi ulikuwa wa kengele; najua… aibuuu!), Makame akatokea akiwa na kabrasha moja bab’kubwa!

Nikajua leo shughuli ni pevu. Msisimuko wa Uchaguzi ukanisukuma kutafuta karatasi na kalamu ili niweze kunakili matokeo na kuja kutoa maoni yangu hapa.

Basi, kama kawaida yake, akaanza polepole, “Jimbo la kumi na moja: Biharamulo Magharibi… Kuga Peter Mziray, APPT – Maendeleo…”

Akatulia kama sekunde tano hivi, akaangalia glasi ya maji iliyopo kwenye meza upande wake wa kuume, kisha akarudisha macho kwenye karatasi yenye matokeo. Nikawa najiuliza, nini kinaendelea pale? Nikasimama chap chap kwenda kutafuta kalamu na karatasi kwenye chumba cha pili.

Wakati narudi na kuketi, ndio Makame anamalizia taratibu, “… kura 21,640 ambazo ni asilimia 50 nukta 22 ya kura zilizopigwa.”

Mi’ nikadhani kwenye hilo jimbo (la kwanza kutangazwa siku hiyo) Slaa au Lipumba nd’o washindi, kwasababu wakati naondoka kwenda chumba cha pili nd’o alikuwa anaanza kutangaza kura za mgombea wa Chama Cha Mapinduzi, CCM, Kikwete Jakaya Mrisho.

Eneweiz, kwasababu sikuwa na uhakika nikasema ngoja nisubiri. Wakati nachora majedwali kwa ajili ya kufuatilia viti vya Ubunge vilivyochukuliwa na kambi ya upinzani, nasikia Makame akisema, “Slaa Willibrood Peter, CHADEMA, kura 18,343, ambazo ni asilimia 42 nukta 57.” Kabla akili yangu haijaelewa kinachoendelea, nikasikia, “Lipumba Ibrahim Haruna, Chama cha Wananchi, CUF, kura 441 ambazo ni asilimia 1 nukta 02.”

Kwasababu ni muda mwingi tu ulikuwa umepita, nikadhani Makame alikuwa ameshaanza kutangaza matokeo ya jimbo la pili.

Sasa, hiki ndicho kilinitibua; Makame anaendelea, “Jimbo la kumi na mbili: Busanda.”

Uf*&a! Yaani muda wote huu kumbe alikuwa anatangaza matokeo ya jimbo moja tu! Yaani, nimeenda chumba cha pili kutafuta karatasi, nimerudi, bado alikuwa hajamaliza kutangaza ya jimbo la kwanza?

Ahh! Nikajipoza kwa kujisemea mwenyewe, “Labda ilibidi awe anataja majina matatu ya kila mgombea na vyama husika kama utambulisho rasmi wakati anaanza kutangaza matokeo. Polepole. Baadae huko awe anatupa tarakimu tu.” Nikavuta pumzi na kuendelea kumsikiliza.

Mara nasikia, tena, “Kuga Peter Mziray, APPT – Maendeleo…” Kabla sijakaa vizuri, nasikia, “Kikwete Jakaya Mrisho, CCM…, Slaa Willibrood Peter, CHADEMA…, Lipumba Ibrahim Haruna, CUF…, Rungwe Hashim Spunda, NCCR Mageuzi…, Mgaywa Muttamwega Bhatt, TLP…, Dovutwa Yahmi Nassoro Dovutwa, UPDP…”

Jazba zikachukua ukumbi kwasababu mi’ niliona ni upuuzi kuendelea kutaja majina matatu au zaidi ya kila mgombea — taratibu. Ni kupoteza muda hasa ukizingatia kuna majimbo mengine zaidi ya 220 yalikuwa yanatusubiri.

Hivi, huyu Dovutwa Yahmi Nassoro Dovutwa… jamani, majina yote yale? Kuna haja ya kupachika ‘Dovutwa’ mara mbili? Kutamka silabi za majina yake tu ni mbinde! Halafu hapo sijamtaja Mgaywa Muttamwega Bhatt!!!

Nifikishieni huu ujumbe kwa hao wahusika wawili (naona uvivu hata kukopi na kupesti majina yao!): Hivi, mngejiondoa kwenye kinyang’anyiro mnadhani labda kasi ya kutangaza matokeo ingeongezeka kidogo?

Basi, Makame akawa anaendelea kwa mwendo huo huo wa kinyonga, akihakikisha anatamka majina matatu au zaidi ya kila mgombea kwa ufasaha.

Kama hiyo mizengwe yote haitoshi, kituko ni pale alipofika kwenye jimbo la kumi na nne (la nne kutangazwa siku hiyo). Makame akanena, “… Kura zilizoharibika ni 176 ambazo ni asilimia sifuri nukta 32. Jumla ya kura ni 55,370 ambazo ni asilimia 100.” Akaanza kufunga makabrasha yake huku akisema, “Tutaendelea kutangaza matokeo ya majimbo mengine kesho!”

Kusema ukweli sikuamini nilichoshuhudia. Nikadhani labda jamaa anatupiga fiksi tu. Siriaazz, jamaa akafunga mkutano! Na waliokuwa kwenye hai-tebo wakakipa! Wakati yote haya yakiendelea kulikuwa na mwandishi wa habari ambaye alikuwa bado anajitahidi kurekebisha kipaza sauti kwenye hai-tebo, akidhani ndio kwanza mkutano wa leo umeanza.

Mi’ niliahirisha shughuli zangu zote siku ile ili kufuatilia matokeo ya Uchaguzi, kwahiyo natafuta wenzangu ambao walikutwa na yaliyonikuta. Nia hasa ni kutafuta kibali cha kuandamana kwenda NEC kudai muda wetu waliotupotezea siku ya Jumanne, Novemba 2, mwaka 2010.

Pia, tutajaribu kuwafundisha na kuwaonesha njia za kutangaza matokeo fasta. Haya mambo ya kutangaza matokeo ya majimbo manne kwa siku ni upuuzi!

Hivi, Makame ana watoto? Na aliwaaga Jumanne ile kuwa anaenda kazini? Mi’ jamaa angekuwa dingi yangu ningempa laivu tu! Mwalimu angekuwepo nadhani lazima angetembeza bakora…

Hivi hii katuni ilichapishwa?
Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 10 Comments

10
  1. Hahaha! Makame angekuwa dingi yako ungetakiwa umchape bakora! Stori ya kweli na inafurahisha jinsi ilivyotungwa/andikwa…Kusema kweli incompetence ya NEC imeonekana wazi mwaka huu…

  2. Aise blunder za mwaka huu watu walitakiwa wajiuzulu. Bongo tambarare, vyeo havipewi kwa merit bali kwa ukomredi. Haingii akilini kura za watu milioni chini ya 10 zinachukua siku 5 kuhesabu, je walioandikishwa wote 19 milioni wangepiga kura ingekuwaje? Si tungekaa mwezi mzima kusibiri?

    We have no urgency, na kila mtu kimyaaa!

  3. Kama unafikiri NEC ilikuwa slo katika kutangaza matokeo ya urais, hebu tafakari kuhusu mambo hayo yafuatayo:

    1) Leo ni siku ya 23 tangu uchaguzi uishe na mpaka sasa hivi NEC haijathibitisha wala kujumulisha wala kutangaza matokeo ya ubunge kwa majimbo yote 239. Sisi wananchi tunachokijua tu ni majina na vyama vya wabunge hao ambao tayari wameapishwa na kuanza kupiga makofi bungeni. Lakini nijuavyo mimi, hakuna mtu ambaye anaweza kunipa takwimu rasmi kwa wabunge wote hawa, yaani walipata kura ngapi na walishinda majimbo yao kwa asilimia ngapi?

    2) Achana na ubunge nao. Yu wapi mwenye kunieleza vizuri kuhusu matokeo ya udiwani? Je, vyama vyote vilishinda kata ngapi? Halmashauri ngapi ziko chini ya majority ya chama gani?

    NEC inapaswa kutueleza yote hayo. Mpaka sasa kimya tu. Kulikoni?

  4. Halafu Wabongo tumesizi tu…

    Klinton, unadhani matokeo ya majimbo na kata yangetupa taswira fulani ambayo labda ingetoa mtiririko mzuri wa jinsi wananchi walivyopiga kura za kiti cha Urais?

  5. SN: Swali zuri sana. Nawaza pia kama kweli kura zote zile zilizopigwa kwenye vile vituo 54,000 zimehesabika vizuri au kuna hitilafu ya kikalkulata hapa na pale?

  6. Hivi NEC hawatumii MS Excel ku-compile voter’s data/election results? Na zile computers zote walizonazo na mabilioni ya pesa waliyotumia ku-print kura zote, si wangewekeza tu kwenye kura ya Ndiyo/Hapana kwenye kila mtaa, kata au kijiji cha Tanzania. Kama watu wameweza kutumia mabilioni ya pesa kuprint kura ambazo hazikuhesabiwa au hazijamalizwa kusesabiwa then hawa watu wa NEC wanatakiwa kufikishwa mahakamani kujibu kesi za ufisadi. Je, huwa kuna financial auditing kila baada ya uchaguzi?

  7. kuna tatizo kubwa sana kwenye tume ya uchaguzi, tatizo lenyewe ni kwamba NEC hawaamini katika demokrasi bali matumbo na maslahi yao.

  8. Klinton, nimekutana na watu wachache ambao walipigia kura vyama tofauti. Yaani, kwa mfano, kura ya urais inaenda kwa mgombea wa chama fulani, halafu ya ubunge inaenda kwa mgombea wa chama kingine. Na walikuwa na hoja zao.

    Sasa, suala la kura ya mtu ni siri na hatuwezi kujua fika watu walipigaje kura. Lakini, bahati mbaya tunafikiria watu wote wakipiga kura wanapigia wagombea wa chama kimoja tu. Kuna ukweli wowote? Tuna ushahidi?

    Hapo ndipo tunaporudi kwenye lile suala la kutokuwa na imani na Tume ya Uchaguzi. Ni tatizo dogo kwenye macho ya “walio juu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend